Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Marekani na Iran zajadili duru ya pili ya mazungumzo kukiwa na wasiwasi wa muda wa usitishaji mapigano

Msemaji wa Ikulu ya White House Karoline Leavitt amesema mazungumzo ya kurefusha makubaliano ya kusitisha mapigano kwa zaidi ya wiki mbili yamekuwa yenye tija na yanayoendelea.

Moja kwa moja

Na Mariam Mjahid

  1. Lebanon yatilia shaka madai ya mazungumzo ya Trump

    Afisa katika ofisi ya rais wa Lebanon ameiambia BBC kuwa nchi hiyo haina taarifa yoyote kuhusu mawasiliano yajayo na Israel, kufuatia ujumbe wa Rais wa Marekani Donald Trump uliodokeza uwezekano wa mazungumzo kati ya viongozi wa mataifa hayo mawili.

    Trump alisema usiku uliopita kuwa mazungumzo kati ya viongozi wa Israel na Lebanon yanatarajiwa kufanyika “leo”.

    Siku ya Jumanne, maafisa wa Israel na Lebanon walifanya mazungumzo mjini Washington, D.C., ikiwa ni mara ya kwanza kwa pande hizo kufanya mazungumzo ya moja kwa moja tangu mwaka 1993.

    Lebanon ilielezea mazungumzo hayo kuwa “yenye tija”, huku Israel ikisema kuwa pande zote ziko “upande mmoja wa mlinganyo”, ingawa mashambulizi ya Israel dhidi ya kundi la Hezbollah yanaendelea.

  2. Marekani yakamata meli yenye bendera ya Iran

    Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani (CENTCOM) imesema kuwa imekamata meli ya mizigo yenye bendera ya Iran iliyokuwa ikijaribu kukwepa marufuku iliyowekwa kwa meli zote zinazoingia au kutoka katika bandari za Iran.

    CENTCOM ilisema meli hiyo ilikamatwa Jumanne baada ya kuondoka katika mji wa bandari wa Bandar Abbas na kupita katika Mlango-Bahari wa Hormuz.

    Pia iliongeza kuwa meli ya Jeshi la Wanamaji la Marekani, USS Spruance, ilifanikiwa kuigeuza mwelekeo meli hiyo, ambayo sasa inarejea Iran.

    CENTCOM ilisema pia kuwa imezirudisha nyuma meli 10 kuelekea Iran, na kwamba hakuna meli iliyokiuka zuio hilo tangu lilipoanza kutekelezwa Jumatatu.

  3. Uingereza yasema mzozo wa kijeshi wa Marekani dhidi ya Iran ulikuwa kosa

    Waziri wa Fedha wa Uingereza Rachel Reeves amesema kuwa kumalizika kwa mazungumzo ya kidiplomasia na Iran na kuanza kwa mzozo wa kijeshi ni kosa lililofanywa na Marekani.

    Akizungumza na kipindi cha CNBC cha Invest in America, Rachel Reeves alisema kwamba “sera bora ya kiuchumi kwa sasa, si tu kwa Uingereza bali kwa dunia nzima, ni kupunguza mvutano.”

    Serikali ya Uingereza imesema kuwa haitashiriki katika kizuizi cha kijeshi cha Marekani katika Mlango-Bahari wa Hormuz ili kuongeza shinikizo kwa Iran.

    Alipoulizwa kama tofauti zinazoongezeka kati ya Marekani na Uingereza kuhusu mzozo huo zimeathiri uhusiano maalum kati ya nchi hizo mbili, Rachel Reeves alikataa hilo, akisema halijawa na athari.

    Hata hivyo, alisema pia kwamba “kuna nafasi ya kutofautiana kati ya marafiki.”

  4. Idara ya Hazina ya Marekani yatangaza vikwazo vipya dhidi ya Iran

    Idara ya Hazina ya Marekani imetangaza msururu wa vikwazo vipya dhidi ya watu binafsi, mashirika na meli zinazohusishwa na Iran.

    Kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa kwenye tovuti ya idara hiyo, vikwazo vimewekwa dhidi ya watu watatu, meli tisa na taasisi 17, ambapo neno “taasisi” linaweza kujumuisha kampuni au mashirika mbalimbali.

    Katika taarifa yake, Idara ya Hazina ya Marekani imesema imeweka vikwazo dhidi ya mtandao wa usafirishaji mafuta unaoendeshwa na Mohammad Hossein Shamkhani, mtoto wa afisa wa zamani wa usalama wa Iran Ali Shamkhani.

    Anatuhumiwa kuhusika katika usafirishaji na uuzaji wa mafuta ya Iran kupitia mtandao mpana wa majini.

    Kwa mujibu wa maafisa wa Marekani, mtandao huo umeingiza mapato ya mabilioni ya dola.

    Idara hiyo pia imeweka vikwazo dhidi ya malengo yanayohusishwa na mpango tata wa kifedha unaohusishwa na kundi la Lebanon la Hezbollah, unaodaiwa kupangwa kupitia vituo vya kubadilisha dhahabu na hatimaye kunufaisha utawala wa kijeshi wa Iran.

    Kwa mujibu wa maafisa wa Marekani, mpango huo unahusisha kubadilisha akiba ya dhahabu kuwa fedha taslimu, ambazo hutumika kufadhili shughuli za Hezbollah huku ukikwepa vikwazo kupitia mitandao ya biashara na usambazaji.

    Soma zaidi:

  5. Mohsen Rezaei: Sikubaliani na kuongeza muda wa usitishaji mapigano

    Mohsen Rezaei, mwanachama wa Baraza la Uamuzi wa Maslahi ya Mfumo nchini Iran, amesema: “Hatutauacha Mlango wa Hormuz hadi haki zetu zitakapopatikana kikamilifu.”

    Rezaei, ambaye pia aliwahi kuwa Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi (IRGC), amesema katika mahojiano yake mapya yaliyoripotiwa na vyombo vya habari vya ndani ya Iran: “Tofauti na Wamarekani wanaoogopa vita vya muda mrefu, sisi tumejiandaa kikamilifu na tumezoea vita vya muda mrefu.”

    Katika mahojiano hayo, akirejelea kauli za Donald Trump na Waziri wa Vita wa Marekani Pete Hegseth kuhusu kuharibiwa kwa Jeshi la Wanamaji la Iran, alihoji: “Ikiwa Jeshi la Wanamaji la Iran limeharibiwa, kwa nini Marekani haijathubutu kupita katika Mlango wa Hormuz?”

    Rezaei pia amesisitiza kuwa licha ya kufuata maamuzi ya viongozi wa nchi, maoni yake binafsi ni kwamba Iran haipaswi kukubali kurefushwa kwa usitishaji mapigano wa wiki mbili na Marekani.

    Soma zaidi:

  6. Israel yaendelea na operesheni dhidi ya Hezbollah nchini Lebanon - Netanyahu

    Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema Jeshi la nchi yake linaendelea na operesheni dhidi ya wanamgambo wanaoungwa mkono na Iran Hezbollah nchini Lebanon licha ya shinikizo la kimataifa kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano.

    Bwana Netanyahu amesema majeshi ya Israel yako karibu kuudhibiti mji wa kusini mwa Lebanon wa Bint Jbeil ambao anautaja kuwa ngome ya Hezbollah.

    Baraza la Mawaziri la Israel linaripotiwa kukutana kujadili uwezekano wa kufikiwa makubaliano ya kusitisha mapigano lakini bado hakujatangazwa uamuzi wao kuhusiana na hilo.Iran inasisitiza kuwa Lebanon sharti ijumuishwe katika makubaliano yoyote ya kuvimaliza vita vya Mashariki ya Kati.

    Soma zaidi:

  7. Papa Leo akemea ufisadi, aihimiza Cameroon kuheshimu haki za binadamu

    Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Leo ametoa wito kwa Serikali ya Cameroon kupambana dhidi ya ufisadi.

    Baada ya kukaribishwa kwa vifijo na nderemo na maelfu ya waumini waliojitokeza katika Mji Mkuu Yaounde, Papa Leo aliwahutubia viongozi wa Serikali akiwemo Rais wa muda mrefu wa Cameroon Paul Biya akiwataka viongozi wa nchi hiyo kuzisuta nafsi zao, kuvunja minyororo ya ufisadi na kuheshimu haki za binadamu.

    Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki amesema viongozi wanapaswa kuwa madaraja na sio chanzo cha migawanyiko.

    Asasi za kiraia zimelaani ukandamizaji unaofanywa na Serikali dhidi ya wanaopinga kuchaguliwa tena kwa muhula wa nane kwa Rais Biya katika uchaguzi uliofanyika mwezi Oktoba mwaka jana.

    Soma zaidi:

  8. Marekani na Iran zajadili duru ya pili ya mazungumzo kukiwa na wasiwasi wa muda wa usitishaji mapigano

    Marekani imesema inajadili uwezekano wa kufanyika duru ya pili ya mazungumzo ya kutafuta amani na Iran.

    Gazeti la Wall Street Journal limeripoti kuwa pande hizo mbili zimefikia makubaliano ya awali ya kukutana tena, ingawa muda na mahali pa mkutano huo havijabainishwa. Hata hivyo, Tehran imesema kuwa “misimamo ya Marekani inayobadilika na kukinzana inafanya kuwa vigumu kudumisha uaminifu wa makubaliano yoyote.”

    Msemaji wa Ikulu ya White House amekanusha taarifa kwamba Marekani iliomba kurefushwa rasmi kwa usitishaji mapigano na Iran, akisema madai hayo “si ya kweli.”

    Caroline Leavitt amesema, “tunaendelea kushiriki kikamilifu katika mazungumzo haya,” na kuongeza kuwa mazungumzo hayo ni “ya kujenga na yanaendelea.”

    Akijibu taarifa kuhusu uwezekano wa mazungumzo ya moja kwa moja kati ya Iran na Marekani, Leavitt alisema: “Majadiliano haya yanaendelea, lakini hakuna jambo lililo rasmi hadi litakapotangazwa hapa Ikulu ya White House.”

    Aliongeza kuwa iwapo mazungumzo yatafanyika, kuna uwezekano mkubwa yakafanyika katika eneo lile lile la duru ya kwanza, yaani Islamabad, mji mkuu wa Pakistan.

    Leavitt pia alisema kuwa kutekeleza matakwa ya Donald Trump, ambayo aliyataja kuwa “wazi na yasiyo na utata,” kutakuwa “kwa manufaa ya Iran.”

    Ujumbe kutoka Pakistan ukiongozwa na mkuu wa majeshi Asim Munir uko Tehran kama sehemu ya juhudi za upatanishi.

    Duru ya kwanza ya mazungumzo iliyofanyika mwishoni mwa juma lililopita mjini Islamabad, ilifeli kufikia makubaliano yoyote ya kuumaliza mzozo wa Mashariki ya Kati uliozuka tangu mwishoni mwa mwezi wa Februari.

    Soma zaidi:

  9. Hujambo na karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja ya Alhamisi ya tarehe 16 Aprili 2026.