Miji bora zaidi duniani mwaka 2026 na siri za mafanikio yake

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Lindsay Galloway
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Ni nini kinachoufanya mji uwe wa kuvutia kiasi cha watu kutaka kuishi humo, kufanya kazi au hata kuutembelea?
Kwa mujibu wa Global Cities Index 2026, jibu si uchumi imara au majengo mazuri pekee. Mambo kama utamaduni, teknolojia, mazingira, elimu na ubora wa maisha pia yana nafasi kubwa.
Oxford Economics World Cities Index 2026 imeorodhesha miji 1,000 duniani kwa kuzingatia mambo matano: utawala, uchumi, rasilimali watu, mazingira na ubora wa maisha.
Mwaka huu, New York, London na Paris ndizo zilizoongoza, huku miji kama Seattle na Dublin pia zikiingia katika nafasi za juu.
1. Huvutia watu kutoka kila pembe ya dunia
Miji inayoongoza duniani mara nyingi huwa na kitu kimoja kwa pamoja: watu wengi wenye ujuzi, elimu na mitazamo tofauti.
Hiki ndicho kinachopimwa kupitia kipengele cha rasilimali watu. Watu kutoka maeneo mbalimbali wanapokuja mjini, huleta pamoja mawazo, ujuzi na tamaduni ambazo zinaweza kubadilisha kila kitu kuanzia biashara na chakula hadi sanaa na maisha ya kila siku.
Chukua mfano wa Boston, iliyoshika nafasi ya saba. Jiji hilo lina vyuo vikuu na taasisi nyingi maarufu za elimu ya juu, jambo ambalo limeifanya kuwa kitovu cha maarifa na vipaji.
Uchumi wa Boston unaotegemea maarifa umeifanya kuwa miongoni mwa miji yenye viwango vya juu zaidi vya kipato duniani.
Uchumi wake unaotegemea maarifa pia umechangia kuwa na viwango vya juu vya kipato.
Sehemu ya utajiri huo imeelekezwa katika kuboresha maeneo ya umma. Mfano mzuri ni Rose Kennedy Greenway, eneo ambalo hapo zamani lilikuwa barabara kuu iliyoinuka lakini sasa limegeuzwa kuwa eneo lenye bustani, chemchemi na sanaa za umma.
Na kama unapenda sanaa, taasisi kama Harvard Art Museums pia ziko wazi kwa umma.

Chanzo cha picha, Getty Images
Dublin nayo ina hadithi inayofanana. Jiji hilo lina nguvu kazi yenye ujuzi mkubwa, ikisaidiwa na taasisi kama Trinity College Dublin. Hali hii imevutia kampuni kubwa za kimataifa kama Google, Meta, Microsoft na Accenture.
Uwepo wa kampuni hizo haujabadilisha tu uchumi wa Dublin. Pia umesaidia kufufua maeneo ya zamani ya ufukweni na maeneo ya umma kandokando ya Mto Liffey.
Halafu kuna London.
London inashika nafasi ya kwanza katika kipimo cha rasilimali watu na huvutia watu kutoka karibu kila sehemu ya dunia. Karibu asilimia 40 ya wakazi wake wamezaliwa nje ya Uingereza.
Utofauti huo unaonekana wazi katika maisha ya jiji hasa kwenye chakula. Ukiwa London, ni rahisi kupata vyakula na ladha kutoka pembe nyingi za dunia.
2. Huwekeza katika utamaduni
Uchumi mzuri ni muhimu, lakini hauwezi kufanya mji uwe wa kuvutia peke yake.
Paris ni mfano mzuri. Ilishika nafasi ya tatu kwa jumla, lakini imefanya vizuri sana katika kipengele cha ubora wa maisha.
Sababu mojawapo ni upatikanaji mkubwa wa utamaduni. Paris ina takribani makumbusho 130. Tangu mwaka 2001, makumbusho 11 yanayomilikiwa na manispaa yamekuwa yakitoa kiingilio cha bure katika maonyesho yao ya kudumu, bila kujali uraia au nchi anayotoka mgeni.
Na si hayo tu. Makumbusho mengine mengi pia hutoa kiingilio cha bure angalau mara moja kwa mwezi.

Chanzo cha picha, Getty Images
Seattle nayo ina upande wake wa kitamaduni. Jiji hilo limejijengea sifa kupitia sanaa na muziki. Seattle Art Museum ni mojawapo ya taasisi zake maarufu, huku historia yake ya muziki wa grunge ikiwa imezaa bendi zinazojulikana duniani kama Nirvana na Pearl Jam.
Hivi karibuni, jiji hilo lilikamilisha ujenzi wa bustani yake ya ufukweni. Mradi huo umebadilisha barabara kuu iliyokuwa imechakaa na kuweka njia ya watembea kwa miguu inayojumuisha gati mpya za umma na njia za baiskeli.
3. Maisha ya mjini yaliyo safi na rahisi zaidi

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mji unaweza kuwa wa kusisimua na wenye utajiri mkubwa wa kitamaduni, lakini hewa chafu au usafiri usio rahisi unaweza kuharibu haraka uzoefu wa mgeni.
Licha ya ukubwa wake mkubwa, London imefanya vizuri sana katika vipimo vya mazingira kwa kuzingatia ukubwa wa jiji hilo. Oxford Economics inaelekeza kwenye sera kama tozo ya msongamano wa magari (Congestion Charge) na Eneo la Uzalishaji Mdogo wa Uchafuzi (Low Emission Zone) kama baadhi ya hatua zilizosaidia kupunguza msongamano wa magari na uchafuzi wa mazingira.
Mabadiliko hayo yanaonekana hasa katika mitaa ya katikati ya jiji, ambako magari hayatawali tena mazingira kama ilivyokuwa hapo awali.
San Francisco pia imepata alama za juu katika kipengele cha mazingira. Faharasa hiyo inataja mtandao wa usafiri wa jiji kama mojawapo ya sababu zinazowafanya wakazi na wageni kutokuwa na utegemezi mkubwa wa magari. Hali hiyo husaidia kuweka uzalishaji wa hewa chafu katika viwango vya chini na kudumisha ubora wa hewa.
Dublin pia imefanya vizuri, kutokana na viwango vyake vya chini vya uchafuzi wa mazingira na mipango yake kabambe ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, ikiwemo lengo la kufikia kutokuwa na uzalishaji wa hewa ukaa ifikapo mwaka 2030.
4. Haziogopi mabadiliko, zinaongoza
Teknolojia inachochea ukuaji wa baadhi ya miji inayopanda kwa kasi katika faharasa hiyo.
San Jose, iliyoshika nafasi ya nane kwa jumla, ina Pato la Taifa kwa kila mwananchi la juu zaidi katika faharasa hiyo. Hii inahusishwa kwa kiasi kikubwa na uwepo wa kampuni za teknolojia za Silicon Valley, kama Alphabet - kampuni mama ya Google - Apple na Nvidia.
Katika San Francisco iliyo karibu, ambako kuna makao ya kampuni kama Meta, Uber na Salesforce, magari yasiyo na dereva sasa yameanza kuwa sehemu ya usafiri wa kila siku. Hali hiyo inawapa wasafiri na wakazi taswira ya jinsi usafiri wa mijini unavyoweza kuwa katika maeneo mengine duniani siku zijazo.
Tallinn, mji mkuu wa Estonia, pia iliingizwa katika orodha ya "miji inayojitokeza" kutokana na ukuaji wake wa haraka katika sekta ya teknolojia na kiwango chake cha juu cha matumizi ya akili bandia ikilinganishwa na miji mikuu mingine ya Ulaya.
Miradi ya kisasa kama Rail Baltica, ambayo inatarajiwa kuunganisha nchi za Baltic ifikapo mwaka 2030, inabuniwa na kujengwa kwa kuzingatia kikamilifu dhana ya "digital-first", yaani kuweka teknolojia za kidijitali mbele tangu hatua za awali za ujenzi na uendeshaji.
Mfumo huo utawezesha reli nzima kutumia nishati inayoweza kurejeshwa, pamoja na mifumo ya mawasiliano ya simu ya 5G, badala ya kutegemea taa za kawaida za ishara za reli.
Kwa ujumla, miji inayoongoza duniani mwaka 2026 haitegemei kipengele kimoja pekee. Uchumi imara, watu wenye ujuzi, utamaduni unaochangamka, mazingira bora, teknolojia na ubora wa maisha vinaungana kuifanya miji hiyo kuwa maeneo yenye mvuto kwa wakazi na wasafiri kutoka sehemu mbalimbali za dunia.
Miji 10 Bora Duniani mwaka 2026
Kwa mujibu wa Global Cities Index 2026:
New York, Marekani
London, Uingereza
Paris, Ufaransa
Seattle, Marekani
San Francisco, Marekani
Dublin, Ireland
Boston, Marekani
San Jose, Marekani
Tokyo, Japan
Zurich, Uswisi
Imetafsiriwa na Mariam Mjahid na kuhaririwa na Ambia Hirsi































