Ndani ya mtandao wa siri wa hujuma dhidi ya Putin nchini Urusi

Putin
    • Author, Monica Garnsey
    • Nafasi, BBC Eye
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 7

Wanaume wawili raia wa Urusi wanaodai kushirikiana kisiri na vyombo vya ujasusi vya Ukraine wametoa maelezo nadra kuhusu operesheni walizosema zililenga miundombinu na wafanyakazi wa kijeshi ndani ya Urusi.

Mmoja wao, anayefahamika kwa jina la kubuniwa la Ivan, anadai alishiriki katika kusaidia mashambulizi ya ndege zisizo na rubani za Ukraine dhidi ya ndege za kivita za kimkakati na viwanda vya kutengeneza silaha nchini Urusi.

Kauli yake imejumuishwa katika makala ya BBC World Service inayochunguza mtandao wa siri wa watu wanaofanya hujuma dhidi ya Urusi kutoka ndani ya mipaka yake.

Makala hiyo pia inamnukuu Foma, raia wa Urusi anayeishi uhamishoni nchini Poland, ambaye anasema anaongoza mtandao wa watu wanaokusanya taarifa za kijasusi kuhusu maafisa waandamizi wanaolengwa na shirika la ujasusi wa kijeshi la Ukraine, GUR.

Foma anasisitiza kuwa watu wanaoshirikiana naye hutoa taarifa pekee na hawashiriki moja kwa moja katika mashambulizi. Hata hivyo, baada ya kuuawa kwa Luteni Jenerali Fanil Sarvarov mjini Moscow Desemba mwaka jana, alikiri kuwa mtandao wake uliwapatia Waukraine taarifa za kijasusi kuhusu afisa huyo.

Luteni Jenerali Fanil Sarvarov aliuawa mjini Moscow mwaka jana katika shambulio la bomu lililokuwa limefichwa chini ya gari lake.
Maelezo ya picha, Luteni Jenerali Fanil Sarvarov aliuawa mjini Moscow mwaka jana katika shambulio la bomu lililokuwa limefichwa chini ya gari lake.

Ingawa kumekuwa na ripoti za mara kwa mara kuhusu vikundi vya Warusi vinavyofanya hujuma dhidi ya serikali ya Moscow, ni nadra kupata ushuhuda wa moja kwa moja kutoka kwa watu wanaodai kushiriki operesheni hizo, kama ilivyo kwa Ivan.

Shirika la Ujasusi wa Kijeshi la Ukraine (GUR) limethibitisha kuwa Ivan na Foma wanashirikiana nalo, ingawa limekiri kuwa haliwezi kuthibitisha kwa uhakika kila shughuli wanazodai kushiriki. Alipoulizwa iwapo Ivan ni mtu wa kuaminika, mmoja wa wasimamizi wake alijibu: "Simwamini mtu yeyote isipokuwa mimi mwenyewe."

Kutokana na hali ya usiri inayozunguka operesheni hizi, GUR pamoja na watu hao wawili wamekuwa waangalifu kuhusu taarifa wanazotoa. Hali hiyo imefanya kuwa vigumu kuthibitisha kwa njia huru madai yao kuhusu operesheni walizoshiriki.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili WhatsApp bofya kutufuatilia
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Hata hivyo, mbinu wanazoelezea zinafanana na mkakati ambao Ukraine imekiri kuutumia katika vita dhidi ya Urusi, ukiwemo matumizi ya ndege zisizo na rubani kushambulia malengo ya kijeshi ndani ya Urusi na kuendesha operesheni za siri kupitia mawakala wake.

Tangu kuanza kwa vita hivyo, maafisa kadhaa wa ngazi za juu nchini Urusi wameuawa katika mazingira ya kutatanisha. Ingawa Ukraine kwa kawaida haikubali wala kukanusha kuhusika katika mashambulizi yaliyolengwa, afisa mmoja wa ujasusi wa Ukraine aliwahi kuthibitisha kwa BBC kuhusika kwa Kyiv katika mauaji ya Luteni Jenerali Igor Kirillov mnamo Desemba 2024.

Idadi kamili ya Warusi wanaoshirikiana na Ukraine katika operesheni hizo za siri haijulikani. Foma anakadiria kuwa ni kati ya watu 300 na 500, lakini madai hayo hayajathibitishwa na vyanzo huru.

Ivan na Foma wanasema wanapinga si tu vita vya Urusi nchini Ukraine, bali pia utawala wa Rais Vladimir Putin. Wanaamini kuwa mustakabali wa kisiasa wa kiongozi huyo unategemea kwa kiasi kikubwa matokeo ya vita hivyo.

"Kwa sasa, nadhani utawala wa Putin unaweza kuyumba ikiwa Urusi itashindwa vita. Kupitia shughuli zetu, tunajaribu kuharakisha mchakato huo," Ivan alisema.

Alimweleza mwandishi Marcin Mamon kwamba jukumu lake lilihusisha kufuatilia maeneo ya kijeshi na kutambua sehemu za kuficha vipuri vya ndege zisizo na rubani kwa ajili ya maandalizi ya mashambulizi dhidi ya mali za kijeshi za Urusi.

"Vipuri hivyo vikikusanywa pamoja, vinageuka kuwa silaha yenye uwezo mkubwa wa uharibifu, ambayo kwa shambulio moja inaweza kuharibu mali yenye thamani ya mamilioni ya dola," alisema.

Ivan pia alimtumia Mamon video inayodaiwa kumuonyesha akificha vilipuzi karibu na uwanja wa ndege wa kijeshi nchini Urusi.

Iwapo angekamatwa, angeweza kushtakiwa kwa makosa ya ugaidi na kukabiliwa na kifungo kirefu gerezani.

Tofauti na Ivan, Foma hufanya kazi akiwa uhamishoni nje ya Urusi. Anasema huwapa mafunzo ya mtandaoni watu wanaojitolea nchini humo. Mwandishi Marcin Mamon anasema alishuhudia moja ya mafunzo hayo, yaliyolenga mbinu za kuwafuatilia maafisa waandamizi wa kijeshi na kukusanya taarifa za kijasusi kuwahusu.

Foma alisema amekuwa akiwafunza watu wanaojitolea kwa siri ndani ya Urusi kuwafuatilia maafisa waandamizi na kukusanya taarifa kuwahusu.
Maelezo ya picha, Foma alisema amekuwa akiwafunza watu wanaojitolea kwa siri ndani ya Urusi kuwafuatilia maafisa waandamizi na kukusanya taarifa kuwahusu.

"Utapokea faili kutoka kwangu au kwa mmoja wa wenzangu lenye maelezo ya mtu anayelengwa," Foma aliwaeleza watu wake wanaojitolea. Alisema faili hilo lingekuwa na picha, taarifa binafsi, tarehe ya kuzaliwa, umri na maelezo mengine ya mhusika, pamoja na taarifa kuhusu gari analotumia ikiwa analo.

Pia aliwataka kuwa waangalifu wanapotekeleza majukumu yao. "Unapokwenda kumfuatilia mtu anayelengwa, usibebe simu," aliwaambia.

Foma, ambaye anasema aliwahi kuwa sehemu ya tabaka la juu la watawala nchini Urusi, anaamini mtandao wake wa mawasiliano unampa uwezo wa kupata taarifa za ndani mara kwa mara.

Alimwonyesha mwandishi Marcin Mamon jinsi anavyofuatilia malengo ya kijeshi kupitia hifadhidata aliyohifadhi kwenye kompyuta yake.

"Hapa kuna taarifa za maghala ya kuhifadhi vifaa, vituo vya kijeshi, makazi ya majenerali na hata marubani wa ndege za kimkakati zinazoshambulia Ukraine," alisema.

Kwa mujibu wake, kufahamu namna mfumo unavyofanya kazi ni hatua muhimu ya kuweza kuubaini udhaifu wake.

"Ili kuudhoofisha mfumo, lazima kwanza uuelewe. Ukishafahamu namna unavyofanya kazi, unaweza kulenga maeneo yake dhaifu," alisema.

Foma alisema mtandao wake una takribani watu 30 waliotawanyika nchini Urusi, Ukraine na mataifa mengine ya Ulaya. Walioko nje ya Urusi hutoa msaada wa kiutendaji, ikiwa ni pamoja na kufuatilia taarifa za kidijitali za watu wanaolengwa.

Anasema malengo ya kufuatiliwa hupendekezwa na Shirika la Ujasusi wa Kijeshi la Ukraine (GUR), lakini yeye na wenzake hufanya uchunguzi wao wenyewe kabla ya kukubali kushiriki.

"Kwa kawaida tunathibitisha taarifa za mhusika kwanza. Baada ya hapo ndipo tunaamua kama tutashiriki au la," alisema.

Foma anatetea shughuli za mtandao wake akidai kuwa lengo ni kuwafanya wanaohusika katika vita vya Urusi dhidi ya Ukraine watambue kuwa wanaweza kuwajibishwa kwa matendo yao.

"Nataka wale wanaotekeleza vitendo hivi kwa niaba ya Putin na Urusi nchini Ukraine waelewe kuwa siku moja watawajibika. Nataka waogope," alisema.

Hata hivyo, anasisitiza kuwa jukumu lake ni kukusanya na kusambaza taarifa za kijasusi pekee, na kwamba mtandao wake hauhusiki moja kwa moja katika utekelezaji wa mauaji.

Akizungumzia kuuawa kwa Luteni Jenerali Fanil Sarvarov mwezi Desemba 2025, Foma alimwandikia Mamon ujumbe akisema: "Kumfuatilia kulihitaji juhudi kubwa. Aliishi kati ya nyumba ya mpenzi wake na ya mwenzake wa kazi, huku akibadilisha ratiba yake mara kwa mara ili kuficha mienendo yake."

Tofauti na Foma, Ivan alikuwa mwangalifu zaidi katika kueleza shughuli alizodai kushiriki, hata baada ya operesheni hizo kutekelezwa.

Baada ya kufanya uchunguzi wake mwenyewe, Foma alihitimisha kuwa huenda Ivan alihusika katika mpango wa kushambulia kiwanda kikubwa zaidi cha kutengeneza ndege za kijeshi zisizo na rubani nchini Urusi, kilichopo Yelabuga. Mtu mmoja aliripotiwa kuuawa katika tukio hilo.

Ivan alisisitiza kuwa lengo la operesheni hizo ni kuepuka kuwadhuru raia kadri inavyowezekana.

Hata hivyo, alikiri kuwa kazi hiyo imekuwa na hatari kubwa kwake.

"Tukio la hatari zaidi lilikuwa wakati gari langu liliposimamishwa kwa ukaguzi nikiwa nimebeba vilipuzi nilivyotengeneza mwenyewe. Hatari ilikuwa kubwa sana, lakini sikugundulika," alisema.

Ili kupunguza uwezekano wa kufichuliwa, Ivan alisema mtandao wao hauna muundo rasmi na kwamba washiriki wengi hawafahamiani.

Foma pia anafuata kanuni hiyo.

"Mara tu watu wanapoanza kukusanyika katika vikundi au mazungumzo ya pamoja mtandaoni, uwezekano wa kugunduliwa na kukamatwa huongezeka sana," alisema.

Kwa mujibu wa Ivan, watu wachache sana wamebaki nchini Urusi ambao wako tayari kushiriki shughuli za aina hiyo kwa misingi ya itikadi.

"Wengi waliokuwa na misimamo ya upinzani tayari wameondoka nchini au wamefungwa gerezani," alisema.

BBC inaeleza kuwa baadhi ya Warusi wanaohusishwa na hujuma ndani ya nchi yao huenda hawafahamu jukumu lao, kama madereva wanaosafirisha mizigo iliyohujumiwa bila wao kujua. Wengine hushawishiwa kwa malipo ya fedha.

Ivan, hata hivyo, anasema anashiriki shughuli hizo kwa misingi ya imani zake za kisiasa. Akiwa mwanachama wa zamani wa upinzani nchini Urusi, alitarajiwa kuwa chini ya uangalizi wa karibu wa mamlaka. Hivyo, ilizua mshangao kwamba aliweza kuondoka nchini humo na kurejea mara kwa mara bila kuzuiwa.

Marcin Mamon is wearing a white t-shirt and dark glasses. He is standing with his hands in his pockets waiting by a stone wall.
Maelezo ya picha, Marcin alipanga kukutana na Ivan nchini Georgia, akishangazwa na jinsi alivyoweza kusafiri kwa uhuru mara kwa mara licha ya madai ya kuhusika katika operesheni za siri dhidi ya Urusi.

Mwandishi Marcin Mamon alimshawishi Ivan wakutane katika eneo la mbali nchini Georgia ambako wangeweza kuzungumza kwa uhuru. Hapo ndipo alipomuuliza ni kwa namna gani maafisa wa ujasusi wa Ukraine waliweza kumuamini.

"Unasafiri kwenda nchi ya tatu, ambako mawakala wa Ukraine hukutana nawe na kukufanyia vipimo vya kugundua uongo," Ivan alimjibu.

Baadaye, Mamon alimwomba Ivan amuunganishe na mmoja wa wasimamizi wake katika Shirika la Ujasusi wa Kijeshi la Ukraine (GUR). Msimamizi huyo alipiga simu mara moja na kuzungumza naye kupitia spika ya simu, jambo lililoonekana kuashiria kuwa Ivan alikuwa akifanya kazi chini ya uangalizi wake. Mazungumzo yao yalitumia lugha ya mafumbo, wakirejelea kile walichokiita "matengenezo shuleni."

Hata hivyo, baadaye msimamizi huyo alikiri kuwa hawezi kuondoa kabisa uwezekano kwamba Ivan huenda alikuwa akifanya kazi kwa maslahi ya Urusi pia, iwe kwa hiari au kwa shinikizo.

Kwa upande wake, Foma anaamini kuwa uwezo wa Ivan wa kusafiri kwa uhuru haupaswi kutafsiriwa moja kwa moja kuwa kuna jambo lisilo la kawaida.

"Kuna mianya mingi katika mfumo. Ukiifahamu vizuri, au ukibahatika tu, unaweza kuitumia na kuendelea kuishi ndani ya mfumo huo," alisema. "Kama panya ndani ya kipande cha jibini."

Hoja mojawapo inayounga mkono madai ya Ivan ni kwamba kama angekuwa pia akishirikiana na shirika la usalama la Urusi la FSB, huenda angekuwa ametoa taarifa kuhusu baadhi ya mipango ya mashambulizi ya Ukraine.

Kwa mujibu wa Mamon, zaidi ya mwaka mmoja kabla ya shambulio kubwa la ndege zisizo na rubani za Ukraine dhidi ya viwanja vya ndege vya kijeshi vya Urusi, Ivan alikuwa amedokeza kuwa mashambulizi makubwa dhidi ya ndege za kivita za kimkakati yalikuwa yanapangwa, ingawa hakufichua lini wala yangefanyika wapi.

Alipoulizwa jinsi anavyokabiliana na shinikizo la kazi hiyo, Ivan alisema hofu imekuwa sehemu ya maisha yake ya kila siku.

"Hofu ipo wakati wote. Inanifuata kila mahali. Hata usipofanya chochote, bado unaihisia. Hii ni Urusi," alisema.

Pamoja na hayo, alisema ana matumaini kwamba hali ya kisiasa nchini humo haitabaki hivyo milele.

"Putin hataishi milele," alisema.

Imetafsiriwa na Ambia Hirsi