Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
BBC: Jinsi hospitali zilivyolengwa makusudi na wapiganaji wa RSF Sudan
Uchunguzi wa BBC umebaini ushahidi kwamba wapiganaji wa kikosi cha kijeshi cha Rapid Support Forces (RSF) waliharibu mfumo wa huduma za afya wa mji wa el-Fasher wakati wa kuuzingira kwa muda mrefu na baada ya kuuteka mji huo katika eneo la Darfur mwaka mmoja uliopita.
Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Türk, alielezea matokeo hayo kuwa "ya kutia wasiwasi mkubwa", akisema mashambulizi mengi ya RSF dhidi ya miundombinu ya kiraia, ikiwemo hospitali na vituo vya afya, ni ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa za kibinadamu na yanaweza kufikia kiwango cha uhalifu wa kivita.
RSF imekataa matokeo ya uchunguzi huo. Waziri wa afya wa kundi hilo la kijeshi alisema madai hayo ni propaganda na jaribio la makusudi la jeshi la taifa la Sudan pamoja na washirika wake kuchafua sifa ya RSF.
Kwa kutumia vyanzo vilivyokuwa ndani ya el-Fasher, BBC imebaini taarifa za takribani mashambulizi 43 tofauti dhidi ya hospitali na maeneo ya huduma za afya kati ya Mei 2024 na Oktoba 2025, huku baadhi ya vituo vikishambuliwa mara kadhaa.
Kwa mujibu wa sheria za kimataifa, ni kinyume cha sheria kushambulia vituo vya afya au wafanyakazi wake wakati wa vita.
Uchunguzi huo pia umeonesha athari kubwa kwa wahudumu wa afya katika mji huo wa magharibi mwa Sudan. Kati ya Aprili 2023 na Oktoba 2025, takwimu za BBC zinaonesha kuwa wahudumu 120 walijeruhiwa, 55 waliuawa, na 10 walitoweka kwa kulazimishwa au kutekwa nyara.
"RSF walikuwa wakijaribu kuziondoa hospitali kwenye huduma na kuzifanya zishindwe kufanya kazi, kwa sababu mfumo wa afya ndiyo nguzo kuu ya mji wowote au taifa lolote," alisema Dk. Muhamed Suliman, daktari bingwa wa upasuaji ambaye alikuwa akifanya kazi el-Fasher wakati wa kuzingirwa kwa mji huo.
"RSF ilianza kushambulia maeneo haya, hivyo raia hawakuwa tena na njia yoyote ya kuendelea kuishi huko. Mashambulizi yalikuwa makali. Yalifanywa kwa makusudi. Yalipangwa."
Uchunguzi huu umekuja mwaka mmoja baada ya kuanguka kwa mji wa el-Fasher, moja ya sura za kikatili zaidi za vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyozuka mwezi Aprili 2023 kati ya RSF na jeshi la Sudan.
Pande zote mbili zimetuhumiwa kwa kushambulia vituo vya afya.
Mwezi Machi 2026, Shirika la Afya Duniani (WHO) lililaani bomu lililoipiga Hospitali ya al-Daein iliyoko katika eneo linalodhibitiwa na RSF mashariki mwa Darfur.
Shambulio hilo liliua watu kadhaa na kulazimisha hospitali kufungwa. Inaaminika kuwa jeshi la Sudan lilitekeleza mashambulizi hayo kwa kutumia ndege zisizo na rubani, ingawa limekanusha kuhusika.
Hata hivyo, WHO imesema matukio yaliyotokea el-Fasher yanawakilisha "moja ya mifano iliyo wazi zaidi na mibaya zaidi ya athari pana za vita kwa huduma za afya nchini Sudan."
Wachunguzi wa Umoja wa Mataifa wameripoti kuwa mapigano ya el-Fasher yalikuwa na "dalili za mauaji ya kimbari", ambapo uhasama wa muda mrefu wa kikabila umeshuhudia wanamgambo wa Kiarabu, ambao sasa ni uti wa mgongo wa vikosi vya RSF, wakilenga makundi yasiyo ya Kiarabu kama yale yanayoishi katika mji huo.
Uchunguzi wa BBC umefichua kwa mara ya kwanza mlolongo wa kina wa mashambulizi dhidi ya sekta ya afya wakati wa kuzingirwa kwa muda mrefu kwa mji wa el-Fasher.
Baadhi ya vituo vya afya mjini el-Fasher vilifungwa ndani ya wiki chache baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan kuanza mwezi Aprili 2023.
Muhimu zaidi, mojawapo ya hospitali kuu za mji huo, Hospitali ya Kufundishia , iliyokuwa katika eneo la mapigano katikati ya mji, ililazimika kusitisha huduma zake.
Huduma zake zilihamishiwa South Hospital ya el-Fasher. Huko, huduma za afya ziliendelea kutolewa, ingawa zilikuwa zikikumbwa na changamoto kubwa za kukatika kwa umeme na upungufu wa vifaa tiba.
Hali ilibadilika kwa kiwango kikubwa mwaka mmoja baadaye wakati RSF ilipoanzisha kuizingira el-Fasher.
Mwishoni mwa Mei na mwanzoni mwa Juni 2024, Hospitali ya Kusini ilishambuliwa kwa mabomu mara kadhaa huku wapiganaji wa RSF wakisonga mbele kutoka maeneo yao ya mashariki mwa mji.
Dk. Suliman anasema shambulio la kwanza lilikuja kama mshtuko mkubwa.
Eneo la hospitali lililopigwa lilikuwa "limejaa watu wengi sana kwa sababu ilikuwa hospitali pekee iliyokuwa ikifanya kazi mjini humo na kutoa huduma za upasuaji," alisema.
Siku hiyo, wafanyakazi wa afya walifanya upasuaji kwa wagonjwa 16 waliojeruhiwa, aliongeza.
Mashambulizi hayo yalifikia kilele kwa uvamizi wa RSF tarehe 8 Juni. Wafanyakazi wa hospitali walikamatwa na mshangao; wengi wao walitoroka kwa kuruka ukuta wa nyuma wakati wapiganaji wa RSF walipoingia ndani ya jengo, anasema Dkt. Mustafa Ahmed, mtaalamu wa dawa.
Hata hivyo, mkurugenzi mkuu wa hospitali hiyo, daktari bingwa wa upasuaji Izzeldin Ahmed Dawaud Asow, alikutana na kundi la wanamgambo hao nje ya ofisi yake.
Anasema hawakujua kuwa yeye ni daktari, lakini walimtukana kwa maneno ya kibaguzi ya kikabila.
"Hakuna raia hapa. Nyinyi ni Falangi," walisema, wakitumia neno la dharau linalodokeza kwamba Wasudani wasiokuwa Waarabu ni wageni.
Dkt. Asow anasema alipigwa kwa vitako vya bunduki na kupoteza fahamu kwa muda. Hatimaye aliokoa maisha yake kwa kujifanya amekufa.
"Waliweka mkono wao kifuani kwangu, nami nikasimamisha kupumua. Kisha wakasema: 'Mwache, mwache. Huyu taka tayari amekufa. Mwacheni.' Wakaniacha," alisema.
Siku hiyo hiyo, RSF ilifukuzwa eneo hilo na jeshi la Sudan pamoja na washirika wake. Dkt. Asow alirudi hospitalini na kukuta miili ya wagonjwa kadhaa, huku vifaa vya upasuaji katika chumba chake cha upasuaji vikiwa vimeharibiwa kabisa, alisema.
Hospitali hiyo ilifungwa na baadaye ikaangukia mikononi mwa RSF baada ya jeshi kujiondoa.
Dk. Alaa Eldin Nugud, daktari bingwa wa upasuaji wa Sudan ambaye amejiunga na serikali ya kiraia inayoungwa mkono na RSF kama Waziri wa Afya, alisisitiza kuwa South Hospital ilikuwa ikitumika kama kambi ya kijeshi.
Kwa mujibu wa sheria za kimataifa, hospitali zinaweza kupoteza ulinzi wake ikiwa zinatumiwa na upande mmoja wa mgogoro kufanya "kitendo kinachomdhuru adui".
Katika mahojiano na BBC, Dk. Nugud alisema kuwa mitambo ya kurushia makombora ilikuwa imewekwa ndani ya eneo la hospitali. Pia alishiriki video iliyoonesha mabaki ya silaha, iliyorekodiwa zaidi ya mwaka mmoja baada ya hospitali kufungwa, akisema kuwa video hiyo inaunga mkono madai yake.
Aidha, alituonesha kile alichodai kuwa ni ramani za maeneo yaliyowekewa mabomu ya ardhini kuzunguka Teaching Hospital, ambayo iko karibu na makao makuu ya jeshi la Sudan.
Madaktari waliiambia BBC kwamba hospitali hiyo haikuwa sehemu ya kambi ya kijeshi na kwamba waliitembelea wakati wa vita kwa ajili ya kuchukua vifaa vya matibabu.
BBC haijapata ushahidi wowote huru unaothibitisha madai ya Dk. Nugud. Serikali ya eneo la Darfur pia ilikataa madai hayo kabisa.
Baada ya Hospitali ya Kusini kufungwa, wafanyakazi wake na vifaa vilivyobaki vilihamishiwa katika Hospitali ya Wazazi ya Saudi iliyoko magharibi mwa jiji, ambako jeshi lilikuwa na ngome zake kuu.
Ndani ya siku chache, kasi ya mashambulizi dhidi ya kituo hicho iliongezeka. Katika hatua hii, shirika la madaktari wasio na mipaka, Médecins Sans Frontières (MSF) lilitoa tahadhari.
"Hatujui kama hospitali zinashambuliwa kwa makusudi, lakini wapiganaji hawaoneshi kuchukua tahadhari zozote za kuzilinda hospitali," lilisema shirika hilo katika taarifa.
Hata hivyo, katika uchunguzi wetu, tulizungumza na madaktari sita ambao walieleza kuwepo kwa mtindo wa mashambulizi ya kimfumo dhidi ya vituo vya afya.
Walituambia jinsi Hospitali ya Saudi ilivyoshambuliwa mara kwa mara. Siku nyingine ilishambuliwa hadi mara 25, kwa mchanganyiko wa mashambulizi ya mizinga na ndege zisizo na rubani (drones). Drones hizo zilitumia kile walichokiita "makombora yenye akili", ambayo yana uwezo wa kulenga shabaha kwa usahihi mkubwa.
Vituo vidogo vya afya pia vilikumbwa na mashambulizi. Mlolongo wa matukio uliorekodiwa na BBC unaonyesha jinsi hospitali binafsi na zahanati za mitaani zilivyolazimika kufungwa hatua kwa hatua.
Aidha, baadhi ya taasisi hizo za afya zilipojaribu kuhamishia huduma zao katika maeneo mengine, maeneo hayo mapya nayo yalishambuliwa.
Hospitali Maalum ya Watoto, ambayo ilifungwa mwanzoni mwa vita pamoja na Hospitali ya Kufundishia, ilihamia katika maeneo mawili tofauti. Hata hivyo, maeneo yote mawili yalishambuliwa kwa mabomu na kulazimika kufungwa.
Vilevile, kituo kikuu cha huduma za usafishaji damu (dialysis) kilishambuliwa, na baada ya kuhamishiwa eneo jingine, kililengwa tena kwa mashambulizi.
Kufikia wakati RSF ilipoteka mji huo mwezi Oktoba 2025, Hospitali ya Saudi ndiyo iliyokuwa kituo pekee cha afya kilichokuwa bado kinatoa huduma.
Wahudumu wa afya waliokuwa wakifanya kazi hapo waliunganisha nguvu zao ili kuendelea kuhudumia wagonjwa licha ya hali kuwa mbaya zaidi siku hadi siku.
Madaktari walieleza jinsi walivyoweka mifuko ya mchanga kuzunguka jengo ili kulilinda dhidi ya mashambulizi.
Pia walijenga makazi ya chini ya ardhi kwa kutumia makontena ya chuma na kuanzisha maeneo mbadala ya kupokea wagonjwa, kuwahifadhi na kufanya upasuaji, huku tishio la mashambulizi na uharibifu wa jengo kuu ukiendelea kuongezeka.
Dk. Asow alisema kuwa kituo hicho cha muda cha upasuaji kilishambuliwa mara tano mwaka 2025.
Katika tukio moja, alisema alikuwa akimfanyia mgonjwa upasuaji wa shingo wakati mlipuko ulipotikisa jengo zima. Wahudumu wengine wa afya walikimbia nje kwa hofu, lakini yeye alibaki kuendelea na upasuaji.
Katika tukio jingine, wafanyakazi wa afya walikuwa wamejiandaa kufanya upasuaji katika chumba cha upasuaji. Hata hivyo, Dk. Asow aliwaelekeza wamhamishie mgonjwa sehemu nyingine kwa sababu chumba hicho kilihitaji kusafishwa kwa kina kutokana na idadi kubwa ya wagonjwa waliokuwa wakihudumiwa.
Muda mfupi baadaye, chumba hicho kiliharibiwa kabisa na makombora ya mizinga. Kwa bahati nzuri, mgonjwa huyo alinusurika.
"Kuanzia siku hiyo, baadhi ya wafanyakazi wangu walianza kuniita 'Bwana Usafi wa Kina' kwa sababu wanaamini kwamba uamuzi wa kufanya usafi wa kina ndio uliookoa maisha ya mgonjwa huyo," alisema.
Dk. Asow pia alieleza jinsi ndege zisizo na rubani zilivyokuwa zikifuatilia mienendo ya wagonjwa.
Alisema kwamba tarehe 15 Machi 2025, watu waliokuwa wakiwabeba majeruhi kutoka eneo la shambulio kwenda katika moja ya wodi za muda walifuatiliwa na droni ya kivita.
Kwa mujibu wake, droni hiyo ilishambulia walipofika kwenye lango la jengo hilo, na kuua watu tisa.
Pia aliiambia BBC kwamba tarehe 17 Agosti 2025, mkokoteni wa punda ulikuwa ukitumiwa kuwasafirisha wagonjwa kwenda kwenye chumba mbadala cha upasuaji kwa sababu magari yote ya wagonjwa yalikuwa tayari yameharibiwa.
Alisema mkokoteni huo ulishambuliwa na droni, na kusababisha vifo vya wagonjwa wawili, dereva wa mkokoteni pamoja na punda aliyekuwa akiuvuta.
Waziri wa afya wa RSF alipuuza madai hayo, akiyataja kuwa ni "muendelezo wa uongo" unaosambazwa na Jeshi la Sudan (SAF) pamoja na washirika wake wa eneo hilo wanaojulikana kama Jeshi la pamoja.
"Hata wahudumu wa afya, na watu wengi waliokuwepo, kutokana na mgogoro huu, masuala haya ya kikabila na ubaguzi wa rangi, walikuwa wakiiunga mkono Jeshi la Pamoja na Jeshi la Sudan (SAF). Ndiyo maana huwezi kutegemea simulizi hiyo pekee," alisema.
Madaktari waliiambia BBC kwamba waliamini wapiganaji wa RSF walilenga kwa makusudi vituo vya afya kwa sababu baadhi ya wagonjwa waliokuwa wakitibiwa humo walikuwa wanajeshi au wapiganaji washirika wa jeshi la serikali.
Msururu huo wa mashambulizi ya mizinga na mabomu ulifikia kilele tarehe 25 Oktoba 2025, wakati wapiganaji wa RSF walipoivamia Hospitali ya Saudi, katikati ya madai ya mauaji makubwa yaliyosababisha vifo vya zaidi ya wagonjwa 460 na watu waliokuwa wameandamana nao.
RSF imekanusha kwamba mauaji hayo ya halaiki yalitokea. Hata hivyo, Shirika la Afya Duniani (WHO) lililaani vikali mauaji yaliyoripotiwa, huku picha za satelaiti zikionekana kuonesha makundi ya miili kwenye maeneo ya hospitali yaliyokuwa yametapakaa damu.
BBC ilishirikisha maelezo ya uchunguzi wake na Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, ambaye alisema matokeo hayo yalikuwa "ya kutisha sana" na yanaendana na uchambuzi uliofanywa na ofisi yake.
"Ufuatiliaji na nyaraka zetu unaonesha kuwa RSF ilishambulia mara kwa mara hospitali kuu za el-Fasher pamoja na vituo vya muda vya afya, ikiviharibu au kuvitia uharibifu mkubwa na kuathiri kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa huduma za afya kwa maelfu ya raia waliokwama ndani ya mji huo," alisema Türk.
Kwa sasa, huduma za afya mjini el-Fasher zinaendeshwa na serikali inayoungwa mkono na RSF. Serikali hiyo imetoa video kadhaa zikionesha kuwa Hospitali ya Saudi na Hospitali ya Kufundishia zimefunguliwa tena, zimesafishwa, na zimeanza kuhudumia baadhi ya wagonjwa.
Dk. Nugud alisema pia kuwa Hospitali ya South inatarajiwa kufunguliwa tena hivi karibuni. Alikanusha madai kwamba madaktari walitekwa na kulazimishwa kufanya kazi, akiiambia BBC kwamba waliamua kubaki kwa hiari yao ili kuendelea kutoa huduma za matibabu.
"Nina video nikiwa mbele ya Hospitali ya Watoto, wakati tulipomwokoa daktari bingwa mmoja, daktari mwingine pamoja na wafanyakazi sita wa afya ambao walikuwa wakifanya kazi na SAF. Baadaye, wakati el-Fasher ilipokombolewa, wote walisamehewa.
"Sisi tuliwaweka huru," alisema.
BBC ilizungumza na mmoja wa madaktari waliokuwa kwenye video hiyo, Dk. Al-Haj Mohamed Ahmed. Alituambia kwamba hakuwa na hiari yoyote kuhusu uwepo wake hapo.
"Nililazimishwa kuwepo hapo. Ikiwa ningesema jambo ambalo halingewafurahisha, wangenipiga risasi kichwani," alisema.
Alikuwa miongoni mwa wahudumu kadhaa wa afya waliokamatwa walipokuwa wakijaribu kutoroka mji huo na kisha kurudishwa, pamoja na Dk. Mustafa Ahmed.
Madaktari hao walijitokeza kwa uwezo wao wa kudhibiti mlipuko wa kipindupindu uliokuwa umezuka katika gereza la muda lililokuwa ndani ya hospitali ya watoto. Baada ya kufanikiwa kusaidia kukabili mlipuko huo, walipelekwa kufanya kazi katika Hospitali ya Saudi.
"Walianza kusema kwamba ninyi ni watu wa mji huu, na sisi tumeuteka mji huu, hivyo tunapaswa kufanya kazi pamoja kwa ajili ya manufaa ya mji," alisema Dk. Mustafa Ahmed.
Dk. Mustafa Ahmed pia alieleza hali mbaya iliyokuwapo gerezani, akisema kwamba kwa siku kadhaa mfululizo alikuwa akiamka asubuhi na kukuta wafungwa 50 wamefariki kutokana na kipindupindu.
Mwaka mmoja baada ya kuanguka kwa el-Fasher, majeraha ya kisaikolojia na kumbukumbu za kipindi hiki cha giza katika vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Sudan bado yanaendelea kuwa makali na yenye uchungu kwa walioathirika.
Mstari wa mbele wa mapigano sasa umehamia maeneo mengine, lakini hakuna dalili zozote za kupatikana kwa suluhisho la haraka la mzozo huo.
Wakati huo huo, mashambulizi dhidi ya vituo vya afya yanaendelea, yakiwa sehemu ya mgogoro mpana wa kibinadamu ambao umesababisha maafa makubwa.