Ujumbe wa Khamenei kwa mataifa ya Ghuba: Tunachofahamu kuhusu afya yake

Chanzo cha picha, EPA/Shutterstock
Kiongozi Mkuu wa Iran, Mojtaba Khamenei, ametoa wito kwa viongozi wa nchi za Kiislamu, hasa zile za Mashariki ya Kati na eneo la Ghuba, kuungana dhidi ya Marekani na Israel, katika ujumbe uliochapishwa na shirika rasmi la habari la Iran, IRNA.
Ujumbe huo umetolewa miezi sita baada ya mashambulizi ya Marekani na Israel kusababisha kifo cha baba yake, aliyekuwa Kiongozi Mkuu Ali Khamenei, na kumjeruhi vibaya Mojtaba, kulingana na vyanzo vya karibu na mzunguko wake wa ndani vilivyozungumza na shirika la habari la Reuters.
Katika ujumbe uliotolewa wakati wa Wiki ya Umoja wa Kiislamu, Khamenei alisema kuwa viongozi wa nchi za eneo hilo lazima "wamtambue adui halisi, waelewe mipango yake na kuikabili," akiashiria Marekani na Israel, kwa mujibu wa IRNA.
Aliongeza kuwa Washington na Israel si maadui wa Jamhuri ya Kiislamu na "mhimili wa upinzani" pekee, bali pia wa nchi zote za Kiislamu katika eneo la Asia Magharibi na Afrika Kaskazini, hata zile zinazoshirikiana nao.
Huu ni ujumbe wa pili alioutoa katika siku za hivi karibuni kusisitiza mshikamano wa ndani, huku akionya, katika ujumbe uliochapishwa tarehe 28 Agosti,dhidi ya kauli zinazoweza kusababisha mgawanyiko katika jamii, kulingana na vyombo rasmi vya habari vya Iran.
Hata hivyo, kauli zote zinazohusishwa na Khamenei tangu aingie madarakani zimetolewa kwa njia ya maandishi. Hajajitokeza hadharani, na mamlaka za Iran hazijatoa picha, rekodi za sauti, wala video zozote zake tangu alipoteuliwa kuwa Kiongozi Mkuu, jambo linalozua maswali kuhusu afya yake na kiwango cha udhibiti wake halisi juu ya masuala ya nchi.
Je, mtazamo kuelekea nchi za Ghuba umebadilika?
Ujumbe wa Khamenei ulitolewa baada ya miezi kadhaa ya mvutano mkali kati ya Iran na mataifa ya Ghuba, kufuatia hatua ya Tehran kushambulia kambi za kijeshi za Marekani na maeneo mengine katika nchi za eneo hilo wakati wa vita.
Kabla ya kuzuka kwa vita, Saudi Arabia, Qatar, na Oman zilikuwa zikijaribu kuishawishi Washington isishambulie Iran. Mrithi wa Ufalme wa Saudi Arabia, Mohammed bin Salman, pia alimhakikishia Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, kuwa nchi yake haitaruhusu ardhi au anga yake kutumika katika hatua yoyote ya kijeshi dhidi ya Tehran, kulingana na shirika la habari la Reuters.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Hata hivyo, Iran ilijibu mashambulizi ya Marekani na Israel kwa kufyatua makombora na ndege zisizo na rubani (droni) yaliyolenga mataifa sita wanachama wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba, kulingana na uchunguzi wa Reuters.
Mashambulizi hayo hayakukomea kwenye kambi za Marekani pekee, bali pia yaliyalenga viwanja vya ndege, miundombinu ya mafuta na maeneo ya kiraia.
Vikwazo vilivyowekwa na Iran pia vimesababisha kupungua kwa kasi kwa shughuli za usafirishaji wa meli katika Lango la Bahari la Hormuz, jambo lililosababisha usumbufu katika usafirishaji wa nishati na biashara katika eneo hilo.
Mashambulizi hayo yaliibua hasira kubwa katika eneo la Ghuba. Waziri mkuu wa Qatar alielezea vitendo vya Iran kama "uhaini," akisema vilikuja licha ya hakikisho la mataifa ya Ghuba la kutoegemea upande wowote. Waziri wa mambo ya nje wa Saudia alisema imani yao kwa Tehran "imevunjwa" na kwamba nchi yake ina haki ya kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya Iran.
Mvutano uliongezeka tena mwezi Agosti wakati Iran ilipoonya kwamba itashambulia vituo vya nishati vya nchi za Ghuba ikiwa Marekani itaanzisha mashambulizi mapyadhidi yake.
Baada ya kugundua makombora mawili ambayo Abu Dhabi ilisema yalirushwa kutoka Iran, Umoja wa Falme za Kiarabu UAE, ilisitisha shughuli zote za kibiashara na Tehran hadi itakapotangazwa tena.
Hata hivyo, njia za mawasiliano hazikukatizwa, baada ya Oman na Qatar kuendeleza juhudi zao za upatanishi kati ya Iran na Marekani, hasa katika mazungumzo yaliyolenga kumaliza vita na kufungua tena Mlango-bahari wa Hormuz.
Tofauti na vitisho vya awali vya Iran, ujumbe wa Khamenei ulikuwa na sauti iliyoelekea zaidi kuzihutubia nchi za Ghuba kwa lugha ya ushirikiano, huku akiwataka viongozi wake kusimama pamoja na Tehran dhidi ya Marekani na Israel.
Hata hivyo, ujumbe huo haukugusia mashambulizi ya Iran dhidi ya nchi za Ghuba, wala haukuwa na mpango wowote wa kivitendo wa kurekebisha uhusiano, na ulikuwa na shutuma zisizo za moja kwa moja kuhusu kuendelea kwa ushirikiano wa baadhi ya nchi za eneo hilo na Washington.
Je, Mojtaba Khamenei alikuwaje Kiongozi Mkuu?
Mojtaba Khamenei alichukua uongozi wa Iran baada ya baba yake kuuawa katika mashambulizi ya Marekani na Israel yaliyoanza tarehe 28 Februari.
Mojtaba alijeruhiwa katika mashambulizi hayo hayo. Watu watatu walio karibu naye waliambia shirika la habari la Reuters kuwa alipata majeraha usoni na miguuni, na kwamba uso wake uliharibika vibaya, ingawa shirika hilo lilisema halikuweza kuthibitisha taarifa hiyo kwa njia huru.
Mamlaka za Iran hazijatoa taarifa yoyote inayofafanua hali ya majeraha yake.
Mojtaba Khamenei alichaguliwa kuwa Kiongozi Mkuu tarehe 8 Machi, siku nane baada ya vita kuanza, wakati ambapo Iran ilikuwa ikikabiliwa na mojawapo ya migogoro mikubwa zaidi ya kisiasa na kijeshi tangu mapinduzi ya mwaka 1979.
Kabla ya vita, Mojtaba alifanya kazi kwa siri kama msaidizi mkuu wa baba yake, na mara chache sana alionekana hadharani.
Hata hivyo, kutokuwepo kwake kabisa machoni pa umma tangu ashike wadhifa wa juu kabisa nchini humo kumezua utata unaozidi kuongezeka, ikizingatiwa kuwa Kiongozi Mkuu ndiye mwenye kauli ya mwisho katika masuala muhimu ya kisiasa na kijeshi.
Kwa nini bado hajaonekana hadharani?
Maafisa wa Iran wanahusisha kutokuwepo kwa Khamenei na kuendelea kupona kwake kutokana na majeraha, pamoja na hofu kwamba Marekani au Israel zinaweza kujaribu kumshambulia tena.
Afisa mmoja mwandamizi wa Iran aliliambia shirika la habari la Reuters kuwa ni idadi ndogo tu ya maafisa wanaowasiliana naye moja kwa moja, na kwamba mamlaka hazitoi taarifa zozote kumhusu kwa kuhofia kuvuja kwa habari ambazo zingeweza kuisaidia Marekani kumtambua alipo.
Shirika hilo lilimnukuu mtu wa karibu naye akisema kuwa afya yake inaendelea kuimarika kwa kiasi kikubwa, na kwamba bado yuko makini na anashiriki katika kufanya maamuzi.
Hata hivyo, mamlaka hazijatoa taarifa yoyote ya umma kuhusu hali yake ya kiafya. Pia hazijachapisha picha, rekodi za sauti, au video zozote za hivi karibuni zinazomwonyesha tangu kuteuliwa kwake, kulingana na mashirika ya AFP na Reuters.
Khamenei pia hakuwepo kwenye mazishi ya baba yake na aliwasiliana na wananchi wa Iran kupitia taarifa za maandishi zilizosomwa kwenye vyombo rasmi vya habari pekee, kulingana na Reuters.
Je, ni kweli anaitawala Iran?
Maafisa na vyanzo kadhaa vya Iran viliiambia Reuters kuwa Khamenei ndiye mwenye kauli ya mwisho katika masuala muhimu, na kwamba hufanya mikutano ya mara kwa mara na maafisa wa ngazi ya juu pamoja na kupokea taarifa kuhusu vita, uchumi, na sera za kigeni.
Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, alisema mnamo Agosti 10 kuwa alifanya mkutano wa saa saba na Khamenei, kulingana na shirika la habari la Reuters.
Shirika hilo lilimnukuu afisa wa Iran akisema kuwa kuendelea kufanya kazi kwa taasisi za serikali na umoja wa misimamo yao kuhusu sera za kigeni kunaashiria kuwa Kiongozi Mkuu bado anaiongoza nchi hiyo.
Hata hivyo, hakuna ushahidi huru wa hadharani unaothibitisha namna Khamenei anavyoshiriki katika mikutano hiyo au kiwango cha dhima yake katika kufanya maamuzi.
Kutokuonekana kwake hadharani kumechochea uvumi miongoni mwa Wairani, wakiwemo baadhi ya wafuasi wa utawala huo. Reuters ilimnukuu mwanachama wa kikosi cha wanamgambo wa Basij akisema kuwa kusikia sauti ya Kiongozi Mkuu au kuona uthibitisho wa kuwepo kwake kungeliimarisha imani kwa uongozi wa nchi.
Pia ilimnukuu mfanyabiashara wa Iran anayeunga mkono mageuzi akihoji taarifa rasmi na kusema kuwa hakuna ushahidi unaoonyesha kuwa Khamenei bado yu hai au anashiriki katika kufanya maamuzi.
Iran inaendeshwa vipi wakati kiongozi wake haonekani hadharani?
Shirika la habari la Reuters, likinukuu vyanzo vya Iran, linasema kuwa Khamenei amekabidhi mamlaka mapana ya kusimamia shughuli za kila siku kwa kundi la maafisa wa ngazi ya juu, huku akibaki na mamlaka ya mwisho katika maamuzi ya kimkakati, kulingana na vyanzo hivyo.
Kwa mujibu wa vyanzo vilivyozungumza na shirika hilo, kundi la viongozi wakuu wanaoendesha nchi linajumuisha viongozi wa ngazi ya juu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi (Revolutionary Guard), pamoja na Rais Masoud Pezeshkian, Spika wa Bunge Mohammad Baqer Qalibaf, na maafisa wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa.
Reuters inasema kuwa ushawishi wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi umeongezeka tangu kuzuka kwa vita, na kwamba limekuwa na ushiriki mkubwa zaidi katika mchakato wa kufanya maamuzi ndani ya mfumo wa serikali, ambao umepangwa upya ili kuzunguka Baraza Kuu la Usalama wa Taifa.
Hali hii inaendana na makadirio yaliyochapishwa na vituo vya utafiti, ikiwemo Carnegie Endowment for International Peace na Gulf International Forum, ambayo ilionyesha kuwa utawala wa nchi hiyo umekuwa wa mshikamano zaidi, huku Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi likiwa na ushawishi unaoongezeka katika maamuzi ya kimkakati.
Katika makala ya uchambuzi iliyochapishwa na Taasisi ya Carnegie, mtafiti Mohammad Ayatollahi Tabar aliandika kuwa uongozi nchini Iran hauwezi kuhusishwa na mtu mmoja au kundi dogo tu, na kwamba maamuzi hutolewa na mtandao mpana wa taasisi na viongozi; baadhi ya maamuzi hayo yakionyesha makubaliano kati ya Kiongozi Mkuu na makamanda wa ngazi ya juu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi.
Alex Vatanka, kutoka Taasisi ya Mashariki ya Kati (Middle East Institute) mjini Washington, anaamini kuwa kutokuwepo kwa muda mrefu kwa Khamenei kunaweza kuruhusu vituo vya madaraka vinavyoshindana ndani ya utawala huo kudai kuwa misimamo yao inaakisi matakwa ya Kiongozi Mkuu.
Je, anakabiliwa na changamoto zipi?
Ujumbe wa Khamenei unakuja wakati ambapo Iran inakabiliwa na madhara ya miezi sita ya vita, vikwazo vya Marekani, na vizuizi dhidi ya mauzo yake ya mafuta.
Katika kipindi hiki, mfumo wa kisiasa uliendelea kudumisha mshikamano wake licha ya kuuawa kwa aliyekuwa Kiongozi Mkuu na makamanda kadhaa wa ngazi ya juu.
Iran bado ina uwezo wa kuvuruga usambazaji wa nishati na kushambulia maeneo ya Marekani pamoja na yale ya washirika wa Washington katika eneo hilo.
Hata hivyo, uchumi wa Iran unakabiliwa na shinikizo kubwa kutokana na gharama za vita, vikwazo, na kupungua kwa mauzo ya mafuta; hali ambayo imesababisha kushuka kwa thamani ya sarafu na kuongezeka kwa hofu ya kurejea kwa maandamano ya ndani.
Kwa mujibu wa vyanzo vilivyozungumza na shirika la habari la Reuters, uongozi wa Iran umepanga upya vipaumbele vyake kwa kuzingatia kulinda utawala, kurejesha uwezo wake wa kuzuia mashambulizi ya adui, na kuzuia madhara ya kiuchumi kusababisha kuyumba kwa nchi.
Fatanka alisema kuwa kufikia makubaliano ya kweli na Washington, au kuamua kuendeleza vita vya muda mrefu na vya gharama kubwa, kunahitaji idhini ya wazi na isiyo na shaka kutoka kwa Khamenei.
Imetafsiriwa na Ambia Hirsi












