Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Samora Machel: Miaka 40 tangu kifo chake bado Afrika yamlilia
- Author, Florian Kaijage
- Nafasi, BBC Swahili
- Akiripoti kutoka, Dar es Salaam
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 4
Leo Oktoba 19, 2026 imetimia miaka 40 tangu Rais wa kwanza wa Msumbiji, Samora Machel alipofariki dunia mwaka 1986 katika ajali ya ndege iliyotokea katika Milima ya Lebombo Jirani na kijiji cha Mbuzini, nchini Afrika Kusini.
Ndege ya rais Machel aina ya Tupolev Tu-134 ilitumbukia na kuanguka ndani ya ardhi ya Afrika Kusini, jirani sana na mipaka ya Msumbiji na Eswatini ya sasa-Zamani Swaziland, ikitokea katika mkutano wa viongozi wa Afrika nchini Zambia.
Kati ya watu 44 waliokuwemo kwenye ndege hiyo, watu 33 walipoteza maisha akiwemo Rais Machel aliyekuwa na umri wa mika 53, na wajumbe wa msafara wake, marubani, na waandishi wa habari, huku 10 pekee wakinusurika.
Ripoti rasmi za awali za mahakama nchini Afrika Kusini mnamo 1987 zilipeleka kwa marubani kuwa lilikuwa kosa la kibinadamu. Lakini kulikuwa na madai na dhana kubwa kuwa serikali ya sera ya ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini ilihusika kwa kutumia mfumo wa mawimbi bandia ya redio (false beacon) kuipotosha ndege hiyo njia.
Serikali na mamlaka mbalimbali zimeendelea kupitia upya au kufungua upya uchunguzi wa tukio hilo baada ya kuibuka kwa ushahidi mpya unaodai uingiliaji wa vyombo vya usalama vya wakati huo, kufuatia taarifa kama zile zilizoripotiwa.
Eneo la ajali huko Mbuzini Afrika Kusini limejengwa mnara na makumbusho Samora Samora Machel kwa ajili ya kuadhimisha kumbukumbu ya shujaa huyo na wenzake na kuhimiza mshikamano wa kitaifa.
Mwalimu Julius Nyerere ambaye alikuwa mwenyekiti wa nchi zilizo mstari wa mbele katika ukombozi wa kusini mwa Afrika hakuamini kabisa kuwa ajali hiyo ilikuwa ya kawaida. Katika kauli zake, aliuhtumu waziwazi utawala wa kibaguzi wa rangi wa Afrika Kusini kwa kuhusika na kifo cha Samora Machel. Nyerere alieleza kuwa Samora alikuwa tishio kubwa kwa utawala wa makaburu kutokana na msimamo wake thabiti wa kuwasaidia wapigania uhuru wa ANC ya Afrika Kusini) na ZANU PF ya Zimbabwe.
Samora Machel ni nani?
Samora Moisés Machel alikuwa mwanamapinduzi, mpigania uhuru na mwanasiasa wa Msumbiji aliyeliongoza taifa hilo kupata uhuru kutoka kwa utawala wa kikoloni wa Ureno na kuwa rais wake wa kwanza baada ya uhuru mwaka 1975. Hadi wa leo, anakumbukwa kama mmoja wa viongozi mashuhuri zaidi wa harakati za ukombozi barani Afrika.
Kutoka muuguzi hadi mpigania uhuru
Machel alizaliwa tarehe 29 Septemba 1933 katika Mkoa wa Gaza, uliokuwa sehemu ya Msumbiji iliyotawaliwa na Ureno. Baada ya kupata elimu yake ya awali, alifanya kazi ya uuguzi, ambako alishuhudia ubaguzi wa rangi na hali ngumu zilizowakabili Waafrika chini ya utawala wa kikoloni. Uzoefu huo ulimhamasisha kujiunga na harakati za kupigania uhuru.
Katika miaka ya 1960, alijiunga na FRELIMO (Front for the Liberation of Mozambique), vuguvugu lililoongoza mapambano dhidi ya utawala wa Kireno. Baada ya kuuawa kwa kiongozi wa FRELIMO, Eduardo Mondlane, mwaka 1969, Machel alichukua uongozi wa harakati hizo na kuimarisha mapambano ya ukombozi.
Rais wa kwanza wa Msumbiji huru
Baada ya Msumbiji kupata uhuru tarehe 25 Juni 1975, Machel aliapishwa kuwa rais wa kwanza wa taifa hilo.
Akiwa madarakani, alitekeleza sera za ujamaa, akapanua huduma za afya na elimu, na kuhimiza umoja wa kitaifa. Aliamini kuwa maendeleo ya taifa yalihitaji wananchi kujiona kwanza kama Wamsumbiji badala ya kutanguliza tofauti za kikabila au kikanda.
Mchango katika ukombozi wa Kusini mwa Afrika
Mbali na kuiongoza Msumbiji, Machel aliunga mkono harakati za ukombozi katika nchi nyingine za Kusini mwa Afrika, ikiwemo Zimbabwe na Afrika Kusini wakati wa mapambano dhidi ya utawala wa kibaguzi wa makaburu. Serikali yake ilitoa msaada kwa wanaharakati wa kupinga ubaguzi wa rangi, jambo lililoifanya Msumbiji kuwa moja ya mataifa muhimu katika mapambano ya ukombozi wa kanda hiyo.
Kauli mbiu yake maarufu,"A Luta Continua" yenye maana ya"Mapambano yanaendelea", iligeuka kuwa nembo ya harakati nyingi za ukombozi barani Afrika. Kwa Machel, kupata uhuru wa kisiasa hakukumaanisha mwisho wa mapambano, bali mwanzo wa juhudi za kuleta haki za kijamii, elimu, afya na maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi.
Kifo cha kutatanisha
Tarehe 19 Oktoba 1986, Machel alifariki dunia katika ajali ya ndege karibu na eneo la Mbuzini nchini Afrika Kusini alipokuwa akirejea kutoka mkutano wa viongozi wa nchi za ukanda huo uliofanyika Zambia. Ajali hiyo iliua watu 35, akiwemo Machel mwenyewe.
Hata hivyo, mazingira ya ajali hiyo yameendelea kuzua maswali kwa miaka mingi, huku baadhi ya watu wakihusisha utawala wa kibaguzi wa Afrika Kusini wa wakati huo na tukio hilo, madai ambayo hayajawahi kuthibitishwa rasmi.
Urithi wake
Leo, Samora Machel anatambuliwa kama:
- Baba wa uhuru wa Msumbiji.
- Mmoja wa viongozi wakuu wa harakati za ukombozi Kusini mwa Afrika.
- Mtetezi wa umoja wa Afrika na mshikamano wa Waafrika.
- Kiongozi aliyesisitiza kuwa uhuru wa kisiasa unapaswa kuambatana na maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Zaidi ya miongo minne baada ya kifo chake, Samora Machel bado anaheshimiwa katika Msumbiji na sehemu mbalimbali za Afrika kama mmoja wa viongozi waliotoa mchango mkubwa katika mapambano ya ukombozi wa bara hilo.