Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Kauli tata za wanasiasa wanaohama vyama Tanzania
Mabadiliko ya uhamaji wa kisiasa nchini Tanzania yameendelea kuwa chanzo cha mijadala mikali ya kitaifa, hasa pale wanasiasa wanapohama kutoka chama kimoja kwenda kingine na baadaye kurejea tena walikotoka. Matukio ya hivi karibuni ya Joseph Selasini, Peter Msigwa na Patrick Assenga yameibua upya mjadala kuhusu kauli zao walizowahi kuzitoa wakiwa ndani ya vyama walivyovihama na baadaye kurejea.
Msigwa, ambaye alikuwa CHADEMA na baadaye kuhamia CCM kabla ya kurejea tena CHADEMA wiki hii, Selasini aliyewahi kuondoka CHADEMA kwenda NCCR-Mageuzi na sasa kutangaza kurejea CHADEMA, pamoja na Assenga aliyepitia CHAUMA kabla ya kurudi CHADEMA, wote wamechangia kuibua maswali kuhusu uthabiti wa misimamo ya kisiasa na kauli zao za zamani.
Ingawa kisheria kuhama chama ni haki ya kikatiba ya kila mwanasiasa, mjadala mkubwa hubaki kwenye maneno waliokuwa wakiyasema wakati wakiwa kwenye vyama wanavyovihama, maneno ambayo mara nyingi huonekana kugongana na hatua zao za baadaye.
Wapo pia wanasiasa wengine waliopitia njia hiyo hiyo, akiwemo Waziri Mkuu mstaafu Edward Lowassa, ambaye alihama CCM kwenda CHADEMA na baadaye kurejea CCM, Wilbroad Slaa, Katibu Mkuu wa zamani wa CHADEMA aliyeenda CCM kabla ya kuwatosa tena, hali inayoongeza uzito wa mjadala huu wa kisiasa wa "kauli dhidi ya matendo."
Kwa ujumla, uhamaji wa vyama umekuwa sehemu ya siasa za Tanzania, lakini kinachobaki akilini mwa wananchi ni kauli tata za viongozi hao, kauli ambazo mara nyingi hubadilika kulingana na mazingira ya kisiasa wanayokutana nayo.
Peter Msigwa - "Siwezi kuuza utu wangu kwa vipande 30 vya fedha au cheo"
Peter Msigwa, mbunge wa zamani wa Iringa Mjini na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ni miongoni mwa wanasiasa waliowahi kutoa kauli zinazoleta utata. Wakati akiwa CHADEMA aliyekaa kwa muda mrefu alipoulizwa na chombo kimoja cha habari kama atahamia CCM alisema:
"Siwezi kuuza utu wangu kwa vipande 30 vya fedha au cheo… CCM siendi, bora nisiwe Mbunge."
Kauli hiyo aliitoa Disemba 30, 2023 akiwa kiongozi wa CHADEMA. Hata hivyo, baadaye mwaka 2024 alihamia CCM, kabla ya kurejea CHADEMA wiki hii.
Akiwa CHADEMA, Msigwa pia alikuwa akiikosoa sana CCM kuhusu demokrasia na katiba, pamoja na masuala kama utekaji na usalama kwa ujumla, lakini baadaye akiwa CCM alibadilisha msimamo na kusema wananchi wako salama chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.
Akitangaza kurejea CHADEMA alihusisha pia matukio ya usalama akisema:
"Matukio hayo yaliniumiza na kunifanya nishindwe kuendelea kuishi katika huzuni kubwa na ukimya."
Septemba 7, 2024, alipokuwa akifanya mahojiano na Kipindi cha Medani za Siasa cha Star TV, alisema “nuru imeniangazia, nilipokuwa Chadema nilikuwa sina ufahamu, nimegundua kuwa napigania vitu ambavyo havipo, nadaganywa.”
Kauli hizi zimezua mjadala mkali kuhusu mabadiliko ya msimamo wake wa kisiasa. Na sasa anasema "mimi sio mti, CHADEMA ikipoteza misingi nitaondoka tena".
Joseph Selasini - "CHADEMA sio chama cha siasa"
Joseph Selasini, aliyekuwa Mbunge wa Rombo kupitia CHADEMA, naye amepitia safari ndefu ya kisiasa yenye mabadiliko ya vyama. Mwaka 2008 Alitoka NCCR - Mageuzi akajiunga CHADEMA. Mwaka 2020, alihamia NCCR-Mageuzi akikanusha madai ya kuhamia CCM, huku akitaja changamoto za ndani ya CHADEMA kama moja ya sababu za kuondoka kwake, ikiwa ni pamoja na kuondolewa kwenye majukwaa ya mawasiliano ya chama.
Selasini alisema, pamoja na mambo mengine kuondolewa kwenye jukwaa la WhatsApp la wabunge wa CHADEMA lilimpa tafsiri ya kwamba hatakiwi CHADEMA.
"Akufukuzae hakwambii toka, utaona tu kama amekaa anafagia anaelekeza vumbi upande wako", Alisema selasini akisisitiza kwamba kundi hilo la Whatsapp lilikuwa kundi la kazi, na kiungo muhimu cha taarifa.
Akizungumza mbele ya waandishi wa habari April 2020 akiendelea kutangaza kuhamia NCCR Mageuzi alisema ukitaka kupendwa kwa sasa ndani ya CHADEMA (wakati huo), lazima uwe tayari kuimba wimbo wa kumsifia Freeman Mbowe, Mwneyekiti wa wakati huo, na kwamba bila yeye hakuna chama.
"Kwa msingi huo hiki sio chama cha siasa", akionyesha katika miaka 12 ya uanachama wake wakati huo alikua akitengwa.
Hata hivyo, kabla ya hapo, Kamati Kuu ya CHADEMA ilikuwa tayari imewafukuza baadhi ya wabunge wakiwemo Selasini kutokana na tuhuma za kukiuka taratibu za chama.
Ingawa hakuwa mkosoaji sana wa vyama vya upinzani vingine, hakuonekana kukubaliana na chama chake CHADEMA na kukitupia lawama kadhaa, lakini wiki hii ametangaza kurejea CHADEMA, hatua inayoendelea kuzua maswali kuhusu misimamo ya viongozi wa siasa za upinzani.
La pili kauli zao juu ya vyama wanavyovihama na baadaye kukanyaga matapishi yao.
Stephen Wasira - "Sikwenda upinzani kwa sababu ya kupingana na sera za CCM"
Stephen Wasira ni miongoni mwa wanasiasa wa muda mrefu wenye historia ya kuhama na kurejea CCM. Ndiye Makamu Mwenyekiti wa CCM kwa sasa, akiwa sehemu ya siasa za Tanzania toka enzi za Mwalimu akihudumu kwa nafasi mbalimbali ndani ya chama na serikali.
Baada ya kushindwa katika kura za maoni ndani ya CCM mwaka 1995, akiangushwa na Jaji Joseph Warioba alihamia NCCR-Mageuzi ambako alifanikiwa kuchaguliwa kuwa Mbunge.
Wengi hukubaliana kwamba, mwanasiasa akihamia chama fulani, ni kwa sababu ya kukubaliana na sera na muelekeo wa chama hicho na si chama alichotoka, kama angekuwa anakubaliana na chama chake alichotoka maana yake asingetoka.
Lakini Wassira anaeleza kupitia Mwananchi, "nataka mwelewe kwamba mimi sikwenda upinzani (NCCR-Mageuzi) kwa sababu nilikuwa napingana na sera za CCM. Kwanza 1985 nilikuwa mbunge na ndiyo maana Rais Ali Hassan Mwinyi aliniteua kuwa waziri wa kilimo".
Hata hivyo, baadaye uchaguzi wake ulitenguliwa na Mahakama Kuu kutokana na tuhuma za kasoro za uchaguzi. Uchaguzi mdogo ulipo fanyika mwaka 1999 Wasira hakushiriki kabla ya kurejea CCM na mwaka 2005 alipita bila kupingwa katika jimbo la Bunda.
Kwa ufupi Wasira anasena hakuwa upinzani kwa sababu ya kupinga sera za CCM bali kulisababishwa na michakato ya kura za maoni.
Esther Bulaya - "Nakwambia mara tano, haiwezi kutokea" (kuhama chama)
Esther Bulaya ni miongoni mwa wanawake waliowahi kuibua ushawishi mkubwa ndani ya upinzani baada ya kuondoka CCM.
Baada ya kuhudumu kama mbunge wa viti maalum kupitia CCM, alihamia CHADEMA na kushinda ubunge wa Bunda Mjini dhidi ya Stephen Wasira, hatua iliyomfanya kujijengea jina kubwa kisiasa.
Hata hivyo, baada ya uchaguzi Mkuu wa 2020, alikumbwa na mgogoro wa kisiasa ndani ya CHADEMA, akiwa miongoni mwa wanachama 19 wanawake akiwemo Halima Mdee, kwenda kuapishwa bungeni kama wabunge wa viti maalumu, kinyume na msimamo wa chama, hali iliyosababisha kufukuzwa kwao.
Baada ya kufukuzwa, yeye na wenzake walipinga Mahakamani, na waligoma kuondoka kwenye chama.
Bulaya alisema": "Hakuna chama kingine, Esther Bulaya anasema ni CHADEMA damu na hana pakwenda. Haiwezi kuwa tofauti",.
Alipoulizwa na mmoja wa waandishi kama ataendelea kuwa Chadema mpaka Uchaguzi wa 2025, Bulaya alisisitiza: "Nakwambia mara tano, haiwezi kutokea,.. haiwezi kutokea.... haiwezi kutokea.....haiwezi kutokea......haiwezi kutokea, chadema damu chama la wana".
Lakini muda mfupi kabla ya uchaguzi mkuu wa 2025, akarudi CCM na akachukua fomu ya kugombea ubunge Bunda Mjini. Matokeo ya Kura za maoni CCM Jimbo hilo, Bulaya alishika nafasi ya tatu kwa kura 625, nyuma ya Robert Chacha Maboto- kura 2545 aliyeongoza na Kambarage Masato Wasira - kura 2032, aliyekuwa wa pili. Chama hicho kilimpitisha na kushinda ubunge anaoutumikia mpaka sasa.
Baada ya kurudi CCM, Bulaya akakifananisha chama hicho na Klabu ya mpira wa miguu ya Barcelona nchini Hispani na Chadema akaifananisha na Klabu ya Leicester City ya England. Bulaya akasema: "Chama Cha Mapinduzi kimerudisha usajili wa wachezaji wake wa Barcelona ambao waliwatuma kwa mkopo kwenye timu ya Leicester City ambayo imeshuka daraja", kauli hii imeendelea kuibua mjadala.
Frederick Sumaye - "Kwangu mimi suala la kurudi CCM hapana!
Frederick Sumaye, Waziri Mkuu mstaafu, naye ameingia kwenye siasa za kuhama na kurejea vyama.
Mapema mwaka 2012, Waziri mkuu huyu mstaafu na kada wa CCM wa muda mrefu, alikuwa akinyooshewa kidole kuteta na CHADEMA kuhusu mustakabali wake kisiasa, hasa baada ya kushindwa kwenye nafasi ya ujumbe wa NEC katika uchaguzi wa Hanang, ambapo Marry Nagu aliibuka mshindi.
Wengi walisema anahamia CHADEMA, lakini Sumaye alijitokeza akasema,
"Napenda kueleza wazi kwamba, sina nia wala ndoto ya kuhama CCM kwenda Chama chochote, mimi sipo CCM kwa sababu ya cheo".
Lakini kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, Sumaye alitangaza kujiondoa CCM na kujiunga na CHADEMA, akionyesha kutofurahishwa na michakato ya ndani ya demokrasia ya chama hicho.
Akiwa CHADEMA ukavuka uvumi kwamba huenda anarejea CCM, baada ya uwepo wa kundi la wanasiasa wa upinzani waliokuwa wanaunga juhudi chama (CCM) kwa kuachama na upinzani na kujiunga na CCM, Sumaye akasema:
"Kwangu mimi suala la kurudi CCM hapana! tunachojenga ni demokrasia, sina chuki na CCM, sina chuki Rais John Magufuli, Rais Mstaafu Jakaya Kikwete, Rais Mstaafu Benjamin Mkapa wala uongozi."
Hata hivyo, kabla ya uchaguzi Mkuu wa 2020, alitangaza kuachana na CHADEMA huku akidai alikosea kudhani kuna demokrasia ndani ya chama hicho na kukituhumu kuminya demokrasia na kumfedhehesha katika mchakato wa uchaguzi wa ndani.
Sumaye alikuwa akitetea kiti chake cha mwenyekiti wa Kanda ya Pwani na kuangukia pua. Katika uchaguzi huo uliofanyika Novemba 28, 2019 Sumaye alipata kura za Ndiyo 28 tu na Hapana 48.
Februari, 2020 akatangaza kurudi Chama cha Mapinduzi (CCM) kile kile alichokilalamikia awali kwamba michakato ya demokrasia ndani haikua sawa.
Sumaye amewahi kusisitiza kuwa alihamia upinzani ili kuleta changamoto ya kisiasa, si kwa chuki dhidi ya CCM au viongozi wake.