Mtoto wa Mugabe akiri kosa la kumnyooshea mtu bunduki Afrika Kusini
Mtoto wa rais wa zamani wa Zimbabwe, Robert Mugabe amekiri kosa la kumtishia mtu na bunduki na kuwa nchini Afrika Kusini kinyume cha sheria.
Bellarmine Mugabe amekubali mashtaka hayo mawili baada ya kukamatwa mwezi Februari kufuatia tukio la kumpiga risasi kijana wa miaka 23 nyumbani kwake mjini Johannesburg.
Kijana huyo mwenye umri wa miaka 28 amekuwa akizuiliwa pamoja na mtuhumiwa mwenza Tobias Matonhodze, na amefikishwa mahakamani mjini Alexandra hii leo.
Mawakili wa wawili hao waliiambia mahakama kuwa wateja wao, wako tayari kurejea nchini kwao Zimbabwe kwa gharama zao wenyewe ikiwa hawatapewa adhabu ya kifungo.
Matonhodze, mwenye umri wa miaka 33, alikiri pia mashtaka ya jaribio la kutekeleza mauaji, kuzuia haki kutendeka, kuingia nchini Afrika Kusini kinyume cha sheria na kumiliki risasi.
Bellarmine Mugabe, ambaye pia awali alishtakiwa kwa jaribio la mauaji, alizungumza tu kuthibitisha kuwa anaelewa mashtaka yanayomkabili na atakubali mashtaka baada ya kuafikia makubaliano na waendesha mashtaka.
Wawili hao walikamatwa tarehe 19 mwezi Februari baada ya polisi kuitwa nyumbani kwa Mugabe katika eneo la kifahari la Hyde Park mjini Johannesburg.
Mwanaume anayeaminika kuwa mlinzi wa lango, alipelekwa hospitalini akiwa hali mahututi baada ya kupigwa risasi.
Hukumu ya kesi hiyo inatarajiwa kutolewa tarehe 24, mwezi Aprili.
Pia unaweza kusoma: