Moja kwa moja, Watu 7 hawajulikani walipo baada ya jengo kuporomoka Eastleigh, Kenya

Waziri wa Mambo ya Ndani, Kipchumba Murkomen, amezitaka familia ambazo ndugu au jamaa zao hawajulikani walipo kufuatia kuporomoka kwa jengo hilo kutoa taarifa kwa Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya kupitia nambari ya dharura ya 1199.

Ruka Video uendelee
  • xx
  • Wicknell Chivayo
  • Kijanangoma
  • xx
  • Besigye
  • .
  • xx
  • xx
  • xx
  • Lungu
  • xx
  • xx
  • d
  • s
  • a
  • Sonko
  • xx
  • xx
  • xx

Moja kwa moja

Na Mariam Mjahid

  1. Infantino adai kuungwa mkono na idadi kubwa ya wadau wa soka duniani

    n

    Rais wa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), Gianni Infantino, amesisitiza kuwa anaungwa mkono na idadi kubwa ya wadau wa soka duniani, huku akipuuza kwa kicheko maswali kuhusu iwapo aliwahi kufikiria kujiuzulu kufuatia utata ulioibuka kuhusu mpango wa kuuza haki za kibiashara za mashindano ya Kombe la Dunia.

    Katika mahojiano na BBC Sport, Infantino alionyesha msimamo wa kutoyumbishwa kuhusu nafasi yake, kufuatia malalamiko yaliyoibuliwa na pendekezo lenye utata la Fifa Forward Enterprise (FFE). Amesema si rahisi kila wakati kuwakutanisha watu wenye mitazamo tofauti na kuwafanya wakubaliane.

    “Hakuna ubaya kutokubaliana,” amesema. “Tunaona hilo kila siku katika nchi nyingi duniani. Ni sawa kutokubaliana na kuwa na mitazamo tofauti, lakini baadaye tunapaswa kuweza kusonga mbele.”

    Miezi miwili iliyopita, Infantino alikuwa akikabiliwa na shinikizo lililoongezeka la kutaka ajiuzulu kutoka nafasi ya urais wa FIFA, taasisi ambayo ameiongoza tangu mwaka 2016.

    Viongozi wa Shirikisho la Soka Ulaya (UEFA), Shirikisho la Soka Asia (AFC) na Concacaf, linalosimamia soka Amerika Kaskazini na Amerika ya Kati, walitia saini barua wakimtuhumu Infantino kwa kuvunja imani yao kupitia kile walichokitaja kuwa ni udanganyifu.

    Wiki iliyopita, UEFA iliitaka FIFA kutoa nyaraka zote muhimu zinazohusiana na mpango wa FFE kabla ya Novemba 2. Katibu Mkuu wa UEFA, Theodore Theodoridis, alisema FIFA ilikuwa imeshindwa kujibu “maswali kadhaa ya msingi”.

    Chini ya mpango wa FFE, ambao Infantino aliufuta ndani ya siku chache baada ya kuwasilishwa, sehemu ya haki za kibiashara za mashindano yanayoendeshwa na FIFA ingeuziwa kampuni binafsi ya uwekezaji.

    Tangu kuwasilishwa kwa barua hiyo, Infantino amekuwa akisafiri katika mataifa mbalimbali, akiwemo Morocco, Jamhuri ya Dominika, Cape Verde na Japan, katika juhudi za kuimarisha uungwaji mkono wake.

    Hali hiyo imeimarisha nafasi yake kiasi kwamba kuchaguliwa kwake tena kwa muhula wa nne katika uchaguzi wa urais wa FIFA mwaka ujao kunaonekana kuwa na uwezekano mkubwa.

    Infantino pia amependekeza kuongeza kwa dola bilioni 3.4 za Marekani kiasi cha fedha kinachotolewa kwa ajili ya kuendeleza soka duniani kote.

    “Ninatoka Tokyo, ambako Shirikisho la Soka Asia limenipa uungwaji mkono kamili. Nilikuwa Cape Verde, ambako nchi zote wanachama wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) zimeunga mkono azma yangu. Ninaendelea kuzungumza na vyama vya soka kila mahali duniani,” amesema Infantino.

    Tarehe ya mwisho kwa wagombea kuthibitisha nia yao ya kuwania urais dhidi ya Infantino katika uchaguzi wa Machi ni Novemba 18. Hata hivyo, hadi sasa hakuna mgombea mwingine aliyewasilisha jina lake, hivyo Infantino anaweza kuwania nafasi hiyo bila mpinzani.

    Soma Pia:

  2. Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja ataka wahandisi wachunguzwe baada ya jengo la Eastleigh kuporomoka

    d

    Gavana wa Nairobi, Kenya, Johnson Sakaja, ametaka uchunguzi ufanyike dhidi ya mbunifu wa majengo, mhandisi na mpangaji wa matumizi ya ardhi waliohusishwa na ujenzi wa jengo la ghorofa 12 lililoporomoka Eastleigh, akisema ujenzi uliendelea bila mipango ya ujenzi kuidhinishwa na kaunti.

    Sakaja amezitaka bodi za kitaaluma zinazowasimamia wasanifu majengo, wahandisi, wakadiriaji wa gharama za ujenzi na wakandarasi kuwachunguza wanachama wao ili kubaini kama walizingatia viwango vya taaluma na kanuni za ujenzi.

    Akizungumza siku ya pili ya operesheni za utafutaji na uokoaji zilizohusisha taasisi mbalimbali, Sakaja amesema rekodi za Kaunti ya Nairobi zinaonyesha kuwa kibali pekee kilichotolewa kwa mradi huo kilikuwa cha kubadili matumizi ya jengo kutoka makazi kwenda matumizi ya biashara na makazi.

    Kaunti iliidhinisha mabadiliko hayo Oktoba 17, 2024, kufuatia maombi yaliyowasilishwa na mpangaji wa matumizi ya ardhi, Nathan Mutunga Kiiti. Hata hivyo, mipango ya usanifu iliyowasilishwa na mbunifu Emmanuel Mwangi Maina Novemba 20, 2024, haikuidhinishwa.

    Nyaraka za uhandisi wa kiraia na miundo ziliwasilishwa kupitia kampuni ya Precise Civil Engineering Ltd, huku Stromax Holdings E.A. Limited ikitajwa kuwa mkandarasi wa mradi huo. Maina alitajwa kuwa mbunifu wa mradi, na Joseph Mutturi Mugu kuwa mhandisi wa miundo.

    Sakaja amesema tofauti kati ya kibali cha kubadili matumizi ya jengo na mipango ya ujenzi ambayo haikuidhinishwa ni muhimu katika kubaini uwajibikaji kuhusu kuporomoka kwa jengo hilo.

    “Wataalamu ambao taarifa zao zilitumika katika mchakato wa maendeleo ya mradi wana wajibu wa kuhakikisha kuwa ujenzi unazingatia mipango iliyoidhinishwa, kanuni za ujenzi na viwango vya usalama,” amesema Sakaja.

    Ameeleza tukio hilo kuwa ni hali ya “kutokuwajibika kabisa”, akizitaka bodi husika za kitaaluma kubaini kama wanachama wao walitimiza wajibu wao na kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya watakaobainika kuwajibika kwa ukiukaji wowote.

    Soma Pia:

  3. Lissu kuanza mgomo wa kula Jumatatu akidai kunyimwa haki - Wakili

    d

    Mwanasheria wa CHADEMA, Dkt. Rugemeleza Nshala, amesema Mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu, anatarajia kuanza mgomo wa kula Jumatatu, Oktoba 26, 2026, kupinga kunyimwa haki ya kufanya mazungumzo ya faragha na mawakili wake.

    Akizungumza katika makao makuu ya CHADEMA, Mikocheni, Dar es Salaam, Oktoba 24, Dkt. Nshala amesema hatua hiyo inatokana na kile alichokitaja kuwa ni kutoheshimiwa kwa uamuzi wa Mahakama ulioruhusu Lissu kuzungumza na mawakili wake kwa faragha.

    Dkt. Nshala ameongeza kuwa Lissu amedhamiria kuanza mgomo huo na kusitisha matumizi ya dawa kuanzia Jumatatu, kama njia ya kushinikiza mamlaka kuheshimu haki zake za kisheria.

    Akirejelea Katiba ya Tanzania, Ibara ya 26(1), Dkt. Nshala amesema kila mtu ana wajibu wa kutii Katiba na sheria za nchi, akiwemo kila aliyepewa jukumu la kuzisimamia.

    Amehoji kwa nini sheria hazizingatiwi, akisema: “Je, tunakwenda wapi kama nchi? Kwa nini tunafika hapo? Kwa nini tunasema tuko chini ya sheria, lakini sheria hazifuatwi bila masharti?”

    Dkt. Nshala amedai kuwa kutotekelezwa kwa uamuzi wa Mahakama kunazua wasiwasi kuhusu utawala wa sheria nchini, akisema sheria zinaonekana kutumiwa kwa namna tofauti, ikiwemo kukandamiza wanaopinga au kukosoa walio madarakani.

    Kuhusu afya ya Lissu iwapo ataanza mgomo wa kula na kusitisha matumizi ya dawa, Dkt. Nshala amesema suala hilo linaachiwa wananchi kulitafakari.

    Haya yanajiri baada ya Mahakama kusema itahitaji muda wa kutosha ili iweze kutoa maamuzi sababu kesi inayomkabili Lissu ni shauri la namna yake.

    Watanzania wanasubiri kujua hukumu itakayotolewa dhisi ya Lissu iliyoartibiwa kufanyika tarehe sita mwezi wa kumi na moja saa tatu asubuhi.

    Unaweza kusoma;

  4. Ufaransa yakabiliwa na maandamano mapya yanayopinga kupanda kwa gharama za maisha

    r

    Ufaransa inakabiliwa na wimbi jipya la maandamano yanayopinga kupanda kwa gharama za maisha na kuzorota kwa hali ya elimu shuleni, huku kukiwa na hofu ya kurudiwa kwa vurugu na uporaji wa maduka ulioshuhudiwa mwishoni mwa wiki iliyopita.

    Serikali imesema itatuma maafisa 70,000 wa polisi katika maeneo mbalimbali nchini humo na kuahidi kuchukua hatua mara moja iwapo dalili zozote za machafuko zitajitokeza.

    “Hatutavumilia kitendo chochote cha uvunjifu wa sheria,” amesema Waziri wa Mambo ya Ndani, Laurent Nuñez.

    Ameongeza kuwa serikali haitakuwa na msamaha kwa waharibifu wa mali, waporaji na wote wanaojihusisha na vitendo vya vurugu. Amesema pia kuwa, mbali na maandamano yaliyopangwa, kumekuwa na jumbe nyingi za uchochezi wa vurugu kwenye mitandao ya kijamii kutoka kwa makundi ya mrengo wa kushoto na mrengo mkali wa kushoto.

    Mjini Paris, wafanyabiashara wamefunga au kuimarisha ulinzi wa maduka yao kuzuia uharibifu unaoweza kutokea. Mji wa Orléans, kusini mwa Paris, ni miongoni mwa maeneo yanayotia wasiwasi mkubwa.

    Katika siku za hivi karibuni, mamia ya watu wamehukumiwa kifungo kwa uharibifu wa mali, uchomaji moto na uporaji, baada ya kusikilizwa kwa kesi zao kwa utaratibu wa haraka.

    Hasira na kukata tamaa vimeongezeka miongoni mwa wananchi wa Ufaransa, ambao wanakabiliwa na gharama za maisha zinazozidi kupanda. Hali hiyo inazidishwa na tahadhari zinazotolewa kuwa serikali zijazo huenda zikapunguza kwa kiasi kikubwa matumizi ya umma.

    Maandamano hayo yalianza kwa wanafunzi wa shule za sekondari kudai kuboreshwa kwa mazingira ya kujifunzia na kutatuliwa kwa uhaba wa walimu na wafanyakazi wengine. Hata hivyo, baadaye baadhi ya maeneo yalikumbwa na vurugu.

    Chama cha mrengo wa kulia mkali cha National Rally kinafanya mkutano wake wa mwaka katika mji huo. Kiongozi wake, Marine Le Pen, anatarajiwa kutangaza rasmi nia yake ya kugombea urais katika uchaguzi wa mwaka ujao.

    Soma pia:

  5. Ubalozi wa Marekani nchini Jordan waimarisha usalama

    m

    Ubalozi wa Marekani nchini Jordan umetangaza kuimarishwa kwa hatua za usalama kufuatia shambulizi lililotokea katika kanisa moja siku ya Ijumaa.

    Kwa mujibu wa taarifa ya ubalozi huo, ulinzi umeimarishwa katika vituo vya kibiashara, balozi za kigeni na maeneo mengine nchini Jordan.

    Mamlaka za Jordan zimelitaja shambulizi hilo kuwa kitendo cha kigaidi kilichotekelezwa na watu wenye misimamo mikali.

    Mkuu wa taasisi ya usalama wa umma nchini humo amesema watu saba waliuawa na wengine wengi kujeruhiwa baada ya watu wenye silaha kuwafyatulia risasi waumini waliokuwa wamekusanyika kanisani kwa ajili ya ibada.

    Mashambulizi ya aina hiyo si ya kawaida nchini Jordan, ingawa mamlaka zinasema zimefanikiwa kuzuia mashambulizi yaliyopangwa na watu wenye misimamo mikali katika miaka ya hivi karibuni.

    Mamlaka za Jordan zimesema bado zinawatafuta waliohusika na shambulizi hilo. Aidha, zimeeleza kuwa ni mapema kubaini iwapo washambuliaji hao wana uhusiano na makundi yaliyoko ndani au nje ya nchi hiyo.

    Pia Unaweza Kusoma:

  6. Kenya yaonya kuhusu mvua kubwa, upepo mkali, mawimbi makubwa na joto kali

    h

    Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini Kenya imetoa tahadhari ya mvua kubwa, upepo mkali, mawimbi makubwa baharini na joto kali, huku baadhi ya maeneo yakitarajiwa kupata mvua inayozidi milimita 20 ndani ya saa 24.

    Katika taarifa iliyotolewa Oktoba 23, mamlaka hiyo imesema mvua ya wastani hadi kubwa inatarajiwa kuanzia Oktoba 24 hadi 28, 2026, katika maeneo ya Pwani, Kaskazini Mashariki, Nyanda za Juu Magharibi na Mashariki mwa Bonde la Ufa, Nyanda za Juu za Kati, ikiwemo baadhi ya maeneo ya Nairobi, pamoja na sehemu za Nyanda za Chini Kusini Mashariki.

    Mvua hiyo inatarajiwa kuongezeka kati ya Oktoba 26 na 28, huku upepo mkali wa kusini hadi kusini mashariki, wenye kasi ya kilomita 25 kwa saa au zaidi, ukitarajiwa katika maeneo ya Pwani, mashariki na kaskazini mwa nchi.

    Mamlaka hiyo pia imetabiri mawimbi ya bahari yenye urefu wa zaidi ya mita mbili Jumapili, Oktoba 25, huku joto kali likitarajiwa kuendelea katika baadhi ya maeneo, hasa kaskazini mwa Kenya.

    Katika maelekezo yake, mamlaka hiyo imewataka wakazi wa maeneo yaliyoathiriwa kuwa waangalifu kutokana na uwezekano wa mafuriko ya ghafla na uoni hafifu barabarani.

    “Wakazi katika maeneo yote yaliyotajwa wanapaswa kuwa macho kutokana na uwezekano wa mafuriko ya ghafla na uoni hafifu,” taarifa hiyo imesema.

    Aidha, wananchi wameshauriwa kuepuka kujihifadhi chini ya miti au karibu na madirisha yenye vyuma wakati wa mvua za radi, na kuhakikisha wanakunywa maji ya kutosha na kuepuka kukaa juani kwa muda mrefu katika maeneo yenye joto kali.

    Wanaoshiriki shughuli za baharini pia wametakiwa kuzingatia tahadhari kutokana na upepo mkali na mawimbi makubwa yanayotarajiwa.

    Haya yanajiri baada ya taasisi za mazingira ulimwenguni kutabiri mvua kubwa ya el nino.

    Pia unaweza kusoma:

  7. Pentagon yadai taasisi za Confucius kuwa tishio kwa usalama wa taifa la Marekani

    v

    Wizara ya Ulinzi ya Marekani, inayojulikana kama Pentagon, imetangaza kuwa taasisi za Confucius, zinazofundisha lugha na utamaduni wa China, ni tishio kwa usalama wa taifa la Marekani.

    Katika video iliyochapishwa kwenye mitandao ya kijamii, Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Pat Hegseth, amezifananisha taasisi hizo na “vituo vya propaganda”, akisema kuwa vituo kadhaa vimeanzishwa katika vyuo vikuu mbalimbali nchini Marekani kwa kutumia majina tofauti.

    Ameyatuhumu taasisi hizo kwa kuiba mali miliki na, kwa maneno yake, kujaribu “kuingilia fikra za wanafunzi wa Marekani”.

    Kwa mujibu wa Hegseth, Wizara ya Ulinzi ya Marekani inaendelea kuzivunja taasisi hizo kwa utaratibu.

    Ubalozi wa China mjini Washington bado haujatoa maoni kuhusu suala hilo.

    Taasisi za Confucius ni vituo vilivyoanzishwa katika vyuo vikuu vya nchi mbalimbali kwa msaada wa kifedha kutoka China. Vituo hivyo hutoa mafunzo ya lugha ya Kichina na kuandaa shughuli zinazohusiana na utamaduni wa nchi hiyo.

    Mpango huo ulianza mwaka 2004, wakati kituo cha kwanza kilipoanzishwa mjini Seoul, mji mkuu wa Korea Kusini. Mwaka huohuo, kituo kama hicho kilianzishwa katika Chuo Kikuu cha Maryland nchini Marekani. Kwa kawaida, vituo hivyo vimekuwa vikishirikiana na vyuo vikuu vya China pamoja na vile vya nchi vinakopatikana.

    Idadi ya vituo hivyo nchini Marekani ilifikia takribani 100 kufikia mwaka 2019. Hata hivyo, katika miaka iliyofuata, vituo vingi vilifungwa kutokana na wasiwasi kuhusu usalama wa taifa na uhuru wa kitaaluma wa vyuo vikuu.

    h
  8. Trump: Marekani yafikiria kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya Iran

    d

    Kwa mujibu wa tathmini ya mashirika ya ujasusi ya Marekani, Iran imeongeza kwa kiasi kikubwa juhudi za kuwalenga wanadiplomasia na maafisa wengine wa Marekani katika Mashariki ya Kati na maeneo mengine duniani.

    Inadaiwa kuwa mpango wa Iran umefikia kilele chake.

    Kauli ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani imetolewa wakati Washington ikipunguza idadi ya wanadiplomasia wake walioko katika moja ya nchi za Mashariki ya Kati.

    Rais Donald Trump amesema Marekani inafikiria kuchukua hatua mpya za kijeshi dhidi ya Iran.

    Kauli ya Trump inatolewa wakati Marekani na Israel zimekuwa katika vita na Iran kwa karibu miezi minane, huku kupanda kwa bei ya mafuta kukitarajiwa kuathiri uchaguzi wa katikati ya muhula nchini Marekani.

    “Tunaweza kufanya operesheni nyingine ndogo kama Epic Fury, au wao (Iran) wanaweza kufikia makubaliano,” Trump alisema katika mkutano wa kampeni huko Florida, Ijumaa, Oktoba 23.

    Aliongeza kuwa iwapo viongozi wa Iran wangekuwa na busara, wangesema: “Tuanze mazungumzo ya dhati.” Hata hivyo, Trump alisema ana shaka kama uongozi wa Iran una busara hiyo.

    Operation Epic Fury ndilo jina linalotumiwa na jeshi la Marekani kurejelea vita dhidi ya Iran.

    Katika hotuba yake, Trump alitetea tena uamuzi wake wa kuiondoa Marekani katika mkataba wa nyuklia wa Iran (JCPOA) wakati wa urais wake.

    Alidai kuwa Marekani iliharibu uwezo wa Iran wa kurutubisha urani kupitia operesheni ya Midnight Hammer, na baadaye kuisababishia Iran uharibifu zaidi kupitia operesheni ya Epic Fury.

    Trump alisema Marekani imeishambulia Iran kwa pigo kubwa, akidai kuwa uchumi wa nchi hiyo kwa sasa unakabiliwa na mojawapo ya hali ngumu zaidi duniani.

    Mapema Ijumaa, Trump alisema pia kuwa vita dhidi ya Iran vinaweza kumalizika hivi karibuni. Hata hivyo, aliibua swali la iwapo Washington inapaswa kujaribu kumaliza vita mara moja au kuviacha vikome taratibu.

    Trump amekuwa akitoa malengo na ratiba tofauti za kumaliza vita katika nyakati mbalimbali. Mapema Oktoba, alisema Marekani haitafanya shambulio jipya dhidi ya Iran kabla ya uchaguzi wa katikati ya muhula wa Bunge, uliopangwa kufanyika Novemba 3.

    Soma pia:

  9. Tetesi za soka Jumamosi: Aston Villa yafikiria kujiondoa kumsajili Garnacho

    d

    Aston Villa inaweza kujiondoa katika mpango wa kumsajili winga Alejandro Garnacho kutoka Chelsea kwa mkataba wa kudumu, iwapo kiwango cha raia huyo wa Argentina, mwenye umri wa miaka 22 hakitaboreka. Kwa sasa yuko Aston Villa kwa mkopo kutoka Chelsea.(Football Insider)

    Jadon Sancho, winga wa England mwenye umri wa miaka 26 ambaye kwa sasa hana klabu, anataka kukutana na kocha wa Getafe kabla ya kuamua kujiunga na timu hiyo ya Uhispania kwa mkataba hadi mwisho wa msimu. (Telegraph - subscription required)

    Brighton haitamuuza kiungo wa Paraguay, Diego Gomez, mwenye umri wa miaka 23, katika dirisha la usajili la Januari, licha ya kuwavutiwa Atletico Madrid na AC Milan.(Teamtalk)

    Antonio Rudiger, beki wa Ujerumani mwenye umri wa miaka 33, ameelekeza nguvu zake Real Madrid, licha ya kuhusishwa na Tottenham.(Bild - in German)

    Wanaowania kuchukua nafasi ya Michael Carrick kama kocha wa Manchester United wanaamini kuwa hali katika chumba cha kubadilishia nguo cha timu hiyo haidhibitiwi ipasavyo, huku wachezaji wakitajwa kuzungumza kupita kiasi. (Telegraph - subscription required)

    Liverpool iko tayari kutumia kipengele cha euro milioni 55 (pauni milioni 46) kumsajili beki wa Barcelona, Ronald Araujo, kwa mkataba wa kudumu, iwapo raia huyo wa Uruguay mwenye umri wa miaka 27 ataendelea kuonyesha kiwango kizuri akiwa kwa mkopo. (Marca - in Spanish)

    Mustakabali wa mshambuliaji wa Brazil, Endrick, katika Real Madrid bado haujafahamika. Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 20 anaweza kuondoka kwa mkopo mwezi Januari, huku AC Milan na Roma zikivutiwa naye, licha ya kocha Jose Mourinho hivi karibuni kupinga uwezekano huo. (Marca - in Spanish)

    Dani Olmo, mshambuliaji wa Uhispania mwenye umri wa miaka 28, hana mpango wa kuondoka Barcelona licha ya kuhusishwa na Bayern Munich. (Sky Sports Germany)

    Atletico Madrid iko tayari kutumia kipengele cha euro milioni 25 (pauni milioni 21) kumsajili mshambuliaji wa Canada, Jonathan David, kwa mkataba wa kudumu kutoka Juventus, ambako yuko kwa mkopo. Hata hivyo, uamuzi wa mwisho bado haujafanywa. (Sky Sports Germany), external

    Soma pia:

  10. TEC yaagiza misa maalumu kuwaombea waathiriwa wa uchaguzi Tanzania

    N

    Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) limeagiza kuadhimishwa kwa misa maalumu tarehe 29 Oktoba 2026, kwa ajili ya kuwaombea na kuwakumbuka watu waliouawa, kujeruhiwa na kuathiriwa na matukio ya uchaguzi mkuu nchini humo.

    Katika barua ya tarehe 23 Oktoba 2026, iliyosainiwa na Askofu wa Lindi na Rais wa TEC, Wolfgang Pisa, baraza hilo limesema misa hiyo itaadhimishwa katika parokia, vituo vya sala na taasisi za Kanisa Katoliki.

    “Tunaaomba Misa Takatifu ziadhimishwe kwa nia hizo; waliouawa, kupotea na kulilombea Taifa letu,” sehemu ya barua hiyo inasema.

    TEC imesema waumini wanaweza kutumia misa ya asubuhi ya kawaida au misa nyingine yoyote inayofaa, huku masomo ya siku hiyo yakitumika katika misa hizo.

    Baraza hilo pia limewataka waumini kuungana katika sala za kuombea amani, ukweli, haki, upendo na maridhiano nchini Tanzania.

    Katika barua hiyo, TEC imesisitiza umuhimu wa kuwaombea waliojeruhiwa, waliopoteza wapendwa wao na wote walioathiriwa na vurugu, pamoja na viongozi wa nchi na wananchi kwa ujumla.

    “Tunashukuru Misa hiyo ifanyike katika Parokia, vituo vya sala na Taasisi za Kanisa kadiri iwezekanavyo siku ya Alhamisi 29 Oktoba 2026,” barua hiyo imeeleza.

    Takriban watu 518 waliuawa wakati wa machafuko ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025 nchini Tanzania, tume ya uchunguzi ya serikali imebaini.

    Huku idadi ya waliofariki wakati wa vurugu ikiwa ni watu 518, idadi ya waliofariki wanaume 490 sawa na asilimia 94.6, na wanawake 28, sawa na asilimia 5.4.

    Haya yanajiri baada ya ripoti ya Jaji Chande kutaja sababu za kisiasa, ikiwemo madai ya Tume huru ya uchaguzi, changamoto za kiuchumi ajira ugumu wa maisha, kijamii kama vile kukosekana kwa uzalendo kuwa miongoni mwa vyanzo vya ghasia za uchaguzi wa Oktoba 29. Soma zaidi:

  11. Watu 7 hawajulikani walipo baada ya jengo kuporomoka Eastleigh, Kenya

    C

    Watu saba hawajulikani walipo baada ya jengo la ghorofa lililokuwa likijengwa kuporomoka katika eneo la Eastleigh, kaunti ya Nairobi, nchini Kenya huku juhudi za uokoaji zikiendelea.

    Waziri wa Mambo ya Ndani, Kipchumba Murkomen, amesema watu 67 waliokuwa wakifanya kazi ya ujenzi wakati jengo hilo lilipoporomoka wamehesabiwa wote.

    Kati yao, 66 walinusurika bila majeraha, huku mmoja akijeruhiwa na kulazwa hospitalini kwa matibabu ya ziada.

    Katika taarifa yake, Murkomen amesema maduka 11 yaliyokuwa kwenye ghorofa ya chini na kwenye orofa ya chini ya ardhi yalikuwa na watu wakati wa tukio hilo.

    “Juhudi za uokoaji zinaendelea, na timu imefanikiwa kuwasiliana na baadhi ya watu wanaoripotiwa kutoweka,” amesema Murkomen.

    Timu ya mashirika mbalimbali, ikiwemo Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF), Huduma ya Polisi ya Taifa, serikali ya kaunti ya Nairobi, Huduma ya Vijana kwa Taifa (NYS) na Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya, inaongoza shughuli za utafutaji na uokoaji.

    Murkomen amewataka watu ambao ndugu au jamaa zao hawajulikani walipo kufuatia kuporomoka kwa jengo hilo kutoa taarifa kwa Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya kupitia nambari ya dharura ya 1199.

    Aidha, amesema serikali inatoa msaada unaohitajika ili kuharakisha shughuli za uokoaji, huku mipango ya kutoa usaidizi wa kisaikolojia kwa waathiriwa na familia zilizoathirika ikiendelea.

    Chanzo cha kuporomoka kwa jengo hilo kitachunguzwa na taasisi husika za serikali ya kitaifa na kaunti kwa kushirikiana na mashirika ya kitaaluma. Murkomen amesema waliohusika watapasa kuwajibishwa baada ya uchunguzi kubaini chanzo cha tukio hilo.

    Jengo hilo liliporomoka Ijumaa alasiri wakati shughuli za kawaida zilikuwa zikiendelea kando yake.

  12. Hujambo na karibu kwa matangazo ya moja kwa moja ya tarehe 24/10/2026.