Mgawanyiko mkubwa wa kisiasa waikabili Israel kabla ya uchaguzi muhimu

Chanzo cha picha, Reuters
Israel inajiandaa kwa uchaguzi mkuu unaotarajiwa kuamua mustakabali wa kisiasa wa Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu, huku nchi hiyo ikiwa imegawanyika kuhusu usalama, uchumi, uongozi na mwelekeo wa taifa baada ya miaka ya vita katika eneo la Mashariki ya Kati.
Uchaguzi huo unafanyika baada ya karibu miaka mitatu ya vita vilivyoathiri Gaza na maeneo mengine ya Mashariki ya Kati, huku kukiwa na maswali kuhusu namna serikali ilivyoshughulikia mashambulizi ya Oktoba 7, 2023, na matokeo ya operesheni zake za kijeshi.
Kura za maoni zinaashiria ushindani mkali kati ya muungano unaoongozwa na Netanyahu na kambi ya upinzani, ambayo inajaribu kumwondoa madarakani baada ya miaka kadhaa ya utawala wake.
Miongoni mwa wapinzani wake wakuu ni Gadi Eisenkot, aliyekuwa mkuu wa majeshi ya Israel na ambaye sasa anaongoza chama cha mrengo wa kati cha Yashar. Katika baadhi ya kura za maoni za hivi karibuni, chama chake kimeonyesha ushindani mkubwa dhidi ya Likud ya Netanyahu.
Hata hivyo, mfumo wa kisiasa wa Israel unategemea vyama kujenga miungano ili kupata wingi wa viti bungeni na kuunda serikali. Hivyo, hata kama chama kimoja kitaibuka na viti vingi kuliko vingine, huenda kikahitaji washirika kadhaa ili kupata wingi unaohitajika wa kuunda serikali.
Usalama, uchumi na utambulisho wa Israel
Kwa wapiga kura wengi, uchaguzi huu si tu kuhusu nani atakuwa waziri mkuu, bali pia kuhusu mwelekeo wa nchi baada ya mashambulizi ya Oktoba 7 na vita vilivyofuata.
Eisenkot amesema uchaguzi huo utahusu masuala ya usalama, uchumi, elimu na utambulisho wa Israel. Anataka nchi hiyo iwe ya Kiyahudi na kidemokrasia, huku ikilinda misingi ya uhuru, uvumilivu na usawa.
Wafuasi wa upinzani wanakosoa serikali ya Netanyahu kwa kile wanachokitaja kuwa kushindwa kuunganisha taifa na kwa juhudi zake za kufanya mabadiliko katika mfumo wa mahakama. Pia wanataka kuundwa kwa tume huru ya uchunguzi kuhusu namna mashambulizi ya Oktoba 7 yalivyoweza kutokea licha ya Israel kuwa na mifumo mikubwa ya kiusalama.
Netanyahu amepinga wito wa kuundwa kwa tume hiyo kwa hoja kwamba mfumo wa mahakama hauko huru kutokana na kile anachodai kuwa upendeleo dhidi yake. Hata hivyo, suala la uwajibikaji limeendelea kuwa miongoni mwa mambo yanayowagawa wapiga kura.
Kwa upande wake, Netanyahu anasisitiza kuwa serikali yake imepunguza vitisho dhidi ya Israel kupitia operesheni za kijeshi dhidi ya Hamas huko Gaza na makundi mengine katika eneo hilo, pamoja na hatua dhidi ya Iran.
Kauli mbiu yake ya kampeni, "No Surrender" — yaani, kutosalimisha msimamo — inaakisi ujumbe wake kwamba Israel inahitaji uongozi thabiti wa kiusalama. Amewashutumu wapinzani wake kwa kuwa dhaifu katika masuala ya usalama na ameibua hofu kuhusu uwezekano wa baadhi ya vyama vya Kiyahudi kuunda miungano na vyama vya Waarabu.
Hata hivyo, wapinzani wake wanasema usalama wa muda mrefu hauwezi kutegemea nguvu za kijeshi pekee, na kwamba nchi inahitaji pia uongozi unaoweza kushughulikia mgawanyiko wa ndani na kujenga dira ya kisiasa kwa siku zijazo.
Vita vimebadili mitazamo ya baadhi ya wapiga kura

Chanzo cha picha, Getty Images
Mashambulizi ya Oktoba 7, 2023, yaliyofanywa na Hamas kusini mwa Israel, yaliua karibu watu 1,200 na kusababisha wengine 251 kutekwa na kupelekwa Gaza.
Tangu wakati huo, vita na operesheni za kijeshi zimeathiri kwa kina jamii ya Israel. Ingawa baadhi ya wananchi wanamlaumu Netanyahu kwa kushindwa kuzuia mashambulizi hayo, wengine wanasema hatua kali za kijeshi ndizo njia pekee ya kuzuia mashambulizi mengine.
Baadhi ya wapiga kura wameelekea zaidi upande wa mrengo wa kulia kutokana na hofu ya usalama. Eyal Hajbi, mkazi wa Sderot, ni miongoni mwa wanaosema wanataka hatua kali zaidi dhidi ya maadui wa Israel. Anasema amebadilisha msimamo wake wa kisiasa na sasa anaunga mkono chama cha mrengo mkali wa kulia cha Jewish Power.
Mwelekeo huo unaonekana pia miongoni mwa baadhi ya vijana wanaopiga kura kwa mara ya kwanza, ambapo kura za maoni zimeonyesha uungwaji mkono kwa vyama vya mrengo mkali wa kulia.
Hata hivyo, maoni kuhusu vita hayafanani katika jamii nzima. Wengine wanahoji kuwa operesheni za kijeshi hazijatatua changamoto za usalama na badala yake zimesababisha vifo vingi vya raia wa Palestina na kuongeza gharama za kiuchumi na kijamii.
Kwa mujibu wa Wizara ya Afya inayoendeshwa na Hamas huko Gaza, zaidi ya Wapalestina 74,000 wameuawa tangu vita vilipoanza. Takwimu hizo zimetumiwa na Umoja wa Mataifa na mashirika mengine katika kufuatilia athari za vita.
Katika kijiji cha Nir Oz, ambacho kilishambuliwa na Hamas Oktoba 7, wakazi wanajaribu kujenga upya maisha yao baada ya watu 47 kuuawa na wengine 76 kutekwa katika shambulizi hilo.
Baadhi ya wakazi wanataka mabadiliko ya uongozi, wakisema taifa linahitaji zaidi ya mikakati ya kijeshi. Galia, mmoja wa wakazi hao, anaunga mkono Eisenkot kwa matumaini kwamba anaweza kuleta mwelekeo tofauti.
Mwanaye Gal bado anafikiria ni mgombea gani wa kumuunga mkono, lakini anasema matatizo yanayokabili Israel hayahusu usalama pekee. Uchumi, elimu, afya na changamoto za kijamii pia zinahitaji kushughulikiwa.
Je, upinzani una mpango tofauti kuhusu Wapalestina?

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Licha ya tofauti zao na Netanyahu, viongozi kadhaa wa upinzani hawajaonyesha msimamo ulio wazi wa kuunga mkono kuanzishwa kwa taifa huru la Palestina.
Eisenkot amesema anapendelea aina fulani ya kujitawala kwa Wapalestina, au mfumo unaofanana na taifa lenye mamlaka yaliyopunguzwa, huku Israel ikiendelea kudhibiti masuala muhimu ya usalama.
Baadhi ya vyama vikuu vya upinzani pia vinaunga mkono kwa namna tofauti kuendelezwa kwa makazi ya Israel katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu. Makazi hayo yanachukuliwa kuwa kinyume cha sheria za kimataifa.
Hivyo, kuondoka kwa Netanyahu madarakani hakumaanishi moja kwa moja kuwa sera za Israel kuhusu Wapalestina zitabadilika kwa kiasi kikubwa.
Eisenkot amesema anataka kumaliza utawala wa Hamas huko Gaza ndani ya miezi 18, kupitia mpango wa amani unaoongozwa na Marekani au kwa kutumia nguvu za kijeshi.
Kwa upande mwingine, Netanyahu anaendelea kuonya kuhusu vitisho kutoka Iran na washirika wake, huku wanaharakati wakionya pia kuhusu uwezekano wa kuongezeka kwa ghasia za walowezi wa Israel dhidi ya Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi.
Mgogoro wa kujiunga na jeshi waongeza mgawanyiko

Suala jingine linalochochea mgawanyiko nchini Israel ni msamaha wa muda mrefu wa utumishi wa kijeshi kwa wanaume wengi wa jamii ya Kiyahudi ya Kiorthodoksi, wanaojulikana kama Haredi.
Wengi wao huona kusoma Torati na kujitolea kwa maisha ya kidini kuwa wajibu wao mkuu, na wanapinga kujiunga na jeshi kwa lazima. Kwa muda mrefu, mipango maalumu iliwaruhusu baadhi yao kuendelea na masomo ya dini badala ya kutumikia jeshini.
Lakini vita vya miaka ya karibuni na uhaba wa wanajeshi vimeongeza shinikizo la kutaka jamii hiyo nayo ichangie katika utumishi wa kijeshi kama Waisraeli wengine.
Mwaka 2024, Mahakama Kuu ya Israel iliamua kuwa hakuna tena msingi wa kisheria wa kuendelea kuwapa wanaume wa Haredi msamaha wa jumla wa kujiunga na jeshi. Uamuzi huo umechochea maandamano na mvutano kati ya viongozi wa kidini, serikali na wanaotaka utumishi wa kijeshi uwe wa usawa.
Netanyahu, ambaye hutegemea uungwaji mkono wa vyama vya Kiorthodoksi ili kudumisha muungano wake wa kisiasa, amekuwa katika hali ngumu. Anapaswa kusawazisha matakwa ya washirika hao na shinikizo kutoka kwa wananchi wanaotaka kila anayestahili kujiunga na jeshi atimize wajibu huo.
Eisenkot na baadhi ya wapinzani wake wanataka sheria za kujiunga na jeshi zitekelezwe kwa usawa zaidi. Kwa hiyo, mjadala huu hauhusu dini pekee, bali pia haki, wajibu wa raia na mustakabali wa muungano utakaounda serikali ijayo.
Matokeo ya uchaguzi yanaweza kuamua si tu kama Netanyahu ataendelea kuwa waziri mkuu, bali pia kama Israel itaweza kuunda serikali yenye wingi wa kutosha kutekeleza sera zake. Ikiwa kambi zinazoshindana hazitapata viti vya kutosha, mazungumzo magumu ya kuunda muungano yanaweza kuendeleza hali ya kutokuwa na uhakika wa kisiasa.
Wayahudi wa Kiorthodoksi ni akina nani?

Chanzo cha picha, Reuters
Wayahudi wa Kiorthodoksi, wanaojulikana pia kama Haredi, ni jamii yenye msimamo mkali wa kidini ambayo huishi kwa kufuata kwa karibu mafundisho na mila za dini ya Kiyahudi.
Ingawa kwa muda mrefu walikuwa kundi dogo ndani ya Israel, idadi yao imekuwa ikiongezeka kwa kasi katika miongo ya karibuni. Inakadiriwa kuwa wanaunda karibu asilimia 14 ya wakazi wa Israel na idadi hiyo inaendelea kuongezeka kutokana na viwango vya juu vya kuzaliwa katika jamii hiyo.
Wengi wao husoma katika taasisi maalumu za kidini zinazojulikana kama yeshiva. Kwa jamii hii, kujifunza maandiko ya dini si shughuli ya kawaida tu bali ni jukumu muhimu la maisha.
Kutokana na mtazamo huo, vijana wengi wa Haredi wamekuwa wakisamehewa kujiunga na jeshi ili waendelee na masomo ya dini.
Mpangilio huo ulianza katika miaka ya mwanzo ya kuanzishwa kwa taifa la Israel, wakati idadi ya Wayahudi wa Kiorthodoksi ilikuwa ndogo sana na wengi wao walikuwa manusura wa mauaji ya Holocaust waliokuwa wakijaribu kujenga upya maisha yao na taasisi zao za kidini.
Kwa nini wanapinga kujiunga na jeshi?

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Kwa viongozi wengi wa Haredi, suala la kujiunga na jeshi si tu kuhusu usalama wa taifa bali ni suala la kuhifadhi utambulisho wao wa kidini.
Wanaamini kuwa mazingira ya kijeshi yanaweza kuwaweka vijana wao karibu na mitazamo, tabia na mfumo wa maisha ambao unaweza kuwafanya kuachana na mila za jamii yao.
Kwao, kuendelea kusoma dini na kuhifadhi mafundisho ya Kiyahudi ni jukumu lenye umuhimu mkubwa sawa au hata zaidi kuliko huduma ya kijeshi.
Baadhi ya viongozi wa dini wamekuwa wakisisitiza kuwa masomo ya dini yana mchango mkubwa katika ulinzi wa taifa kwa njia ya kiroho.
Mtazamo huo unaungwa mkono na sehemu kubwa ya jamii ya Haredi, ambayo inaamini kuwa kulinda urithi wa dini ya Kiyahudi ni jukumu la msingi kwa mustakabali wa Wayahudi duniani kote.
Kutokana na sababu hizo, juhudi za kuwalazimisha vijana wao kujiunga na jeshi zimekuwa zikionekana kama tishio kwa mfumo wao wa maisha.
Kwa nini suala hili linamsumbua Netanyahu?

Chanzo cha picha, Reuters
Mgogoro huu pia umegeuka kuwa tatizo kubwa la kisiasa kwa Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu.
Kwa miaka mingi, vyama vya Wayahudi wa Kiorthodoksi vimekuwa sehemu muhimu ya miungano ya kisiasa iliyomsaidia kubaki madarakani.
Kwa sababu hiyo, Netanyahu amekuwa akilazimika kusawazisha maslahi ya washirika wake wa kidini na shinikizo kutoka kwa sehemu kubwa ya wananchi wanaotaka mabadiliko.
Iwapo ataimarisha hatua za kuwalazimisha Haredi kujiunga na jeshi, anaweza kupoteza uungwaji mkono wa washirika wake wa kisiasa.
Lakini iwapo ataendelea kutetea mfumo wa sasa, anaweza kukosolewa na wapigakura wengine wanaohisi kuwa kuna upendeleo usiofaa.
Ndiyo maana suala hili limekuwa moja ya mijadala mikubwa zaidi katika siasa za Israel.






























