'Tunasubiri matokeo ya mazungumzo yanayoendelea Iran' - Marco Rubio
Leo, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Pakistan, Mohsin Naqvi, amekutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, mjini Tehran kwa lengo la kujadili mapendekezo ya kutatua tofauti kati ya Iran na Marekani.
Muhtasari
- Mkuu wa Jeshi la Pakistan, Asim Munir, awasili Iran kwa mazungumzo ya kusitisha mapigano Mashariki ya kati
- Rubio: Tunasubiri matokeo ya mazungumzo yanayoendelea Iran
- Rio Ferdinand asema ziara yake Tanzania si ya kisiasa
- Tuchel ataja kikosi cha wachezaji 26 cha England kwa Kombe la Dunia
- Clara Luvanga aiongoza Al Nassr kutwaa Kombe la Wanawake Saudi Arabia
- Mkuu wa Nato apongeza uamuzi wa Marekani kutuma wanajeshi 5,000 nchini Poland
- Slot akataa kuthibitisha kama Salah amechaguliwa kwa mechi ya mwisho Anfield
- Rais Ruto wa Kenya apunguza bei ya mafuta ya dizeli kwa shillingi 10
- Madini ya urani yatabaki Iran - Mojtaba Khamenei
- Marekani yasema imepiga hatua katika mazungumzo na Iran
- Marekani yamuwekea vikwazo Mafwele kwa ukiukaji wa haki za binadamu
- Tutachukua na kuharibu madini ya Urani ya Iran - Trump
- Umati wenye ghadhabu wachoma moto hospitali ya Ebola eneo la Ituri, DRC
- Cuba ni tishio kwa usalama wa Marekani - Marco Rubio
Moja kwa moja
Na Beldeen Waliaula & Mariam Mjahid
Mkuu wa Jeshi la Pakistan, Asim Munir, awasili Iran kwa mazungumzo ya kusitisha mapigano Mashariki ya kati

Chanzo cha picha, Iranian Parliament Communication Office/Handout via Getty Images
Mkuu wa Jeshi la Pakistan, Field Marshal Asim Munir, amewasili tena mjini Tehran leo.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya serikali ya Pakistan, mkuu huyo wa jeshi ameondoka kuelekea Tehran kwa ziara ya kikazi.
Shirika la habari la AP, likinukuu vyanzo vya kiusalama, limesema kuwa Asim Munir atafanya mazungumzo na maafisa wa Iran kuhusu “mazungumzo yanayoendelea kati ya Iran na Marekani, amani na utulivu wa kikanda, pamoja na masuala mengine yenye maslahi ya pamoja.”
Munir aliitembelea Tehran pia siku 40 zilizopita, ambapo alikutana na Mohammad Bagher Ghalibaf pamoja na wajumbe wa timu za mazungumzo za Iran na Marekani.
Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Pakistan, Mohsin Naqvi, pia amekuwa mjini Tehran kwa mara ya pili ndani ya wiki hii kwa ajili ya mazungumzo na viongozi wa Iran.
Kwa upande wake, Marco Rubio amesema kuwa Washington inasubiri matokeo ya mazungumzo hayo na hatua zitakazofuata baada yake.
Pia unaweza kusoma:
Rubio: Tunasubiri matokeo ya mazungumzo yanayoendelea Iran

Chanzo cha picha, TANSIM
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani amesema kuwa Washington inasubiri kujua matokeo ya mazungumzo yanayoendelea kati ya Iran na Pakistan mjini Tehran.
Marco Rubio pia amesema, kando ya mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa NATO nchini Sweden, kwamba “kuna baadhi ya maendeleo” yaliyopatikana.
Leo, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Pakistan, Mohsin Naqvi, amekutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, mjini Tehran.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Fars, mkutano huo ulikuwa na lengo la kujadili mapendekezo ya kutatua tofauti kati ya Iran na Marekani.
Wakati huohuo, mkuu wa jeshi la Pakistan, Field Marshal Asim Munir, pia ameondoka kuelekea Tehran kwa lengo la kusaidia upatanishi kati ya Iran na Marekani.
Mshauri wa Rais wa UAE: Makubaliano ya Iran na Marekani lazima yashughulikie masuala ya msingi

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Mshauri wa masuala ya kidiplomasia wa Rais wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) amesema kuwa makubaliano yoyote kati ya Iran na Marekani “lazima yashughulikie chanzo cha msingi cha migogoro.”
Anwar Gargash ameonya kuwa mzunguko mpya wa mapigano kati ya Marekani na Iran unaweza kuzorotesha hali ya usalama katika eneo hilo.
Gargash amesema, “Suluhisho lolote la kisiasa lazima lishughulikie masuala ya msingi, ili kuepusha kuibuka kwa migogoro na changamoto mpya katika siku zijazo.”
Baada ya mashambulizi ya Marekani na Israel na kuanza kwa vita, Iran ilifanya mashambulizi ya droni na makombora yaliyolenga UAE na nchi nyingine za eneo hilo ambako kuna kambi za kijeshi za Marekani.
Tangu wakati huo, mvutano kati ya Iran na UAE umeendelea kuongezeka, huku pande zote mbili zikibadilishana tuhuma na ukosoaji mkali.
Tehran imeishutumu UAE kuwa “mshirika hai” anayesaidia Marekani na Israel katika mashambulizi dhidi ya Iran, wakati UAE nayo imeishutumu Iran kwa “kujaribu kuhalalisha” mashambulizi yake dhidi ya nchi hiyo.
Baada ya ripoti kwamba UAE ilihusika moja kwa moja katika mashambulizi dhidi ya Iran wakati wa vita vya hivi karibuni, UAE imesema kuwa hatua zake zote zilikuwa za kujilinda na zililenga kulinda mamlaka ya nchi, raia wake na miundombinu muhimu.
Pia unaweza kusoma:
Mawaidha ya Ijumaa yaliyotolewa katika miji mbalimbali ya Iran zatoa onyo kwa Marekani na Israel

Chanzo cha picha, Wikipedia
Katika hotuba za sala ya Ijumaa zilizotolewa leo katika miji mbalimbali ya Iran, maimamu wametoa onyo kwa Marekani na Israel kuhusu uwezekano wa shambulio jingine.
Katika mji wa Tehran, Mohammad Javad Hajj Ali Akbari, ambaye ni imamu wa muda wa sala ya Ijumaa katika mji mkuu, amewaambia Marekani na Israel:
“Kama mtachukua hatua ya kijinga, wakati huu mtaona Iran tofauti, na tutajaribu makombora mapya ambayo hamjawahi kuyawazia.”
Ahmad Alam-ul-Huda pia ametoa onyo kwa Marekani na Israel akisema kuwa moja ya matokeo ya vita vya hivi karibuni ni kwamba teknolojia ya Iran ya droni na makombora ya gharama nafuu imeweza kushindana na teknolojia ya gharama kubwa ya Marekani, akidai kuwa sasa Iran imekuwa miongoni mwa mataifa makubwa ya kijeshi duniani.
Abdul Hossein Ghobishawi, imamu wa msikiti wa Abadan, mojawapo ya miji muhimu ya mafuta Iran, amesema:
“Jeshi halitaheshimu mipaka yoyote iwapo vita vingine vitazuka nchini humo.”
Mohammad Nabi Mousavifard, imamu wa Ahvaz, mji mkuu wa mkoa wa Khuzestan, ametoa onyo kali zaidi akisema vita vingine vinaweza kutokea:
“Tutazisambaratisha Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu, Kuwait na Bahrain.”
Mojtaba Mirdamadi naye amesema:
“Mustakabali wa eneo la Ghuba ya Uajemi utakuwa bila Marekani, na hawana nafasi katika Ghuba hiyo isipokuwa chini ya maji yake.”
Pia unaweza kusoma:
Iraq, Uzbekistan na Kazakhstan zatuma misaada ya kibinadamu Iran
Naibu mkuu wa Shirika la Msalaba Mwekundu la Iran amesema kuwa Iraq, Uzbekistan na Kazakhstan zimetuma misaada ya kibinadamu nchini Iran, na kwamba misaada hiyo tayari imewasili nchini humo.
Razia Alishundi amesema:
“Misaada hii inajumuisha chakula, dawa na vifaa vya matibabu vilivyotolewa kwa Shirika la Hilali Nyekundu ili kusaidia juhudi za uokoaji na kukidhi mahitaji ya watu walio katika mazingira hatarishi.”
Kwa mujibu wa Msalaba Mwekundu wa Iran, Iraq ilituma malori tisa yaliyobeba takribani tani 180 za chakula, dawa na vifaa vya matibabu; Uzbekistan ilituma malori 15 yaliyobeba tani 300; huku Kazakhstan ikituma mabehewa 30 ya treni yaliyobeba tani 1,700 za misaada kwenda Iran.
Naibu mkuu wa Shirika la Hilali Nyekundu la Iran amesema kuwa sehemu kubwa ya misaada kutoka Kazakhstan ni unga na sukari.
Pia unaweza kusoma:
Rio Ferdinand asema ziara yake Tanzania si ya kisiasa

Chanzo cha picha, Screengrab/Social
Rio Ferdinand, nyota wa zamani wa Manchester United na timu ya taifa ya England, amesema ziara yake nchini Tanzania haina uhusiano wowote na siasa, akisisitiza kuwa hajihusishi na masuala ya kisiasa popote duniani, ikiwemo nchini kwake.
''Mimi sio mwanasiasa, sikuja hapa kufanya siasa, hakuna wa kuniambia nini nifanye/nisifanye-Rio
Ferdinand amesema hakuna mtu mwenye mamlaka ya kumwelekeza nini afanye au asifanye, huku akieleza kufurahishwa kwake kwa kupewa heshima ya kuwa balozi wa utalii wa Tanzania.
"Nashukuru kwa heshima hii na ninaiona kama fursa ya kuitangaza Tanzania kwa ulimwengu," amesema Ferdinand.
Haya yanajiri baada ya kukosolewa kwa kile kinachoitwa “sportswashing” yaani kutumia michezo kusafisha taswira ya nchi, baada ya kuonekana akiunga mkono serikali ya Tanzania ambayo imekuwa na utata.
Ferdinand, 47, aliripotiwa kupokelewa katika ziara yake nchini Tanzania na Waziri wa Utamaduni na Michezo, Paul Makonda, ambaye aliwekewa vikwazo na serikali ya Marekani mwaka 2020 kutokana na kile kilichoelezwa kama “ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu”.
Makonda anasemekana kuhusishwa na kampeni dhidi ya watu wa jinsi moja.
Mke wake pia aliripotiwa kuwekewa vikwazo na Marekani.
Serikali ya Marekani ilisema: "Amehusishwa katika ukandamizaji wa upinzani wa kisiasa, kukandamiza uhuru wa kujieleza na kujumuika, na kulenga watu waliotengwa."
Katika hafla ya mapokezi baada ya Ferdinand kuwasili nchini, ambapo alivishwa bendera ya Tanzania, alinukuliwa akimwita Makonda: "Rafiki yangu Paul".
Mkurugenzi wa kampeni ya Amnesty International UK, Felix Jakens, aliambia The Times: "Amnesty International imekuwa ikifuatilia kwa karibu hali ya haki za binadamu inayotatiza sana nchini Tanzania, ambapo vikosi vya usalama vilitumia nguvu zisizo halali dhidi ya waandamanaji mwishoni mwa 2025, na kuua na kujeruhi mamia."
"Kutokana na hali hiyo, Rio Ferdinand anapaswa kuzungumza dhidi ya ukiukwaji wa haki unaofanyika huko, sio kutoa wasifu wake kuunga mkono serikali."
"Ziara ya watu mashuhuri hayafanyiki kwa urahisi - hutuma ujumbe - na hii ina alama zote za kusafisha taswira ya Tanzania kupitia michezo."
Shirika hilo limemtaka Ferdinand kutumia jukwaa lake kuzungumzia madai ya ukiukwa wa haki za binadamu badala ya kuonekana kuihalalisha serikali kupitia umaarufu wake.
Soma zaidi:
Tuchel ataja kikosi cha wachezaji 26 cha England kwa Kombe la Dunia

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Kocha wa Timu ya England itakayoshiriki Kombe la Dunia 2026 Kocha wa England, Thomas Tuchel, ametangaza kikosi cha wachezaji 26 kitakachoiwakilisha nchi hiyo katika Kombe la Dunia 2026, akisisitiza kuwa amechagua timu yenye uwiano mzuri badala ya kuzingatia vipaji binafsi pekee.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutangaza kikosi hicho, Tuchel amesema amechagua makipa watatu pamoja na Jason Steele, huku akitoa shukrani kwa mlinda mlango huyo na klabu yake ya Brighton & Hove Albion kwa ushirikiano waliouonyesha.
"Tumechagua kikosi chenye uwiano mzuri. Tuna makipa watatu, mabeki tisa kwa nafasi nne, viungo saba kwa nafasi tatu na washambuliaji saba kwa nafasi tatu," amesema Tuchel.
Kocha huyo amesisitiza kuwa kila mchezaji aliyepo kambini amejitolea kikamilifu kwa timu na anaelewa wajibu wake ndani na nje ya uwanja.
"Ninaweza kuwahakikishia mashabiki wote kwamba tuna wachezaji 26 waliojitolea kwa asilimia 100. Wanaelewa majukumu yao na wako tayari kuweka mbele maslahi ya timu kuliko yao binafsi," aliongeza.
Tuchel amesema tangu alipoanza kazi hiyo, lengo lake limekuwa kujenga timu bora zaidi na siyo kukusanya wachezaji 26 wenye vipaji vikubwa zaidi.
"Kuanzia siku ya kwanza tulikuwa wazi kwamba tunataka kujenga timu bora zaidi. Hii haimaanishi kuchukua wachezaji 26 wenye vipaji vikubwa zaidi. Timu ndizo hushinda mataji, jambo hilo ni rahisi kiasi hicho. Kile tunachotaka kukifikia msimu huu wa joto kinawezekana tu kwa kufanya kazi kama timu," alisema.
Kuhusu wachezaji ambao hawakupata nafasi katika kikosi hicho, Tuchel amesema amewasiliana binafsi na kila mmoja wao kueleza sababu za maamuzi yake.
"Ninawashukuru sana wachezaji wote waliotusaidia kufuzu na wale ambao wamekuwa nasi katika kambi mbalimbali. Niliwapigia simu binafsi kuwaeleza maamuzi yangu, hata pale ambapo ujumbe ulikuwa wa kusikitisha au wa kukatisha tamaa. Niliona ni muhimu wausikie kutoka kwangu moja kwa moja," alisema Tuchel.
Tangazo la kikosi hicho sasa linaweka wazi sura ya England kuelekea kampeni yake ya kutafuta taji la Kombe la Dunia 2026 chini ya kocha huyo raia wa Ujerumani.
Soma zaidi:
Clara Luvanga aiongoza Al Nassr kutwaa Kombe la Wanawake Saudi Arabia

Chanzo cha picha, Al-Nassr FC
Mshambuliaji wa Tanzania, Clara Luvanga, ameendelea kuandika historia baada ya kuiongoza timu ya wanawake ya Al Nassr kutwaa kwa mara ya kwanza Kombe la Wanawake la Saudi Arabia.
Luvanga alikuwa nyota wa mchezo wa fainali dhidi ya Al Hilal Women baada ya kufunga mabao yote matatu katika ushindi wa mabao 3 dhidi ya mabao 2, matokeo yaliyoiwezesha Al Nassr kutwaa taji hilo la kihistoria.
Kutokana na kiwango chake bora katika mashindano hayo, Luvanga alitunukiwa tuzo ya Mchezaji Bora wa Kombe la Wanawake la Saudi Arabia msimu wa 2025/26.
Msimu huu umekuwa wa mafanikio makubwa kwa nyota huyo wa Tanzania ambaye ameisaidia Al Nassr kutwaa mataji manne makubwa, yakiwemo Ligi Kuu ya Wanawake ya Saudi Arabia, Kombe la Wanawake, Super Cup na Winter Cup.
Mbali na mafanikio hayo ya timu, Luvanga pia amemaliza msimu akiwa mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Wanawake ya Saudi Arabia kwa mabao 24.
Mafanikio hayo yanaendelea kumweka Luvanga miongoni mwa wachezaji wa kike wa Tanzania wanaong'ara zaidi katika soka la kimataifa huku akiendelea kuipeperusha bendera ya Tanzania katika medani ya soka duniani.
Soma zaidi:
Mkuu wa Nato apongeza uamuzi wa Marekani kutuma wanajeshi 5,000 nchini Poland

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Rais Donald Trump amesema Marekani itatuma wanajeshi wa ziada 5,000 nchini Poland, wiki moja baada ya Pentagon kufuta mpango wa awali wa kupeleka wanajeshi 4,000 nchini humo.
Katibu Mkuu wa Nato, Mark Rutte, amepongeza hatua hiyo kabla ya mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje unaofanyika nchini Sweden, akisema kuwa mwelekeo wa Ulaya kupunguza utegemezi wake kwa Marekani "utaendelea".
Akiandika kwenye jukwaa lake la Truth Social siku ya Alhamisi, Trump alisema uamuzi huo umetokana na uhusiano wa Marekani na Rais wa Poland, Karol Nawrocki, ambaye aliungwa mkono na Trump wakati wa uchaguzi wa urais mwaka jana.
Hata hivyo, hakutoa maelezo zaidi kuhusu iwapo wanajeshi hao wa ziada ni sehemu ya mpango uliokuwa umefutwa awali au ni operesheni tofauti.
Katika wiki za karibuni, Ikulu ya Marekani imeashiria kuwa inapanga kupunguza idadi ya wanajeshi wake barani Ulaya kama sehemu ya sera yake ya "America First".
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, anatarajiwa kuzitaka nchi wanachama wa Nato kubeba sehemu kubwa zaidi ya mzigo wa ulinzi katika mazungumzo yatakayofanyika Ijumaa mjini Helsingborg.
Akizungumza na waandishi wa habari Ijumaa asubuhi, Rubio alisema:
"Rais amekuwa akionesha kutoridhishwa na baadhi ya washirika wetu wa Nato na namna walivyoitikia operesheni zetu za Mashariki ya Kati."
Aliongeza kuwa pamoja na tofauti hizo, maeneo mengine ya ushirikiano yanaendelea, akitolea mfano tangazo la kutumwa kwa wanajeshi wa ziada nchini Poland.
Soma Zaidi:
Slot akataa kuthibitisha kama Salah amechaguliwa kwa mechi ya mwisho Anfield

Chanzo cha picha, Getty Images
Kocha wa Liverpool, Arne Slot, amekataa kuweka wazi iwapo Mohamed Salah atakuwa sehemu ya kikosi kitakachoshuka dimbani dhidi ya Brentford Jumapili katika mechi inayoweza kuwa ya mwisho kwa nyota huyo wa Misri katika Uwanja wa Anfield.
Kauli ya Salah aliyoiandika kwenye mitandao ya kijamii wikendi iliyopita, akitaka Liverpool ibadili mtindo wake wa uchezaji, imezua mjadala mkubwa miongoni mwa mashabiki na wachambuzi wa soka.
Wengi waliitafsiri kama ukosoaji wa moja kwa moja wa mfumo unaotumiwa na Slot.
Salah, ambaye anatarajiwa kuondoka Liverpool mwishoni mwa msimu huu baada ya kuitumikia kwa miaka tisa, aliwahi pia kuachwa nje ya kikosi kilichocheza dhidi ya Inter Milan katika Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kukiri kuwa uhusiano wake na Slot ulikuwa umeharibika.
Akizungumza kabla ya mchezo wa Brentford, ambao Liverpool inahitaji angalau pointi moja kujihakikishia tiketi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, Slot alikwepa kutoa jibu la moja kwa moja kuhusu ushiriki wa Salah.
“Sizungumzii uteuzi wa kikosi. Kitu muhimu kwangu ni kuhakikisha tunafuzu Ligi ya Mabingwa na kwamba Salah pamoja na wachezaji wengine wanaandaliwa vizuri kwa mchezo huo,” alisema Slot.
Kocha huyo wa Uholanzi alikiri kutoridhishwa na namna Liverpool ilivyocheza katika sehemu kubwa ya msimu huu, akisisitiza kuwa analenga kuijenga timu yenye uwezo wa kushindana kwa mataji huku ikicheza soka linalovutia zaidi.
“Nataka timu icheze aina ya soka ninayopenda. Nikilipenda mimi, naamini mashabiki pia watalipenda. Kwa kweli sijafurahishwa na sehemu kubwa ya mchezo wetu msimu huu,” alisema.
Hata hivyo, Slot alisisitiza kuwa yeye na Salah wana lengo moja. “Sote tunataka Liverpool ifanikiwe. Hilo ndilo jambo muhimu zaidi.”
Alipoulizwa kama kauli za Salah kuhusu Liverpool kurejesha utambulisho wake zilikuwa zinapunguza mamlaka yake kama kocha, Slot alikataa tafsiri hiyo.
“Soka limebadilika na linaendelea kubadilika. Lakini sisi sote tunataka Liverpool ishindanie mataji. Hilo ndilo jambo la msingi,” alisema.
Kuhusu baadhi ya wachezaji wa Liverpool kuonyesha kuunga mkono ujumbe wa Salah kwenye mitandao ya kijamii, Slot alisema hafuatilii sana shughuli za majukwaa hayo.
“Ninachojali ni kile ninachokiona mazoezini. Na sijashuhudia mabadiliko yoyote katika mwenendo wa wachezaji ukilinganisha na msimu mzima,” alisema.
Mechi ya Jumapili sasa inasubiriwa kwa hamu kubwa, huku mashabiki wa Liverpool wakitaka kujua kama watapata nafasi ya kumuaga mmoja wa wachezaji walioandika historia kubwa zaidi ya klabu hiyo katika miaka ya hivi karibuni.
Rais Ruto wa Kenya apunguza bei ya mafuta ya dizeli kwa shillingi 10

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Rais William Ruto Rais wa Kenya William Ruto, ametangaza kupunguza bei ya mafuta ya dizeli kwa shillingi kumi zaidi, katika mabadiliko ya bei ya mafuta yatakayo tangazwa mwezi Juni na Julai.
Iwapo pendekezo la Rais litatekelezwa, bei ya mafuta ya dizeli itashuka na kufikia shillingi 222.86 au dola 1.72 kutoka shillingi 242.92 (dola 1.87)
Awali serikali ilikuwa imetangaza kupunguza bei ya mafuta ya dizeli kwa shillingi kumi, huku rais Ruto akilaumu vita eneo la Mashariki ya Kati, kuwa vimechochea kupanda kwa bei ya mafuta.
Rais Ruto alitoa taarifa hiyo baada ya kukutana na viongozi wa vyama na miungano ya magari ya uchukuzi, ambao walifanya mgomo mapema wiki hii wakilalamikia kupanda kwa bei ya mafuta.
Viongozi wa muungano wa wamiliki magari ya uchukuzi maarafu matatu, wametangaza kuwa wamesitisha mgomo wao kabisa, baada ya kuafikiana na serikali kufanya mageuzi katika bei ya mafuta na kubadilishwa kwa sera zinazoiendesha sekta hiyo.
Pia unaweza kusoma:
Madini ya urani yatabaki Iran - Mojtaba Khamenei

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Picha ya Mojtaba Khamenei Kiongozi mkuu wa Iran, Mojtaba Ali Khamenei, ametoa agizo kuwa madini ya urani yaliyorutubishwa, hayafai kuruhusiwa kutoka nje ya Iran, shirika la habari la Reuters limeripoti.
Iran imesisitiza kuwa hawako tayari kusalimisha madini hayo, licha ya Marekani kusisitiza kuwa wanafaa kusitisha mpango wao wa nyuklia.
Agizo la Mojtaba Khamenei, huenda likalemaza juhudi za kupatikana kwa amani nchini humo kupitia mazungumzo ya amani yanayoendelea.
Trump aidha amesema hapo jana kuwa, hawataruhusu Iran kumiliki madini hayo au kuendelea na mpango wao wa nyuklia
Pia unaweza kusoma:
Marekani yasema imepiga hatua katika mazungumzo na Iran

Chanzo cha picha, Reuters
Maelezo ya picha, Marco Rubio akizungumza na wanahabari Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani, Marco Rubio amesema kwamba anatumai ziara ya mkuu wa jeshi la Pakistan nchini Iran, itasaidia kuendeleza diplomasia ya kumaliza vita, na kusema kuwa wamepiga hatua katika mazungumzo ya kupatikana kwa amani.
Rubio alielezea kuwa ana matumaini na safari ya maafisa wa Pakistan walioenda Tehran na kusema kuwa safari hiyo itasaidia kuendeleza mazungumzo ya kumaliza vita
Waziri huyo aidha aliikosoa tena jumuiya ya kujihami ya NATO kwa kutoshirikiana na Marekani katika vita dhidi ya Iran.
Pia unaweza kusoma:
Marekani yamuwekea vikwazo Mafwele kwa ukiukaji wa haki za binadamu

Chanzo cha picha, POLISI TANZANIA
Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imemuwekea vikwazo Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi Faustine Jackson Mafwele kuingia nchini Marekani.
Taarifa iliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio imesema kwa kuzingatia taarifa zinazoaminika, Mafwele alihusika katika ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.
“Mwaka jana, jeshi la polisi liliwakamata, kuwatesa na kuwafanyia ukatili wa kingono raia wa Uganda Agather Atuhaire na raia wa Kenya Boniface Mwangi, waliokuwa jijini Dar es Salaam kufuatilia kesi mahakamani dhidi ya kiongozi wa upinzani Tundu Lissu,” imeeleza sehemu ya taarifa ya Rubio.
Mwezi Februari mwaka huu kitengo cha uchunguzi cha BBC Africa Eye kilitoa filamu iliyoitwa ‘Hali ya hofu Tanzania’ na kuchunguza juu ya wimbi la matukio ya utekaji Tanzania. Katika filamu hiyo manusura wa matukio hayo wakiwemo Atuhaire na Mwangi walimtaja Mafwele kama mhusika mkuu wa kadhia zilizowafika.
Jeshi la Polisi na Mafwele hawakuwapa ushirikiano BBC licha ya kutafutwa. Hata hivyo serikali ya Tanzania iliiambia BBC Africa Eye kuwa wawili hao waliingia Tanzania kwa madhumuni ya utalii lakini uchunguzi wa idara ya uhamiaji ukagundua kuwa walikusudia kuhudhuria kesi kinyume na tamko lao la kuingia nchini.
“Kukamatwa kwao kulifanyika kisheria. Idara ya uhamiaji inakanusha madai yoyote ya makosa,” serikali ya Tanzania iliiambia BBC Africa Eye.
Unaweza kusoma;
Tutachukua na kuharibu madini ya Urani ya Iran - Trump

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Picha ya Donald Trump Rais wa Marekani Donald Trump amesisitiza kuwa watachukua akiba ya madini ya urani yaliyorutubishwa kutoka Iran.
“Tutachukua madini hayo. Hatuitaji, hatuitaki. Huenda hata tukaiteketeza baada ya kuichukua, lakini hatutawaruhusu waitumie au kumiliki madini hayo,” alisema Trump
Rais huyo aliongezea kuwa Marekani inaendelea na mazungumzo na Iran, na kwamba lengo lake kuu ni kuhakikisha Iran haina silaha za nyuklia.
“Hatuwezi kuruhusu Iran iwe na silaha za nyuklia. Hatuwezi kuruhusu hilo. Kutakuwa na vita vya nyuklia Mashariki ya Kati, na vita hivyo vitafika huku na hata Ulaya.Hatuwezi kuruhusu hilo litokee. Na halitatokea,” aliongezea Trump.
Shirika la habari la Reuters liliripoti awali kuwa, Kiongozi Mkuu wa Iran alitoa agizo la kutoruhusu madini ya Urani yaliyorutubishwa kutolewa nje ya nchi hiyo.
Kwa upande mwingine, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema vita vya Iran havitamalizika hadi Iran iondoe akiba yake ya urani iliyorutubishwa, ikome kuziunga mkono makundi yaliyojihami na isitishe mradi wake wa kutengeneza makombora.
Pia unaweza kusoma:
Umati wenye ghadhabu wachoma moto hospitali ya Ebola eneo la Ituri, DRC

Chanzo cha picha, Reuters
Maelezo ya picha, Eneo la hospitali ya Rwampara, Ituri Umati wenye hasira ulichoma moto sehemu ya hospitali inayowashughulikia wagonjwa wa Ebola mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, baada ya familia na marafiki wa kijana aliyefariki katika hospitali hiyo kuchukua mwili wake kwa nguvu kwa ajili ya mazishi.
“Walianza kurusha mawe. Hata walichoma mahema yaliyokuwa yakitumika kama wodi za kuwahifadhi wagonjwa waliotengwa,” mwanasiasa wa eneo hilo, Luc Malembe, aliiambia BBC kuhusu tukio lililoshuhudiwa katika Hospitali Kuu ya Rwampara.
Polisi walilazimika kufyatua risasi hewani kuwatawanya waandamanaji.
Mwili wa mtu aliyefariki kutokana na Ebola huwa na uwezo mkubwa wa kueneza ugonjwa huo, hivyo mamlaka hulazimika kuhakikisha mazishi yanafanyika kwa njia salama ili kuzuia kuenea kwa virusi hivyo.
Wahudumu wa afya katika hospitali ya Rwampara, iliyoko karibu na mji wa Bunia katika jimbo la Ituri, ambako karibu visa vyote vya Ebola vimeripotiwa, wapo chini ya ulinzi wa jeshi huku polisi wakijaribu kurejesha utulivu eneo hilo.
Jean Claude Mukendi, anayesimamia uratibu wa usalama dhidi ya ugonjwa Ebola eneo la Ituri, amesema kuwa kijana huyo aliyefariki alikuwa maarufu katika jamii hiyo na watu waliokuwa wameghadhabishwa na kifo chake hawaelewi hatari wa ugonjwa huo.
Pia unaweza kusoma:
Cuba ni tishio kwa usalama wa Marekani - Marco Rubio

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Picha ya Marco Rubio Waziri wa Mambo ya kigeni wa Marekani Marco Rubio amesema kuwa taifa la Cuba ni tishio kwa usalama wa taifa la Marekani, na kuwa hakuna uwezekano wa kuafikiwa kwa makubaliano ya amani kati ya nchi hizo mbili.
Kauli hiyo imejiri siku moja tu baada ya Marekani kumshtaki rais wa zamani wa Cuba, Raúl Castro, kwa kosa la mauaji kuhusiana na kuangushwa kwa ndege mbili mwaka wa 1996, tukio lililosababisha vifo vya raia wa Marekani.
Aidha Rubio alisema kuwa, Washington bado inatumia njia ya diplomasia kutatua tofauti kati yao na Cuba ila akaonya kuwa “Rais Trump ana haki na wajibu wa kuilinda Marekani dhidi ya tishio lolote”
Rubio pia aliishutumu Cuba kuwa miongoni mwa wafadhili wakuu wa ugaidi, madai ambayo Waziri wa Mambo ya kigeni wa Cuba Bruno Rodríguez ameyakanusha vikali kupitia mtandao wa X.
Rodríguez alimshutumu Rubio kwa kusema uongo na kwa kujaribu kuchochea uvamizi wa kijeshi, huku akiilaumu serikali ya Marekani kwa kutaka kuishambulia Cuba kimakusudi.
Pia unaweza kusoma:
Hujambo na karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja Ijumaa ya leo
