Kwa nini Wahouthi bado wanafanikiwa kuishambulia Saudi Arabia?

- Author, Lamis Al-Talibi, Ahmed Munaim, Dalal Gabriel, Mark Allison
- Nafasi, BBC Fact Check
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 4
Kadri mvutano kati ya Saudi Arabia na kundi la Wahouthi (Ansar Allah) unavyozidi kuongezeka, macho mengi yanaelekezwa kwenye silaha zinazotumiwa na pande hizo mbili. Licha ya Saudi Arabia kuwa miongoni mwa mataifa yanayotumia fedha nyingi zaidi duniani katika sekta ya ulinzi, Wahouthi wameendelea kuonyesha uwezo wa kutekeleza mashambulizi kwa kutumia makombora na droni zenye uwezo mkubwa.
Lakini ni silaha zipi hasa zinazotumiwa na kila upande, na kwa nini baadhi ya mashambulizi yanafanikiwa licha ya mifumo ya kisasa ya ulinzi iliyopo?
Wahouthi wanatumia silaha gani?

Chanzo cha picha, Office of the Military Media for the Houthis
Katika miaka ya karibuni, Wahouthi wamebadilika kutoka kundi la waasi hadi kuwa nguvu ya kijeshi yenye uwezo wa kutumia silaha za kisasa zinazoweza kufika mamia au hata maelfu ya kilomita kutoka maeneo wanayoyadhibiti.
Miongoni mwa silaha zinazowavutia zaidi wataalamu wa masuala ya usalama ni makombora ya balistiki yenye uwezo wa kushambulia malengo ya mbali. Baadhi ya makombora hayo yanaaminika kuwa yametokana na teknolojia ya Iran, ingawa Tehran imeendelea kukana kuwapatia Wahouthi silaha moja kwa moja.
Mojawapo ya makombora yanayojulikana ni Zulfiqar (Barkan 3), ambalo linaelezwa kuwa na uwezo wa kufika umbali wa zaidi ya kilomita 1,200 na kubeba mamia ya kilo za vilipuzi.
Wahouthi pia wanadai kuwa na makombora ya kasi ya juu aina ya hypersonic, yanayoweza kusafiri kwa kasi inayozidi mara kadhaa kasi ya sauti na kufanya iwe vigumu zaidi kuyazuia yanapokuwa angani.
Droni zimebadili sura ya vita
Mbali na makombora, droni zimekuwa moja ya silaha muhimu zaidi kwa Wahouthi.
Droni aina ya Rajum hutumika kwa mashambulizi ya karibu na inaweza kubeba makombora ya chokaa. Aidha, kundi hilo linamiliki droni za upelelezi kama Samad-1, ambazo zinaweza kutumika kukusanya taarifa za kiintelijensia au kufanyiwa marekebisho na kubeba vilipuzi kwa ajili ya mashambulizi.
Kwa gharama ndogo ikilinganishwa na ndege za kivita, droni zimewapa Wahouthi uwezo wa kulenga vituo vya kijeshi, viwanja vya ndege na miundombinu muhimu ndani ya Saudi Arabia.
Saudi Arabia inajibu kwa nguvu kubwa za kijeshi
Upande wa Saudi Arabia una moja ya majeshi yenye vifaa vya kisasa zaidi katika Mashariki ya Kati.
Nchi hiyo inatumia ndege za kivita za kisasa, mifumo ya ulinzi wa anga na helikopta za mashambulizi aina ya Apache, ambazo zina uwezo wa kubeba makombora na kufanya operesheni za usiku na mchana.
Saudi Arabia pia imeanza kutumia droni za kisasa kama SkyWasp, ambazo zinaweza kufanya kazi za upelelezi pamoja na mashambulizi katika umbali mrefu.
Lakini silaha zinazovutia zaidi katika ghala la kijeshi la Riyadh ni mifumo ya ulinzi wa anga ya Patriot na THAAD, iliyotengenezwa Marekani.

Chanzo cha picha, Getty Images
Kwa nini Saudi Arabia haiwezi kuzuia kila shambulio?
Swali ambalo wengi huuliza ni: ikiwa Saudi Arabia ina mifumo ya kisasa kiasi hiki, kwa nini bado baadhi ya makombora na droni za Wahouthi zinafanikiwa kuvuka ulinzi wake?
Kwa mujibu wa Nawaf Obaid, mtafiti mwandamizi katika Idara ya Masomo ya Vita ya King's College London, ukweli kwamba baadhi ya mashambulizi yanafanikiwa hauonyeshi kuwa mifumo hiyo imeshindwa.
Anasema makadirio yanaonyesha kuwa Saudi Arabia imefanikiwa kuharibu kati ya asilimia 89 na 90 ya makombora na silaha nyingine zilizorushwa na Wahouthi.
Changamoto kubwa ni ukubwa wa Saudi Arabia yenyewe. Taifa hilo lina eneo kubwa sana, huku vituo vya mafuta, viwanja vya ndege, bandari na miundombinu mingine muhimu vikiwa vimetawanyika katika maeneo mbalimbali.
Zaidi ya hayo, mashambulizi mengi hufanywa kwa wakati mmoja kwa kutumia makombora ya balistiki, makombora ya cruise na droni, jambo linaloongeza ugumu wa kuyazuia yote kwa wakati mmoja.
Vita ya teknolojia ya kisasa
Mgogoro huu umeonyesha jinsi vita vya kisasa vinavyozidi kutegemea teknolojia kuliko idadi ya wanajeshi pekee.
Kwa upande mmoja, Saudi Arabia inategemea mifumo ya gharama kubwa ya ulinzi wa anga na ndege za kisasa. Kwa upande mwingine, Wahouthi wanatumia makombora na droni ambazo mara nyingi hugharimu fedha kidogo zaidi lakini zinaweza kusababisha madhara makubwa zikifaulu kufika kwenye lengo.
Matokeo yake ni vita ya teknolojia ambapo kila upande unajaribu kumpiku mwenzake kwa kutumia ubunifu wa kijeshi na mifumo ya kisasa ya mashambulizi na ulinzi.
Na kadri mzozo huo unavyoendelea, swali kubwa linabaki: je, mifumo ya ulinzi ya gharama kubwa inaweza kuendelea kuhimili wimbi la mashambulizi ya droni na makombora ya bei nafuu yanayozidi kuwa ya kisasa? Hilo ndilo swali ambalo vita vya Saudi Arabia na Wahouthi vinaendelea kulijibu kila siku.


































