Moja kwa moja, Rubani 'shujaa' azuia janga angani baada ya kuchomwa kisu na mwenzake

Abiria na wahudumu wa ndege walifanikiwa kumdhibiti mshambuliaji huyo na kurejesha udhibiti wa ndege.

Muhtasari

Ruka Video uendelee
  • Wicknell Chivayo
  • Kijanangoma
  • xx
  • Besigye
  • .
  • xx
  • xx
  • xx
  • Lungu
  • xx
  • xx
  • d
  • s
  • a
  • Sonko
  • xx
  • xx
  • xx

Moja kwa moja

Na Asha Juma

  1. Mfungwa wa Marekani anusurika sindano mbili za kifo

    .

    Mfungwa aliyehukumiwa kifo katika jimbo la Tennessee nchini Marekani, Christa Pike, amepelekwa hospitalini baada ya moyo wake kuendelea kudunda licha ya kudungwa sindano mbili za dawa ya kutekeleza hukumu ya kifo, kwa mujibu wa wakili wake.

    Timu yake ya mawakili iliwasilisha ombi la dharura la kusitisha utekelezaji wa hukumu hiyo wakati ikiendelea, ikisema:

    “Bi Pike amepoteza fahamu lakini moyo wake bado unapiga na anatoa sauti ya kukoroma.”

    Mmoja wa mawakili wake aliiambia BBC kuwa Pike, mwenye umri wa miaka 50, alikuwa akipewa matibabu ya kuokoa maisha hospitalini baada ya kupewa dozi mbili za dawa iitwayo pentobarbital.

    Pike alihukumiwa kifo mwaka 1996 kwa kumuua Colleen Slemmer, mwenye umri wa miaka 19.

    Jaribio la kutekeleza hukumu hiyo lilifanyika katika Gereza la Riverbend Maximum Security Institution, mjini Nashville, karibu saa 20:00 Jumatano kwa saa za eneo.

    Kwa mujibu wa shirika la habari la Associated Press, Pike alipewa dozi mbili za pentobarbital, huku pazia ya chumba cha mashahidi ikifungwa mara mbili wakati wa mchakato huo. Shirika hilo pia liliripoti kuwa waandishi wa habari waliombwa kuondoka katika eneo hilo wakati fulani.

    Timu ya mawakili wa Pike ilisema katika taarifa kwa gazeti la The Tennessean:

    “Usiku wa leo, Serikali ya Tennessee imeshindwa tena kutekeleza hukumu ya kifo kwa mujibu wa sheria.”

    Wakaongeza: “Hatufurahii kwamba tulikuwa sahihi, lakini wasiwasi ulioelezwa na Bi Pike umeonekana kuwa wa kweli: ugumu wa kupata mshipa, mishipa kuharibika, pentobarbital kuwa imeharibika, na kutokuwepo kwa huduma za dharura za matibabu wakati mambo yanapokwenda vibaya, huku yote yakifanyika chini ya utaratibu ambao bado umezungukwa na usiri.”

    Baada ya utekelezaji wa hukumu hiyo kwa kutumia sindano kuonekana kutofanyika kama ilivyotarajiwa, mawakili wa Pike waliwasilisha ombi la dharura la kusitisha utekelezaji huo na kuomba apewe huduma za matibabu.

  2. Uingereza yaishutumu Iran kuhusika na tukio la RAF Fairford

    .

    Serikali ya Uingereza inaamini kuwa Iran ilihusika kwa namna fulani katika tukio la RAF Fairford lililosababisha wanaume watano kukamatwa na baadaye kuachiliwa kwa dhamana, amesema Waziri Mkuu wa Uingereza, Andy Burnham.

    "Kuna dalili thabiti kwamba Iran ilihusika katika kile kilichotokea mwishoni mwa wiki katika RAF Fairford," Burnham aliiambia BBC.

    Hata hivyo, hakutoa maelezo zaidi kuhusu ushahidi ulioifanya serikali kufikia hitimisho hilo.

    Iran imejibu madai hayo, huku Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, Abbas Araghchi, akisema kiongozi huyo wa Uingereza "anapoteza mwelekeo".

    "Naweza kuthibitisha imani ya Iran kwamba kuwaachilia kwa dhamana wanaodaiwa kuwa magaidi wanaofanya kazi kwa niaba ya nchi za kigeni kunaeleza kila kitu," Araghchi aliandika kwenye mitandao ya kijamii.

    Burnham pia alijibu maswali kuhusu kwa nini watuhumiwa hao walipewa dhamana, hatua ambayo imekosolewa hadharani na Rais wa Marekani, Donald Trump.

    Akizungumza katika Ikulu ya White House Jumatatu, Trump alisema: "Nitawaambia, mimi ningesema wasipewe dhamana. Nimeshangazwa kwamba wameachiliwa. Mimi nisingefanya hivyo."

    Hata hivyo, Burnham alitetea uamuzi huo, akisisitiza kuwa watuhumiwa hao wako chini ya masharti makali sana ya dhamana.

    "Watu wanapaswa kuelewa kwamba kuachiliwa hakumaanishi kile ambacho wengi wanaweza kudhani. Kuna masharti makali zaidi ya dhamana," alisema.

    "Mamlaka zinaidhibiti hali hii kwa karibu sana, na ninaweza kuwahakikishia hilo."

    Kauli za Burnham zimekuja baada ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, kusema Jumatatu kwamba tukio la RAF Fairford "kwa wazi linahusisha mhusika wa kigeni".

    Pia unaweza kusoma:

  3. Ronaldo aondoka kambini mwa Ureno, aahidi kusema ukweli baadaye

    .

    Mshambuliaji nyota wa Ureno, Cristiano Ronaldo, amesema ameondoka kambini mwa timu ya taifa na kwamba atafichua sababu za uamuzi wake huo "kwa wakati muafaka".

    Hatua hiyo imekuja baada ya kocha mkuu Jorge Jesus kukanusha madai ya kuwepo kwa mgogoro kati yake na nahodha huyo wa Ureno, kufuatia ripoti zilizodai kuwa Ronaldo alikuwa amekataa kufanya mazoezi.

    Ronaldo, ambaye alisema aliwahi kufikiria kustaafu soka la kimataifa baada ya Kombe la Dunia la mwaka huu lakini akaamua kuendelea akilenga kufikisha mabao 1,000 katika kari yake, alijumuishwa kwenye kikosi cha wachezaji 25 cha Ureno kwa mechi za kimataifa za mwezi huu.

    Mchezaji huyo wa Al-Nassr alianza katika mchezo wa kwanza wa Ureno kwenye Ligi ya Mataifa dhidi ya Wales siku ya Jumapili, lakini hakucheza katika ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Norway mjini Oslo.

    Baada ya mechi hiyo, Ronaldo hakwenda kuwashukuru mashabiki pamoja na wachezaji wenzake, badala yake alielekea moja kwa moja vyumbani, hali iliyozua uvumi kuwa hakuwa na furaha na kocha wake.

    Akizungumza na wanahabari kabla ya mechi dhidi ya Denmark, Jesus alisema:

    "Hakukuwa na tukio lolote. Mchezaji yeyote akitumia dakika 20 au 30 kupasha misuli joto halafu asiingie uwanjani, hawezi kufurahia hali hiyo."

    Kocha huyo alisema alimweleza Ronaldo kabla ya mchezo kwamba hangeanza katika kikosi cha kwanza lakini angeweza kuingizwa baadaye kulingana na mazingira ya mchezo.

    "Baadaye, kama kocha, niliamua kutomuingiza. Hilo si jambo la kuleta mjadala mkubwa," alisema.

    Jesus pia alikanusha taarifa zilizodai kuwa Ronaldo aligoma kufanya mazoezi, akisema mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 41 alikuwa akifanya mazoezi maalum ya kuimarisha mwili na misuli.

    Hata hivyo, Ronaldo hakuonekana uwanjani pamoja na wachezaji wenzake nchini Denmark, huku vyombo vya habari vya Ureno vikichapisha video ikimuonyesha akiondoka katika Uwanja wa Parken.

    Baadaye, Ronaldo alitangaza kupitia Instagram kuwa ameondoka kambini.

    "Baada ya mkutano wa waandishi wa habari wa timu ya taifa na baada ya mazungumzo na rais wa Shirikisho la Soka la Ureno, nimeamua kuondoka kambini."

    "Kwa wakati muafaka, nitawaambia Wareno wote ukweli kuhusu sababu zilizonifanya kuchukua uamuzi huu."

    Pia aliwatakia kila la heri wachezaji wenzake katika mechi zijazo.

    Soma Zaidi:

  4. Wicknell Chivayo: Salamu za rambirambi zaendelea kumiminika baada ya kifo chake

    .

    Salamu za rambirambi zinaendelea kutolewa kufuatia kifo cha mfanyabiashara mashuhuri wa Zimbabwe, Wicknell Chivayo, na mkewe Lucy Muteke, waliokuwa miongoni mwa watu sita waliofariki dunia baada ya helikopta kuanguka eneo la Marondera Rural, mashariki mwa Harare, Jumatano. Mamlaka zilisema hakuna aliyenusurika.

    Akiwa anajulikana kwa utajiri wake, misaada kwa jamii na uhusiano mpana na viongozi wa kisiasa na kidini barani Afrika, Chivayo alikuwa mmoja wa wafanyabiashara waliotambulika zaidi nchini Zimbabwe.

    William Ruto: "Rafiki yangu wa karibu"

    Rais wa Kenya, William Ruto, ameongoza salamu za rambirambi, akimtaja Chivayo kuwa "rafiki wa karibu" ambaye uchangamfu wake uliwagusa watu wengi. Ruto alisema atamkumbuka kwa urafiki wake, nguvu zake na imani yake katika uwezo wa Afrika, huku akituma pole kwa familia za waliofariki, Emmerson Mnangagwa na wananchi wa Zimbabwe.

    Ruto na Chivayo walikuwa na uhusiano uliovutia umma, huku mfanyabiashara huyo mara kwa mara akichapisha picha za mikutano yao, ikiwemo ziara zake katika State House Nairobi.

    Familia ya Chivayo: "Tumekosa maneno"

    Familia ya Wicknell Chivayo imethibitisha kuwa yeye na mkewe, Lucy Muteke, ni miongoni mwa watu waliofariki dunia katika ajali hiyo ya helikopta.

    Msemaji wa familia, Herbert Chivayo, alithibitisha vifo hivyo kwa Shirika la Utangazaji la Zimbabwe (ZBC).

    Alisema: "Tumekosa maneno kufuatia tukio hili la kusikitisha."

    Highlanders FC wamuomboleza mfadhili wao

    Klabu ya soka ya Zimbabwe, Highlanders FC, imetoa salamu za rambirambi kwa Chivayo, ambaye alikuwa mmoja wa wafadhili wake wakubwa.

    Ripoti zinasema alitoa mchango wa takriban shilingi milioni 32.4 za Kenya kwa klabu hiyo Jumatano, saa chache kabla ya ajali hiyo, jambo lililofanya msaada huo kuwa miongoni mwa matendo yake ya mwisho ya ukarimu kwa jamii.

    Viongozi wa Afrika waliokuwa na uhusiano na Chivayo

    Chivayo alikuwa akijulikana kwa kukutana na viongozi mbalimbali wa Afrika, wakiwemo Samia Suluhu Hassan, Emmerson Mnangagwa, Hakainde Hichilema, Yoweri Museveni, Bola Ahmed Tinubu na Mfalme Mswati III.

    Hata hivyo, mbali na taarifa ya Rais Ruto, hakukuwa na salamu nyingine rasmi za rambirambi kutoka kwa viongozi hao zilizokuwa zimethibitishwa kwa kujitegemea wakati makala hii ikichapishwa.

    Chapisho lake la mwisho kwenye mitandao ya kijamii

    Chapisho la mwisho la umma la Wicknell Chivayo kwenye mtandao wa X pia limezua mjadala mkubwa baada ya taarifa za kifo chake kuibuka.

    Chivayo alichapisha ujumbe huo asubuhi ya tarehe 30 Septemba, saa chache kabla ya helikopta aliyokuwa akisafiria kupata ajali.

    Ulikuwa ujumbe wa kuwapongeza mawakili wawili ambao alisema walikuwa wamemuunga mkono kwa miongo kadhaa. Alianza chapisho hilo kwa maneno haya ya Kiingereza: "APPRECIATING RELATIONSHIPS BUILT OVER DECADES... SAVED THE BEST FOR LAST."

    Chapisho hilo lilijumuisha ahadi za kutoa magari ya kifahari na zawadi kubwa za fedha kwa watu aliokuwa akiwashukuru.

    Baada ya habari za kifo chake kusambaa, ujumbe huo umevutia hisia na mjadala miongoni mwa watumiaji wa mitandao ya kijamii kutokana na kuchapishwa saa chache kabla ya ajali iliyogharimu maisha yake.

    Soma Zaidi Hapa:

  5. Rubani "shujaa" azuia janga angani baada ya kudungwa kisu na mwenzake

    .

    Rubani mmoja amekamatwa baada ya kumchoma kisu rubani mwenzake kwenye ndege iliyokuwa ikisafiri kutoka Dubai kwenda Tel Aviv na "inaonekana alijaribu kuiangusha ndege hiyo", kwa mujibu wa Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu.

    Abiria na wahudumu wa ndege walifanikiwa kumdhibiti mshambuliaji huyo na kurejesha udhibiti wa ndege ya shirika la Flydubai, ambayo baadaye ilitua salama katika uwanja wa ndege wa Tabuk, kaskazini-magharibi mwa Saudi Arabia, ikiwa na zaidi ya watu 170 ndani.

    Abiria hao, ambao wengi wao walikuwa raia wa Israel, waliwasili baadaye Jumatano mjini Tel Aviv kwa ndege maalum ya kuwarejesha nyumbani.

    Rubani aliyechomwa kisu, aliyetambulika kama raia wa India Kapteni Smit Machchhar, amelazwa hospitalini lakini hali yake inaelezwa kuwa imara.

    Netanyahu pamoja na Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi, wamemsifu Kapteni Machchhar na kumtaja kama "shujaa" kutokana na mchango wake katika kusaidia kuzuia tukio hilo na kuokoa maisha ya watu waliokuwa ndani ya ndege.

    "Licha ya kudungwa kisu na kujeruhiwa vibaya, alipambana, akajitetea, akafungua mlango wa chumba cha marubani na kuwawezesha abiria pamoja na wahudumu wa ndege kumdhibiti mshambuliaji huyo, na hivyo kuzuia janga kubwa ambalo lingeweza kutokea angani," Netanyahu aliandika kwenye mtandao wa X.

    "Aliokoa maisha ya watu 174, wakiwemo raia wa Israel na mataifa mengine."

    Ubalozi wa India nchini Saudi Arabia umesema Kapteni Smit Machchhar anaendelea kupatiwa matibabu hospitalini na hali yake ni thabiti.

    Akitoa pongezi zake kwa rubani huyo, Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi, aliandika kwenye mtandao wa X: "Katika hali ya hatari kubwa sana, na licha ya kujeruhiwa vibaya, alionyesha ujasiri wa hali ya juu na azma isiyoyumba ya kulinda maisha ya wengine."

    "India inajivunia Kapteni Machchhar."

    Kauli hiyo ilikuja huku Kapteni Smit Machchhar akiendelea kupatiwa matibabu hospitalini baada ya kudungwa kisu akiwa kwenye ndege ya shirika la Flydubai iliyokuwa ikielekea Tel Aviv. Benjamin Netanyahu na Narendra Modi wamemsifu rubani huyo kwa kusaidia kuzuia kile walichosema kingegeuka janga kubwa angani

    Sababu ya tukio hilo bado haijajulikana, na rubani anayeshukiwa alikuwapo chini ya uchunguzi wa mamlaka za Saudi Arabia, kwa mujibu wa Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu.

    Akizungumza na kituo cha habari cha Fox News usiku wa Jumatano, Netanyahu alisema rubani huyo alitarajiwa kurejeshwa katika Falme za Kiarabu (UAE), ambako ndege hiyo ilianzia safari yake, baada ya taratibu za uchunguzi kukamilika.

    Soma Zaidi Hapa:

  6. Hujambo. Karibu katika matangazo yetu mubashara. Tarehe ni 01/10/2026.