Mwanamke mmoja ameokolewa kutoka chini ya vifusi vya jengo
la ghorofa 13 lililoporomoka eneo la Eastleigh, Nairobi, huku hofu ikitanda
kwamba watu wengine huenda bado wamenasa.
Kamanda wa
Polisi wa Nairobi, Issa Mahamud, amesema mwanamke huyo alipata majeraha na
anapatiwa matibabu katika hospitali iliyo karibu.
“Alijeruhiwa
na hali yake inaendelea vizuri. Hata hivyo, kulingana na taarifa tulizonazo,
kuna uwezekano wa watu wengine kunasa chini ya vifusi,” amesema Mahamud.
Amesema pia
kuwa mama mmoja alisikika akilia kutoka chini ya vifusi, lakini baadaye sauti
yake ilinyamaza.
“Hatujui
kama bado yuko hai, lakini juhudi za kumuokoa zinaendelea,” amesema.
Polisi
waonya umma kujiepusha na eneo la tukio
Mahamud
ameeleza kuwa umati wa watu uliokusanyika eneo la tukio umekuwa mojawapo ya
changamoto zinazokwamisha shughuli za uokoaji.
Amesema
polisi walilazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya watu na kuwataka
kuondoka ili kutoa nafasi kwa wahudumu wa dharura kufanya kazi.
“Hapa
hakuna sinema ya kutazama. Kuna uwezekano wa jengo hilo kuanguka zaidi, kwa
sababu linaegemea jengo jingine,” amesema.
Ameonya
kuwa watu wanaokusanyika karibu na eneo hilo wanajiweka katika hatari, hasa
kutokana na uwezekano wa jengo hilo kuendelea kuporomoka.
Mamlaka
hazijui watu wangapi walikuwa ndani ya jengo
Afisa mkuu
wa masuala ya majanga wa Kaunti ya Nairobi, Bramwell Simiyu, ameiambia BBC kuwa
mamlaka bado hazijui ni watu wangapi huenda walikuwa ndani ya jengo hilo
lilipoporomoka.
Amesema
mamlaka zimearifiwa kuwa huenda baadhi ya ghorofa za chini zilikuwa zikitumiwa
kwa shughuli ambazo hazikuwa zimeidhinishwa.
“Tumearifiwa
kuwa kulikuwa na shughuli ambazo hazikuruhusiwa katika baadhi ya ghorofa za
chini za jengo hilo. Baadhi ya watu walikuwa wakiendesha shughuli zao humo,”
amesema Simiyu.
Ameongeza
kuwa serikali ya kaunti imeanzisha operesheni ya kutafuta na kuokoa watu, huku
juhudi za kuhamasisha na kupeleka vifaa vinavyohitajika katika eneo la tukio
zikiendelea.
Ghorofa ya chini na ya kwanza ya jengo hilo ziliripotiwa
kuwa na maduka, jambo linalozua wasiwasi kuhusu usalama wa wafanyabiashara,
wateja na watu wengine ambao huenda walikuwa ndani au karibu na jengo hilo.
Sakaja ataka wananchi watoe taarifa za watu waliopotea
Gavana wa Nairobi, Johnson Sakaja, aliyefika eneo la tukio,
amesema kipaumbele cha serikali ya kaunti ni kuendeleza shughuli za uokoaji.
Amesema Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya limeweka hema
kwa ajili ya kuwahudumia walioathirika na kutenga eneo kwa watu wanaotafuta
taarifa kuhusu ndugu na jamaa zao.
“Shirika la Msalaba Mwekundu limeweka hema kwa ajili ya
kuwahudumia walioathirika. Kwa wale ambao hawajui walipo wapendwa wao, tuna
matumaini kwamba tutawapata. Tunaomba muwe watulivu,” amesema Sakaja.
Amewataka watu ambao ndugu au jamaa zao huenda walikuwa
katika eneo hilo na hawajulikani walipo kutoa majina yao ili yaingizwe katika
orodha ya watu wanaotafutwa.
Sakaja amehakikishia umma kuwa vikosi mbalimbali vya usalama
vimepelekwa eneo la tukio kusaidia shughuli za uokoaji na kudhibiti hali.
Wahudumu wa dharura wanaendelea na juhudi za kutafuta watu
ambao huenda wamenasa chini ya vifusi. Idadi ya watu walioathirika na chanzo
cha kuporomoka kwa jengo hilo bado havijathibitishwa rasmi.