Kuanzia Makonda hadi Mafwele, hawa ni 'vigogo' 5 Afrika Mashariki waliopigwa marufuku kuingia Marekani

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 5

Marekani imekuwa ikitumia vikwazo vya visa kama moja ya njia zake muhimu za kidiplomasia, hasa dhidi ya maafisa wa serikali na viongozi wanaotuhumiwa kwa ukiukwaji wa haki za binadamu, rushwa au kudhoofisha misingi ya demokrasia.

Hatua hizi mara nyingi hutangazwa moja kwa moja na Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani na hujumuisha marufuku ya kuingia nchini humo kwa wahusika pamoja na familia zao.

Vikwazo hivi hutokana na sera inayojulikana kama Section 7031(c), ambayo hutumiwa dhidi ya maafisa wa kigeni wanaohusishwa na rushwa kubwa au ukiukwaji wa haki za binadamu.

Nchi za Afrika Mashariki, vikwazo hivi vimewahi kugusa majina makubwa ya kisiasa na kiusalama, kutoka Tanzania, Kenya, hadi Rwanda na Uganda. Wakati mwingine hatua hizi huwa za moja kwa moja na za hadharani, na wakati mwingine huwekwa kama vizuizi vya kidiplomasia visivyo na orodha ndefu ya majina.

Miongoni mwa matukio ya hivi karibuni kabisa ni hatua dhidi ya afisa wa Jeshi la Polisi Tanzania, Faustine Jackson Mafwele, ambaye ametajwa na Marekani kama mmoja wa maafisa wanaozuiwa kuingia nchini humo kutokana na madai ya ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu. Tangazo hilo limeweka jina lake kwenye orodha mpya ya watu wa Afrika Mashariki walioguswa moja kwa moja na smarufuku hiyo ya Marekani.

1. Faustine Jackson Mafwele - Tanzania

Faustine Mafwele ni afisa wa Jeshi la Polisi Tanzania ambaye ametajwa na Marekani mwezi Mei, 2026 kuwekwa kikwazo cha kuingia nchini humo kwa madai ya ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu. Kwa mujibu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, hatua hiyo inamzuia yeye pamoja na familia yake ya karibu kuingia Marekani.

Marekani inamuhusisha Mafwele na kukamatwa kwa wanaharakani wa Kenya walioingia nchini Tanzania mwaka jana.

"Mwaka jana, jeshi la polisi liliwakamata, kuwatesa na kuwafanyia ukatili wa kingono raia wa Uganda Agather Atuhaire na raia wa Kenya Boniface Mwangi, waliokuwa jijini Dar es Salaam kufuatilia kesi mahakamani dhidi ya kiongozi wa upinzani Tundu Lissu," imeeleza sehemu ya taarifa ya Wizara hiyo ya Marekani ilisema.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania Mahmoud Thabit Kombo aliiambia BBC kwamba serikali bado haijapokea rasmi taarifa ya hatua hiyo, ambayo inamzuia Mafwele kuingia nchini Marekani.

2. Paul Makonda - Tanzania

Paul Makonda, Waziri wa Habari, Utamaduni,Sanaa na Michezo alipigwa marufuku kuingia Marekani mwaka 2020 wakati huo akiwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.

Marufuku hiyo ilimgusa pia mkewe Mary Felix Masenge.

"Kwa nafasi hiyo, (Makonda) anahusishwa na ukandamizaji wa siasa za upinzani, ukandamizaji wa haki za kujieleza na kukusanyika na kulenga makundi ya wachache", ilisema taarifa ya Wizara ya mambo za Nje ya Marekani, wakati huo ikiwa chini ya Waziri Michael Pompeo

Hadi sasa, hakuna taarifa rasmi za kuondolewa kwa vikwazo hivyo, iliyotolewa rasmi na Serikali ya Tanzania ama Makonda mwenyewe.

3. Mike Sonko - Kenya

Mike Sonko, aliyewahi kuwa Gavana wa Nairobi, aliwahi kupigwa marufuku kuingia Marekani mwaka 2022. Marekani ilimtaja kutokana na tuhuma za rushwa kubwa akiwa katika nafasi ya uongozi wa mji huo mkuu na wakibiashara wa Kenya.

Hatua hiyo ilimzuia yeye pamoja na familia yake ya karibu kupata visa ya kuingia Marekani, jambo aliloonyesha kutofurahishwa nalo, wakati huo akihudhuria kesi iliyofunguliwa kutokana na tuhuma hizo.

"Nimeshangazwa. Mke wangu na watoto wangu hawajawahi kuomba kandarasi yoyote nikiwa Gavana wa Nairobi. Tuna magavana wengine wanakabiliwa na mashitaka pamoja na watoto wao. Wa kwangu hawajashitakiwa", alisema Sonko akifafanua kuhusu vikwazo hivyo, akiinyoshea kidole zaidi Serikali.

Hata hivyo, Mahakama ya Nairobi ilimuachia huru, katika kesi ya utakatishaji fedha, baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuwasilisha ushahidi wa kutosha kuthibitisha tuhuma za utakatishaji fedha dhidi ya Sonko, jambo lililosababisha kuondolewa kwa shtaka hilo.

Hata hivyo, Mahakama iliamua kuwa pamoja na kuondoa shitaka hilo, bado Sonko ana kesi ya kujibu katika mashtaka mengine yanayohusiana na utoaji wa zabuni usiofuata utaratibu wakati wa uongozi wake.

Sonko amedai kwambaa marufuku ya kuingia Marekani iliondolewa na baadaye akaushukuru hadharani utawala wa Marekani kwenye akaunti yake rasmi ya X (zamani ya Twitter).

4. Kale Kayihura - Uganda

Kale Kayihura, aliyewahi kuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi la Uganda, amewahi kukumbwa na vikwazo vya Marekani kutokana na madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu akiwa madarakani. ar

Marekani ilimtaja kama mmoja wa maafisa waliotumia mamlaka ya usalama kwa njia iliyozua wasiwasi kuhusu uhuru wa raia na wanasiasa wa upinzani.

Wakati wa uongozi wake, Uganda ilikumbwa na malalamiko ya ukandamizaji wa kisiasa, na hatua za Marekani zilionekana kama sehemu ya shinikizo la kimataifa la uwajibikaji.

Ingawa baadaye alikabiliwa pia na changamoto za kisheria ndani ya Uganda, vikwazo vya Marekani viliendelea kubaki kama sehemu ya rekodi yake ya kimataifa.

5. James Kabarebe - Rwanda

James Kabarebe, Jenerali wa zamani na waziri wa ulinzi wa Rwanda, amewahi kuhusishwa na vikwazo vya Marekani vinavyohusiana na migogoro ya Mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Marekani imemhusisha katika muktadha wa mvutano wa kikanda unaohusisha masuala ya kijeshi na vikundi vya waasi katika eneo hilo.

Ikimtaja kama mmoja wa watu wanaohusika moja kwa moja na mgogoro huo.

Kabarebe ni miongoni mwa maafisa wa kijeshi wa Rwanda waliotajwa mara kwa mara katika mijadala ya kidiplomasia kati ya Marekani a nchi za Maziwa Makuu. Hata hivyo, nafasi yake ndani ya serikali imekuwa ikibadilika kwa muda, na suala la vikwazo vyake limekuwa sehemu ya mvutano wa muda mrefu wa kikanda.

Ukiacha Kabarebe, Makonda, Sonko, Mafwele na Kayihura, wapo viongozi wengi waliozuiwa na wengine kupigwa marufuku kuingia Marekani kwa sababu zinazotofautiana, lakini hawa waliotajwa waligusa mijadala mipana katika nchi zao na nchi jirani.