Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Je, Manchester City wana nafasi yoyote ya kushinda rufaa yao?
- Author, Dale Johnson
- Nafasi, Football issues correspondent
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Manchester City inakabiliwa na "vikwazo vikubwa" ikiwa inataka kuwa na nafasi yoyote ya kushinda rufaa yake baada ya kupatikana na hatia ya kukiuka kanuni za kifedha za Ligi Kuu ya England (Premier League), mwanasheria mashuhuri ameiambia BBC Sport.
City imepatikana na hatia ya makosa yote yanayohusiana na ukiukaji wa kanuni za kifedha za Premier League kati ya misimu ya 2009-10 na 2017-18, pamoja na kuunda "mikataba ya kujifanya" ili kuongeza thamani ya mikataba ya udhamini kwa pauni milioni 830.
Klabu hiyo imesema haina hatia dhidi ya tuhuma zilizotolewa na Premier League na ina "ushahidi usiopingika" kwamba uamuzi huo "una makosa ya wazi ya msingi katika sheria, kanuni na ukweli, na hivyo hauwezi kuaminika".
Katika rufaa yao, City itadai kwamba malipo hayo yalifanywa na serikali ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) kama mwanahisa wa kampuni zilizodhamini klabu hiyo, huku kukiwa na kutokuwiana katika uamuzi wa Tume.
Kwa hiyo, City inasema kiasi cha fedha kilichotolewa kupitia mikataba ya udhamini kilikuwa halali na hakikuongezewa fedha na wamiliki wa klabu.
James Severn, mwanachama wa Chama cha Wanasheria wa Madai cha London (LSLA) na mshirika katika kampuni ya uwakili ya Penningtons Manches Cooper, aliiambia BBC Sport kwamba rufaa hiyo "si fursa tu ya kuomba jopo jipya libadilishe uamuzi uliotolewa".
"City itahitaji kubainisha kosa la msingi katika sheria, kanuni au ukweli, au ukiukaji mkubwa wa taratibu za haki, ambao uliathiri kwa kiasi kikubwa uamuzi wa Tume," Severn alisema.
"Pamoja na hayo, Bodi ya Rufaa ina mamlaka mapana ya kuruhusu au kutupilia mbali rufaa, kubadilisha uamuzi au kutoa amri nyingine yoyote itakayoona inafaa."
City lazima ithibitishe kuwa ushahidi uliopo ulitafsiriwa vibaya
Etihad Airways, mmoja wa wadhamini wakuu wa City na kiini cha kesi hiyo, ilikuwa imesema awali kwamba serikali ya Abu Dhabi haikulipia udhamini wake wa Manchester City.
Kauli hiyo ilijitokeza katika nyaraka za mahakama zilizowasilishwa kama sehemu ya uchunguzi uliofanywa nchini Marekani, mjini New York, mwaka 2015.
City itadai kwamba kauli hiyo haikuzingatia muktadha mzima wa hali hiyo na haithibitishi kwamba klabu ilitoa ushahidi unaokinzana.
Klabu hiyo inasisitiza kwamba nyaraka za serikali zinaunga mkono kikamilifu hoja yake. Hata hivyo, Severn alisema kwamba ikiwa nyaraka hizo zilikuwa tayari zimewasilishwa kwa Tume, huenda zisiwe na manufaa makubwa katika rufaa.
"Taarifa za benki, kumbukumbu za serikali na nyaraka za malipo zilizotayarishwa wakati wa matukio husika zinaweza kuwa ushahidi wenye nguvu ikiwa zitathibitisha kwa uwazi mnyororo wa miamala unaoonyesha kwamba fedha zinazozua mzozo zilitoka kwa serikali ya Abu Dhabi badala ya wamiliki wa klabu," Severn aliongeza.
"Hata hivyo, ikiwa ushahidi huo ulikuwa tayari umewasilishwa mbele ya Tume, ambayo licha ya ushahidi huo ilihitimisha kwamba mipango hiyo ilikuwa ya kujifanya, City itakabiliwa na changamoto kubwa kuthibitisha kwamba uamuzi huo ulikuwa na kosa la msingi."
Muda mfupi kabla ya kuthibitishwa kwa rufaa ya City, Etihad Airways ilitoa taarifa ikisema kwamba haikuwahi kupewa "fursa na Premier League ya kuwakilishwa, kutoa taarifa muhimu au kuhakikisha usahihi na haki ya taarifa zilizotumiwa".
Severn alisema malalamiko ya Etihad Airways "hayathibitishi yenyewe kwamba kulikuwa na ukiukaji wa taratibu za haki".
"Etihad haikuwa upande unaotuhumiwa katika kesi hiyo na kuna uwezekano haikuwa na haki huru ya kushiriki katika mashauri hayo," Severn alisema. "Inaonekana kila upande ulikuwa na fursa ya kupata na kuwasilisha ushahidi huo kwa Tume.
"Ikiwa Bodi ya Rufaa itakubali kuzingatia ushahidi mpya kutoka Etihad, ushahidi huo huenda ukapewa uzito mkubwa zaidi ikiwa utaungwa mkono na nyaraka zilizotayarishwa wakati wa matukio husika."
City inaweza kudai kulikuwa na 'kosa la msingi la ukweli'
Sehemu muhimu ya utetezi wa City itakuwa hoja kwamba Tume Huru ilitegemea kupita kiasi barua pepe zilizopatikana kupitia nyaraka zilizovuja za Football Leaks.
"Ikiwa City itaweza kuthibitisha kwamba Tume ilielewa vibaya barua pepe hizo kwa kiwango kikubwa, ilishindwa kuzingatia muktadha wake sahihi au ilifikia hitimisho linalokinzana na nyaraka nyingine zilizotayarishwa wakati wa matukio husika, hilo linaweza kuchukuliwa kuwa kosa la msingi la ukweli," Severn aliongeza.
"Changamoto ya City ni kwamba Tume ilisikiliza ushahidi mwingi kutoka kwa mashahidi na kupitia nyaraka mbalimbali, lakini bado ilifikia hitimisho zito kwamba kulikuwa na mipango ya udanganyifu na ufadhili wa wamiliki uliofichwa."
Kieran Maguire, profesa wa masuala ya fedha katika soka katika Chuo Kikuu cha Liverpool, aliiambia BBC Sport kwamba Tume ilihitimisha kuwa "nyaraka zilibadilishwa na kurekebishwa ili ziendane na kosa lililodaiwa kufanyika".
"Tume lazima iwe ilihitimisha kwamba ushahidi na uaminifu wa mashahidi waliowasilishwa na Manchester City vilikuwa dhaifu," Maguire alisema.
"Hata hivyo, kwa mtazamo wa kisheria, hili ni eneo ambalo wanaweza kupinga ikiwa timu ya wanasheria ya Manchester City itaweza kuthibitisha kwamba muundo wa Tume wenyewe ulikuwa na dosari, kwa maana kwamba wajumbe wake waliteuliwa na Premier League badala ya Manchester City, na hivyo klabu ilikuwa katika mazingira yasiyo ya haki tangu mwanzo.
"Lakini uwezekano huo unaonekana kuwa mdogo."
Severn aliongeza kwamba majaji wakuu wastaafu na mawakili mashuhuri walioketi katika Tume hiyo wametumia maisha yao ya kikazi kutafsiri ukweli tata, kushughulikia ushahidi wa mashahidi na kutathmini uzito unaopaswa kupewa ushahidi mbalimbali.
Ingawa alisema kuwa "haiwezekani kutathmini kwa uhakika" nafasi za City kushinda rufaa yake, Severn aliongeza kwamba "haitakuwa rahisi".
Hata hivyo, Maguire anaamini kwamba licha ya ugumu wa kushinda rufaa hiyo, "bado kuna njia ya kufanikiwa".
City imeajiri Mark Howard KC kuishauri klabu hiyo katika rufaa yake, huku Etihad Airways ikiajiri kampuni mashuhuri ya uwakili ya Quinn Emanuel.
Maguire alisema: "Kwa kuzingatia mawakili walioajiriwa na Manchester City, huenda wakaamua kutumia mbinu ambayo nimeelezwa kuwa ni ya kuibua mkanganyiko na kelele nyingi.
"Hii ina maana ya kujaribu kutilia shaka kila kitu kinachohusiana na mchakato wa Tume, badala ya kupinga moja kwa moja ushahidi uliowasilishwa.
"Nimeziona nyaraka ambazo Abu Dhabi iliwasilisha katika kesi ya New York. Mimi si mwanasheria, lakini kwa mtazamo wa uhasibu, nyaraka hizo zinaweza kutafsiriwa kwa namna zaidi ya moja."
Ingawa kanuni za Premier League zinasema kwamba rufaa lazima isikilizwe ndani ya wiki 12, au ifikapo mkesha wa Krismasi, Severn aliongeza kwamba "kwa kuzingatia ukubwa na ugumu wa mashauri haya, huenda ikachukua muda kabla ya uamuzi wa mwisho kujulikana".