Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Jengo laporomoka Eastleigh, Nairobi, shughuli za uokoaji zaendelea

Mashuhuda waliokuwepo eneo la tukio wamesema kulikuwa na vurugu na uporaji ulianza, huku watu waliokuwa wakiiba wakizirusha ambulansi mawe.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Beldeen Waliaula & Mariam Mjahid

  1. Na kufikia hapo tunakamilisha matangazo ya moja kwa moja. Usiku mwema.

  2. Israel yaanza kubomoa majengo ya Wapalestina mjini Hebron

    Jeshi la Israel limeanza kubomoa majengo ya Wapalestina katika mji wa Hebron, baada ya wanajeshi wawili wa Israel kuuawa katika shambulio lililofanywa na washambuliaji wawili wa Kipalestina.

    Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, amesema jeshi litaharibu kitongoji walikotoka washambuliaji hao, akiongeza kuwa Israel iko tayari kuchukua hatua kubwa katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu.

    Maafisa wanasema wanajeshi wengine watatu walijeruhiwa katika shambulio hilo lililotokea kwenye kituo cha ukaguzi nje ya Hebron, kabla ya washambuliaji hao kuuawa kwa kupigwa risasi.

    Shambulio hilo limetokea wakati mvutano ukiendelea kuongezeka, huku walowezi wa Kiyahudi wenye misimamo mikali wakiwalenga Wapalestina wakati wa msimu wa kila mwaka wa uvunaji wa zeituni. Uchaguzi mkuu wa Israel unatarajiwa kufanyika baada ya siku nne.

    Picha za video zilizothibitishwa na BBC zinaonyesha mapambano makali ya risasi kati ya wanajeshi na washambuliaji hao.

    Picha nyingine za kamera za usalama, ambazo hazijathibitishwa, zinaonekana kuwaonyesha washambuliaji wawili wakishuka kwenye gari wakiwa na silaha zinazofanana na bastola na bunduki ya kivita, kisha kuanza kuwafyatulia risasi wanajeshi katika kituo cha ukaguzi kabla ya wanajeshi hao kujibu mashambulizi.

  3. Watu saba wauawa katika shambulio la risasi kanisani nchini Jordan

    Watu saba wameuawa na wengine 28 kujeruhiwa baada ya watu wenye silaha kufyatua risasi wakati wa mazishi katika kanisa lililoko katika kijiji cha Hmoud, mkoa wa Karak, katikati mwa Jordan, siku ya Ijumaa.

    Msemaji wa serikali ya Jordan, Mohammad al-Momani, amelitaja tukio hilo kuwa shambulio la kikatili.

    Kwa mujibu wa taarifa, washambuliaji hao walifika kwa gari, wakaingia kanisani na kuanza kuwafyatulia risasi waombolezaji kabla ya kutoroka.

    Mfalme Abdullah II wa Jordan amesema mamlaka zitakabiliana na shambulio hilo, alilolitaja kuwa la kigaidi, kwa kutumia adhabu kali zaidi.

    Khaled Burqan, mmoja wa waombolezaji waliokuwapo kanisani wakati wa shambulio hilo, ameiambia televisheni ya taifa ya Jordan, al-Mamlaka, kuwa watu kadhaa walikuwa wamekusanyika kwa ajili ya mazishi wakati milio ya risasi ilipoanza.

    Amesema washambuliaji wawili waliokuwa na bunduki na bastola waliendelea kuwafyatulia risasi waombolezaji kwa dakika kadhaa.

    Picha za kamera za usalama zilizothibitishwa na BBC zinaonekana kuonyesha watu watatu wenye silaha wakielekea kanisani kutoka barabarani.

    Wawili kati yao wanaonekana kuingia katika eneo la lango la magari la kanisa, kisha kurudi nyuma kwa muda kabla ya kurejea pamoja na mtu wa tatu. Wote watatu wanaonekana wakiwa na bastola.

  4. Mamlaka zamtafuta mmiliki wa jengo lililoporomoka Eastleigh, Nairobi

    Mamlaka za Kenya zinaendelea kumtafuta mmiliki wa jengo lililoporomoka katika eneo la Eastleigh, jijini Nairobi, huku timu ya pamoja ya usalama kutoka taasisi mbalimbali za serikali ikitumwa kusimamia shughuli za uokoaji.

    Watu kadhaa wanahofiwa kunaswa chini ya vifusi vya jengo hilo, huku wahudumu wa uokoaji wakiendelea na juhudi za kuwatafuta manusura.

    Baadhi ya wafanyakazi wa ujenzi wamesema jengo hilo lilikuwa na ghorofa 18, kinyume na taarifa za awali zilizolitaja kuwa na ghorofa 16. Wamesema baadhi ya wafanyakazi waliokuwa katika eneo hilo walifanikiwa kujiokoa kabla ya jengo hilo kuporomoka.

    Kwa mujibu wa wafanyakazi hao, baadhi yao walihisi jengo likitikisika kabla ya kuporomoka. Hata hivyo, chanzo cha tukio hilo bado hakijabainishwa rasmi.

    Ghorofa ya chini na sehemu ya chini ya jengo hilo, iliyokuwa chini ya usawa wa ardhi, ziliripotiwa kuwa na maduka.

    Aidha, Polisi wametumia gesi ya kutoa machozi kutawanya umati uliokusanyika katika eneo la tukio, huku shughuli za uokoaji zikiendelea.

    Gavana wa Nairobi, Johnson Sakaja, amesema hema la kutoa taarifa na kusaidia familia za watu wanaohofiwa kuathiriwa na tukio hilo limewekwa katika eneo hilo.

    Mamlaka zinaendelea kuratibu juhudi za uokoaji na kutathmini hali katika eneo la tukio, huku wasiwasi ukiongezeka kuhusu usalama wa watu ambao huenda walikuwa ndani ya jengo hilo lilipoporomoka.

  5. Nairobi: Mwanamke aokolewa, huku kukiwa na hofu ya wengine kunaswa kwenye vifusi

    Mwanamke mmoja ameokolewa kutoka chini ya vifusi vya jengo la ghorofa 13 lililoporomoka eneo la Eastleigh, Nairobi, huku hofu ikitanda kwamba watu wengine huenda bado wamenasa.

    Kamanda wa Polisi wa Nairobi, Issa Mahamud, amesema mwanamke huyo alipata majeraha na anapatiwa matibabu katika hospitali iliyo karibu.

    “Alijeruhiwa na hali yake inaendelea vizuri. Hata hivyo, kulingana na taarifa tulizonazo, kuna uwezekano wa watu wengine kunasa chini ya vifusi,” amesema Mahamud.

    Amesema pia kuwa mama mmoja alisikika akilia kutoka chini ya vifusi, lakini baadaye sauti yake ilinyamaza.

    “Hatujui kama bado yuko hai, lakini juhudi za kumuokoa zinaendelea,” amesema.

    Polisi waonya umma kujiepusha na eneo la tukio

    Mahamud ameeleza kuwa umati wa watu uliokusanyika eneo la tukio umekuwa mojawapo ya changamoto zinazokwamisha shughuli za uokoaji.

    Amesema polisi walilazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya watu na kuwataka kuondoka ili kutoa nafasi kwa wahudumu wa dharura kufanya kazi.

    “Hapa hakuna sinema ya kutazama. Kuna uwezekano wa jengo hilo kuanguka zaidi, kwa sababu linaegemea jengo jingine,” amesema.

    Ameonya kuwa watu wanaokusanyika karibu na eneo hilo wanajiweka katika hatari, hasa kutokana na uwezekano wa jengo hilo kuendelea kuporomoka.

    Mamlaka hazijui watu wangapi walikuwa ndani ya jengo

    Afisa mkuu wa masuala ya majanga wa Kaunti ya Nairobi, Bramwell Simiyu, ameiambia BBC kuwa mamlaka bado hazijui ni watu wangapi huenda walikuwa ndani ya jengo hilo lilipoporomoka.

    Amesema mamlaka zimearifiwa kuwa huenda baadhi ya ghorofa za chini zilikuwa zikitumiwa kwa shughuli ambazo hazikuwa zimeidhinishwa.

    “Tumearifiwa kuwa kulikuwa na shughuli ambazo hazikuruhusiwa katika baadhi ya ghorofa za chini za jengo hilo. Baadhi ya watu walikuwa wakiendesha shughuli zao humo,” amesema Simiyu.

    Ameongeza kuwa serikali ya kaunti imeanzisha operesheni ya kutafuta na kuokoa watu, huku juhudi za kuhamasisha na kupeleka vifaa vinavyohitajika katika eneo la tukio zikiendelea.

    Ghorofa ya chini na ya kwanza ya jengo hilo ziliripotiwa kuwa na maduka, jambo linalozua wasiwasi kuhusu usalama wa wafanyabiashara, wateja na watu wengine ambao huenda walikuwa ndani au karibu na jengo hilo.

    Sakaja ataka wananchi watoe taarifa za watu waliopotea

    Gavana wa Nairobi, Johnson Sakaja, aliyefika eneo la tukio, amesema kipaumbele cha serikali ya kaunti ni kuendeleza shughuli za uokoaji.

    Amesema Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya limeweka hema kwa ajili ya kuwahudumia walioathirika na kutenga eneo kwa watu wanaotafuta taarifa kuhusu ndugu na jamaa zao.

    “Shirika la Msalaba Mwekundu limeweka hema kwa ajili ya kuwahudumia walioathirika. Kwa wale ambao hawajui walipo wapendwa wao, tuna matumaini kwamba tutawapata. Tunaomba muwe watulivu,” amesema Sakaja.

    Amewataka watu ambao ndugu au jamaa zao huenda walikuwa katika eneo hilo na hawajulikani walipo kutoa majina yao ili yaingizwe katika orodha ya watu wanaotafutwa.

    Sakaja amehakikishia umma kuwa vikosi mbalimbali vya usalama vimepelekwa eneo la tukio kusaidia shughuli za uokoaji na kudhibiti hali.

    Wahudumu wa dharura wanaendelea na juhudi za kutafuta watu ambao huenda wamenasa chini ya vifusi. Idadi ya watu walioathirika na chanzo cha kuporomoka kwa jengo hilo bado havijathibitishwa rasmi.

    Soma Zaidi:

  6. Israel yasema wanajeshi wawili wameuawa katika shambulio Ukingo wa Magharibi

    Jeshi la Israel limesema wanajeshi wake wawili wameuawa katika shambulio la watu wenye silaha wanaoshukiwa kuwa Wapalestina, lililotokea asubuhi ya leo katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa na Israel.

    Kwa mujibu wa jeshi hilo, Waisraeli wengine watatu wamejeruhiwa, huku washukiwa wawili wa Kipalestina waliokuwa na silaha wakipigwa risasi na kuuawa na wanajeshi wa Israel.

    Video zilizosambazwa zinaonyesha makabiliano ya muda mrefu ya risasi kati ya wanajeshi wa Israel na watu wenye silaha karibu na kituo cha ukaguzi wa kijeshi katika lango la kaskazini la kuingia mji wa Hebron.

    Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, amesema jeshi limezuia kile alichokitaja kuwa shambulio kubwa. Pia ameagiza chama chake cha Likud kusitisha shughuli za kisiasa, ikiwa zimesalia siku tano kabla ya uchaguzi mkuu nchini humo.

    Netanyahu amesema Israel inapanga kutekeleza operesheni kubwa katika Ukingo wa Magharibi, ikiwemo kufunga mji wa Hebron na vijiji vinavyouzunguka, kufanya upekuzi wa nyumba kwa nyumba na kubomoa miundombinu ambayo Israel inadai inahusishwa na shughuli za kigaidi.

    Amesema jeshi pia litachunguza uwezekano wa kupanua hatua hizo katika miji mingine, pamoja na kuharakisha ubomoaji wa majengo yaliyojengwa kando ya barabara ambayo Israel inasema yanahatarisha usalama wa vikosi vyake.

    Wakati huohuo, ghasia kati ya Wapalestina na walowezi wa Israel zimeongezeka katika miezi ya hivi karibuni. Katika matukio ya hivi karibuni, walowezi wenye msimamo mkali wameripotiwa kuwashambulia Wapalestina waliokuwa wakivuna mizeituni.

    Mchambuzi wa Israel amesema usalama katika Ukingo wa Magharibi unatarajiwa kuwa mojawapo ya masuala muhimu katika uchaguzi huo, wakati Netanyahu akikabiliwa na changamoto za kisiasa na tafiti za maoni ya wapiga kura zinazoashiria kuwa huenda asifanye vizuri.

  7. Bingwa wa dunia Jepchirchir apatikana na hatia ya kutumia dawa zilizopigwa marufuku

    Kitengo cha Uadilifu katika Riadha (Athletics Integrity Unit) kimemsimamisha kwa muda mwanariadha wa Kenya Peres Jepchirchir, bingwa wa dunia wa mbio za marathoni, baada ya sampuli yake kuonyesha matokeo chanya ya matumizi ya EPO, dawa iliyopigwa marufuku katika michezo.

    Kwa mujibu wa kitengo hicho, sampuli iliyochukuliwa kutoka kwa Jepchirchir kabla ya ushindi wake katika mbio za marathoni za Sydney mwezi Agosti ndiyo iliyoonyesha matokeo hayo.

    EPO, au erythropoietin, ni homoni inayozalishwa kiasili na figo na huchochea utengenezaji wa chembechembe nyekundu za damu.

    Inapotumiwa kwa njia ya sindano, EPO huongeza chembechembe hizo ambazo husafirisha oksijeni kutoka kwenye damu hadi kwenye misuli. Hali hii inaweza kuongeza uwezo wa mwanariadha kustahimili mazoezi na kufanya vizuri zaidi katika mashindano.

    Hata hivyo, EPO inaweza kugundulika katika damu au mkojo kwa kipindi kifupi baada ya kutumiwa, kutegemea muda uliopita na aina ya kipimo kinachotumika.

    Jepchirchir mwenye umri wa miaka 33 alishinda medali ya dhahabu ya mbio za marathoni katika Michezo ya Olimpiki ya Tokyo ya mwaka 2020. Pia ameshinda mara nne mashindano ya World Marathon Majors.

    Kusimamishwa kwake kwa muda kunamaanisha kuwa hataruhusiwa kushiriki mashindano wakati suala hilo likiendelea kushughulikiwa.

  8. Ukraine na Urusi zakubaliana kubadilishana wafungwa wa kivita

    Ukraine na Urusi zimebadilishana wafungwa wa vita kwa mara ya kwanza baada ya miezi kadhaa, kwa mujibu wa Wizara ya Ulinzi ya Urusi, kama ilivyoripotiwa na mashirika ya habari ya serikali ya Urusi. Vyanzo vya BBC News Ukraine pia vimethibitisha kubadilishana huko.

    “Wanajeshi wa Kikosi cha Ulinzi wa Taifa wanarejea nyumbani, wakiwemo wanajeshi wa kikosi cha Azov, walinzi wa mipaka, wanajeshi wa vikosi vya ulinzi wa maeneo, wanajeshi wa Jeshi la Wanamaji, Jeshi la Nchi Kavu, vikosi vya mashambulizi ya angani na Huduma ya Usafiri Maalumu wa Serikali, pamoja na raia tisa. Wengi wao wamekuwa mateka tangu mwaka 2022,” rais Zelensky aliandika.

    Zelensky pia amesema kuwa wengi wa walioachiliwa ni wanajeshi waliopigana kulinda mji wa Mariupol nchini Ukraine.

    Wanajeshi waliokuwa wakilinda maeneo ya Donetsk, Luhansk, Kharkiv, Zaporizhia, Kherson, Kyiv, Mykolaiv na Chernihiv pia wanarejea nyumbani.

    “Wengi wao walihukumiwa kinyume cha sheria nchini Urusi. Miongoni mwa wanaorejea ni watu watano ambao iliaminika walikuwa wamefariki katika shambulio la Urusi dhidi ya gereza la Olenivka mwezi Julai mwaka 2022,” Zelensky aliandika.

    Kwa mujibu wa upande wa Urusi, jumla ya wanajeshi 540 wamebadilishana, kila upande ukiwakabidhi wanajeshi 270.

    Baadaye mchana, Kamishna wa Haki za Binadamu alitangaza kuwa pande hizo pia zimefanikiwa kubadilishana raia. Raia saba wa Ukraine wamerejeshwa kutoka maeneo yanayokaliwa na Urusi.

    Tangu mwanzoni mwa mwaka 2026, Ukraine na Urusi zimefanya jumla ya mabadilishano 18 ya wafungwa.

    Haya ni mabadilishano ya kwanza ya wafungwa katika msimu wa vuli wa mwaka 2026. Mabadilishano yaliyotangulia yalifanyika wakati wa kiangazi.

    Agosti 19, pande hizo zilibadilishana wafungwa wa vita 103 kwa 103, na Agosti 24, wanajeshi wengine 10 walirejeshwa Ukraine.

    Mwezi Juni 26, mabadilishano yalifanyika kwa mfumo wa wanajeshi 160 kwa 160. Wanajeshi 160 walirejea Ukraine, wakiwemo waliokuwa Mariupol na katika kiwanda cha chuma cha Azovstal. Miongoni mwao walikuwa maafisa 58.

    Mnamo Juni 5, 2026, Ukraine ilipokea raia wake 186 waliokuwa wamerejeshwa, wakiwemo wanajeshi 185 na raia mmoja.

  9. Habari za hivi punde, Kenya: Jengo laporomoka Eastleigh, shughuli za uokoaji zaanza

    Jengo la ghorofa nyingi lililokuwa likijengwa limeporomoka kando ya Barabara ya 9, eneo la Eastleigh, Nairobi, na kuzua hofu kwamba watu kadhaa huenda wamenasa kwenye vifusi.

    Wahudumu wa dharura wamewasili katika eneo la tukio kuendesha shughuli za uokoaji, huku Serikali ya Kaunti ya Nairobi ikituma mashine kusaidia kuondoa vifusi na kufikia maeneo ambayo huenda kuna watu walionasa.

    Katika taarifa yake, serikali ya kaunti imesema mashine hizo zimetumwa kusaidia kuondoa vifusi na kurahisisha shughuli za kuwafikia watu ambao huenda wameathirika. Afisa anayehusika na misaada pia amearifiwa, huku juhudi za kutafuta rasilimali zaidi zikiendelea.

    Maafisa wa Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya na Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF) pia wameripotiwa kufika eneo la tukio kusaidia shughuli za uokoaji.

    Shirika la Msalaba Mwekundu limewataka wananchi kukaa mbali na eneo hilo ili wasikwamishe shughuli za uokoaji na kuwawezesha wahudumu wa dharura kufanya kazi kwa usalama.

    Ghorofa ya chini na ya kwanza ya jengo hilo zilikuwa na maduka, hali inayozua wasiwasi kuhusu usalama wa wafanyabiashara, wateja na watu wengine ambao huenda walikuwa ndani au karibu na jengo hilo lilipoporomoka.

    Idadi ya watu walioathirika bado haijafahamika.

    Mkuu wa polisi Nairobi, Issa Mohamed, amesema mamlaka zilikuwa zikisubiri taarifa zaidi huku wahudumu wa dharura wakikimbilia eneo la tukio kuokoa maisha. Amesema maafisa zaidi wa polisi wametumwa kusaidia kuratibu shughuli za wahudumu wa dharura.

    Jengo hilo limeporomoka takriban saa 7 mchana, wakati eneo la Eastleigh huwa na shughuli nyingi za kibiashara, hali inayozua hofu kwamba hata wapita njia huenda wameathirika.

    Mashuhuda wamesema kulikuwa na vurugu na uporaji katika eneo la tukio. Kwa mujibu wa mashuhuda hao, baadhi ya watu walirusha mawe dhidi ya ambulansi, na kuzilazimisha kubadili njia kwa muda kabla ya kufika eneo la tukio kuanza shughuli za uokoaji.

    Polisi waliofika eneo hilo walitumia mabomu ya machozi kuwatawanya watu waliokuwa wamekusanyika, huku maafisa wa usalama wakidhibiti umati.

    Chanzo cha kuporomoka kwa jengo hilo, pamoja na idadi ya watu waliojeruhiwa au kufariki, bado hakijafahamika. Shughuli za uokoaji zinaendelea huku wahudumu wa dharura wakitafuta watu ambao huenda wamenasa kwenye vifusi.

  10. Chanjo ya saratani ya ngozi yaonyesha matokeo ya kutia moyo katika majaribio

    Chanjo ya saratani iliyoundwa kulingana na vinasaba vya kila mgonjwa imepunguza kwa asilimia 42 hatari ya saratani ya ngozi kujirudia au mgonjwa kufariki, inapotumiwa pamoja na matibabu ya kawaida yanayochochea mfumo wa kinga ya mwili kupambana na saratani.

    Matokeo hayo yametokana na utafiti mkubwa uliofanywa na kampuni za dawa za Moderna na MSD.

    Utafiti huo ulihusisha wagonjwa zaidi ya 1,100 waliokuwa na melanoma, aina hatari ya saratani ya ngozi. Vivimbe vya saratani kwa wagonjwa hao vilikuwa vimeondolewa kwa upasuaji.

    Washiriki wote walipatiwa Keytruda, dawa ya tiba ya kinga inayosaidia mfumo wa kinga ya mwili kutambua na kushambulia seli za saratani.

    Takriban theluthi mbili ya washiriki pia walipatiwa chanjo ya majaribio inayoitwa intismeran.

    Watafiti walibaini kuwa wagonjwa waliopokea chanjo hiyo pamoja na tiba ya kinga walikuwa na uwezekano mdogo zaidi wa saratani kujirudia. Pia, katika kipindi cha miaka miwili, hatari ya saratani kusambaa hadi sehemu nyingine za mwili ilipungua kwa asilimia 38 ikilinganishwa na wagonjwa waliopokea tiba ya kinga pekee.

    Chanjo hiyo inatumia teknolojia ya mRNA, inayotumika pia katika baadhi ya chanjo za Covid 19.

    Hata hivyo, tofauti na chanjo za kawaida, chanjo hii hutengenezwa mahsusi kwa kila mgonjwa kwa kutumia taarifa za kijenetiki kutoka kwenye uvimbe wake wa saratani. Lengo ni kuufundisha mfumo wa kinga ya mwili kutambua na kuharibu seli za saratani iwapo zitajirudia.

    Wanasayansi walioshiriki katika utafiti huo wanasema matokeo hayo yanaweza kuwa hatua muhimu katika kuendeleza matibabu ya saratani yanayolenga mahitaji ya kila mgonjwa.

    Profesa Pippa Corey, daktari bingwa wa saratani aliyeshiriki katika utafiti huo, ameelezea matokeo hayo kuwa uthibitisho wa umuhimu wa teknolojia hiyo.

    Mbinu hiyo pia inafanyiwa majaribio kwa wagonjwa wenye aina nyingine za saratani, zikiwemo za figo, kibofu cha mkojo na mapafu.

    Hata hivyo, wataalamu huru wameonya kuwa bado kuna haja ya kufuatilia wagonjwa kwa muda mrefu zaidi ili kubaini iwapo matibabu hayo yanaongeza muda wa kuishi kwa ujumla.

    Profesa Alan Melcher wa Taasisi ya Utafiti wa Saratani amesema matokeo hayo ni ya kutia moyo, lakini mafanikio katika kutibu melanoma hayamaanishi kuwa mbinu hiyo itafanya kazi kwa kila aina ya saratani.

    Moderna na MSD zimesema zinaendelea kujadiliana na mamlaka za udhibiti kuhusu matokeo hayo, huku uwezekano wa kuwasilisha maombi ya kuidhinisha chanjo hiyo ukitarajiwa ndani ya mwaka ujao.

    Utafiti huo utaendelea kuwafuatilia wagonjwa kwa muda mrefu zaidi. Matokeo kamili yanatarajiwa kuwasilishwa katika mkutano wa saratani utakaofanyika Madrid. Hata hivyo, matokeo hayo bado hayajachapishwa katika jarida la kitaalamu la tiba linalopitia tafiti kabla ya kuchapishwa.

    Soma Pia:

  11. Marekani imetumia dola bilioni 11 kuilinda Israel - Araqchi

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araqchi, ameishutumu Marekani kwa kutumia dola bilioni 11 za fedha za walipa kodi kuunga mkono mfumo wa ulinzi wa makombora wa Israel katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.

    Katika ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wa X, Araqchi pia amedai kuwa Marekani imerusha makombora mengi zaidi ya ulinzi wa anga kuliko Israel yenyewe, katika juhudi za kuilinda nchi hiyo.

    Akihitimisha ujumbe wake, waziri huyo alizungumzia uhusiano kati ya Marekani na Israel, akisema: “Huu si uhusiano wa kunufaishana, bali ni uhusiano wa upande mmoja kuutegemea upande mwingine.”

  12. Saudi Arabia yatoa tahadhari ya mashambulizi ya makombora Riyadh

    Mamlaka ya Ulinzi wa Raia nchini Saudi Arabia imetoa tahadhari kwa wakazi wa mji mkuu Riyadh Ijumaa asubuhi, ikiwataka kuelekea maeneo salama kujilinda dhidi ya mashambulizi yaliyotarajiwa kutokea muda mfupi baadaye.

    Hata hivyo, dakika chache baadaye, mamlaka hiyo iliondoa tahadhari hiyo.

    Wakati huohuo, ilichapisha ujumbe kwenye mitandao yake ya kijamii ikipiga marufuku kurekodi video au kusambaza picha na video za mifumo ya ulinzi wa anga dhidi ya makombora na ndege zisizo na rubani.

    Baadhi ya vyombo vya habari vimeripoti kusikika kwa mlipuko katika mji wa Riyadh. Hata hivyo, hadi sasa hakuna maelezo ya kina kuhusu tukio hilo yaliyothibitishwa na mamlaka au vyanzo vingine huru.

    Pia Soma:

  13. Bei ya mafuta yapanda baada ya mashambulizi mapya Saudi Arabia

    Bei ya mafuta ghafi imepanda huku wasiwasi ukiongezeka kuwa vita katika Mashariki ya Kati vinaweza kuvuruga usambazaji wa nishati kutoka eneo hilo.

    Bei ya mafuta ya Brent imepanda kwa asilimia 0.5 hadi kufikia dola 113.75 kwa pipa, huku mafuta ya West Texas Intermediate (WTI) ya Marekani yakipanda kwa asilimia 0.7 hadi dola 100.13 kwa pipa.

    Alhamisi, Oktoba 22, bei ya mafuta ya Brent ilifunga biashara katika kiwango chake cha juu zaidi tangu Mei 4.

    Kampuni ya mafuta ya Saudi Aramco inayomilikiwa na serikali ya Saudi Arabia, iliwaagiza wafanyakazi wake kuondoka katika makao makuu yake jijini Dhahran Alhamisi, kutokana na wasiwasi wa kiusalama kufuatia mashambulizi ya hivi karibuni dhidi ya miundombinu yake ya mafuta.

    Hatua hiyo inakuja wakati mapigano kati ya Saudi Arabia, ambayo ndiyo muuzaji mkubwa zaidi wa mafuta duniani, na waasi wa Houthi nchini Yemen yakizidi kushika kasi, kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters.

    Wachambuzi wa taasisi ya kifedha ya ING wamesema katika taarifa yao ya Ijumaa kuwa masoko ya mafuta na gesi yanazidi kuwa na wasiwasi kuhusu uwezekano wa kuibuka tena kwa mvutano katika Ghuba ya Uajemi, hali inayoweza kuathiri zaidi usambazaji wa mafuta.

    Pia unaweza kusoma:

  14. Iran: Marekani haina tena udhibiti wa Mlango-Bahari wa Hormuz

    Kamanda wa Jeshi la Wanamaji la Walinzi wa Mapinduzi ya Iran, Ali Azmaei, amedai kuwa Marekani imeondoka katika Ghuba ya Uajemi.

    Katika taarifa yake, Azmaei amesema: “Leo, Wamarekani hawapo katika Ghuba ya Uajemi. Wamejiondoa hadi umbali wa kilomita 600 hadi 700 kutoka Mlango-Bahari wa Hormuz, na meli zao hazionekani katika eneo hili.”

    Ameongeza kuwa Marekani haina tena nafasi yoyote katika Mlango-Bahari wa Hormuz.

    Kauli hiyo inakuja siku mbili baada ya Marekani kuwaagiza raia wake kuondoka katika eneo la Ghuba.

    Saa chache zilizopita, Rais wa Marekani Donald Trump aliishutumu Iran kwa kujaribu kupandisha bei ya mafuta ghafi kabla ya uchaguzi wa katikati ya muhula nchini Marekani, kwa kueneza kile alichokiita habari za uongo kuhusu milipuko ya mabomu ya baharini na mashambulizi dhidi ya meli katika Mlango-Bahari wa Hormuz.

    Trump amesema kwa sasa mafuta mengi zaidi yanasafirishwa kupitia Mlango-Bahari wa Hormuz kuliko kabla ya vita, akidai kuwa Iran inajaribu kutumia njia mbalimbali kupandisha bei ya mafuta.

    Leo, bei ya pipa moja la mafuta ghafi ya Brent imepanda na kuvuka dola 113 za Marekani, kiwango cha juu zaidi katika kipindi cha miezi mitano iliyopita.

    Soma zaidi:

  15. Mamia ya raia wa Ethiopia wakimbilia Kenya baada ya mapigano kuzuka mpakani Moyale

    Shirika la Msalaba Mwekundu nchini Kenya limesema limeanza kutoa misaada ya kibinadamu kwa familia zilizokimbilia nchini Kenya baada ya mapigano kuzuka katika mji wa Moyale, mpakani mwa Ethiopia.

    Shirika hilo limesema awamu ya kwanza ya msaada huo inalenga kufikia kaya 1,000.

    Mamia ya raia wa Ethiopia, wengi wao wakiwa wanawake, watoto na vijana, wamevuka kuingia nchini Kenya tangu mapigano kuzuka siku ya Jumatano.

    Wakazi wa mji wa Moyale wamesema milio ya risasi ilikuwa bado inasikika upande wa Ethiopia hadi hapo jana.

    Soma pia:

  16. Rais Zelensky aishtumu Urusi kwa kutumia mabomu ya vishada dhidi ya Kyiv

    Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, ameishtumu Urusi kwa kutumia makombora na mabomu ya vishada katika mashambulizi yaliyofanyika usiku wa kuamkia leo.

    Watu wanne wameuawa katika mashambulizi hayo mjini Kyiv na maeneo mengine, kulingana na Wizara ya Mambo ya Kigeni ya Ukraine. Zelensky amesema watu 34, wakiwemo watoto watano, pia wamejeruhiwa.

    Katika taarifa yake kwenye mtandao wa X, Zelensky amesema,“Usiku wa kuamkia leo, Warusi wametumia makombora matatu ya balistiki yenye vichwa vya mabomu ya vishada, miongoni mwa silaha nyingine, dhidi ya Kyiv.”

    Alisema sifa ya kipekee ya makombora hayo ni kwamba hulipuka hewani yanapofika karibu na shabaha, na kushambulia kila kitu ndani ya eneo lengwa.

    Mabomu ya vishada yamepigwa marufuku katika zaidi ya nchi 100 chini ya Mkataba wa Mabomu ya Vishada, uliopitishwa mwaka wa 2008. Silaha hizi hurusha vilipuzi vidogo katika eneo kubwa, hali inayoweza kusababisha mashambulizi kulenga maeneo ya raia.

    Hata hivyo, Urusi na Marekani si miongoni mwa nchi zilizosaini mkataba huo.

    Soma pia:

  17. Maandamano yazuka Tunisia baada ya kifo cha mwanaume aliyekuwa akizuiliwa na polisi

    Polisi nchini Tunisia wametumia mabomu ya machozi kuwatawanya waandamanaji katika eneo la Ettadhamen, viungani mwa mji mkuu,Tunis, baada ya kifo cha mwanamume aliyekuwa amezuiliwa kwa tuhuma za kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya.

    Kumekuwa na makabiliano kati ya polisi na waandamanaji katika miji miwili ya kusini mwa Tunisia.

    Makabiliano ya hapo jana yametokea wakati nchi hiyo inakabiliwa na kuongezeka kwa mgogoro wa kiuchumi, kijamii na kisiasa, hali inayozidisha hofu ya kutokea kwa wimbi kubwa zaidi la maandamano kutokana na hasira za wananchi kuhusu kudorora kwa hali ya maisha na huduma duni za umma.

    Familia ya mwanamume huyo imesema alifariki kutokana na vitendo vya ukatili wa maafisa wa polisi baada ya kukamatwa. Familia hiyo imetaka mazingira ya kifo chake yafafanuliwe na waliohusika wawajibishwe.

    Hata hivyo, vyombo vya habari vya eneo hilo vimeripoti kuwa mwanamume huyo alifariki baada ya kumeza dawa za kulevya. Wizara ya Mambo ya Ndani ya Tunisia bado haijatoa maoni kuhusu tukio hilo.

    Soma pia:

  18. Trump aishtumu Iran kwa kuchochea kupanda kwa bei ya mafuta

    Rais wa Marekani Donald Trump ameishtumu Iran kwa kufanya kila juhudi kuongeza bei ya mafuta kabla ya uchaguzi wa katikati ya muhula wa Bunge la Marekani.

    Trump amesema kuwa Iran inatunga taarifa kuhusu mashambulizi, mabomu ya baharini na matukio mengine katika Mlango Bahari wa Hormuz, akidai kuwa hatua hizo zinalenga kupandisha bei ya mafuta.

    Katika ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wake wa Truth Social, Trump amesema kiasi cha mafuta kinachosafirishwa kupitia Mlango Bahari wa Hormuz kwa sasa ni kikubwa kuliko ilivyokuwa awali kabla ya kuanza kwa mzozo huo.

    Kauli hiyo inajiri huku Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi la Iran likitishia kulenga kambi za kijeshi za Marekani zilizoko Mashariki ya Kati iwapo jeshi la Marekani litaendelea kusindikiza meli zinazopita katika Mlango Bahari wa Hormuz.

    Iran imezuia usafirishaji wa meli katika njia hiyo muhimu kwa usambazaji wa nishati duniani tangu kuanza kwa vita tarehe 28 Februari, huku ikishambulia mara kwa mara meli zinazojaribu kupita katika Mlango-Bahari wa Hormuz bila idhini yake.

    Soma pia:

  19. Eneo la Tibet lashuhudia tetemeko kubwa la ardhi, zaidi ya watu 16 wamefariki

    Tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa kipimo cha 7 katika kipimo cha Richter, limetokea eneo la Nagqu, eneo kubwa la milima kaskazini mashariki mwa Lhasa, mji mkuu wa Tibet, hii ni kulingana taarifa za vyombo vya habari vya eneo hilo.

    Takriban watu 16 wamefariki dunia, huku idadi ya waliojeruhiwa ikifikia 65, wakiwemo watu 11 waliojeruhiwa vibaya.

    Mamia ya nyumba zimebomoka katika eneo hilo, barabara na huduma za umeme zimekatika katika maeneo yaliyoathiriwa.

    Kulingana na shirika la habari la serikali ya China,Xinhua, takriban nyumba 339 zimebomoka, huku tathmini ya kiwango cha uharibifu ikiendelea.

    Hili ndilo tetemeko la ardhi lililosababisha vifo vingi zaidi katika eneo hilo tangu mwaka wa 2023, ambapo watu 120 walifariki kufuatia tetemeko la ukubwa wa 6.2 katika mkoa jirani wa Gansu nchini China.

    Rais wa China, Xi Jinping, ametoa agizo la kuanzishwa kwa operesheni kubwa ya uokoaji kufuatia tetemeko hilo.

    Tibet ni mojawapo ya maeneo yanayofuatiliwa kwa karibu zaidi nchini China. Upatikanaji wa taarifa katika eneo hilo unadhibitiwa kwa kiasi kikubwa na serikali ya China, huku uandishi huru wa habari ukikabiliwa na vikwazo vingi.

    Soma pia: