Kenya yathibitisha visa vinne vipya vya Ebola, idadi yafikia saba

f
Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 3

Wizara ya Afya nchini Kenya imethibitisha visa vinne vipya vya Ebola inayosababishwa na virusi vya Bundibugyo, na kufikisha jumla ya visa saba vilivyothibitishwa, akiwemo mgonjwa wa kwanza aliyefariki dunia.

Visa hivyo vipya vinamhusisha ndugu wa karibu wa kiume wa mgonjwa aliyefariki na wahudumu watatu wa afya waliomhudumia mgonjwa huyo hospitalini kati ya tarehe 3 na 4 Oktoba 2026, haya ni kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa Afya, Dkt. Patrick Amoth.

Kwa mujibu wa wizara hiyo, wagonjwa wote wanne walianza kuonyesha dalili za homa, wakatengwa mara moja na kufanyiwa vipimo katika Maabara ya Kitaifa ya Marejeo ya Virology na maabara ya Taasisi ya Utafiti wa Kimatibabu nchini Kenya, KEMRI. Vipimo vyao vyote vilithibitisha maambukizi ya Ebola ya virusi vya Bundibugyo.

Aidha Wizara hiyo imesema wagonjwa hao kwa sasa wanapatiwa matibabu ya kusaidia mwili kukabiliana na ugonjwa huo katika kituo maalumu cha matibabu.

"Wagonjwa wa pili na wa tatu wako katika hali nzuri na wanaendelea kuitikia vyema matibabu ya kusaidia mwili kukabiliana na ugonjwa huo," wizara hiyo imesema, na kuongeza kuwa itaendelea kutoa taarifa kuhusu maendeleo ya wagonjwa wote.

Wizara imesema mgonjwa mpya wa kiume alikuwa tayari amewekwa karantini tangu tarehe 6 Oktoba 2026. Wahudumu watatu wa afya, wanaume wawili na mwanamke mmoja wenye umri wa miaka 29, 35 na 32 mtawalia, wamekuwa karantini tangu tarehe 9 Oktoba.

Kwa mujibu wa wizara hiyo, kuwaweka wagonjwa hao karantini mapema kumewezesha kugundua maambukizi yao katika hatua za awali, hivyo kupunguza hatari ya kusambaa kwa ugonjwa huo kwa familia zao na jamii kwa ujumla.

Tahadhari kwa Wakenya

Hata hivyo, Wizara ya afya imewahakikishia Wakenya kuwa hatari ya maambukizi kwa umma kwa sasa ni ndogo, ikisema hakuna ushahidi wa maambukizi yanayosambaa ndani ya jamii.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili WhatsApp bofya kutufuatilia
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Hadi sasa, watu 128 kati ya 130 waliotambuliwa kuwa wamekutana na wagonjwa wamefikiwa na kuwekwa karantini. Jitihada zinaendelea kuwatafuta watu wawili ambao bado hawajapatikana.

Hata hivyo, wizara imeonya kuwa visa vingine vinaweza kugunduliwa miongoni mwa watu walio katika karantini kabla ya kukamilika kwa kipindi cha ufuatiliaji cha siku 21. Watu watakaoanza kuonyesha dalili watafanyiwa uchunguzi na kupatiwa matibabu haraka.

Aidha, wizara hiyo ya Afya imeeleza kuwa inaendelea kuwafuatilia kwa karibu wanafamilia wanne wa mgonjwa wa kwanza aliyefariki pamoja na wahudumu wa afya waliomhudumia hospitalini.

Watu wote waliowekwa karantini wanaendelea kupata msaada wa kisaikolojia na kijamii.

Vile vule, Serikali imesema shughuli za biashara nchini zinaendelea kama kawaida, bila kuwepo kwa vizuizi vya usafiri, biashara au mikusanyiko ya umma.

Wizara imewataka Wakenya kuwa watulivu na kuendelea kuchukua tahadhari, ikisisitiza kuwa serikali inachukua hatua zote zinazowezekana kudhibiti mlipuko huo.

E

Ebola ni nini?

Ebola ni ugonjwa adimu lakini hatari unaosababishwa na virusi.

Virusi vya Ebola kwa kawaida huambukiza wanyama, hasa popo wa matunda, lakini milipuko kwa binadamu wakati mwingine huanza pale watu wanapokula au kushika wanyama walioambukizwa.

Huchukua siku mbili hadi 21 kwa dalili kujitokeza. Dalili huanza ghafla na kufanana na mafua, kama vile homa, maumivu ya kichwa, na uchovu

Ebola husambaa vipi?

D

Ebola huenea kwa kugusana moja kwa moja na damu au majimaji ya mwili wa mtu aliyeambukizwa au aliyefariki kutokana na ugonjwa huo, wala haisambai kwa njia ya hewa.

Mtu yeyote anayepata dalili kama homa, uchovu usio wa kawaida, maumivu ya misuli au viungo, maumivu ya koo, kutapika, kuharisha au kutokwa na damu bila sababu inayojulikana anashauriwa kuripoti mara moja katika kituo cha afya kilicho karibu naye.