Marekani imepata hasara kiasi gani katika vita vya Iran, kuanzia ndege za kivita hadi droni?

Chanzo cha picha, Getty Images
Ripoti mpya ya Bunge la Marekani imefichua ukubwa wa hasara za kijeshi ambazo Marekani ilipata wakati wa vita dhidi ya Iran, ikieleza kuwa jumla ya ndege 42 za kijeshi ziliharibiwa au kuangamizwa katika mapigano hayo.
Ripoti hiyo imeandaliwa na Idara ya Utafiti ya Bunge la Marekani, CRS, kwa kutumia taarifa kutoka Pentagon, Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani Mashariki ya Kati (CENTCOM) pamoja na ripoti za vyombo vya habari.
Ripoti hii inapatikana pia kwenye tovuti ya Bunge la Marekani.
CRS hutoa uchanganuzi kuhusu masuala ya sera kwa wanachama wa mabaraza yote mawili ya Bunge la Marekani, bila kujali mfungamano wa vyama vya siasa.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, hasara hizo zilihusisha ndege za kivita, ndege zisizo na rubani, helikopta na ndege maalum za kijeshi.
Ripoti hiyo pia imenukuu afisa wa Pentagon, Jules W. Hurst, akiliambia Bunge kuwa gharama za vita dhidi ya Iran zimezidi dola bilioni 29 za Marekani, kiwango kinachojumuisha matengenezo na ukarabati wa ndege zilizoharibiwa.
Ndege aina ya F 15E Strike Eagle

Chanzo cha picha, Getty Images
Miongoni mwa ndege zilizotajwa ni pamoja na ndege nne za kivita aina ya F 15E Strike Eagle.
CENTCOM ilisema kuwa baadhi ya ndege hizo zilianguka nchini Kuwait kutokana na kile ilichokiita "shambulio la washirika".
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Katika tukio hilo, wafanyakazi sita wa ndege zote mbili walifanikiwa kuondoka wakiwa salama.
Mnamo Aprili 5, 2026, Centcom iliripoti kwamba ndege ya F-15E ya Marekani ilianguka wakati wa shambulio la anga nchini Iran, na marubani wote wawili waliokolewa salama wakati wa operesheni tofauti ya utafutaji na uokoaji.
Ripoti hiyo imenukuu taarifa ya Machi 19 iliyosema kuwa katika kila operesheni ya kivita, ndege ya kivita ya Marekani aina ya F 35A iliharibiwa kutokana na mashambulizi ya mfumo wa ulinzi wa ardhini wa Iran.
Wakati huo, Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani Mashariki ya Kati, CENTCOM, ilithibitisha kuwa ndege ya kivita ya Marekani aina ya F 35 ilifanya kutua kwa dharura katika uwanja mmoja wa ndege Mashariki ya Kati baada ya kushiriki operesheni ya kivita ndani ya anga ya Iran.
Katika taarifa yake, CENTCOM ilisema ndege hiyo ilitua salama na rubani wake alikuwa katika hali thabiti.
Hata hivyo, CENTCOM haikutoa maelezo zaidi kuhusu tukio hilo, ingawa shirika la habari la Marekani, CNN, liliripoti kuwa ndege hiyo ililengwa na mashambulizi ya Iran.
Ripoti ya Bunge la Marekani pia ilisema kuwa katika mkutano na waandishi wa habari Aprili 6, 2026, Mwenyekiti wa Wakuu wa Majeshi ya Marekani, Jenerali Dan Kane, alisema kuwa Aprili 3 ndege ya mashambulizi ya karibu ya anga aina ya A 10 ilidunguliwa na adui kabla ya kuanguka, huku rubani wake akifanikiwa kujirusha nje kwa usalama kwa kutumia mfumo wa kujinusuru.
Ndege ya mafuta ya KC-135
Aidha, ndege za kuongeza mafuta angani aina ya KC 135 zilihusika katika ajali ya kugongana angani nchini Iraq, iliyosababisha vifo vya wahudumu sita.
Ndege nyingine tano za aina hiyo ziliharibiwa katika shambulizi la makombora na droni lililolenga kambi ya Prince Sultan nchini Saudi Arabia.
Ripoti hiyo pia ilithibitisha kuharibiwa kwa ndege ya mfumo wa upelelezi na uongozi wa anga aina ya E 3 Sentry katika shambulizi jingine nchini Saudi Arabia.
Picha zilizothibitishwa baadaye zilionyesha ndege hiyo ikiwa imepasuka vipande viwili.
Ndege ya E 3 Sentry ya mfumo wa onyo la mapema na udhibiti wa operesheni za anga

Chanzo cha picha, Getty Images
Kulingana na ripoti hiyo, gazeti la habari la tarehe 28 Machi liliripoti kuwa ndege aina ya E 3 iliharibiwa wakati wa shambulio la makombora na droni za Iran dhidi ya kambi ya anga ya Prince Sultan nchini Saudi Arabia.
Tarehe 7 Mei ilielezwa kuwa ndege hizo zilikuwa zimeegeshwa kwenye njia ya kurukia na kutua isiyo salama.
Wakati huo, baadhi ya picha zilizothibitishwa kutoka uwanja wa ndege nchini Saudi Arabia zilionyesha ndege ya Jeshi la Anga la Marekani iliyoharibika.
Picha hizo zilizochapishwa kwa mara ya kwanza kwenye ukurasa wa Facebook uliolenga habari za kijeshi za Marekani zilionyesha ndege ya E 3 Sentry ikiwa imevunjika sehemu mbili.
Uhakiki wa BBC Verify ulithibitisha kuwa picha hizo zilipigwa katika kambi ya anga ya Prince Sultan, iliyoko takriban kilomita mia moja kutoka mji mkuu wa Saudi Arabia, Riyadh. Miundombinu iliyoonekana kwenye picha kama nguzo, ghala za kuhifadhi na vibao vya maelekezo ililingana na picha za setilaiti.
Ndege ya operesheni maalum ya MC 130J Commando

Chanzo cha picha, FACEBOOK
Tarehe 5 Aprili 2026, ripoti ya habari ilisema kuwa ndege mbili aina ya MC 130J zilizo kuwa zikisaidia katika operesheni ya utafutaji na uokoaji wa ndege ya F 15E iliyopata ajali zililemazwa kwa makusudi.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, ndege hizo zilishindwa kuruka kwa wakati na zikawa hazifanyi kazi zikiwa ardhini, lakini wahudumu wake waliokolewa salama.
Inafahamika kuwa Iran ilikuwa imeiangusha ndege ya kijeshi ya Marekani aina ya F 15E na mmoja wa wahudumu wa ndege hiyo alipotea nchini Iran, hali iliyosababisha Marekani kuanzisha operesheni kubwa ya utafutaji na uokoaji.
Kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari vya Marekani, pia kulikuwa na mapigano kati ya vikosi vya Marekani na Iran wakati wa jaribio la kumwokoa mhudumu wa pili wa ndege hiyo ya kivita ya Marekani iliyodondoka nchini Iran.
Rais Trump alieleza tukio hilo kuwa operesheni kubwa ya mapigano ambapo ndege nyingi za Marekani zilishiriki ndani ya Iran.
Helikopta ya shughuli za uokoaji

Chanzo cha picha, Getty Images
Kulingana na ripoti hiyo, tarehe 6 Aprili, Jenerali Dan Kane alithibitisha katika mkutano na waandishi wa habari kuwa helikopta ya Marekani aina ya HH 60W iliharibiwa wakati wa operesheni ya uokoaji iliyofanyika tarehe 5 Aprili.
Alikuwa akirejelea operesheni ya uokoaji iliyolenga kumtafuta rubani wa Marekani, ambaye alikuwa mmoja wa wahudumu wa ndege ya F 15E iliyodhaniwa kuangushwa katika shambulio la Iran.
Droni

Chanzo cha picha, Getty Images
Ripoti ya Bunge ilitaja taarifa ya habari ya tarehe 9 Aprili iliyosema kuwa ndege zisizo na rubani 24 za Marekani ziliharibiwa wakati wa Operesheni Epic Fury.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kati ya ndege hizo zilikuwepo droni aina ya MQ 9, ambazo hutumika kufanya upelelezi na mashambulizi, zikiruka katika mwinuko wa chini na pia wa juu.
Pia ilielezwa kuwa droni moja kubwa ya upelelezi ya mwinuko wa juu aina ya MQ 4C iliharibiwa wakati wa mapigano.
Inafahamika kuwa maafisa wa Marekani wamedai kuwa wamefanikiwa kufikia sehemu kubwa ya malengo yao wakati wa vita hivyo vya Iran.
Rais Trump naye amerudia mara kadhaa kusema kuwa jeshi la anga, jeshi la ardhini na jeshi la majini la Iran yameharibiwa.
Kwa upande mwingine, Iran bado haijatoa taarifa za kina kuhusu hasara iliyopata katika vita hivyo, na inaendelea kudai kuwa bado ina uwezo wa kuendeleza mapambano dhidi ya Marekani.












