Ajali 6 mbaya zaidi za majini zilizotikisa dunia

Chanzo cha picha, (Crédit photo : JOEL NITO/AFP via Getty Images)
- Author, Abdou Aziz Diedhiou
- Nafasi, BBC News Afrique
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 8
Mwishoni mwa Septemba, watu nchini Senegal hukumbuka moja ya matukio yenye uchungu mkubwa ambayo wamewahi kupitia kama taifa.
Mnamo Septemba 26, 2002, meli ya Le Joola, iliyokuwa ikitoa huduma ya usafiri wa majini kati ya Ziguinchor, kusini mwa Senegal, na Dakar, ilizama katika pwani ya Gambia.
Janga hilo, lililosababisha vifo vya zaidi ya watu 1,800, bado linachukuliwa kuwa ajali mbaya zaidi ya majini kuwahi kurekodiwa barani Afrika.
Lakini kwa kiwango cha dunia, kumekuwa na majanga mabaya zaidi. Mataifa mengine pia yamelazimika kuomboleza kutokana na ajali mbaya za majini.
Baadhi ya majanga hayo yameacha alama katika historia, kutokana na mazingira yaliyosababisha kutokea kwake pamoja na idadi kubwa sana ya watu waliopoteza maisha.
Katika makala haya, BBC News Africa inakuletea simulizi kuhusu majanga sita ya majini yaliyotikisa dunia, sababu zilizosababisha na idadi ya watu waliopoteza maisha.
6. Estonia – Septemba 28, 1994: Vifo 852

Chanzo cha picha, Georges DeKeerle/Sygma via Getty Images
Nchini Estonia, Sweden na Finland, makumbusho yamejengwa kwa ajili ya kuwakumbuka waathiriwa wa ajali hiyo ya majini isiyosahaulika, ya Estonia, iliyotokea Septemba 28, 1994.
Estonia ilikuwa feri iliyokuwa ikitoa huduma ya usafiri wa majini kati ya Tallinn, mji mkuu wa Estonia ulioko katika Ghuba ya Finland, na Stockholm, mji mkuu wa Sweden.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Janga hilo lilitokea usiku wa Septemba 27-28, 1994. Usiku huo, utabiri wa hali ya hewa ulionyesha kuwepo kwa upepo mkali na mawimbi makubwa sana.
Baada ya kuondoka Tallinn jioni ya Septemba 27, Estonia ilikumbana na upepo mkali sana na mawimbi makubwa ilipokuwa katikati ya safari kuelekea Stockholm.
Takriban saa 7 usiku, mlango wa mbele wa feri hiyo hatimaye ulishindwa kuhimili nguvu ya mawimbi.
Maji mengi yalianza kuingia ndani ya meli hiyo, ambayo ilipoteza uwiano kabla ya kupinduka ghafla na kuzama katika maji ya baridi ya Bahari ya Baltic ndani ya muda usiozidi saa moja.
Walionusurika walielezea tukio hilo kama "usiku wa kuzimu", huku abiria walioshtushwa na kasi ya matukio wakinaswa ndani ya meli kutokana na njia za kutokea kuzuiwa baada ya meli hiyo kupinduka.
Kati ya abiria na wafanyakazi 889 waliokuwa ndani ya feri hiyo, ni watu 137 pekee waliookolewa.
Watu 852, wengi wao wakiwa Wasweden 501 na Waestonia 285, walipoteza maisha katika janga hilo, pamoja na watu kutoka mataifa mengine kadhaa.
Uchunguzi wa kimataifa ulihitimisha kuwa kulikuwa na hitilafu ya kiufundi katika mlango wa mbele wa feri hiyo. Hata hivyo, nadharia mbalimbali za njama zinazohusiana na janga hilo zimeendelea kusambaa hadi leo.
5. Al-Salaam Boccaccio – Februari 6, 2006 (Misri): Vifo 1,028

Chanzo cha picha, Marco Di Lauro/Getty Images
Mnamo Februari 3, 2006, takriban watu 1,400 walipanda feri ya As-Salam Boccaccio 98, meli ya Misri iliyokuwa na umri wa miaka 35.
Feri hiyo ilikuwa imeondoka katika bandari ya Douba nchini Saudi Arabia kuelekea bandari ya Safaga nchini Misri, upande mwingine wa Bahari ya Shamu, takriban kilomita 600 kusini-mashariki mwa Cairo.
Muda mfupi baada ya kuondoka Douba, moto ulizuka, lakini hilo halikumzuia nahodha wa meli hiyo kuendelea na safari.
Wasafiri wengi walikuwa mahujaji kutoka Misri waliokuwa wakirejea kutoka Makka.
Moto ulipoanza kuenea ndani ya meli, baadhi ya abiria waliokata tamaa walijitosa majini.
Idadi ndogo ya boti za kuokoa maisha ilimaanisha kuwa watu wengi zaidi hawakuweza kuokolewa. Ni watu 354 pekee walionusurika katika janga hilo.
Moto huo uliifanya meli hiyo kupinduka, na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 1,000 huku mamia ya manusura wakipata majeraha makubwa na mshtuko wa kihisia.
4. Titanic – Aprili 14-15, 1912 (Uingereza): Vifo 1,550

Chanzo cha picha, History/Universal Images Group via Getty Images
Vyombo vya habari vya wakati huo viliielezea meli maarufu ya Titanic kama "ikulu inayoelea." Ikiwa na urefu wa mita 269 na upana wa mita 28.5, ghorofa nane, lifti na uwezo wa kubeba watu 3,000, Titanic ilionekana kuwa jitu la baharini ambalo hakuna jambo lingeweza kulipata.
Ilikuwa na kila kitu ambacho mtu angehitaji kwa upande wa starehe: umeme na mfumo wa kupasha joto, vyumba vya kulala vyenye bafu, kumbi za kifahari, bwawa la kuogelea na huduma nyingine.
Katika safari yake ya kwanza, meli hiyo iliondoka Southampton nchini Uingereza Aprili 10, 1912, ikiwa njiani kuelekea New York.
Takriban watu 2,200 walikuwa ndani ya meli hiyo, wakiwemo wafanyakazi na abiria, baadhi yao wakiwa matajiri ambao hawakutaka kukosa safari hiyo ya kipekee.
Siku nne baada ya kuanza safari, meli hiyo, iliyokuwa ikichukuliwa kuwa mojawapo ya meli salama zaidi duniani, ilipata ajali katika Bahari ya Atlantiki baada ya kugonga jiwe la barafu saa 11:40 usiku Aprili 14, 1912.
Maji yalianza kuingia ndani ya meli hiyo na ndani ya muda usiozidi saa tatu, Titanic ilizama kabisa takriban kilomita 900 kutoka pwani ya Newfoundland.
Upungufu wa boti za kuokoa maisha pamoja na taharuki ulifanya isiwezekane kuwaokoa wote.
Takriban watu 1,550 walipoteza maisha, huku manusura 711 pekee wakirejeshwa New York.
Kuzama kwa Titanic kulifanya janga hilo kuwa mojawapo ya ajali kubwa zaidi za majini na baadaye likawa mada ya filamu iliyofanikiwa sana mwishoni mwa miaka ya 1990.
3. Le Joola – Septemba 26, 2002 (Senegal): Vifo 1,864

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Mnamo Septemba 26, 2002, Le Joola iliondoka katika bandari ya Ziguinchor, kusini mwa Senegal, ikiwa njiani kuelekea Dakar.
Ndani ya meli hiyo kulikuwa na takriban abiria 2,000, licha ya kuwa ilikuwa na uwezo wa kubeba watu wasiozidi 550.
Kabla ya kuanza kwa mwaka wa masomo wa 2002, familia nyingi, wanawake, watoto na wanafunzi walikuwa wamepanda meli hiyo Ziguinchor na walitarajia kufika Dakar mapema asubuhi ya Septemba 27.
Takriban saa 4:30 usiku, meli hiyo ilipokuwa katika pwani ya Gambia, dhoruba ya kitropiki iliikumba. Mmoja wa injini zake pia ulikuwa umeharibika.
Mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali wenye kasi ya mafundo 35, sawa na kilomita 65 kwa saa, iliipiga meli hiyo, na kuwalazimisha abiria waliokuwa kwenye sitaha ya upande wa kulia kuhamia upande mwingine kwa ajili ya kujikinga.
Katika sehemu ya chini ya meli, bidhaa na magari ambayo hayakuwa yamefungwa vizuri vilianza kuelemea upande mmoja, na kusababisha Le Joola kuinamia kwa hatari upande wake wa kushoto.
Meli hiyo ilipoanza kuinama, maji yaliingia kupitia madirisha na kuanza kujaa ndani ya chombo hicho. Ghafla, feri hiyo ilipinduka kwa kasi.
Walionusurika walielezea hali ya vurugu ndani ya meli hiyo, huku kukiwa na mayowe, watu walionaswa na wengine wakitafuta njia ya kutokea.
Kwa jumla, watu 1,864 waliripotiwa rasmi kufariki katika ajali hiyo ya meli, huku ni watu 64 pekee walionusurika.
Wakati familia zikiendelea kutaka meli hiyo itolewe baharini, serikali ya Senegal imejenga Makumbusho ya Kumbukumbu ya janga hilo katika bandari ya Ziguinchor, eneo ambako feri hiyo ilianza safari yake.
2. Doña Paz – Desemba 20, 1987 (Ufilipino): Vifo 4,386

Chanzo cha picha, Gabriel Mistral/Getty Images
Doña Paz ilikuwa feri ya Ufilipino. Hadi leo, inashikilia rekodi ya idadi kubwa zaidi ya watu waliokufa katika ajali ya majini iliyotokea wakati wa amani.
Usiku wa Desemba 20, 1987, siku chache kabla ya Krismasi, feri hiyo ilikuwa ikisafiri kutoka Tacloban kuelekea Manila.
Rasmi, meli hiyo ilikuwa na uwezo wa kubeba abiria 1,500. Lakini ndani yake kulikuwa na karibu abiria 4,400, wengi wao wakiwa wanasafiri bila tiketi.
Takriban saa 4:30 usiku, Doña Paz iligongana na meli ndogo ya kubeba mafuta, Vector, iliyokuwa imebeba zaidi ya lita milioni moja za mafuta yaliyosafishwa.
Mlipuko wa matangi ya mafuta ya meli hiyo ulisababisha moto kuenea mara moja hadi kwenye Doña Paz. Madhara ya janga hilo yalikuwa makubwa sana.
Ndani ya dakika chache, feri hiyo ilifunikwa na moto. Abiria walinaswa katika vyumba vyao, huku wengine wakiruka baharini ili kukimbia moto, lakini uso wa bahari ulikuwa umefunikwa na mafuta yaliyokuwa yakiteketea.
Idadi rasmi ya waliokufa inakadiriwa kuwa 4,386. Hata hivyo, baadhi ya watu wanaamini kuwa idadi hiyo inaweza kuwa kubwa zaidi kutokana na kuwepo kwa wasafiri waliokuwa wamejificha ndani ya meli bila tiketi.
Ni manusura 26 pekee waliookolewa na boti za uvuvi na meli zilizokuwa zikapita.
Mashahidi walielezea kuona miili iliyoteketea ikielea katika bahari iliyokuwa imejaa moto.
Kuzidi kwa idadi ya abiria na uwezo wa meli hiyo kulitajwa kuwa miongoni mwa mambo yaliyochangia janga hilo, pamoja na kugongana na meli hiyo ya mafuta iliyokuwa ikisafirisha mafuta kinyume cha sheria.
1. Wilhelm Gustloff – Januari 30, 1945 (Ujerumani): Vifo 9,000

Chanzo cha picha, Imagno/Getty Images
Ajali hii inatajwa kuwa janga la majini lililosababisha vifo vingi zaidi katika historia, lakini ni tukio ambalo halijadiliwi sana.
Mnamo Januari 30, 1945, meli ya abiria ya Ujerumani Wilhelm Gustloff ilizama katika maji ya baridi ya Bahari ya Baltic, na kusababisha vifo vya maelfu ya watu, wengi wao wakiwa raia.
Meli hiyo, iliyokuwa inamilikiwa na utawala wa Nazi, iliondoka Kiel nchini Ujerumani ikiwa njiani kuelekea Hamburg Januari 30, 1945, kabla ya kusafiri kwa tahadhari katika maji ya Bahari ya Baltic.
Takriban watu 10,000 walikuwa ndani ya meli hiyo, wakiwemo raia 9,000 waliokuwa wakikimbia kusonga mbele kwa wanajeshi wa Urusi na mabaharia 1,000.
Takriban saa 12 jioni Januari 30, 1945, Wilhelm Gustloff ilionekana na manowari ya Kisovieti S-13, chini ya uongozi wa Kapteni Alexander Marinesko.
Saa 3 usiku, ikiwa ndani ya umbali wa kushambuliwa, meli hiyo ya Ujerumani ilipigwa na torpedo nne.
Watu wengi walikufa kutokana na milipuko hiyo na kwa kuzama baada ya meli hiyo kupinduka.
Idadi ya waliokufa inakadiriwa kuwa kati ya 6,000 na 9,000. Wanahistoria wengi wanakubaliana kwamba takriban watu 9,000 walipoteza maisha.
Baadhi wameita shambulio dhidi ya Wilhelm Gustloff kuwa uhalifu wa kivita. Hata hivyo, wengine wanaamini kuwa uwepo wa mabaharia wa Kijerumani wapatao 1,000 waliokuwa na silaha unaondoa uwezekano wa kulichukulia tukio hilo kama uhalifu wa kivita.
Hadi leo, hakuna ajali ya majini inayojulikana kuwa imesababisha vifo vya watu wengi zaidi.
Muktadha wa Vita vya Pili vya Dunia na baadaye Vita Baridi ulifanya janga hili lisijulikane sana na kufunikwa kabisa na matukio mengine ya kihistoria.



































