Waridi wa BBC: Mfahamu mtoto kutoka Tanzania ambaye ni balozi wa utalii Afrika

Chanzo cha picha, Ringo Mowo
- Author, Anne Ngugi
- Nafasi, BBC Swahili
- Iliyochapishwa
Sharon Ringo ni binti wa miaka 11 pekee yake , ila ametwikwa majukumu ya ubalozi wa utalii kupitia jumuiya ya bunge la Afrika mashariki nchini Tanzania.
Sio jambo la kawaida hasa barani Afrika kwa binti wa rika lake Sharon kutwikwa hadhi aliyo nao na kwa hio, ni majukumu ambayo anayachukulia kwa umuhimu wake kama alivyoelezea.
"Naona ni vizuri kwa sababu sio jambo rahisi , kwani sio kawaida kuwa balozi nikiwa mtoto na kwa hio namshukuru Mungu"Sharon alisema .
Kwa mapenzi yake makuu kwa mambo yanayohusu mazingira , kuanzia wakati alipotimiza umri wa kujifahamu alianza kujihusisha na usafi wa mazingira ikawa ni jambo ambalo alilipigia pondo hata akiwa shuleni.
Ni kupitia majukumu hayo yalioendelea kumsukuma karibu na washika dao katika sekta ya utalii na mazingira nchini Tanzania. Sharon anasema kwamba kuafikia hapo ilibidi pia na yeye afahamu mambo kadha wa kadha kuhusu sekta ya utalii.
"Ili kutangaza utalii na kuwa balozi ilibidi nijifunze sana mambo yanayohusiana nao, kwa hivyo nilisoma vitabu na pia kusafiri sehemu mbalimbali Tanzania ili kujiimarisha katika ufahamu wangu wa sekta ya utalii "anasema Sharon.

Chanzo cha picha, Ringo Mowo
Sharon Ringo ambaye ni kifungua mimba katika familia ya watoto watatu na alizaliwa miaka 11 iliyopita huko Dar-es-salaam, Tanzania amenieleza kwamba yeye ni mmojawapo ya wanafunzi wanaofanya vyema shuleni licha ya majukumu ya kuwa balozi wa utalii.
Sharon anasema kwamba yeye ni kiongozi na umri wake sio hoja ya kumzuia kuwa na ushawishi katika sekta ya utalii Afrika Mashariki, kuwa mmoja ya wakereketwa mabinti wanaotetea mabadiliko ya tabia nchi na pia kama anayezungumzia sana umuhimu wa watu kujihusisha katika biashara tofauti badala ya kutegemea kuajiriwa.
Kuteuliwa balozi wa utalii na Bunge la Afrika Mashariki
Sharon alivutia ofisi ya Spika wa Bunge la Afrika Mashariki, na kuwa mzungumzaji wake mdogo zaidi katika 2019 na 2021.
Uwezo wa uongozi wenye ushawishi na msukumo ulimwezesha kuwa balozi wa utalii nchini Tanzania katika kuunga mkono juhudi ambazo zinawekwa na washikadau.

Chanzo cha picha, Ringo Mowo
"Kujua jinsi utalii ulivyo hatarini kwa Mabadiliko ya Tabia nchi, mimi ninahudumu kama mtetezi wa ajenda ya mabadiliko ya tabia nchi katika kampeni inayoitwa MAMA KANITUMA, "Africa Go Green" ambayo dhamira yake ni kupanda miti milioni mbili Afrika Mashariki," Sharon alisema.
Sharon anasema kwamba kufikia sasa amepanda zaidi ya miti 200 yeye binafsi katika maeneo tofauti nchini Tanzania na Zanzibar.
Kando na hayo Sharon alizungumza kuhusiana na kazi ambazo amezifanya katika kuinua utalii wa afrika mashariki hasa nchini Tanzania. Akiwa Balozi Sharon amefanya shughuli nyingi za kukuza utalii nchini ikiwa ni pamoja na hotuba katika kongamano, na ziara katika Tanzania Bara na Zanzibar ili kujifunza na kuelewa kuhusu vivutio ambavyo watalii wanaweza kupata, vivutio vya utalii na kuvitangaza duniani.

Chanzo cha picha, Ringo Mowo
Katika umri wa miaka 11 amepata fursa ya kufanya mahojiano na Waziri wa Utalii na Maliasili Zanzibar, Mheshimiwa, Lela Muhamed Mussa, katika kipindi hicho alipata kujua zaidi kuhusu utalii Zanzibar, na Uchumi wa Buluu, kampeni iliyoendeshwa na Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi.
Waziri Lela binafsi alimkaribisha Sharon kwa ziara kadhaa Zanzibar, ikiwa ni pamoja na kutembelea mji wa Stone. Yeye pia alikuwa walioalikwa kwa mahojiano na Waziri wa Habari, Vijana na Michezo wa Zanzibar, Mheshimiwa Tabia Mwita, Sharon alipata heshima ya kutoa hotuba katika hafla iliyoangaziwa sana juu ya Siku ya Utalii Duniani.
Mwezi Agosti 2021 mbele ya Waziri wa Utalii na Urithi wa Zanzibar na nyenginezo wajumbe katika umati wa zaidi ya Watu 2000.
Pia alitoa hotuba ya kugusa utalii na mabadiliko ya tabia nchi mbele ya Bunge la Afrika Mashariki ambapo Uongozi wa Jumuiya hiyo ulikuwepo mnamo Septemba 2021, hotuba ambayo ilivuta mawazo ya wajumbe na hatimaye kuteuliwa kuwa Mjumbe wa Kikanda wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Chanzo cha picha, Sharon Ringo
"Ninasisitiza kuhusu haja ya kutangaza utalii wa ndani, na kuongeza ufahamu wa maeneo yetu ya vivutio vya utalii, maana itakuwa ya manufaa kwa watu wetu pamoja na kuvutia watalii na wawekezaji ndani na nje ya Afrika. Ndoto ni kuifanya Afrika Mashariki kuwa kivutio cha utalii duniani, na kuifanya Afrika kuwa ya kijani kibichi kwa kupanda miti. Ninaamini kwamba hili linawezekana na linaweza kufikiwa na sisi "alisema Sharon.
Sharon sasa anasoma darasa la sita katika Shule ya Kimataifa ya Braeburn, Dar es Salaam. Yeye ni mmoja wa wanafunzi bora zaidi darasani, akiwa na vyeti kadhaa vya utambuzi wa kufaulu kitaaluma katika masomo yake. Yeye ni sehemu ya uongozi shuleni darasani na michezo.
Sharon anaishi na wazazi wake, Dar es Salaam. Yeye ni mwimbaji mzuri, muogeleaji na anapenda mpira wa vikapu. Kando na hayo alielezea shauku yake kuu ya usanii mzuri wa kubuni. Amechora picha kadhaa za asili, pamoja na milima, mito, miti na wanyama. Yote yanaonyeshwa kwenye ghala yake nyumbani kwao .












