'Ebola imetutesa': Hofu yatanda mashariki mwa DR Congo huku virusi hatari vikienea

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Hofu imekumba maeneo yaliyoathiriwa na Ebola mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Huku idadi ya vifo ikiendelea kuongezeka, maafisa wanasema wanajitahidi kukabiliana na mlipuko ambao huenda ulikuwa ukienea bila kugunduliwa hapo awali.
"Ebola imetutesa," anasema mhudumu mmoja wa teksi aliye na umri wa miaka 20 hivi katika mji wa Rwampara wenye migodi ya dhahabu.
"Ninaogopa kwa sababu watu wanakufa kwa wingi... Tunaogopa sana."
Kufuatia ziara yake katika jimbo la Ituri, kitovu cha mlipuko huo, wikendi iliyopita, Waziri wa Afya wa Congo Dkt. Samuel Roger Kamba alikiri kwamba timu za afya zinapambana kumaliza kudhibiti kuenea kwa virusi hivyo, ambavyo huenda vilikuwa vikisambaa mapema kuliko ilivyogunduliwa kwa mara ya kwanza tarehe 24 Aprili.
Mgonjwa anayedhaniwa kuwa wa kwanza ni muuguzi aliyefariki katika mji mkuu wa jimbo la Bunia, lakini akazikwa Mongwalu, mji ambao pia unachimba madini ya dhahabu. Visa na vifo vingi vinavyoshukiwa vimeripotiwa huko na katika eneo jirani la Rwampara.
Mkazi wa Rwampara, Fred Kiza, aliiambia BBC kwamba "kuna hofu", ambayo anaiita "kawaida wakati kuna ugonjwa kama huu."
"Ingekuwa vizuri kama wangetupa barakoa ili kujilinda."
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kufikia Jumanne, kulikuwa na visa 514 vinavyoshukiwa, huku watu 136 wakiaminika kufariki kutokana na virusi hivyo, maafisa walisema. Mtu mmoja pia amefariki katika nchi jirani ya Uganda.
Visa pia vimetambuliwa katika jiji la Butembo na Goma inayodhibitiwa na waasi katika jimbo la Kivu Kaskazini, na pia katika jimbo la Kivu Kusini.
Maafisa wa afya wanasema kwamba vifo kadhaa vilitokea katika jamii bila kuripotiwa kwa mamlaka, ikimaanisha kuwa havingeweza kuchunguzwa wakati huo.
Kulingana na wizara ya afya, arifa rasmi za jamii zilisajiliwa kuanzia tarehe 8 Mei pekee.
"Katika ngazi ya kijamii, hii haijawa na ufanisi," Dkt. Kamba alielezea. "Inamaanisha mtu anaweza kuwa alikufa kabla yake, au mtu mwingine anaweza kuwa alikuwa mgonjwa kabla yake, lakini hakuna mtu aliyeripoti.
Aliongeza: "Kwa kweli tunahitaji kuangalia ndani ya jamii ili kuelewa kilichotokea - jinsi watu walivyougua na wakati mwingine hata kufa bila ripoti yoyote kuwasilishwa."
Virusi vilivyojificha mbele ya macho
Mlipuko huo umesababishwa na aina ya virusi vya Bundibugyo ya Ebola. DR Congo - ambayo kwa sasa inakabiliwa na mlipuko wake wa 17 wa Ebola - inafahamiana zaidi na spishi ya Zaïre.
Bundibugyo imesababisha milipuko miwili tu hapo awali - mwaka 2007 na 2012 - ambapo iliua takriban 30% ya watu walioambukizwa.
Dkt. Kamba alielezea dalili: "Kuna kutokwa na damu nyingi kila mahali, homa kali sana. Lakini Bundibugyo inaweza kuonyesha dalili chache dhahiri, ambazo huchelewesha utambuzi kwa sababu watu hufikiria kuwa hii ni malaria tu."
Maafisa wanasema kuchelewa huko kunaweza kuruhusu virusi kuenea kimya kimya.
Huko Mongwalu, baadhi ya vifo vilihusishwa si na ugonjwa, bali uchawi. Imani hiyo ilijulikana hapa kama "jeneza" - wazo kwamba mtu yeyote aliyegusa jeneza la marehemu pia angekufa.

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Shirika la kimataifa la hisani la Save the Children lilisema aina ya virusi vya Bundibugyo haijawahi kuonekana Ituri hapo awali. Majaribio madogo katika jimbo yalikuwa ni kupima aina ya virusi vya Zaïre na haukuonekana.
"Kufikia wakati aina ya virusi vya Bundibugyo ilipogunduliwa, tayari ilikuwa imeenea sana. Sasa inakimbizana kuukabili," mwakilishi wake wa DR Congo Greg Ramm alisema katika taarifa.
Mamlaka imeonya kwamba kuenea kwa virusi hivyo katika vituo vikubwa vya mijini kunaleta changamoto kubwa.
Licha ya ziara ya Dkt. Kamba huko Bunia mwishoni mwa wiki, wakazi wanahisi kwamba hatua za kupunguza kuenea kwa virusi hivyo yamekuwa ya polepole.
"Kama hakuna kituo cha matibabu hapa katika mji mkuu," mkazi mmoja aliuliza, "vipi kuhusu maeneo mengine?"
Bunia huko Ituri, na Butembo na Goma huko Kivu Kaskazini, ni makazi ya mamia ya maelfu ya watu, lakini hakuna hata moja iliyo na kituo cha matibabu cha Ebola kinachofanya kazi kikamilifu siku tano baada ya kutangazwa kwa mlipuko huo.
Wakazi wa Goma - jiji kubwa zaidi mashariki mwa DR Congo - wanaiambia BBC kwamba hatua za msingi za afya ya umma, kama vile kuepuka kusalimiana kwa mikono, kupunguza mikusanyiko na kunawa mikono mara kwa mara, zinapuuzwa sana.
"Ninaelekea mpakani kutoa taarifa kuhusu watu waliokwama huko," alisema José Mutanava, mwandishi wa habari wa eneo hilo. "Nimevaa barakoa, lakini si watu wengi wamevaa barakoa."
Mkazi mwingine, ambaye hakutaka jina lake litajwe, alisema: "Hakuna mtu anayeweza kufuata hatua za kizuia kusambaa kwa ugonjwa - labda tu tunakapoona vifo vingi zaidi. Leo katikati ya jiji nimeona watu wanne pekee wakiwa wamevaa barakoa."
Wengine wanasema majukumu ya kila siku ndio kipaumbele.
"Ni vigumu sana kuwaomba watu wanaojitahidi kujitafutia riziki kufuata sheria hizi," mkazi mmoja alisema.
Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo imeathiriwa vibaya na migogoro, na hivyo kuleta ugumu zaidi katika kukabiliana na virusi hivyo.
Save the Children ilisema mlipuko wa Ebola ni "mgogoro mpya mkubwa juu ya hali ambayo tayari ni ngumu".
"Iko katika eneo la migogoro, eneo la mgogoro wa kibinadamu, huku mamia ya maelfu ya watu wakimbizi, na mifumo ya huduma za afya ikiwa tayari imeathiriwa vibaya," iliongeza.
Kwa sasa, maeneo manne kati ya yaliyoathiriwa yako katika jimbo la Ituri: Mongwalu, kitovu cha mlipuko huo, pamoja na Bunia, Rwampara na Nyakunde.
Katika Kivu Kaskazini, Goma inadhibitiwa na kundi la waasi la M23, huku mji wa pili kwa ukubwa katika jimbo hilo, Butembo, pia ukiathiriwa na shughuli za wanamgambo.
Marekani imetangaza dola milioni 13 (£9.7m) kama msaada wa dharura kwa DR Congo na Uganda na inasema inafikiria ufadhili zaidi kupitia mfuko wa pamoja wa kibinadamu wa Umoja wa Mataifa, pamoja na vikwazo vya usafiri vinavyohusiana na mlipuko huo.

Chanzo cha picha, Getty Images
Raia wa Marekani, Dkt. Peter Stafford, ni miongoni mwa walioambukizwa baada ya kupimwa na kupatikana na virusi alipokuwa akifanya kazi katika Hospitali ya Nyakunde huko Ituri.
Daktari, mkewe na mwenzake mwingine walikuwa wakiwatibu wagonjwa wakati mlipuko ulipoanza, Serge, kundi la wamisionari Wakristo waliokuwa wakifanyia kazi, amesema.
Kulingana na Vituo vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa vya Marekani (CDC), raia wa Marekani alihamishwa hadi Ujerumani kwa matibabu, na kuongeza kuwa inafanya kazi ya kuwahamisha angalau Wamarekani wengine sita walioathiriwa.
Siku ya Jumapili, Shirika la Afya Duniani (WHO) lilitangaza mlipuko huo kuwa dharura ya afya ya umma inayotia wasiwasi kimataifa, baada ya visa vilivyothibitishwa kuripotiwa tarehe 15 Mei.
Kwa sasa, mamlaka za Congo zinasema zinategemea uzoefu wa kujifunza kwa bidii, na hatua za afya ya umma, kukabiliana na mlipuko wa Ebola wa 17 nchini humo.








