Burudani tupu, mabao tele: Ligi ya Mabingwa yaweka rekodi mpya

Chanzo cha picha, Getty Images
Tangu kuanzishwa kwa mfumo mpya wa Ligi ya Mabingwa Ulaya mwanzoni mwa msimu wa 2024-25, mashindano hayo yamekuwa yakitoa kila kitu ambacho mashabiki wanakipenda. Lakini jambo linalojitokeza zaidi msimu huu ni ongezeko kubwa la mabao.
Mabao 187 yamefungwa kufikia sasakatika michuano hiyo, wastani wa mabao 4.16 kwa kila mechi, kiwango cha juu zaidi kuwahi kushuhudiwa katika historia ya Ligi ya Mabingwa.
"Angalia idadi ya mabao yanayofungwa, ni jambo la kushangaza," alisema winga wa zamani wa Manchester United na England, Ashley Young, kupitia BBC Radio 5 Live. "Washambuliaji wamekuwa makini sana mbele ya lango."
Beki wa zamani wa Liverpool, Stephen Warnock, naye alieleza idadi hiyo ya mabao kuwa "ya ajabu". Lakini je, hali hii ni ya kipekee?
Takwimu zafichua nini?
Wastani wa sasa wa mabao kwa kila mechi si rekodi tu katika historia ya Ligi ya Mabingwa, bali pia ni wa tatu kwa ubora katika historia yote ya Kombe la Ulaya. Ni misimu miwili pekee, 1955-56 (4.38) na 1959-60 (4.19), iliyorekodi wastani mkubwa zaidi.
Mabao yanaendelea kunyesha kwa kasi isiyo ya kawaida. Jumanne, mabao 40 yalifungwa katika mechi tisa pekee.
Hata hivyo, siku ya kuvutia zaidi ilikuwa Jumatano iliyopita, ambapo mabao 46 yalifungwa, idadi ya tatu kwa ukubwa kuwahi kushuhudiwa ndani ya siku moja katika historia ya mashindano hayo.
Kwa pamoja, mechi za Jumanne na Jumatano wiki iliyopita zilizalisha mabao 78, na kuifanya raundi ya pili ya mechi kuwa ya mabao mengi zaidi kuwahi kurekodiwa.
Jumla hiyo ilikuwa mabao tisa zaidi ya yale 69 yaliyofungwa katika raundi ya kwanza ya msimu huu. Wakati huo, raundi hiyo ilikuwa tayari imeweka rekodi ya pili ya mabao mengi tangu kuanzishwa kwa mfumo mpya wa hatua ya ligi mwaka 2024-25.
Swali ni je, rekodi nyingine itavunjwa tena wiki hii?
Soma pia:




























