'Hii inaweza kuwa mara ya mwisho kusikia sauti yangu': Mauaji ya kisiasa yaongezeka Iran

.

Chanzo cha picha, KURDPA

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 4

'Hii inaweza kuwa mara ya mwisho kusikia sauti yangu': Mauaji ya kisiasa yaongezeka nchini Iran tangu kuanza kwa vita

Maneno hayaa ni mabaya. Lakini sauti ya Mehrab Abdollahzadeh inasikika vizuri, na kwa kuzingatia mazingira, ina ujasiri.

Anasubiri kunyongwa magharibi mwa Iran. Anazungumza kwa haraka - kana kwamba hana tena muda.

Ni ujumbe wa kukata tamaa.

"Unasikia sauti yangu kutoka Gereza Kuu la Oromiyeh, na hii inaweza kuwa mara ya mwisho kuisikia," anasema katika ujumbe uliopatikana na Mtandao wa Haki za Kibinadamu wa Kurdistan.

"Tangu siku ya kwanza kabisa ya kukamatwa kwangu, walilazimisha kukiri makosa kupitia mateso na vitisho, maungamo ambayo yalikuwa ya uwongo kabisa. Hakuna mashtaka dhidi yangu ambayo ni ya kweli. Wanajua, na Mungu anajua. Sina hatia."

Mehrab alikamatwa mnamo mwaka wa 2022, wakati wa maandamano ya nchi nzima kutoka na kifo cha mwanamke kijana, Mahsa Amini, ambaye alifariki akiwa mikononi mwa polisi wakati amezuiliwa kwa kutovaa vazi lake ipasavyo.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Alituhumiwa kuhusika katika mauaji ya mwanamgambo wa kikosi cha wanamgambo wa Basij cha Iran.

Baada ya miezi 42 ya hofu na kukosa usingizi usiku, alihukumiwa kifo mapema mwezi huu - ikiwa ni sehemu ya kuongezeka kwa hukumu ya kifo kwa wanaotuhumiwa kisiasa na masuala ya kiusalama.

Tangu Marekani na Israel zishambulie Iran tarehe 28 Februari, Umoja wa Mataifa unasema kuwa umethibitisha kunyongwa kwa takriban wafungwa 32 wa kisiasa.

Hii inawakilisha mwaka ambao matukio haya yanayotokea kila mwaka yameongezeka, huku vifo 45 vinavyohusiana na mashtaka ya kisiasa vikitokea katika kipindi cha mwaka mzima wa 2025, kulingana na Amnesty International.

Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa imeonya kuwa adhabu ya kifo inazidi kutumiwa kunyamazisha upinzani wa kisiasa.

Baadhi ya wale waliouawa mwaka huu walishtakiwa kwa ujasusi kwa ajili ya Israel au CIA, wakati wengine walishtakiwa kwa kuhusishwa na kundi la upinzani lililokuwa uhamishoni. Kumi na nne kati yao walikamatwa kuhusiana na vuguvugu la Januari mwaka huu, lililomalizwa kwa kutumia nguvu - na kusababisha maelfu ya vifo.

"Nchini Iran, mamlaka hutekeleza hukumu ya kifo kwa kunyongwa. Hutekelezwa alfajiri," anasema Nassim Papayianni wa Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Amnesty International.

"Watu nchini Iran wamekuwa wakiamkia matangazo ya watu kunyongwa karibu kila siku."

"Wanatumia hukumu ya kifo kama chombo cha ukandamizaji wa kisiasa, kuingiza hofu miongoni mwa watu, na kimsingi kukandamiza na kuzima upinzani wowote unaoweza kuwepo."

Wakati baadhi ya mauaji yanatangazwa hadharani, msemaji wa Ofisi ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa aliiambia BBC kuwa ina wasiwasi matukio mingine ya kunyongwa yanatekelezwa kwa siri.

Mwaka jana, Iran ilitekeleza hukumu ya kifo 2,159, kulingana na shirika la Amnesty International - idadi kubwa zaidi tangu 1981.

Inasema kwamba wengi wao walihukumiwa makosa yanayohusiana na madawa ya kulevya au mauaji.

Umoja wa Mataifa unahofia kuwa idadi hiyo mwaka huu inaweza kuwa kubwa zaidi.

Kwa kuongezeka kwa matumizi ya adhabu ya kifo, serikali inajaribu kurejesha mamlaka baada ya taswira yake kuharibiwa na uasi wa Januari na vita, kulingana na Kaveh Kermanshahi wa Mtandao wa Haki za Kibinadamu wa Kurdistan.

"Katika wakati ambapo inakabiliwa na migogoro mingi ya ndani na nje, inajaribu, kupitia ukandamizaji ulioimarishwa na ongezeko la visa vya adhabu ya kifo, kuonyesha kuwa bado ina nguvu na kutoa ujumbe: 'Bado niko hapa, na bado ninadhibiti hali,'" anasema.

Mwishoni mwa mwezi uliopita, televisheni inayomilikiwa na serikali ilitoa ripoti juu ya utekelezaji wa adhabu ya kifo kwa Sasan Azadvar, bingwa wa karate mwenye umri wa miaka 21 kutoka mji mkuu wa Isfahan. Alikuwa amehukumiwa kwa "moharabeh" au "vita dhidi ya Mungu", na "kwa kushirikiana na adui" kwa kushambulia vikosi vya polisi wakati wa maandamano yaliyotokea mwezi Januari.

Anaonekana akikubali kutumia fimbo kuvunja dirisha la gari la polisi na kuomba petroli ili kuliwasha moto.

Lakini hakushutumiwa kwa kosa lolote la kuua, ambalo - chini ya sheria za kimataifa - ni msingi wa kisheria wa matumizi ya hukumu

.

Chanzo cha picha, IRAN HUMAN RIGHTS

Mamlaka ya Iran haikujibu ombi la BBC la kutoa maoni yao juu ya kuongezeka kwa matumizi ya adhabu ya kifo, ikiwa ni pamoja na dhidi ya Sardar Azadvar, juu ya madai ya mateso.

Lakini tarehe 30 Aprili, mkuu wa mahakama ya Iran, Gholamhossein Mohseni Ejei, alipuuzilia mbali ukosoaji wa kimataifa wa hukumu za kifo unaohusishwa na machafuko ya Januari, akisema kwamba mahakama zake hazitayumbishwa.

Kila mmoja wa waliohukumiwa ana hadithi yake mwenyewe. Lakini wanaharakati wa haki za binadamu wanazungumza kuhusu mifumo inayosumbua. Hukumu ya kifo haitumiki kwa uwiano dhidi ya wanachama wa walio wachache nchini humo.

Erfan Shakourzadeh, mwenye umri wa miaka 29 mwanafunzi wa shahada ya uzamili katika uhandisi wa anga, alinyongwa tarehe 11 Mei. Mahakama ya Iran ilisema kuwa amepatikana na hatia ya kushirikisha habari za siri na ujasusi wa Israel na Marekani.

Lakini shirika la kutetea haki za binadamu la Hengaw lenye makao yake nchini Norway lilichapisha barua wanayosema aliandika kabla ya kifo chake.

"Nilikamatwa kwa mashtaka ya uzushi ya ujasusi na, baada ya miezi minane na nusu ya mateso na kifungo cha upweke, nililazimishwa kukiri uongo. Usiruhusu maisha mengine yasiyo na hatia yamalizwe kimyakimya."

Hengaw alisema inasikitisha sana na kasi ya kesi, hukumu na kunyongwa zimekuwa zikifanyika, pamoja na "ukosefu kamili wa uwazi" katika kesi za mahakama.

"Jamhuri ya Kiislamu inaendelea na ukandamizaji wake wa kimfumo wa idadi ya watu kwa kuwatuhumu kiholela wapinzani na wakosoaji kuwa "majasusi wa Israel" bila kuwasilisha ushahidi wa kuaminika au kuhakikisha viwango haki inatendeka katika kesi," Aywar Shekhi wa kundi hilo aliiambia BBC, akiongeza kuwa "maisha ya wengi yako hatarini".

Katika ujumbe wake wa sauti kutoka gerezani kabla ya kunyongwa, Mehrab Abdollahzadeh alielezea mateso ya kuwa kwenye orodha ya kunyongwa.

"Mtu aliyehukumiwa hufikiri kila usiku na mchana kwamba wakati wowote, anaweza kuitwa na kupelekwa kuuawa. Mtu aliyehukumiwa anaweza kupata amani kidogo tu baada ya saa 1 usiku, labda kuondoa mawazo yao na kulala kwa masaa mawili au matatu", alisema.

Mmiliki huyo wa duka mwenye umri wa miaka 29 aliuawa - kwa mujibu wa Mtandao wa Haki za Binadamu wa Kurdistan - bila onyo la awali kwa jamaa zake au wanasheria, na mwili wake haujarudishwa kwa familia yake.