Mashambulizi ya Houthi dhidi ya Saudi Arabia yataathiri ibada ya Umrah?

.
Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 5

Mashambulizi yanayoendelea ya wanamgambo wa Houthi kutoka Yemen dhidi ya Saudi Arabia na njia muhimu ya bahari ya Bahari ya Shamu (Red Sea) yameibua tena wasiwasi miongoni mwa Waislamu duniani, hususan maelfu wanaopanga kwenda kufanya ibada ya Umrah katika miezi ijayo.

Katika siku za hivi karibuni, wanamgambo hao wameshambulia viwanja muhimu vya ndege nchini Saudi Arabia, ikiwemo Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Riyadh. Shambulio la Ijumaa lilisababisha vifo vya watu watatu na kujeruhi zaidi ya watu kumi.

Ingawa serikali ya Saudi Arabia imeendelea kusisitiza kuwa imechukua hatua kali za kiusalama kulinda Msikiti Mkuu wa Makka na kuhakikisha usalama wa mahujaji, kuongezeka kwa mashambulizi yanayolenga maeneo ya kimkakati nchini humo kumezua maswali miongoni mwa baadhi ya wanaotarajia kufanya Umrah kuhusu iwapo hali hiyo inaweza kuathiri safari zao za ibada.

Kwa miaka kadhaa sasa, mzozo wa Yemen umehusishwa na mashambulizi dhidi ya Saudi Arabia kwa kutumia makombora ya masafa marefu na ndege zisizo na rubani (droni), hali iliyolazimu mamlaka za ufalme huo kuimarisha zaidi mifumo ya ulinzi wa anga pamoja na usalama katika viwanja vya ndege na maeneo mengine nyeti.

Hata hivyo, hadi sasa miji miwili mitakatifu ya Makka na Madina imeendelea kupokea mamilioni ya waumini kutoka sehemu mbalimbali duniani kwa ajili ya kufanya ibada ya Umrah bila kusitishwa.

Hali hii imezua mjadala mpana kuhusu iwapo mashambulizi ya Wahouthi yanaweza kuathiri mipango ya safari za Umrah kwa maelfu ya Waislamu wanaojiandaa kwa ibada hiyo katika miezi ijayo.

Nini chanzo cha mzozo kati ya Wahouthi na Saudi Arabia?

Mchambuzi wa masuala ya Mashariki ya Kati na Falme za Kiarabu, Mohamed Qaddam Sadiq Isah, amesema kuwa chanzo cha mzozo kati ya Wahouthi na Saudi Arabia kinahusiana na vita vya madaraka nchini Yemen vilivyochukua mkondo mpya mwaka 2014.

Kwa mujibu wa Isah, harakati ya Wahouthi imekuwa katika mgogoro wa muda mrefu na serikali ya Yemen kuhusu udhibiti wa mamlaka ya nchi. Mvutano huo uliongezeka baada ya Wahouthi kutwaa maeneo muhimu, yakiwemo mji mkuu wa Sanaa, hatua iliyotikisa utawala uliokuwa ukitambuliwa kimataifa.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili WhatsApp bofya kutufuatilia
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Alieleza kuwa Saudi Arabia iliingia moja kwa moja katika mgogoro huo kwa kuunga mkono serikali halali ya Yemen, jambo lililoifanya kuwa mmoja wa wapinzani wakuu wa Wahouthi. Tangu wakati huo, pande hizo mbili zimekuwa katika mvutano wa kijeshi na kisiasa unaoendelea hadi leo.

Kwa miaka kadhaa, Wahouthi wamekuwa wakitekeleza mashambulizi ya makombora na ndege zisizo na rubani (droni) dhidi ya maeneo mbalimbali ndani ya Saudi Arabia, wakidai ni sehemu ya mapambano yao dhidi ya ushiriki wa ufalme huo katika vita vya Yemen.

Isah anasema kwamba kiini cha mgogoro huo ni mapambano ya kuwania ushawishi na udhibiti wa Yemen, huku athari zake zikivuka mipaka na kuathiri usalama wa Saudi Arabia pamoja na eneo pana la Mashariki ya Kati.

Kabla ya mwaka 2014, Wahouthi walikuwa wamejenga uhusiano wa karibu na Iran, jambo ambalo kwa kiasi kikubwa lilibadili mwelekeo wa harakati zao. Mapambano yao ya awali ya kuwania udhibiti wa Yemen yaligeuka na kuwa sehemu ya ajenda pana ya kuishinikiza Saudi Arabia na mataifa mengine jirani kupitia ushawishi wa kikanda wa Iran, alisema.

Aliongeza kuwa Iran imekuwa ikiwatumia Wahouthi kwa namna inayofanana na jinsi inavyounga mkono makundi mengine yenye ushawishi katika eneo la Mashariki ya Kati, yakiwemo Hezbollah ya Lebanon na Hamas ya Palestina.

Mchambuzi huyo alisema kuwa Saudi Arabia mwaka 2015 iliongoza muungano mpana wa mataifa ya Kiarabu uliolenga kurejesha serikali ya Yemen iliyokuwa ikitambuliwa kimataifa, baada ya Wahouthi kudhibiti maeneo makubwa ya nchi hiyo, ikiwemo mji mkuu, Sanaa.

Kwa mujibu wake, muungano huo ulifanikiwa kurejesha udhibiti wa maeneo mengi yaliyokuwa yametekwa na Wahouthi na kuzuia kuimarika kwa kile kilichoonekana kama mapinduzi dhidi ya serikali halali ya Yemen.

"Muungano huo ulifanikiwa kukomboa sehemu kubwa ya Yemen na kudhoofisha udhibiti wa Wahouthi. Hata hivyo, hapo ndipo mzozo wa moja kwa moja kati ya Saudi Arabia na Wahouthi ulipoanza rasmi," alisema.

Tangu wakati huo, amesema, uhusiano kati ya pande hizo mbili umekuwa wa uhasama wa wazi, huku Wahouthi wakifanya mashambulizi ya mara kwa mara kwa makombora na ndege zisizo na rubani dhidi ya maeneo mbalimbali ndani ya Saudi Arabia, na kuifanya vita ya Yemen kuwa moja ya migogoro yenye athari kubwa zaidi kwa usalama wa eneo la Mashariki ya Kati.

Je, mashambulizi ya Wahouthi yanaathiri ibada ya Umrah?

Katika miaka ya karibuni, Saudi Arabia imeripoti mashambulizi kadhaa yanayohusishwa na Wahouthi, yakiwemo mashambulizi yaliyolenga maeneo ya kimkakati na miundombinu muhimu ya nchi hiyo. Hali hiyo imezidisha wasiwasi miongoni mwa baadhi ya Waislamu wanaojiandaa kusafiri kwa ajili ya ibada ya Umrah.

Mchambuzi wa masuala ya Mashariki ya Kati, Mohamed Qaddam Sadiq Isah, anasema kuwa kwa kuzingatia jiografia ya eneo hilo, Wahouthi wana uwezo wa kufikia maeneo ya ndani ya Saudi Arabia kwa kutumia makombora ya masafa marefu na ndege zisizo na rubani (droni). Alieleza kuwa maeneo yanayodhibitiwa na kundi hilo kaskazini mwa Yemen yako karibu na mpaka wa Saudi Arabia, hali inayorahisisha mashambulizi kuvuka mipaka.

"Kutokana na uwezo wa Wahouthi kutumia silaha za kisasa zenye uwezo wa kushambulia malengo ya mbali, si jambo la ajabu kuona mashambulizi yakifikia maeneo mbalimbali ndani ya Saudi Arabia, ikiwemo maeneo yaliyo karibu na miji mitakatifu ya Makka na Madina," alisema.

Hata hivyo, Wahouthi wamekuwa wakikanusha mara kwa mara madai ya kulenga kwa makusudi miji hiyo mitakatifu, wakisisitiza kwamba mashambulizi yao yanalenga malengo ya kijeshi au ya kimkakati.

Kwa sasa, hakuna ushahidi unaoonyesha kwamba ibada za Umrah zimeathiriwa moja kwa moja na mashambulizi hayo. Makka na Madina zimeendelea kupokea mamilioni ya waumini kutoka sehemu mbalimbali duniani, huku Saudi Arabia ikisisitiza kuwa imeimarisha hatua za usalama ili kuhakikisha mahujaji wanatekeleza ibada zao kwa utulivu na usalama.

Hata hivyo, Qaddam anaonya kuwa iwapo mzozo huo utaongezeka na mapigano kushika kasi zaidi, athari zake zinaweza kuonekana katika shughuli za ibada.

"Iwapo vita vitaongezeka, athari kwa shughuli za kidini haziwezi kuepukika. Baadhi ya viwanja vya ndege vinaweza kusitisha shughuli zake, na mamlaka zinaweza kuweka vikwazo vya muda kwa wageni wanaoingia nchini. Hali hiyo inaweza kuathiri safari za Umrah na Hija, au hata kuzifanya zibaki kwa waumini waliopo ndani ya Saudi Arabia pekee, kama ilivyoshuhudiwa wakati wa janga la UVIKO-19," alisema.

Licha ya tahadhari hizo, mpaka sasa ibada za Umrah zinaendelea kama kawaida, na mamlaka za Saudi Arabia zimeendelea kusisitiza kwamba usalama wa mahujaji na wa maeneo matakatifu unabaki kuwa kipaumbele cha juu.

Kuna uhusiano gani kati ya mzozo huu na mvutano kati ya Iran na Marekani?

Mchambuzi wa masuala ya Mashariki ya Kati, Mohamed Qaddam Sadiq Isah, amesema mzozo wa Wahouthi hauwezi kutenganishwa na mvutano mpana kati ya Iran na Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati.

Kwa mujibu wake, Wahouthi kwa sasa ni miongoni mwa makundi muhimu yanayoungwa mkono na Iran, hasa baada ya makundi mengine washirika wa Tehran, kama Hezbollah na Hamas, kudhoofishwa na migogoro ya hivi karibuni.

"Harakati ya Wahouthi sasa ni miongoni mwa nguvu muhimu zilizosalia zinazoungwa mkono na Iran katika Mashariki ya Kati," alisema.

Aliongeza kuwa umuhimu wa Yemen unatokana pia na nafasi yake ya kimkakati kwenye Mlango-Bahari wa Bab al-Mandab, mojawapo ya njia muhimu zaidi za usafirishaji wa biashara duniani, ambayo Wahouthi wanataka kuwa na ushawishi mkubwa juu yake.

"Kwa hiyo, vita vinavyoendelea Yemen vinaweza kutazamwa kama sehemu ya mwendelezo wa mvutano kati ya Iran na Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati," aliongeza.

Mzozo huu unaweza kumalizwa vipi?

Qaddam Sadiq amesema juhudi za kisiasa na kidiplomasia za kumaliza vita vya Yemen zimeendelea kufanyika kwa miaka kadhaa, lakini bado hazijaleta suluhu ya kudumu.

Kwa mujibu wake, kikwazo kikubwa ni kutokuwepo kwa makubaliano ya kisiasa yatakayowezesha amani ya kudumu na uchaguzi huru nchini Yemen.

"Wahouthi wanaendelea kupinga mchakato wa kisiasa unaoweza kuiongoza Yemen kwenye uchaguzi wa kidemokrasia," alisema.

Aliongeza kuwa kundi hilo limechagua kutumia nguvu za kijeshi kudhibiti mamlaka badala ya kutegemea ushindani wa kisiasa kupitia uchaguzi.

"Kwa hiyo, hatua yoyote ya kumaliza vita hivi haitakuwa rahisi," alihitimisha Mohamed Qaddam Sadiq Isah.