Moja kwa moja, Zaidi ya watu 1000 wakamatwa katika maandamano yaliyoitikisa Ufaransa

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Ufaransa imesema inakadiria kuwa watu 410,000 walishiriki katika maandamano ya hapo jana huku vyama vya wafanyakazi vikikadiria idadi hiyo kufikia takriban 800,000.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Beldeen Waliaula

  1. Mlipuko wasikika mjini Riyadh, Saudi Arabia,huku Uwanja wa Ndege ukifunguliwa tena

    .

    Milipuko imeripotiwa katika mji mkuu wa Saudi Arabia, Riyadh.

    Hii inajiri baada ya mamlaka za Saudi Arabia kutangaza kuwa safari za ndege zitaanza tena katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa King Khalid kuanzia leo.

    Uwanja wa Ndege wa King Khalid ulikuwa umefungwa kwa wiki mbili kufuatia mashambulizi ya mara kwa mara ya waasi Kihouthi.

    Tovuti ya Flightradar, ambayo inafuatilia safari za ndege kote ulimwenguni, pia iliripoti ndege ikipaa alfajiri ya leo kutoka Riyadh.

    Mamlaka ya Saudi Arabia bado haijaelezea chanzo cha mlipuko huo mpya katika mji mkuu.

    Wakati huo huo, msemaji wa jeshi la Wahouthi Yahya Saree, ameonya kwamba uwanja wa ndege bado "si salama" na wanaweza kutekeleza shambulio jingine.

    Wahouthi wamekuwa wakiulenga uwanja wa ndege katika mawimbi kadhaa tangu usitishaji mapigano kuporomoka.

    Shambulio la mapema mwezi huu liliwaua watu 13 na kuwajeruhi zaidi ya 300,hili likiwa shambulio lililosababisha vifo vingi zaidi nchini Saudi Arabia katika muongo mmoja.

    Soma pia:

  2. Iran: Kusitishwa kwa mapigano na Marekani kunategemea kutimizwa kwa masharti yaliyopendekezwa

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araqchi
    Maelezo ya picha, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araqchi

    Katika kauli zake za hivi karibuni, Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Iran, Abbas Araqchi, ameonya kuhusu uwezekano wa mzozo mpya kati ya nchi yake, Marekani na Israel, akisema kuwa "kusitishwa kwa mapigano kunaweza kuafikiwa tu iwapo uhasama utakomeshwa kabisa katika nyanja zote."

    Waziri huyo wa Mambo ya Kigeni, akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa "Kituo cha Nyaraka na Makumbusho ya Kamal Kharrazi," alisema kuwa suala hilo la kumaliza vita limejadiliwa na Marekani katika mazungumzo yote yaliyofanyika kwa upatanishi wa Pakistan na Qatar.

    Kamal Kharrazi, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa zamani wa Iran na mshauri wa kimataifa wa kiongozi wa zamani wa nchi hiyo, alifariki dunia kutokana na majeraha aliyopata katika shambulio la Marekani.

    Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Bw. Araqchi alionya dhidi ya "minong'ono ya uhasama kutoka kwa wachochezi wa vita" na akaonya kuwa Iran itasababisha gharama kubwa kwa upande mwingine.

    "Makombora ya Iran yaliangamiza makumi ya ndege za kivita za Marekani zikiwa ardhini," alisema.

    Kauli hizi zinakuja saa chache baada ya Donald Trump kuzungumzia tena uwezekano wa kuchukua hatua mpya za kijeshi dhidi ya Iran, akisema, "Labda italazimika mimi mwenyewe nimalize kazi hiyo, au labda watakubali." Trump Alisisitiza kuwa bado hana uhakika kuhusu matokeo yatakavyokuwa.

    Soma pia:

  3. Watu 10 wauawa na maduka kuporwa Kaskazini mwa Nigeria

    .

    Watu waliojihami na silaha wameivamia kijiji kimoja katika jimbo la Taraba, kaskazini-mashariki mwa Nigeria, na kuwaua takriban watu 10, na kupora maduka na kuchoma nyumba.

    Kuna hofu kwamba idadi halisi ya waliofariki huenda ikawa ya juu Zaidi.

    Walioshuhudia tukio hilo wanasema takriban watu 20 wameuawa, huku shirika moja lisilo la kiserikali eneo hilo likikadiria kuwa idadi hiyo inaweza kufikia 50.

    Inaripotiwa kuwa washambuliaji hao walifika katika kijiji cha Binnari, eneo la Karim Lamido, wakiwa kwenye pikipiki muda mfupi baada ya sala za mchana za Waislamu siku ya Ijumaa. Walitekeleza mashambulizi yaliyodumu kwa muda was aa nne.

    Polisi wanasema wanawatafuta wahalifu au katika misitu iliyokaribu.

    Hata hivyo, shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limeishutumu serikali ya Nigeria kwa kushindwa kulinda jamii za vijijini.

    Nigeria inaendelea kukabiliwa na mashambulizi ya mara kwa mara ya makundi yenye silaha katika maeneo mbalimbali, yakiwemo maeneo ya kaskazini-magharibi, kaskazini-mashariki na katikati mwa nchi hiyo.

    Soma pia:

  4. Trump amjibu Obama na kudai utawala wake uliiwezesha Iran kupata silaha za nyuklia

    Rais wa Marekani Donald Trump
    Maelezo ya picha, Rais wa Marekani Donald Trump

    Rais wa Marekani Donald Trump amemshambulia vikali rais wa zamani Barack Obama, akijibu ukosoaji wake kwa kusema kuwa Obama aliipa Iran mabilioni ya dola wakati wa utawala wake, na kuiwezesha nchi hiyo kupata silaha za nyuklia.

    “Obama alikuwa kiongozi dhaifu. Aliipa Iran mabilioni ya dola na kufungua njia kwa nchi hiyo kupata silaha ya nyuklia,” alisema Trump kupitia mtandao wake wa kijamii wa Truth Social.

    Rais huyo aliongezea kuwa Obama alikuwa rais asiyekuwa na uwezo, baada ya kuwaunga mkono Hillary Clinton katika uchaguzi wa mwaka 2016 na Kamala Harris katika uchaguzi wa mwaka 2024, ila wagombea wote wawili walishindwa katika chaguzi hizo.

    Katika hotuba zake za kampeni hapo jana, Barack Obama alikosoa sera za serikali ya Trump, ikiwemo vita dhidi ya Iran. Alisema kuwa makubaliano ya nyuklia na Iran yaliyoafikiwa wakati wa utawala wake yalikuwa yameizuia nchi hiyo kupata silaha za nyuklia bila hata kurusha kombora moja.

    Soma pia:

  5. Israel kufunga vivuko vya Ukingo wa Magharibi wakati wa uchaguzi

    .

    Vivuko vyote vya mpakani vya kuingia na kutoka eneo la Ukingo wa Magharibi vitafungwa siku ya Jumanne wakati wa uchaguzi nchini Israel, jeshi la nchi hiyo limesema.

    Aidha, wafanyakazi wa Kipalestina hawataruhusiwa kuingia katika makazi yoyote ya walowezi wa Israel.

    Vikwazo hivyo vinakuja wakati Israel imeimarisha operesheni zake za usalama katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kimabavu, baada ya kuuawa kwa wanajeshi wawili wa Israel na wanamgambo wa Kipalestina katika eneo hilo.

    Jeshi la Israel (IDF) lilitangaza kupiga marufuku kuingia na kutoka kwa wafanyakazi wa Kipalestina katika maeneo yote ya Yudea na Samaria pamoja na Bonde la Mto Jordan, yakiwemo maeneo ya viwanda. Pia, vivuko vyote vya mpakani vitafungwa siku ya Jumanne.

    Kabla ya shambulio lililoongozwa na Hamas dhidi ya Israel tarehe 7 Oktoba 2023, zaidi ya wafanyakazi 100,000 wa Kipalestina waliruhusiwa kuingia Israel kufanya kazi. Tangu wakati huo, ni idadi ndogo tu ambayo walipewa vibali vyao vya kufanya kazi.

    Soma pia:

  6. Brazil kupiga kura katika duru ya pili ya uchaguzi wa urais wenye ushindani mkali

    .

    Raia wa Brazil wanatarajiwa kupiga kura hii leo, kumchagua rais wao mpya, katika duru ya pili ya uchaguzi uliokumbwa na ushindani mkali.

    Chaguo la raia wa Brazil ni kati ya rais wa sasa mwenye umri wa miaka 80, Luiz Inácio Lula da Silva, wa mrengo wa kushoto, ambaye anawania muhula wa nne usiofuatana madarakani, na seneta wa mrengo wa kulia Flávio Bolsonaro, mwenye umri wa miaka 45.

    Bolsonaro ni mwanawe rais wa zamani wa mrengo wa kulia, Jair Bolsonaro, ambaye anatumikia kifungo cha miaka 27 jela kwa kupanga njama ya kupindua serikali baada ya kushindwa katika uchaguzi uliopita wa mwaka wa 2022.

    Flávio Bolsonaro ndiye anayeonekana kuwa na nafasi kubwa ya kushinda uchaguzi huo, au kupoteza ushindi alioukaribia, baada ya kuongoza katika duru ya kwanza ya upigaji kura iliyofanyika Oktoba 4. Rais wa Marekani Donald Trump alielezea matokeo hayo kuwa ushindi “mkubwa sana.”

    Aidha katika duru ya kwanza ya uchaguzi huo, hakuna kiongozi aliyepata Zaidi ya asilimia 50 za kura katika uchaguzi uliofanyika mwezi Oktoba huku duru ya pili ya uchaguzi huo ukiwa na ushindani mkali tayari.

    Soma pia:

  7. Obama amkosoa Trump kuhusu vita vya Iran na kupanda kwa gharama ya maisha

    Picha ya Rais wa zamani wa Marekani, Barrack Obama
    Maelezo ya picha, Picha ya Rais wa zamani wa Marekani, Barrack Obama

    Rais wa zamani wa Marekani, Barack Obama, ameikosoa serikali ya Donald Trump kuhusu vita vya Iran na kupanda kwa bei za bidhaa muhimu.

    Obama aliikosa serikali ya Marekani alipokuwa akifanya kampeni ya kuwaunga mkono wagombea wa chama cha Democratic katika uchaguzi wa katikati ya muhula nchini Marekani.

    “Uchaguzi huu ndio fursa yetu ya mwisho na bora zaidi ya angalau kudhibiti baadhi ya mambo yasiyo na busara yanayofanywa na serikali hii,” Obama aliwaambia wananchi waliohudhuria mkutano huo wa kampeni katika jimbo la Ohio.

    Aidha, Rais wa Marekani Donald Trump,ametetea sera za serikali yake kuhusu uhamiaji na ushuru wa bidhaa katika mkutano wa kampeni alioufanya katika jimbo la Georgia.

    Uchaguzi wa katikati ya muhula, utakaofanyika tarehe 3 mwezi Novemba, utaamua ni chama gani kitakachodhibiti Bunge la Marekani kwa kipindi kilichosalia cha muhula wa Trump. Matokeo hayo yataathiri pia urahisi wa rais kutekeleza mipango yake.

    Upigaji kura wa mapema tayari umeanza, na Trump alipiga kura yake siku ya hapo jana katika jimbo la Florida, akiwa ameandamana na mkewe, Melania Trump.

    Soma pia:

  8. Zaidi ya watu 1000 wakamatwa Ufaransa katika maandamano ya kupinga kupanda kwa gharama ya maisha

    .

    Maafisa wa usalama nchini Ufaransa, wamesema wamewakamata Zaidi ya watu elfu moja, baada ya mamia ya maelfu ya watu kushiriki maandamano nchini humo, ambayo yalishuhudia makabiliano makali ya polisi hapo jana.

    Baada ya siku nzima ya maandamano yaliyokuwa kwa kiasi kikubwa ya amani, polisi walitumia mabomu ya kutoa machozi na magari ya kunyunyizia maji kuwatawanya waandamanaji katika miji kadhaa, ikiwemo Paris.

    Hata hivyo, vizuizi vya barabarani vilichomwa moto katika mji wa Marseille, huku baadhi ya watu wakivunja mbao zilizokuwa zimefunika duka moja katika mji wa Bordeaux.

    Hadi kufikia sasa, maafisa wa usalama wamefanikiwa kuzuia ghasia na uporaji ikilinganishwa na kiwango kilichoshuhudiwa mwishoni mwa wiki iliyopita, ambapo kulishuhudiwa matukio mabaya zaidi ya uharibifu wa amani katika historia ya kisasa ya Ufaransa.

    Wizara ya Mambo ya Ndani ya Ufaransa imesema inakadiria kuwa watu 410,000 walishiriki katika maandamano ya hapo jana huku vyama vya wafanyakazi vikikadiria idadi hiyo kufikia takriban 800,000.

    Mapema wiki hii, Rais Emmanuel Macron alikuwa ameamuru kuwa maandamano yatakayoruhusiwa ni yale tu yaliyoandaliwa na vyama vya wafanyakazi vinavyotambuliwa rasmi.

    Katika siku za hivi karibuni, mamia ya watu wamehukumiwa vifungo vya jela kwa makosa ya uharibifu wa mali, uchomaji moto na uporaji, kufuatia kusikilizwa kwa kesi zao kupitia taratibu za haraka za mahakama.

    Soma pia:

  9. Hujambo na karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja Jumapili ya leo