Moja kwa moja, Mazungumzo ya amani kuendelea leo Islamabad, Marekani na Iran bado katika hali tete

Mapema Iran ilishambulia kwa ndege zisizo na rubani meli kadhaa za kijeshi za Marekani kulipiza kisasi, baada ya Marekani kushambulia na kukamata meli ya mizigo ya Iran katika eneo la Ghuba ya Oman

Moja kwa moja

Na Martha Saranga

  1. Islamabad kuongoza mazungumzo ya Marekani na Iran leo, Iran bado haijathibitisha

    s

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Mazungumzo kati ya Marekani na Iran yanatarajiwa kuanza leo katika mji mkuu wa Pakistan, Islamabad.

    Wageni katika Hoteli ya Serena ya mjini humo, ambako mazungumzo ya awali yaliyoshindwa kufikia makubaliano yalifanyika tarehe 11 Aprili, wameombwa kuondoka ili kuandaa mkutano wa leo. Polisi pia wametangaza kufungwa kwa barabara muhimu kutokana na ujio wa wajumbe hao wa mkutano.

    Rais Donald Trump amesema “wajumbe wake” watawasili Islamabad Jumatatu jioni, akieleza kuwa Makamu wa Rais JD Vance ataongoza ujumbe huo pamoja na Steve Witkoff na Jared Kushner.

    Hata hivyo, Iran bado haijathibitisha rasmi kama itashiriki katika mazungumzo hayo. Vyombo vya habari vya serikali ya Iran vinaripoti kuwa maafisa wake hawatashiriki mazungumzo iwapo vizuizi vya Marekani dhidi ya bandari za Iran vitaendelea.

    Makubaliano ya kusitisha mapigano ya muda wa wiki mbili kati ya Marekani na Iran yanatarajiwa kumalizika Jumatano, huku Trump akiendelea kutoa vitisho vya kuharibu miundombinu ya Iran iwapo makubaliano hayatafikiwa.

    s

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Barabara kadhaa zimefungwa kwa ajili ya usalama
  2. Iran yaanza kujibu mapigo, yashambulia meli za kijeshi za Marekani

    a

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Marekani imeweka kizuizi cha kijeshi kwenye mlango bahari wa Hormuz na kusababisha mvutano zaidi wa kijeshi na Iran

    Iran imeanzisha mashambulizi ya ndege zisizo na rubani (droni) dhidi ya meli za kijeshi za Marekani katika Ghuba ya Oman, shirika la habari la Tasnim huko Iran, limeripoti.

    Hatua hii ya kulipiza kisasi imekuja muda mfupi baada ya jeshi la majini la Marekani kukamata meli ya mizigo yenye bendera ya Iran katika eneo hilo.

    Hakuna taarifa zilizothibitisha uharibifu wowote uliotokea kutokana na mashambulizi hayo ya droni.

    Awali, Makao Makuu ya Khatam al-Anbiya ya Iran, ambayo ndiyo kamandi ya juu ya operesheni za kijeshi nchini humo, yalikosoa operesheni ya Marekani ya majini, yakisema ni uvunjaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano.

    Pia ilisema Iran “italipiza kisasi kwa kitendo hiki cha uharamia wa kijeshi wa Jeshi la Majini la Marekani.”

    A
  3. Ujumbe wa Marekani waelekea Pakistan kwa mazungumzo na Iran, licha ya kukamata meli yao

    s

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Wajumbe wa Marekani wanatarajiwa kuwasili Pakistan leo kwa mazungumzo mapya na Iran yanayolenga kutafuta suluhu ya mgogoro unaoendelea, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kidiplomasia za kumaliza vita na mvutano wa kikanda.

    Mazungumzo hayo yanakuja wakati hali ya uhusiano kati ya mataifa hayo mawili ikiwa tete, baada ya Marekani kukamata meli ya mafuta ya Iran iliyokuwa ikijaribu kuvuka eneo la vizuizi katika Mlango wa Hormuz. Tukio hilo limeongeza hasira kwa upande wa Iran.

    Rais Donald Trump amesema jeshi la majini la Marekani liliizuia meli hiyo na kuidhibiti, akisisitiza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya kuzuia kile anachokiita uvunjaji wa vikwazo vya baharini dhidi ya Iran.

    Iran kupitia vyombo vyake vya habari imekosoa hatua hiyo ikidai ni “uchokozi wa baharini” na imesema vitisho na vizuizi vya Marekani vinachelewesha kufikiwa kwa makubaliano ya amani.

    Wakati huo huo, hali katika Mlango wa Hormuz imeendelea kuwa tete kutokana na mashambulizi dhidi ya meli za biashara na mivutano ya kijeshi, jambo linalofanya mazungumzo ya Pakistan kuwa na uzito mkubwa lakini pia hatari ya kushindwa kufikia muafaka.

  4. Aua watoto wake saba kwa risasi katika ugomvi wa kifamilia Louisiana

    s

    Chanzo cha picha, Reuters

    Mtu mmoja amewaua watoto wake saba pamoja na mtoto mwingine ambaye si wa familia hiyo katika tukio la mauaji ya risasi yaliyotokea Shreveport katika jimbo la Louisiana nchini Marekani, ambalo polisi wameelezea tukio hilo kama “mzozo wa kifamilia”.

    Watoto hao walikuwa na umri wa kati ya mwaka 1 hadi miaka 14, kwa mujibu na shirika la habari la CBS ambalo ni mshirika wa BBC nchini Marekani.

    Maafisa walisema tukio la risasi lilianza karibu saa 05:00 asubuhi (10:00 GMT) siku ya Jumapili. Mshukiwa alipiga risasi watu 10 kabla ya kukimbia kwa kutumia gari lililoibiwa, alisema msemaji wa Polisi wa Shreveport, Chris Bordelon. Polisi walimfukuza na hatimaye kumuua.

    Wanawake wawili watu wazima, wakiwemo mama wa watoto hao, wako katika hali mahututi hospitalini.

    Mshukiwa ametambuliwa kama Shamar Elkins, kulingana na mkurugenzi wa mawasiliano wa meya wa Shreveport, Leigh Anne Evensky, alivyoiambia BBC.

    Inaripotiwa kuwa mshukiwa alimpiga risasi mwanamke mmoja barabarani kabla ya kwenda kwenye nyumba ya karibu ambako aliwaua watoto wanane, “mmoja kati yao hakuwa wa kwake”, polisi walisema.

    Mtoto mmoja alifanikiwa kukimbia na kwenda kwenye nyumba ya jirani na kupiga simu polisi. Pia polisi walisema mshambuliaji alifanya tukio hilo peke yake. Mtoto aliyetoroka wa tisa aliruka kutoka juu ya paa na alikimbizwa hospitalini kwa matibabu, alisema Bordelon.

    Akizungumza mapema Jumapili, Meya wa Shreveport Tom Arceneaux alisema: “Hili ni tukio la kusikitisha, pengine ni tukio baya zaidi la kusikitisha ambalo tumewahi kulipata Shreveport.”

  5. Vizuizi baharini vinaongeza mgogoro wa Marekani na Iran- Balozi Moghadam

    s

    Chanzo cha picha, Iran gvntm

    Reza Amiri Moghadam, balozi wa Iran nchini Pakistan, amesema kwamba "kuendelea kuwepo kwa kizuizi cha baharini kati ya Iran na Marekani kutaendeleza mvutano kati ya mataifa hayo.

    Amiri-Moghaddam aliandika kupitia chapisho lake kwenye X: "Huwezi kuendelea kukiuka sheria za kimataifa, kuimarisha kizuizi, kutishia Iran kwa uhalifu zaidi wa kivita, kusisitiza madai yasiyo na msingi, kuvutana kwa masuala yasiyo na umuhimu na wakati huo huo kujifanya unashiriki katika 'diplomasia'."

    Marekani, kwa upande wake, ilisema imetuma ujumbe kwenda Islamabad kufanya mazungumzo na Iran, lakini Iran ilisema haikuwa na mpango wa kushiriki katika awamu ya pili mazungumzo.

    Taarifa hiyo pia ilisema kwamba shambulio dhidi ya meli ya Iran lilikuwa "kitendo cha uharamia wa Jeshi la wanamaji la Marekani" na ukiukaji wa usitishaji wa mapigano.

  6. Iran yatishia kulipa kisasi baada ya Marekani kukamata meli inayodhaniwa ya nchi hiyo

    s

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Kamanda mkuu wa jeshi la Iran, Khatam al-Anbiya, alitishia kwamba Iran ingejibu hatua ya Marekani kukamata meli ya mizigo yenye bendera ya Iran, ambayo jeshi la wanamaji la Marekani liliishambulia ilipokuwa likielekea Oman, na kuelezea hatua hiyo kama "ukiukaji wa usitishaji mapigano."

    Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na vyombo vya habari vya serikali, msemaji alieleza Marekani "ilikiuka usitishaji mapigano kwa kufyatua risasi kwenye moja ya meli za biashara za Iran katika Ghuba ya Oman, na kudhoofisha mfumo wake wa uendeshaji na kisha kuidhibiti" kwa kutumia wanajeshi wa maji.

    "Vikosi vya Jeshi la Jamhuri ya kiislamu ya Iran vitajibu haraka na kulipiza kisasi kwa kitendo hiki cha uharamia wa kutumia silaha uliofanywa na jeshi la wanamaji la Marekani," taarifa hiyo ilisema.

  7. Tunafahamu nini kuhusu meli yenye bendera ya Iran iliyokamatwa na Marekani?

    Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa awali, Donald Trump alisema kupitia chapisho kwenye mtandao wa Truth Social kwamba jeshi la wanamaji la Marekani lilifyatua risasi dhidi ya meli ya mizigo iliyokuwa na bendera ya Iran iitwayo Touska katika Ghuba ya Oman.

    Data za MarineTraffic,zilieleza meli hiyo iliondoka katika bandari ya Klang tarehe 12 April ikielekea Ghuba ya Oman.

    Taarifa za Mfumo wa utambuzi (AIS) zinaonyesha kuwa Touska ilikuwa baharini umbali wa takribani maili 40 kutoka bandari ya Chabahar kusini mashariki mwa Iran majira ya saa 13:00 GMT leo.

    Kabla ya hapo, meli ilisimama, ikageuka kurudi nyuma, baadaye ikaelekea kidogo mashariki, na hatimaye kusimama kabisa.

    Meli hiyo ya makontena ina urefu wa zaidi ya mita 290 na kina cha mzigo cha takribani mita 13. Inaonekana ilikuwa imebeba mizigo kamili au kwa sehemu.

    Aidha, Touska imo kwenye orodha ya meli zilizowekewa vikwazo na Wizara ya fedha ya Marekani.

  8. Marekani yakamata meli ya mizigo yenye bendera ya Iran- Trump

    s

    Chanzo cha picha, Reuters

    Rais wa Marekani Donald Trump alisema jeshi lake limekamata meli ya mizigo iliyokuwa na bendera ya Iran baada ya kujaribu kukwepa kizuizi cha Marekani.

    Rais Trump alisema kwamba jeshi la Marekani awali lilitoa onyo kwa meli hiyo, lakini ilipoendelea na harakati zake, "waliizuia moja kwa moja kwa kushambulia chumba cha injini," na kusababisha meli hiyo kusimama.

    Aliongeza kuwa vikosi vya Marekani sasa vimedhibiti meli hiyo, ambayo alisema ilijaribu kukwepa kizuizi cha meli zinazotoka Iran siku ya Jumapili. Trump alisema meli hiyo, inayoitwa Touska, ilikamatwa katika Ghuba ya Oman na kupewa "onyo kamili la kusimama."

    Alisema: "Wafanyakazi wa Iran walikataa kusikiliza onyo hilo, kwa hivyo meli yetu ilichukua hatua mara moja ya kulenga injini." Aliongeza kuwa meli hiyo iko chini ya vikwazo vya wizara ya fedha ya Marekani na Jeshi la Wanamaji kwa sasa linachunguza kilichomo ndani. Wakati huo huo, Iran bado haijathibitisha rasmi tukio hili.

  9. Habari na karibu katika habari zetu za moja kwa moja leo Aprili 20, 2026