Watoto hawa waliambukizwa virusi kwa njia gani?

Kuna mji mdogo nchini Pakistan ambako karibu ya watoto 900 wanaishi na virusi vya HIV.

Haya yote yalianza mwezi Aprili mwaka huu, wakati daktari wa eneo hilo aliposhuku alizoziona miongoni mwa watoto ambao walikua wakipelekwa kliniki.

Alipendekeza wafanyiwe vipimo vya HIV; katika kipindi cha siku nane tu, zaidi ya watu 1000 waligundulika kuwa na HIV.

Huu ulikuwa ni mlipuko mkubwa sana wa HIV kuwahi kuikumba nchi hiyo miongoni mwa watoto wa Asia.

Cha kushangaza ni kwamba wengi miongoni mwa watoto walioathiriwa walikuwa chini ya umri wa miaka 12, ambao hawakuwa na historia ya ugonjwa huo katika familia zao.

BBC ilisafiri hadi Ratodero - ambacho ni kituo cha mlipuko huo.

Katika kituo kidogo cha afya, Dokta Uzaffar Ghangro alikuwa akimpima mtoto wa miaka saba.

Mtoto huyo alikuwa amepakatwa na baba yake- alikiwa mtulivu.

Daktari alimtaka mvulana huyo kupandisha fulana yake, ili aweke kipimo kwenye kifua chake, na kumtaka apumue polepole.

Nje ya chumba cha daktari , kulikuwa na wagonjwa zaidi ya 12 wakisubiri zamu yao, baadhi yao wakiwa ni watoto wachanga wenye umri wa wiki chache.

Daktari Ghangro alikuwa ni daktari bingwa maarufu wa waatoto katika eneo hilo- na matibabu yake yalikuwa ni nafuu sana. Lakini mambo yote yalibadilika baada ya kukamatwa kwake.

Unaweza pia kusoma:

Daktari Ghangro alikutana na BBC . Alitoka nje ya kliniki kuzungumza na BBC , huku akiwa anachechemea kidogo. Alishutumiwa kwa kuwaambukiza watoto virusi vya HIV kwa makusudi na akakamatwa kwa mauaji.

Alionekana akiwa mtulivu, na alikuwa anatabasamu , lakini alipoanza tu kuzungumzia kuhusu mlipuko huu alionekana kuwa mwenye wasiwasi na sauti yake ikaanza kupanda.

"Sijafanyakosa lolote", alidai

"Maafisa wa afya walikabiliwa na shinikizo kubwa , walihitaji kuficha ukweli wa kutowajibika kwao na wakaniwajibisha mimi ," alisema .

Wiki chache baadae, baada ya uchunguzi wa pamoja wa serikali na Shirika la Afya duniani, mashtaka dhidi ya Dokta Ghangro yalipunguzwa na kuwa uhalifu wa uzembe.

"Nimekua nikifanya kazi ya matibabu kwa miaka kumi iliyopita. Na hakuna mtu hata mmoja aliyewahi kulalamika kuwa nilitumia sindano mara mbili. Kazi yangu ilikuwa maarufu, kwa hiyo kutokana na wivu baadhi ya madaktari na waandishi walitunga hili ", aliniambia.

Daktari- ambaye binafsi anaishi na HIV - aliachiliwa huru kutoka gerezani kwa dhamana.

'Watu wanawachukia watoto wetu '

Kilomita chache kutoka katika kliniki ya Dokta Ghangro, katika kijiji cha Subhana Khan, watoto 32 wamepatikana na virusi vya HIV. Hakuna mtu katika familia yao ambaye aliyekuwa na historia ya Ukimwi.

BBC ilikutana na baadhi ya mama zao waliokua wameketi chini ya kivuli cha mti. Walionekana wamezongwa na mawazo . Watoto wao walikuwa na utapiamlo na uzito wa miili yao ulikuwa ni wa chini na walikua wanalia muda wote.

"Niliwaomba wapime uzani wa mwili wa mtoto wangu na kumpa vitamini" mama mwenye hasira aliiambia BBC.

"Waliniambia kwamba wanaweza kuniandikia dawa tu , na nitatakiwa kujinunulia mwenyewe. Lakini inagharimu mamia ya rupia na sina uwezo wa kuinunua ."

Serikali inatoa dawa za kupunguza makali ya virusi, lakini wengi hawana uwezo wa kununua dawa za kutibu maambuki mengine ambayo mara nyingi hujitokeza kutokana na HIV.

Lakini ni aibu na tisho ambalo linawasumbua wazazi katika mji wa Ratodero zaidi.

"Watu wanawachukia watoto wetu", alisema mmoja wa wakinamama.''Hata wanatubagua, wanatuambia tusiwasalimie kwa mikono na kutembelea nyumba zao, kwasababu wanahofia kuwa watapata ugonjwa. Tutafanya nini?"

Anasema kwamba watoto katika vijiji vyao hawataki kucheza na watoto walioambukia HIV, na shule zinawashauri wasihudhurie.

Mkanganyiko mkubwa.

Dokta Fatima Mir alikuwa ni Daktari wa kwanza kufika katika eneo hilo baada ya mlipuko.

" Kulikuwa na mkanganyiko mkubwa, kubainika kwa HIV ilikuwa na sawa na kifo, walihisi watoto hawa watakufa baada ya siku chache,'', anakumbuka.

Pakistan ni moja ya nchi 11 zenye kiwango kubwa cha maambukizi ya HIV, kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Mataifa iliyotolewa Julai 2019.

Na chini ya nusu ya wale wanaoishi na HIV wanafahamu kuwa wana virusi.

Visa vya ugonjwa wa ukimwi vimeongezeka karibu mara dufu tangu mwaka 2010 na kufikia 160,000, kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa.

Baada ya Ufilipino, ni nchi hiyo iliyopo Asia ambako mlipuko unaendelea kuongezeka kwa kasi kubwa, anasema Maria Elena Borromeo, Mkurugenzi wa shirika la msaada wa Ukimwi la Umoja wa Mataifa -UN Aids.

Mapambano dhidi ya HIV hayakuwa kipaumbele cha serikali, hii ikimaanisha kuwa tatizo hili halikushughulikiwa.

Lakini mlipuko wa sasa ni onyo kwa serikali, anakiri waziri wa afya wa Pakistan Azra Pechuho

Takriban madaktari 600,000 wasio na taaluma wanadhaniwa kuwa wanafanya kazi kinyume cha sheria nchini humo.

"Matibabu katika hospitali nyingi kote nchini Pakistan si ya kimaadili. Mara nyingi Madaktari hawafikirii juu ya hali bora za wagonjwa wao. Huwadunga sindano hata kama hawazihitaji, kama tiba ya haraka. Na kadri unavyopiga sindano nyingi ndivyo unavyoongeza hatari ya kusambaza maambukizi ."

Mwezi Agosti, msaidizi maalum wa waziri mkuu wa Pakistan wa masuala ya afya Zafar Mirza alisema katika ujumbe wake wa twitter kwamba Pakistan ina viwango vya juu vya matumizi ya sindano kwa mwaka duniani, na kwamba 95% ya matumizi hayo sio ya lazima.

" Ni chanzo cha usambazaji wa hali ya juu wa maambukizi kama vile Hepatitis C na HIV/UKIMWI. Tutatatua ipasavyo tatizo hili ," aliandika

Uelewa

Serikali , kwa saidizi wa mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs), pia inaendesha mipango ya kuwaelimisha watu walio katika hatari ya kupata HIV.

Lakini ngono nje ya ndoa na mapenzi ya jinsia moja ni haramu kisheria nchini Pakistan, kwa hiyo mashirika yasiyo ya kiserikali yanapaswa kuendesha shughuli zao kwa kujificha na hawawezi kuwafikia watu wengi kubwa ya watu.

Mkundi yaliyoambukizwa yanahisi kutokuwa na usalama kutokana na unyanyapaa unaoambatana na ugonjwa wa Ukimwi, Bi Borromeo anasema wengi wa watu katika eneo hilo hawatafuti matibabu kutokana na hofu ya 'kubainika' kuwa maambukizi ya HIV.

Lakini Dokta Mir anatumai kwamba vijana waathiriwa wa Ratodero watasaidia kumaliza unyanyapaa.

"Kunyamaza juu ya mambo hakukufanyi uondokane nayo. Yanarudi na kuwa mazito zaidi," anasema.

"Ni muhimu kutatua mlipuko huu kwa njia inayofaa na kuchukua hatu sasa hivi. Vinginevyo, mlipuko ujao utakuwa ni hata mkubwa zaidi na labda usioweza kudhibitiwa."