Mzozo kati ya Trump na Papa hadharani, utamgharimu vipi kisiasa?

S

Chanzo cha picha, Getty Images

Muda wa kusoma: Dakika 5

Si jambo jipya kwa Rais Donald Trump kukosolewa na viongozi wa kanisa Katoliki.

Sera zake kali za uhamiaji, ambazo wafuasi wake walizikumbatia wakati wa kampeni na kuzipokea vizuri, zililaaniwa vikali na viongozi wa Kanisa.

Kwa miezi kadhaa, sera hizo zimewatenga viongozi wa kanisa Katoliki nchini Marekani pamoja na Wakristo wa kawaida.

Hata hivyo, mambo yamekuwa tofauti tangu siku chache zilizopita, pale Trump alipojipiga picha maarufu (selfie) akiwa na Papa Leo na kuchapisha picha iliyotengenezwa kwa teknolojia ya AI ikimuonyesha kama Yesu Kristo.

Jambo la kushangaza ni kwamba baadhi ya wakosoaji wake ni miongoni mwa Wakatoliki waaminifu sana na wanaofuata kwa karibu misingi ya Kanisa lenyewe.

Watu wengi hawajakerekwa tu na dhihaka ya hadharani ya Donald Trump dhidi ya Papa, bali pia hawakubaliani na vita ya Marekani dhidi ya Iran.

Hata hivyo, Vatican inaeleza kwamba kile tulichoshuhudia katika wiki za hivi karibuni si vita kati ya Papa Leo na Rais Trump, bali ni msimamo thabiti wa Papa kusimamia imani yake katika kupinga vita hiyo.

Malalamiko kuhusu jinsi Trump alivyommzungumzia Papa wa kwanza kutoka Marekani, akimwita "mvumilivu kwa watenda maovu," pamoja na picha ya AI, yamewafanya Wakatoliki wengi wa kihafidhina kubadilisha mitazamo yao tangu vita ilipoanza wiki sita zilizopita.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Katika hatua isiyo ya kawaida, hakuna kiongozi mkuu wa Kanisa Katoliki nchini Marekani ambaye ameunga mkono hadharani vita dhidi ya Iran. Hata Robert Barron, Askofu wa Winona-Rochester, mfuasi mkuu wa Trump, amemtaka rais wa Marekani kuomba msamaha kwa Papa kwa matamshi yake ya hasira.

"Ninaomba kwamba haya yote yawafanye watu waelewe kwamba hatumtazami rais, au wale walio na pesa nyingi au silaha nyingi. Tunamlenga Kristo kila wakati," Askofu Joseph Strickland alisema.

Haya ni maneno ya mtu ambaye mwaka jana alihudhuria maombi ya kuwekwa wakfu kwa makazi ya rais ya Mar-a-Lago.

Mwaka wa 2024, Askofu Strickland alitoa hotuba kuu katika Mkutano wa Kisiasa wa Conservative (CPAC) ambapo Donald Trump alikuwa mgeni wa heshima. Mwaka wa 2020, alitoa hotuba kwa wafuasi wa Trump waliokuwa wakiandamana kudai matokeo ya uchaguzi yabatilishwe.

Askofu Strickland alikuwa mfuasi mkuu wa Donald Trump katika mambo yote.

Msimamo wake wa kisiasa, na upinzani wake wa wazi kwa marehemu Papa Francis, kulisababisha kuondolewa kwake katika kiti cha maaskofu cha Tyler, Texas.

Hata hivyo, wakati wa mvutano kati ya Ikulu ya White House na Vatican kuhusu vita nchini Iran na Mashariki ya Kati, ametoa kauli za kujitenga na utawala.

"Siamini kwamba vita hivi vinastahili kuwa vita vya kweli. Ninamuunga mkono Baba yetu na sauti yake inayoita amani. Hii si siasa, hii ni ukweli unaotegemea huruma," aliiambia BBC, akiongeza kuwa idadi ya watu wanaokufa na mateso kwa raia wasio na hatia hufanya vita hivi kuviita vita "vya kweli".

Zaidi ya hayo, analaani namna Ikulu ya White House inavyochukulia vita hivi, na anawataka wengine kujiepusha na kufanya vivyo hivyo.

"Haikubaliki kabisa kwamba dini inatumika kuhalalisha makosa... kutumia dini kuhalalisha mashambulizi ya mabomu ni kinyume cha imani," anasema Askofu Strickland.

Alipoulizwa kuhusu madai ya dhihaka ya Trump kwa Papa Leo na kile kilichoonekana kama picha ya "Yesu aliyetengenezwa kwa teknolojia ya AI", ambapo Trump alisema alidhani alikuwa daktari badala ya Yesu, Askofu Strickland alisema ilikuwa "jukumu" lake kumkumbusha rais wa Marekani Injili ya Mathayo. Alilenga kifungu kinachofundisha kwamba mamlaka yote ni ya Kristo, si mwanadamu.

"Wakati viongozi wa dunia wanaposahau ukweli huu, kila kitu huwa kibaya sana," anasema.

Mabadiliko haya ya namna Wakatoliki wanavyomchukulia Rais Trump ni changamoto kwa sera zake, kutokana na jinsi uungaji mkono wake kwa uchaguzi wa 2024 miongoni mwa kundi hili umeongezeka kwa kiasi kikubwa.

Kulingana na Pew Research Center, hali si rahisi. Katika uchaguzi huo, suala la ubaguzi wa rangi lilichukua nafasi kubwa, ambapo asilimia 62 ya Wakatoliki wazungu walimpigia kura Donald Trump, ikilinganishwa na asilimia 37 kwa Kamala Harris, huku asilimia 41 ya Wakatoliki wa asili ya Kihispania walimpigia Trump, ikilinganishwa na asilimia 58 kwa Harris.

Hata hivyo, hali hii inaonyesha kuwa kwa ujumla Wakatoliki wanaelemea chama cha Republican, lakini tofauti zao za ndani zinaonekana wazi.

s

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Askofu Joseph Strickland katika Maandamano ya "March for Life" mjini Washington mwaka 2024.

Historia inaonyesha kwamba kwa Wakatoliki wengi nchini Marekani, siasa huja kabla ya imani. Wamegawanyika kulingana na misimamo ya vyama vyao, kwa mujibu wa Greg Smith, mkurugenzi wa masomo ya dini katika Kituo cha Utafiti cha Pew.

Wakatoliki wa Marekani wamegawanyika sana kuhusu masuala muhimu kama vile utoaji mimba na uhamiaji. Ni nadra kuona Wakatoliki wa jadi na wahafidhina wakikubaliana kuhusu suala la vita vya Iran.

Hali hii inaonekana pia katika namna Wakatoliki wanavyomwona kiongozi wa Kanisa Katoliki. Papa Francis anapendwa zaidi na Wakatoliki wa Democrats kuliko wale wa Republican, wakati Papa Leo anapendwa na pande zote mbili, kulingana na Pew.

Papa Francis mara nyingi huonekana kama mtu wa mabadiliko ya ghafla, wakati mwingine akigongana na Wakatoliki wanaopendelea desturi za jadi kwa mfano, kwa kupunguza matumizi ya Misa ya Kilatini, jambo ambalo Papa Leo alilihalalisha.

Papa pia ni mtu anayeweza kukosolewa, kulingana na Peter Wolfgang, mkurugenzi mtendaji wa Family Institute of Connecticut, sauti kubwa ya Wakatoliki wanaopendelea mila za jadi.

"Papa ni Papa, na tunampa heshima inayostahili, lakini sidhani kama Ukatoliki unataka waumini wawe kama mizimu isiyo na uhai. Sisi ni watu walio hai, wenye ufahamu na wanaofikiri," anasema.

Wolfgang, mfuasi wa tahadhari wa Trump aliyewahi kutaka sheria za utoaji mimba zibatilishwe, sasa amekuwa mfuasi thabiti. Anaunga mkono sana uhamishaji wa lazima wa wahamiaji (deportations) na anakubaliana na Makamu wa Rais JD Vance kuhusu maadili ya Kikatoliki na uzalendo.

Hata hivyo, sasa amekuwa mkosoaji mkubwa wa kauli za Rais Trump kuhusu Papa Leo.

"Rais Trump haelewi jinsi Kanisa Katoliki linavyofanya kazi. Papa si tu kiongozi wa dola, bali ni Mtume wa Yesu. Kumshambulia ni kushambulia Kanisa lenyewe. Kadiri anavyomshambulia Papa, ndivyo atakavyopoteza wapiga kura wake Wakatoliki," Wolfgang alimwambia BBC.

Peter Wolfgang anasema imani yake ilimfanya akabiliane na maaskofu wa Kikatoliki walipokosoa sera za uhamiaji za Trump, lakini ni imani hiyo hiyo iliyomfanya ajiingize kwenye "vita" hii.

Katika maandishi yake, Peter Wolfgang mara nyingi hukosoa sana upande wa mageuzi ndani ya Kanisa Katoliki, lakini anaona suala la Iran kwa namna fulani likiunganisha wapinzani, hasa kutokana na Papa Leo kulaani vita kwa nguvu.