Paka mweusi wa ajabu anayepatikana Afrika pekee

Chanzo cha picha, getty
Ushawahi kukutana na paka mweusi, iwe ni usiku ama mchana?
Kama unafikiri ni yule paka wa kawaida anayezunguka mitaani au nyumbani, La hasha sio huyo uliyemzoea.
Hapa tunazungumzia serval mweusi, paka wa porini anayepatikana Afrika, mwenye miguu mirefu, masikio makubwa na manyoya meusi kabisa.
Serval ni paka wa porini mwenye ukubwa wa kati anayepatikana Afrika. Serval wa kawaida tayari ni mnyama wa kuvutia. Ana miguu mirefu sana, shingo ndefu, masikio makubwa na madoa yanayomfanya afanane kidogo na duma.
Lakini serval mweusi ni paka tofauti kabisa.
Manyoya yake huwa meusi sana, karibu kama yamepakwa rangi. Wakati mwingine ukimtazama kwa karibu unaweza kuona madoa hafifu yakijitokeza kwenye weusi huo.
Rangi hiyo ya ajabu inatokana na mabadiliko ya kijenetiki yanayoathiri namna mwili wake unavyotengeneza rangi ya manyoya. Wanasayansi bado hawajaweza kubaini kikamilifu mabadiliko hayo yanayotokea kwenye vinasaba vyake.

Chanzo cha picha, Getty Images
Na usidhani kwa sababu anaonekana kama paka wa kawaida basi hana uwezo mkubwa.
Serval ana miguu mirefu kuliko paka mwingine yeyote kwa uwiano wa ukubwa wa mwili wake. Anaweza kukimbia kwa kasi ya karibu kilomita 64 kwa saa na kuruka hadi mita tatu kwenda juu. Huo ni uwezo unaomsaidia sana wakati wa kuwinda.
Serval hula wanyama wadogo kama panya na mamalia wengine wadogo, pamoja na reptilia na amfibia. Miguu hiyo mirefu humsaidia pia kumkwepa adui kama chui, fisi na mbwa mwitu wa Afrika.
Masikio yake yanashangaza
Masikio ya serval ni makubwa sana ukilinganisha na kichwa chake. Kama masikio ya binadamu yangekuwa na ukubwa sawa kwa uwiano, yangekuwa karibu sawa na sahani kubwa za chakula.
Na masikio hayo si ya mapambo. Serval ana misuli 22 kwenye masikio yake, jambo linalomwezesha kuzungusha kila sikio kivyake hadi nyuzi 180.
La kustaajabisha zaidi ni kuwa anaweza kusogeza sikio moja upande huu na jingine upande mwingine.
Hii inamsaidia sana anapowinda kwenye nyasi ndefu. Mara nyingi mawindo yake huwa hayaonekani kabisa. Lakini serval anaweza kuyasikia hata kama yamejificha chini ya majani au ardhini.
Kwa kutumia masikio yake kama rada, anaweza kubaini mahali ambapo mawindo yake yalipo.
Ndiyo maana serval ni wawindaji wazuri sana. Wakati simba na chui wanaweza kufanikiwa katika takriban uwindaji mmoja kati ya mitatu, serval hufanikiwa zaidi ya nusu ya mara anapojaribu kuwinda.
Kwa nini paka hawa weusi wanaonekana Tsavo?
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kwa muda mrefu, serval weusi walijulikana zaidi katika maeneo yenye misitu minene na baridi, hasa maeneo yaliyo juu ya mita 2,000 kutoka usawa wa bahari.
Kwa mfano, wameonekana katika Milima ya Aberdare nchini Kenya na Nyanda za Juu za Ethiopia.
Wazo lilikuwa kwamba manyoya yao meusi yaliwasaidia kujificha kwenye misitu, hasa kwenye maeneo yenye vivuli vingi.Lakini baadaye jambo la kushangaza likaanza kuonekana.
Serval weusi wakaanza kuonekana Tsavo, eneo kubwa na lenye joto na ukame nchini Kenya. Mazingira hayo yamewafanya wanasayansi kutaka kudadisi kama rangi nyeusi inawasaidia kujificha msituni, wanafanya nini kwenye nyanda hizi zilizo wazi na zenye mwanga mwingi?
Utafiti uliofanywa na Sheldrick Wildlife Trust na Wildlife Works kati ya mwaka 2011 na 2016 ulionyesha jambo la kushangaza.
Karibu asilimia 47 ya serval walioonekana Tsavo walikuwa weusi. Hiyo ni idadi kubwa kuliko ilivyokuwa imeonekana katika maeneo ya misitu yaliyo kwenye mwinuko mkubwa.
Kwa nini kuna serval weusi wengi kiasi hicho Tsavo?
Kuna maelezo kadhaa yanayoweza kueleza kwa nini serval weusi wanaonekana kwa wingi katika baadhi ya maeneo.
Nadharia moja inasema huenda rangi yao nyeusi inawafanya waonekane na kurekodiwa kwa urahisi zaidi katika maeneo hayo. Kwa maana hiyo, huenda si kwamba wako wengi zaidi, bali ni kwamba watafiti wana nafasi kubwa zaidi ya kuwaona. Hii inaweza kuwa changamoto ya namna sampuli zilivyokusanywa.
Nadharia nyingine inaeleza kwamba huenda idadi hiyo imetokana tu na mabadiliko ya nasibu katika mzunguko wa vinasaba. Kwa lugha rahisi, inaweza kuwa ni suala la bahati ya kijenetiki.
Lakini kuna uwezekano mwingine pia. Huenda vinasaba vinavyowafanya wawe na rangi nyeusi vinawapa pia sifa nyingine ambazo si rahisi kuziona, kama uwezo bora wa kudhibiti joto la mwili au kustahimili magonjwa. Ikiwa ndivyo, sifa hizo zinaweza kuwasaidia kuishi kwa muda mrefu na kuzaana zaidi, hivyo kupitisha vinasaba hivyo kwa kizazi kinachofuata.
Kwa sasa, hakuna jibu la uhakika kuhusu sababu hasa wanapatikana katika mazingira ya joto.
Lakini sababu iwe yoyote, serval mweusi bado ni mnyama adimu, wa kuvutia na wa kuvutia macho unapobahatika kuuona porini.
Imetafsiriwa na Mariam Mjahid na kuhaririwa na Ambia Hirsi































