Christa Pike yuko katika hali mahututi baada ya kunusurika sindano mbili za kifo

Chanzo cha picha, Tennessee Department of Correction
Mfungwa wa Tennessee anayekabiliwa na adhabu ya kifo, Christa Pike, yuko katika hali mahututi hospitalini akipatiwa matibabu ya kuokoa maisha baada ya kunusurika majaribio mawili ya kunyongwa kwa sindano yenye sumu, tukio lililosababisha gavana wa jimbo hilo kusitisha utekelezaji wote wa adhabu za kifo kwa mwaka huu.
"Wakati huu hatuna taarifa nyingi kuhusu hali yake ya afya au uwezekano wa kupona, lakini tunajua bado yuko hai," wakili wake Randy Spivey aliwaambia waandishi wa habari Alhamisi.
Mawakili wake sasa wanaitaka hukumu yake ya kifo ibadilishwe. Pike, mwenye umri wa miaka 50, alihukumiwa kifo mwaka 1996 kwa mauaji ya Colleen Slemmer.
Kwa mujibu wa mawakili wake, Pike alidungwa dozi mbili za dawa ya pentobarbital, inayotumika kutekeleza hukumu ya kifo siku ya Jumatano lakini hakufariki. Baadaye alipelekwa hospitalini kwa gari la wagonjwa.
Pike alikuwa na umri wa miaka 18 alipomshambulia, kumtesa na kumuua Slemmer, mwenye umri wa miaka 19, pamoja na aliyekuwa mpenzi wake wakati huo, Tadaryl Shipp.
Jaribio la kutekeleza hukumu yake ya kifo lilikuwa limekumbwa na mvutano wa kisheria wa dakika za mwisho, kabla ya Mahakama Kuu ya Marekani kuruhusu kutumiwa kwa njia hiyo ya kudungwa sindano.
Mama wa Slemmer, May Martinez, ambaye alikuwa miongoni mwa waliotaka Pike auawe na alisafiri hadi Tennessee kushuhudia utekelezaji huo, aliiambia NBC News baada ya jaribio hilo kushindikana kwamba, "kulikuwa na vurugu na mkanganyiko mkubwa."
Alhamisi, mawakili wa Pike walitoa maelezo zaidi kuhusu kilichotokea, wakielezea tukio la kutisha lililofanyika kwa usiri mkubwa.
"Jana usiku timu ya utekelezaji hukumu hiyo ilijaribu kumdunga sindani kwa njia ya mshipa kwa saa moja nzima," alisema Spivey. "Nilihesabu sindano saba alizodungwa kwenye mkono wake wa kushoto pekee, moja ikiwa imepinda ilipotolewa baada ya jaribio kushindikana."
Spivey alisema mashahidi waliokuwa wakifuatilia utekelezaji huo waliwekwa katika chumba chenye giza nyuma ya pazia lililofungwa baada ya dozi ya pili kuingizwa mwilini mwa Pike, huku ikiwa wazi kwamba Pike bado alikuwa anapumua dakika kadhaa baadaye.
"Hakuna aliyekuwa akijua kilichokuwa kinaendelea nyuma ya pazia hilo," alisema. "Sikujua ni lini au kama wataalamu wa afya walianza kumsaidia."
Spivey alisema Gavana wa Tennessee anapaswa sasa kubadilisha hukumu ya kifo ya Christa, ombi ambalo awali lilikuwa limekataliwa.
Wakili mwingine wa Pike, Stephen Ferrell, alisema timu ya utetezi pia inachunguza njia nyingine za kisheria.
"Tunataka kulifikiria suala hili kwa makini na kuhakikisha Christa anapona ili aweze kutoa maoni yake kuhusu hatua anazotaka zichukuliwe," alisema.
Gavana wa Tennessee, Bill Lee, ameagiza uchunguzi huru kufanyika kuhusu jaribio hilo lililoshindikana la kutekeleza hukumu ya kifo na amesema uchunguzi huo utakuwa wa kina.
"Uchunguzi huu utakuwa wa kina na utachukua muda," alisema Alhamisi.
Soma Zaidi:






















