Trump atishia 'kuharibu kabisa' viwanda vya nishati Iran ikiwa makubaliano hayatafikiwa 'haraka'
Wakati huo huo, mashambulizi yanaendelea nchini Iran, Lebanon, na eneo lote - huku kiwanda cha kusafisha mafuta nchini Israel kikichomwa moto na vifusi vya kombora lililozuiwa.
Muhtasari
- "Tuko katika hatari kwa kiasi fulani lakini tunazoea": Maisha mpakani mwa Israel na Lebanon
- Shirika la Ndege Tanzania laendelea kuendeshwa kwa hasara
- Marekani iko kwenye "mazungumzo muhimu" na utawala mpya wa Iran "ulio na busara zaidi" - Trump
- "Vita hivi si vyetu na hatutajiingiza," yasema Uingereza
- "Tuko katika hatari kwa kiasi fulani lakini tunazoea": Maisha mpakani mwa Israel na Lebanon
- Iran yapendekeza mfumo mpya wa kudhibiti Mlango Bahari wa Hormuz
- Ukweli unaozunguka picha ya ndege ya Marekani ilivyovunjwa vipande viwili kambini Saudia
- Shambulio la makombora lapiga kambi ya Jeshi la Iraq
- Israel yazidisha mashambulizi Beirut huku oparesheni ya ardhini ikiendelea
- Iran yathibitisha kifo cha kamanda wa Jeshi la wanamaji la IRGC
- Wanajeshi sita wa Israel wajeruhiwa nchini Lebanon
- Trump asema 'kumekuwa na mabadiliko ya serikali' nchini Iran
- Mkuu wa Jeshi la Myanmar Min Aung Hlaing ateuliwa kuwa rais
- Indonesia yathibitisha kuuawa kwa mwanajeshi wake nchini Lebanon
- Trump ana mpango wa 'kuchimba urani ya Iran' - Wall Street Journal
- 'Mikono iliyojaa damu': Papa Leo 'awakosoa' wale wanaohusika katika vita
- Mafuta yapanda zaidi ya $115 huku hisa za Asia zikishuka thamani
- Trump asema Marekani inaweza 'kuchukua mafuta nchini Iran' na kukiteka Kisiwa cha Kharg
Moja kwa moja
Ambia Hirsi, Martha Saranga & Asha Juma
“Tuko katika hatari kwa kiasi fulani lakini tunazoea”: Maisha mpakani mwa Israel na Lebanon

Chanzo cha picha, Gabriella Kopellowitz
Wakati Israel ikiendelea kusonga mbele kusini mwa Lebanon, BBC imezungumza na wakazi wa mji wa Metula ulioko upande wa Israel, karibu na mpaka.
Gabriella Kopellowitz ni mfanyakazi wa kijamii mwenye umri wa miaka 28 anayefanya kazi katika mji huo. Anasema, “Tuko karibu sana na mpaka kiasi kwamba tunaweza kuona vijiji vilivyoko ndani ya Lebanon kutoka hapa.”
Anaongeza kuwa kuna ving’ora vinavyolia takribani mara tano kwa siku, vikitoa tahadhari ya makombora au roketi zinazokuja.
“Makombora yanapokuja kutoka Iran, tunakuwa na takribani dakika tano za kukimbilia kwenye hifadhi ya kujikinga dhidi ya mabomu, lakini yanapokuja kutoka Hezbollah tunakuwa na chini ya dakika moja.”
Kama mfanyakazi wa kijamii, Gabriella amekuwa akisaidia kuwahamisha watu ambao nyumba zao zimeharibiwa na makombora, na pia huzunguka mjini akiwapelekea chakula wazee ambao hawawezi kutoka nje.
Anasema mji huo ni tulivu zaidi kuliko kawaida.
“Familia nyingi zimeondoka – si jambo la kufurahisha kujua kwamba Hezbollah wanataka kukulenga,” anasema Gabriella.
“Kwa kiasi fulani tuko katika hatari hapa Metula,” anaongeza, lakini pia anasema, “unazoea. Mimi siogopi. Mara nyingi makombora hayo huzuiwa kabla hayajafika.”
Unaweza pia kusoma:
Shirika la Ndege Tanzania laendelea kuendeshwa kwa hasara

Chanzo cha picha, AIR TANZANIA
Kwa mujibu wa taarifa iliyowasilishwa leo na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Dkt. Charles Kichere, Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) linaendelea kujiendesha kwa hasara.
Amesema shirika hilo limepata hasara ya zaidi ya shilingi bilioni 191 ndani ya kipindi cha mwaka mmoja. Kwa ujumla, tangu kuanzishwa kwake, shirika hilo limekusanya hasara ya takribani shilingi bilioni 748.
Katika kipindi hicho cha mwaka mmoja, shirika limelipa zaidi ya shilingi bilioni 310 kwa abiria kama fidia kutokana na safari zilizositishwa au kuahirishwa. Hasara hiyo imechangiwa kwa kiasi kikubwa na gharama za uendeshaji kuwa kubwa kuliko mapato yanayopatikana.
Aidha, matumizi yasiyoridhisha ya ndege ya mizigo yameelezwa kuwa miongoni mwa sababu za hasara. Katika miezi ya hivi karibuni, ndege hiyo ilifanya safari nyingi zisizo na tija na hatimaye kusimamishwa, hali iliyoongeza kiwango cha hasara.
Akizungumzia mashirika mengine ya umma yanayoendeshwa kwa hasara, Dkt. Kichere alilitaja Shirika la Reli Tanzania (TRC).
Alisema licha ya mapato ya reli ya kisasa (SGR) kuongezeka, reli ya zamani imeendelea kupata hasara kutokana na kuongezeka kwa ajali. Ndani ya mwaka mmoja, jumla ya ajali 328 zimeripotiwa, na kusababisha uharibifu wa miundombinu.
Kuhusu hali ya deni la taifa, Dkt. Kichere alisema limeongezeka hadi kufikia shilingi trilioni 110 likijumuisha deni la ndani na la nje. Ndani ya mwaka mmoja, deni hilo limeongezeka kwa zaidi ya shilingi trilioni 12, sawa na asilimia 13.4.
Ongezeko hilo limetokana na kuongezeka kwa mikopo ya nje pamoja na kushuka kwa thamani ya shilingi ya Tanzania dhidi ya dola ya Marekani.
Hata hivyo, alibainisha kuwa pamoja na ongezeko hilo, deni la taifa bado ni himilivu kwani lipo katika kiwango cha asilimia 40.7, ambacho ni chini ya ukomo wa asilimia 55.
Akisoma taarifa ya ukaguzi wa hesabu za vyama vya siasa, Mkaguzi Mkuu alisema vyama viwili CUF na NRA vimepata hati zenye mashaka kutokana na kutokuwasilisha nyaraka zote zinazohitajika. Wakati huo huo, chama kikuu cha upinzani, CHADEMA, hakijakaguliwa kutokana na mashauri yaliyopo mahakamani yanayohusiana na mali za chama hicho.
Kwa upande wake, Rais Samia Suluhu Hassan amesema serikali itafanyia kazi mapendekezo yote yaliyotolewa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali haraka iwezekanavyo.
Baada ya kusomwa kwa taarifa hizo, zinatarajiwa kuwasilishwa bungeni ndani ya siku saba kwa ajili ya kujadiliwa na kutolewa mapendekezo.
Unaweza kusoma pia:
Donald Trump: Marekani iko kwenye “mazungumzo muhimu” na utawala mpya wa Iran “ulio na busara zaidi”

Chanzo cha picha, Reuters
Donald Trump amesema kuwa Marekani iko katika “mazungumzo muhimu” na utawala mpya wa Iran ambao, kulingana na rais huyo, unaweza “kukomesha operesheni za kijeshi za Marekani nchini Iran.”
Kupitia chapisho lake kwenye mtandao Truth Social, Trump aliandika: “Marekani iko katika mazungumzo muhimu na UTAWALA MPYA, NA WENYE BUSARA ZAIDI ili kumaliza operesheni zetu za kijeshi nchini Iran.
Hata hivyo, ametishia "kuharibu kabisa" eneo la kimkakati la Iran la Kisiwa cha Kharg ikiwa makubaliano hayatafikiwa hivi karibuni.
“Maendeleo makubwa yamepatikana, lakini ikiwa kwa sababu yoyote makubaliano hayatapatikana hivi karibuni, ingawa huenda yakapatikana na ikiwa Mlango-Bahari wa Hormuz hautafunguliwa mara moja kuruhusu biashara, tutahitimisha ‘uwepo’ wetu mzuri nchini Iran kwa kulipua na kuharibu kabisa mitambo yao yote ya kuzalisha umeme, visima vya mafuta na Kisiwa cha Kharg (na huenda pia mitambo yote ya kuondoa chumvi kwenye maji ya bahari!), ambayo kwa makusudi bado hatujaigusa.
“Hii itakuwa ni kulipiza kisasi kwa wanajeshi wetu wengi, na wengine, ambao Iran imewaua na kuwachinja katika kipindi cha miaka 47 cha ‘Utawala wa Hofu’ uliopita nchini Iran.
Unaweza kusoma pia:
“Vita hii si yetu na hatutajiingiza,” yasema Uingereza

Chanzo cha picha, PA Media
Waziri mkuu wa Uingereza Keir Starmer amesisitiza kuwa wanajeshi wa Uingereza hawatapelekwa nchini Iran.
Alipoulizwa na waandishi wa habari asubuhi hii kama anafikiria kupeleka wanajeshi wa Uingereza kupigana vita Mashariki ya Kati, Starmer alisema: “Hii si vita yetu na hatutajiingiza.”
Aidha waziri mkuu Starmer aliendelea kutetea msimamo wake kuhusu mzozo huo, akisema kuwa Uingereza inachukua “hatua za kujilinda” kulinda “maisha ya Waingereza, maslahi ya Uingereza na, bila shaka, washirika wetu katika eneo hilo.”
Starmer amesema Uingereza itaendelea kulinda maslahi yake na kushiriki katika jitihada za kufungua tena Mlango-Bahari wa Hormuz, lakini akaongeza: “Hatutaingizwa kwenye vita hii.”
Unaweza pia kusoma:
Iran yapendekeza mfumo mpya wa kudhibiti Mlango Bahari wa Hormuz

Chanzo cha picha, Corbis via Getty Images
Mbunge wa Iran, Alaeddin Boroujerdi, amesema kuwa mpango mpya wa bunge kuhusu mlango bahari wa Hormuz unatarajiwa kupitishwa hivi karibuni.
Kwa mujibu wa Boroujerdi, chini ya “mfumo mpya” unaopendekezwa, hakuna meli itakayoruhusiwa kupita katika mlango huo muhimu bila kupata kibali kutoka Iran.
Aidha, Iran inapanga kuanzisha mfumo wa kutoza ushuru kwa meli zinazopita katika eneo hilo.
Alieleza kuwa kulinda usalama na kutoa huduma kwa meli kunahitaji gharama, hivyo ni muhimu kuweka mfumo wa kukusanya kodi ya usafirishaji.
Katika hatua nyingine, mbunge huyo alisema kuwa “wakati umefika” kwa Iran kujiondoa katika mkataba wa kuzuia usambazaji wa silaha za nyuklia, Treaty on the Non-Proliferation of Nuclear Weapons (NPT).
Alidai kuwa mkataba huo umepoteza umuhimu wake kufuatia mashambulizi yaliyolenga miundombinu ya nyuklia ya Iran, ambayo yalihusishwa na Israel pamoja na Marekani.
Ukweli unaozunguka picha ya ndege ya Marekani ilivyovunjwa vipande viwili kambini Saudia

Chanzo cha picha, Facebook
Picha zilizothibitishwa zinaonyesha ndege ya Marekani yenye kutoa amri katika uwanja wa vita ikiwa imeharibiwa katika kambi ya kijeshi nchini Saudi Arabia.
Picha hizo zinaonekana kusambazwa kwa mara ya kwanza kwenye ukurasa wa Facebook wenye habari za kijeshi za Marekani.
Zinaonyesha ndege ya E-3 Sentry ambayo imevunjwa vipande viwili.
Tumethibitisha kuwa picha hizo zilipigwa katika kambi ya jeshi la wanahewa ya Prince Sultan yapata kilomita 100 (maili 62) kusini-mashariki mwa mji mkuu wa Saudi Arabia Riyadh.
Kile kinachoonekana kwenye picha hizo, ikiwa ni pamoja na nguzo za chuma, vitengo vya kuhifadhia na alama kwenye maeneo ya lami, vinaendana na picha za setilaiti.
Jeshi Kuu la Marekani bado halijatoa maoni yake hadharani kuhusu tukio hilo. BBC imeomba maoni.
Siku ya Ijumaa afisa mmoja wa Marekani aliiambia Reuters kwamba wafanyakazi 12 wa Marekani walikuwa wamejeruhiwa, wawili kati yao wakiwa wamejeruhiwa vibaya katika shambulizi la kijeshi la Iran kwenye kambi ya wanajeshi.
Gazeti la Wall Street Journal liliripoti kwamba takriban ndege mbili za Marekani za kujaza mafuta pia ziliharibiwa.
Siku ya Jumapili shirika la habari la Fars linalohusishwa na Kikosi cha Jeshi la Iran la IRGC lilisema ndege isiyo na rubani ya Shahed ilishambulia ndege ya E-3.
BBC Verify pia imeona ndege aina ya E-3 katika eneo hili katika picha ya setilaiti iliyopigwa tarehe 11 Machi. Hatuwezi kusema kama ni ndege hiyo hiyo
Katika moja ya picha zilizothibitishwa, nambari ya mkia wa ndege inaonekana. Kwa kutumia hii tuliangalia tovuti ya kufuatilia ndege ya Flightradar24 ambayo ilionyesha ilikuwa ikipaa angani karibu na kambi ya kijeshi mnamo Machi 18.
Picha ya setilaiti iliyopigwa Ijumaa inaonekana kuonyesha moto kwenye eneo la kuegesha ndege katika kambi ya kijeshi, yapata mita 1,600 (futi 5,200) mashariki mwa E-3.
Haijulikani wazi kama hii ilikuwa sehemu ya shambulizi lile lile ambapo ndege inaonekana kwenye picha hizi iliharibiwa.

Chanzo cha picha, Getty Images
Boeing E-3 Awacs - imetokana na ndege ya Boeing 707 na ina diski ya rada inayozunguka iliyowekwa nyuma ya mwili wa ndege.
Rada hii inaruhusu kugundua na kufuatilia maeneo yanayoweza kulengwa katika masafa marefu ili kutoa onyo la mapema kuhusu vitisho vinavyoweza kutokea wakati wa vita.
Ndege hiyo inatoa "taarifa kwa makamanda wanaoendesha shughuli zao angani ili kupata na kudumisha udhibiti wa vita vya anga", kulingana na tovuti ya USAF.
Ndege ya kwanza ya aina hiyo ilianza kutumika mwaka wa 1977 na imeripotiwa kwamba E-3 inatarajiwa kuendelea kufanya kazi na USAF hadi 2035.
Soma zaidi:
Shambulio la makombora lapiga kambi ya Jeshi la Iraq

Chanzo cha picha, Iraqi Ministry of Defence
Wizara ya ulinzi ya Iraq imesema kuwa makombora yamelenga kambi ya anga ya Mohammed Alaa, na kuharibu ndege moja ya Jeshi la Iraq.
Hakuna vifo vilivyoripotiwa katika shambulio hilo lililotokea alfajiri ya leo karibu na Baghdad International Airport.
Katika taarifa iliyotolewa kupitia tovuti yake, wizara ya ulinzi ya Iraq imelaani tukio hilo na kulielezea kama “kitendo cha woga na cha kihalifu kinacholenga taasisi ya kijeshi na uwezo wake wa ulinzi”.
Mapema leo, Jeshi la Syria, lilisema limefanikiwa kuzima shambulio kubwa la ndege zisizo na rubani lililolenga vituo vyake kadhaa vya kijeshi karibu na mpaka wa Iraq, kwa mujibu wa shirika la habari la serikali la SANA.
Kamandi ya operesheni ya jeshi hilo iliambia SANA kuwa ndege nyingi zisizo na rubani zilidunguliwa na kuangushwa kabla ya kufikia maeneo yaliyokusudia kulengwa.
Israel yazidisha mashambulizi Beirut huku oparesheni ya ardhini ikiendelea

Chanzo cha picha, Reuters
Jeshi la Israel limetangaza kuwa limeanza kushambulia miundombinu ya kundi la Hezbollah katika mji mkuu wa Lebanon, Beirut.
Picha zilizopigwa asubuhi zinaonyesha moshi ukifuka kutoka katika vitongoji vya kusini mwa mji huo.
Jeshi la Ulinzi la Israel, (IDF) limesema kuwa linalenga “miundombinu ya kigaidi” ya kundi hilo linaloungwa mkono na Iran.
Vyombo vya habari vya Lebanon pia vimeripoti wimbi jipya la mashambulizi ya anga ya Israel katika eneo la kusini mwa Beirut.
Zaidi ya watu milioni moja wamelazimika kuhama makazi yao nchini Lebanon, huku vita vinavyoihusisha Marekani na Israel dhidi ya Iran vikiendelea kuathiri eneo pana la mashariki ya kati.
Mtoto mmoja aliyezungumza na BBC alisema anahisi “aibu” kulala barabarani baada ya familia yake kulazimika kukimbia makazi yao mjini Beirut.
Unaweza pia kusoma:
Iran yathibitisha kifo cha kamanda wa Jeshi la wanamaji la IRGC

Chanzo cha picha, Tasnim News Agency
Iran imethibitisha rasmi kifo cha kamanda wa jeshi la wanamaji kikosi cha (IRGC) Alireza Tangsiri, siku nne baada ya Israel kudai kuwa ilimlenga katika shambulio.
Katika taarifa iliyotolewa na IRGC kupitia shirika la habari la Tasnim News Agency, ilielezwa kuwa Tangsiri alikuwa akiratibu vikosi na kuimarisha ulinzi wa visiwa na maeneo ya pwani, na kwamba alifariki kufuatia majeraha makubwa aliyopata.
Taarifa hiyo iliongeza kuwa vikosi vya jeshi la majini la IRGC, licha ya kutokuwepo kwa kamanda wao katika siku za hivi karibuni, viliendelea kutoa “mashambulizi makali” na kuimarisha udhibiti madhubuti wa katika mlango wa bahari wa Hormuz.
IRGC pia liliapa kuwa halitasalimu amri hadi adui atakaposhindwa kabisa.
Tangsiri, aliyekuwa mmoja wa makamanda wa juu wa IRGC, alihusika katika kusimamia usafirishaji wa meli kupitia mlango bahari wa Hormuz, ambao ni njia muhimu ya biashara ya mafuta duniani.
Kupitia chapisho lake katika mtandao wa kijamii wa X, aliwahi kusema kuwa hakuna chombo chochote kinachohusiana na maadui wa Iran kinachoruhusiwa kupita katika eneo hilo.
Alikuwa pia kamanda mwenye msimamo mkali, aliyetoa kauli nyingi za kukosoa Marekani na Israel hapo awali.
Mwaka 2019, aliwekewa vikwazo na wizara ya fedha ya Marekani ikiwa ni pamoja na makamanda wengine wa IRGC baada ya Iran kuidungua ndege ya upelelezi ya Marekani karibu na mlango huo wa bahari.
Unaweza kusoma pia:
Wanajeshi sita wa Israel wajeruhiwa nchini Lebanon

Chanzo cha picha, Reuters
Maelezo ya picha, Moshi umeonekana ukifuka baada ya shambulio la Israel kusini mwa Lebanon, huku uhasama ukiongezeka kati ya Israel na Hezbollah. Jeshi la Israel linasema wanajeshi wake sita wamejeruhiwa nchini Lebanon katika matukio tofauti.
Wanajeshi wawili walijeruhiwa vibaya baada ya kombora la kifaru kurushwa kuelekea kwao kusini mwa Lebanon jana alasiri, Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) linasema.
Wanajeshi watatu wa IDF walijeruhiwa, mmoja vibaya, baada ya ndege isiyo na rubani kuanguka karibu nao, jeshi linasema.
Mwanajeshi mwengine alijeruhiwa baada ya "ajali ya operesheni", inaongeza.
Wanajeshi hao wamepelekwa hospitali. Mashambulizi mapya ya Israel nchini Lebanon yalianza baada ya Hezbollah inayoungwa mkono na Iran kurusha makombora kaskazini mwa Israel kulipiza kisasi mauaji ya kiongozi mkuu wa Iran na mashambulizi ya karibu ya kila siku dhidi ya Hezbollah.
Tangu wakati huo, mashambulizi ya Israel yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 1,000 nchini Lebanon, kulingana na wizara ya afya ya Lebanon.
Israel pia imesema inakusudia kuchukua udhibiti wa sehemu kubwa ya kusini mwa Lebanon kama sehemu ya kampeni yake ya ardhini dhidi ya Hezbollah.
Pia unaweza kusoma:
Trump asema 'kumekuwa na mabadiliko ya utawala' nchini Iran

Chanzo cha picha, Reuters
Donald Trump amewaambia waandishi wa habari ndani ya ndege ya Air Force One kwamba Marekani inaamini kumekuwa na mabadiliko ya utawala nchini Iran, akirejelea kauli yake kwenye Kituo cha habari cha Fox News wiki iliyopita, ambapo alisema: "Unaweza kusema kumekuwa na mabadiliko ya utawala kwa sababu wameuawa."
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye ndege hiyo, anasema: "Lakini tumekuwa na mabadiliko ya utawala kwa sababu serikali moja iliangamizwa, kuharibiwa, wote wamekufa...''.
''Maafisa wa utawala unaofuata wamekufa zaidi, na utawala wa tatu tunashughulika na watu tofauti kuliko mtu mwengine yeyote hapo awali, ni kundi tofauti kabisa la watu, kwa hivyo ninaamini kwamba serikali inabadilika, na kwa kweli wamekuwa wa busara.
"Kwa hivyo nadhani tumekuwa na mabadiliko ya utawala, ninamaanisha kuwa huwezi kufanya vizuri zaidi ya hapo.
"Tuliondoa utawala wa kwanza ambao ulikuwa mbaya, mbaya sana,.. wa pili aliteuliwa, na wote wamekwenda, wote wamekufa, isipokuwa mmoja ambaye anasuasua," Trump anasema, akitaja idadi ya viongozi wa Iran waliouawa katika vita vya mwezi mzima.
Maelezo zaidi:
Mkuu wa Jeshi la Myanmar Min Aung Hlaing ateuliwa kuwa rais

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Maelezo ya picha, Mkuu wa jeshi la Myanmar Min Aung Hlaing Mkuu wa jeshi la Myanmar Min Aung Hlaing ameteuliwa kuwania kiti cha urais huku bunge likikutana Jumatatu, kufuatia uchaguzi mkuu ambapo vyama vikubwa vya upinzani viliondolewa.
Min Aung Hlaing ana hakika ya kuchaguliwa, kwa vile aliteuliwa bungeni pamoja na wafuasi wawili ambao wanatarajiwa kuwania urais.
Amewekewa vikwazo na nchi nyingi za Magharibi kwa kuongoza mapinduzi ya kijeshi miaka mitano iliyopita.
Katika vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyofuata, maelfu ya watu wameuawa na mamilioni wamekimbia makazi yao.
Maeneo makubwa ya nchi yanasalia chini ya udhibiti wa makundi ya upinzani yenye silaha.
Uchaguzi mkuu, uliofanyika kati ya Desemba na Januari, ulinadiwa na utawala wa kijeshi kama njia ya amani.
Lakini uchaguz huo ulitazamwa na watu wengi kama udanganyifu, na vyama vingi maarufu vilipigwa marufuku kusimama na maeneo makubwa ya nchi hayakuruhusiwa kushiriki kwa sababu ya vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Utawala umepinga ukosoaji huu, ukishikilia kuwa kura ilikuwa huru na ya haki.
Taribani 90% ya wabunge katika bunge jipya la Myanmar wanadaiwa kuwa waaminifu kwa Min Aung Hlaing, ama kuwa maafisa wanaohudumu katika jeshi - ambao wana uhakika wa kupata robo ya viti - au kama wagombea waliochaguliwa kwa chama cha jeshi.
Indonesia yathibitisha kuuawa kwa mwanajeshi wake nchini Lebanon

Chanzo cha picha, Reuters
Tuliripoti hapo jana kwamba afisa wa kikosi cha Umoja wa Mataifa cha kulinda amani nchini Lebanon (UNIFIL) aliuawa baada ya kombora kupiga moja ya kambi zao Jumapili jioni.
Indonesia sasa imethibitisha kuwa mmoja wa walinda amani wake aliuawa na wengine watatu kujeruhiwa wakati wakihudumu na kikosi cha Umoja wa Mataifa.
Wizara ya Mambo ya nje inasema walinda amani hao walikabiliwa na mashambulizi "yasiyo ya moja kwa moja karibu" na kambi yao.
"Tumesikitishwa sana ha tukio hili. Tunatoa heshima zetu za juu kwa mlinda amani aliyefariki kwa kujitolea na huduma yake kwa amani na usalama wa kimataifa," iliandika kwenye mtandao wa kijamii.
"Indonesia inalaani vikali tukio hilo na inataka uchunguzi wa kina na wa uwazi kufanywa kubaini kilichotokea."
Pia unaweza kusoma:
Trump ana mpango wa 'kuchimba urani ya Iran' - Wall Street Journal

Chanzo cha picha, Getty Images
Rais wa Marekani Donald Trump anapanga operesheni ya kijeshi kwa lengo la kuchimba pauni 1,000 za urani nchini Iran, Jarida la Wall Street linaripoti.
Operesheni hiyo "huenda ikaviweka vikosi vya Marekani ndani ya nchi kwa siku kadhaa au zaidi", kulingana na Jarida hilo, ambalo linawanukuu maafisa wa usalama ambao hawakutajwa.
Trump bado hajafanya uamuzi, lakini "kwa ujumla yuko tayari kutekeleza wazo hilo, kulingana na maafisa, kwa sababu inaweza kusaidia kutimiza lengo lake kuu la kuzuia Iran kutotengeneza silaha ya nyuklia."
BBC imewasiliana na Ikulu ya White House na Pentagon kwa maoni kuhusiana na taarifa hii.
Gazeti la New York Times linaripoti kwamba wanajeshi waliopelekwa katika eneo hilo "wanaweza kutumika katika operesheni inayolenga madini ya urani ya Iran iliyorutubishwa sana kwenye eneo la nyuklia la Isfahan" lakini pia wanaweza kutumiwa kuteka Kisiwa cha Kharg au kulinda Mlango- Bahari wa Hormuz.
Mwanzoni mwa mwezi huu Gazeti la New York Times liliripoti kwamba Trump "anazingatia" operesheni ya "kukamata na kuharibu nyenzo za nyuklia za kiwango cha chini kabisa zinazoaminika kuhifadhiwa kwa kiasi kikubwa chini ya mlima huko Isfahan".
Magazeti yote mawili yanaonyesha kuwa operesheni hiyo itakuwa ngumu na hatari zaidi.
Maelezo zaidi:
'Mikono iliyojaa damu': Papa Leo 'awakosoa' wale wanaohusika katika vita

Chanzo cha picha, Vatican Media via Vatican Pool/Getty Images
Huku mzozo katika Mashariki ya Kati ukiendelea, Kiongozo wa Kanisa Katoliliki Duniani Papa Leo XIV ameonekana kuwakosoa wale wanaohusika na vita hivyo.
Akiwahutubia waumini wa kanisa hilo mjini Vatican wakati wa maadhimisho ya Jumapili ya Mitende, Papa alisema Mungu anakataa maombi ya viongozi wanaoanzisha vita na kuwa na "mikono iliyojaa damu", katika kile ambacho kimetafsiriwa kuwa ukosoaji wa wale waliohusika katika vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran.
"Huyu ndiye Mungu wetu: Yesu, mfalme wa amani, anayekataa vita, ambaye hakuna mtu anayeweza kumtumia kuhalalisha vita," anasema Papa.
"Hasikii maombi ya wapiganaji, lakini anakataa." Akinukuu kifungu fulani cha Biblia, anasema: “‘Hata mjaposali sala nyingi, sitasikiliza: mikono yenu imejaa damu’.”
Soma pia:
Mafuta yapanda zaidi ya $115 huku hisa za Asia zikishuka thamani

Chanzo cha picha, EPA/Shutterstock
Bei ya mafuta duniani imepanda na hifadhi kushuka kwa kasi Jumatatu asubuhi huko Asia huku vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran vikiongezeka.
Bei ya mafuta ghafi ya Brent ilipanda kwa zaidi ya 3% hadi zaidi ya dola 115 (£86.77) kwa pipa, huku mafuta yanayouzwa Marekani yakipanda hadi dola 103 baada ya kuimarika kwa 3.5%. Inaiweka Brent kwenye mstari kwa faida yake kubwa zaidi ya kila mwezi.
Masoko ya hisa barani Asia yalishuka thamani, huku Nikkei 225 ya Japani ikishuka kwa 4.5% na Kospi ya Korea Kusini 4% chini.
Haya yanajiri baada ya waasi wa Houthi wanaoungwa mkono na Iran nchini Yemen kujiunga na vita kwa kuishambulia Israel mwishoni mwa juma na Iran kutishia kupanua mashambulizi ya kulipiza kisasi dhidi ya vyuo vikuu na nyumba za maafisa wa Marekani na Israel.
Pia unaweza kusoma:
Trump asema Marekani inaweza 'kuchukua mafuta nchini Iran' na kukiteka Kisiwa cha Kharg

Chanzo cha picha, Getty Images
Rais wa Marekani Donald Trump ameliambia gazeti la Financial Times kwamba anaweza "kuchukua mafuta nchini Iran" na ikiwezekana akakiteka Kisiwa cha Kharg ambacho ni kitovu kikuu cha mafuta nchini humo.
"Kusema ukweli, jambo ninalotaka zaidi ni kuchukua mafuta nchini Iran lakini baadhi ya watu wajinga huko Marekani wanasema: 'Kwa nini unafanya hivyo?' Lakini ni watu wajinga," alisema.
Trump alipendekeza hatua hiyo inaweza kumaanisha kuchukua kisiwa cha Kharg. "Pengine tuchukue Kisiwa cha Kharg, au tuachane nacho. Tuna chaguzi nyingi," Trump aliambia Financial Times. "Inamaanisha pia kuwa tulipaswa kuwa huko [katika Kisiwa cha Kharg] kwa muda."
Alipoulizwa kuhusu ulinzi wa Iran katika kisiwa hicho alisema: "Sidhani kama wana utetezi wowote. Tunaweza kukichukua kwa urahisi sana."
Kauli hiyo ya rais inakuja huku wanajeshi 3,500 zaidi wa Marekani wakiwasili Mashariki ya Kati, hofu ya wanajeshi wa Marekani kijiunga na mashambulizi ya Iran ikiongezeka.
Trump aliongeza kuwa mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Marekani na Iran kupitia "mabalozi" wa Pakistan yalikuwa yanaendelea vizuri, lakini hakugusia suala makubaliano ya kusitisha mapigano yanaweza kufikiwa hivi karibuni.
"Mkataba unaweza kufikiwa haraka," alisema.
Maelezo zaidi:
Natumai Hujambo
