Masuala yanayokwaza mazungumzo kati ya Marekani na Iran

Chanzo cha picha, Anadolu via Getty Images
Marekani na Iran Alhamisi ziliendelea kushikilia misimamo yao tofauti kuhusu akiba ya urani ya Tehran na udhibiti wa Mlango bahari wa Hormuz, lakini Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio alisema kuna "baadhi ya ishara nzuri" kuhusu mazungumzo hayo.
Chanzo kikuu kutoka Iran kililiambia Reuters Alhamisi kwamba bado hakuna makubaliano yaliyofikiwa kati ya Marekani na Iran, lakini kikaashiria kuwa tofauti kati ya pande hizo zinaanza kupungua.
Chanzo hicho kiliongeza kuwa urani iliyorutubishwa ya Iran na udhibiti wa Tehran juu ya Mlango bahari wa Hormuz bado ni miongoni mwa masuala yanayokwaza mazungumzo.
Rais wa Marekani Donald Trump alisema Marekani hatimaye itapata akiba ya Iran ya urani kwa kiwango cha juu, ambayo Washington inaamini inalenga kutengeneza silaha ya nyuklia, huku Tehran ikisema ni kwa matumizi ya amani pekee.
"Tutapata hiyo," Trump aliwaambia waandishi wa habari katika White House. "Hatujihitaji, hatuitaki. Huenda tukaiteketeza baada ya kuipata, lakini hatutawaacha waimiliki."
Marco Rubio aliwaambia waandishi wa habari kwamba suluhisho la kidiplomasia halitawezekana ikiwa Iran itatekeleza mfumo wa kutoza ada za usafiri katika Mlango wa Hormuz. Hata hivyo, aliongeza kuwa kumekuwa na maendeleo fulani katika mazungumzo hayo.
Aliongeza, "Kuna baadhi ya ishara nzuri… Sitaki kuonekana mwenye matumaini kupita kiasi, hivyo tusubiri tuone kitakachotokea katika siku chache zijazo."
Kiongozi Mkuu wa Iran ametoa agizo kwamba akiba ya nchi hiyo ya urani iliyoboreshwa kwa kiwango cha juu, karibu na kiwango cha matumizi ya kijeshi, isipelekwe nje ya nchi, vyanzo viwili vya juu vya Iran viliiambia Reuters. Hatua hiyo inaonyesha msimamo mkali zaidi wa Tehran kuhusu moja ya madai makuu ya Marekani katika mazungumzo ya amani.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Agizo la Mojtaba Khamenei linaweza kuongeza msuguano kwa Rais wa Marekani, Donald Trump na kufanya mazungumzo ya kumaliza vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran kuwa magumu zaidi.
Maafisa wa Israel waliiambia Reuters kwamba Trump aliihakikishia Israel kuwa akiba ya Iran ya urani iliyoboreshwa kwa kiwango cha juu, inayohitajika kutengeneza silaha ya nyuklia, itaondolewa kutoka Iran, na kwamba makubaliano yoyote ya amani yanapaswa kuwa na kifungu kinachohakikisha hilo.
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alisema hatazingatia vita kuwa vimekwisha mpaka urani iliyorutubishwa iondolewe Iran, Tehran ikomeshe uungaji mkono wake kwa makundi washirika, na uwezo wake wa makombora ya balistiki uondolewe.
Moja ya vyanzo vya Iran, ambaye hakutaka kutajwa kwa sababu ya unyeti wa suala hilo, alisema: "Maelekezo ya Kiongozi Mkuu na makubaliano ndani ya utawala yanathibitisha kuwa akiba ya urani haipaswi kuondoka nchini."
Vyanzo hivyo viwili viliongeza kuwa maafisa wa juu wa Iran wanaamini kuwa kupeleka vifaa hivyo nje ya nchi kutafanya taifa hilo kuwa katika hatari zaidi ya mashambulizi ya baadaye kutoka Marekani na Israel.
Kiongozi Mkuu wa Iran ana mamlaka ya mwisho katika masuala makubwa ya taifa.
Akijibu ombi la maoni, msemaji wa White House Olivia Wells alisema: "Rais Trump ameweka wazi mipaka ya Marekani isiyoweza kuvukwa, na atafanya makubaliano yatakayoweka maslahi ya wananchi wa Marekani mbele."
Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran haikujibu ombi la kutoa maoni.
Rais Trump alisema Alhamisi kwamba atajaribu kuhudhuria harusi ya mwanawe mkubwa, akisema muda wake ni "mbaya" kutokana na vita dhidi ya Iran.
Donald Trump Jr., mwenye umri wa miaka 48, atafanya harusi yake ya pili mwishoni mwa wiki hii, na atamuoa Bettina Anderson katika viswa vya Bahama, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Marekani.
"Angependa kuhudhuria harusi ya mwanawe," Trump aliwaambia waandishi wa habari katika Oval Office. "Itakuwa sherehe ndogo ya faragha, na nitajaribu kuhudhuria."
''Mchanganyiko wa mawazo"

Chanzo cha picha, Getty Images
Mamlaka mpya ya Iran inayosimamia Mlango bahari wa Hormuz imetangaza kwamba eneo la udhibiti inalodai linafikia hadi maji yaliyo kusini mwa bandari ya Fujairah katika United Arab Emirates, eneo lenye miundombinu ya mafuta iliyoundwa kupita njia hiyo muhimu ya kimkakati ya baharini. Abu Dhabi imekosoa madai hayo na kuyaita "ndoto za mchana."
Usafirishaji wa meli kupitia Mlango wa Hormuz, ambao ni njia muhimu ya kimataifa ya usafiri wa baharini, umekuwa chini ya udhibiti wa Iran tangu kuzuka kwa vita na Israel na Marekani mnamo Februari 28.
Iran inasisitiza kuwa meli zinazopita katika njia hiyo lazima zipate ruhusa kutoka kwa vikosi vya jeshi vya Iran.
Katika chapisho lililoambatana na ramani kwenye jukwaa la X siku ya Jumatano, "Mamlaka ya Mlango wa Ghuba ya Uajemi" ilisema imefafanua "eneo la udhibiti wa kisheria kusimamia" mlango huo.
Iliongeza kuwa eneo hilo linajumuisha mstari unaotoka "Kuh Mubarak nchini Iran hadi kusini mwa Fujairah katika UAE na mstari unaounganisha ncha ya Kisiwa cha Qeshm nchini Iran na Umm Al Quwain UAE."
Mamlaka hiyo ilieleza kuwa "kupitia eneo hili kwa lengo la kuvuka Mlango wa Hormuz kunahitaji uratibu na Mamlaka ya Mlango wa Ghuba ya Uajemi pamoja na kupata kibali kutoka kwake."
Anwar Gargash, mshauri wa rais wa UAE, alisema katika chapisho kwenye X kwamba: "Baada ya uchokozi mkali wa Iran, utawala huo unajaribu kuweka hali mpya iliyozaliwa kutokana na kushindwa wazi kijeshi."
Alisema kuwa "majaribio ya kudhibiti Mlango wa Hormuz au kuingilia mamlaka ya baharini ya UAE si chochote zaidi ya ndoto zisizowezekana."
Mahusiano kati ya Iran na UAE yamezorota sana tangu vita hivyo kuanza, baada ya Tehran kurusha makombora na ndege zisizo na rubani dhidi ya nchi za Ghuba kujibu mashambulizi ya Marekani na Israel.
Iran wiki iliyopita iliishutumu UAE kwa kuwa na jukumu la moja kwa moja katika vita hivyo, madai ambayo Abu Dhabi ilikanusha.
UAE pia ilipinga vikali udhibiti wa Iran juu kuhusu mlango huo na kuitaka hatua ya pamoja kuhakikisha uhuru wa usafiri wa baharini katika njia hiyo ya maji.
UAE ilitangaza Ijumaa iliyopita kuwa inaharakisha ujenzi wa bomba jipya la mafuta litakalopita nje ya Hormuz kupitia bandari ya Fujairah.
Ofisi ya Vyombo vya Habari ya Abu Dhabi ilisema bomba hilo la magharibi hadi mashariki litazidisha mara mbili uwezo wa kampuni ya taifa ya mafuta ADNOC kusafirisha mafuta kupitia Fujairah, na kuongeza kuwa linatarajiwa kuanza kazi mwaka ujao.
Iran imekuwa ikiishutumu mara kwa mara nchi za Ghuba kwa kuruhusu vikosi vya Marekani kutumia maeneo yao kuanzisha mashambulizi, lakini nchi hizo zimekanusha madai hayo, zikisisitiza hata kabla ya mzozo huo kwamba hazitaruhusu ardhi au anga yao kutumika kushambulia Iran.

Chanzo cha picha, Getty Images
"Mtikisiko katika sekta ya nishati kimataifa"
Shirika la kimataifa la nishati lilisema mzozo huo utasababisha mshtuko mkubwa zaidi wa nishati duniani.
Shirika hilo lilionya Alhamisi kwamba ongezeko la mahitaji ya mafuta wakati wa majira ya joto, pamoja na ukosefu wa usambazaji mpya kutoka Mashariki ya Kati, linaweza kufanya soko kuingia katika "eneo hatari" mwezi Julai na Agosti.
Meli chache sasa zinapita katika Mlango wa Hormuz ikilinganishwa na meli 125 hadi 140 zilizokuwa zikivuka kila siku kabla ya vita.
Islamic Republic News Agency (IRNA) iliripoti kuwa meli 31 zilipitia Mlango wa Hormuz ndani ya saa 24 zilizopita kwa uratibu na jeshi la wanamaji la Iran.












