Hospitali ya muda inayojengwa na jeshi la Marekani katikati mwa Kenya kwa ajili ya kuwahifadhi Wamarekani waliokumbana na virusi vya Ebola itaanza kufanya kazi Ijumaa ikiwa na uwezo wa kuhudumia wagonjwa 50, maafisa wa serikali ya Marekani walisema Alhamisi huku wakitetea uamuzi wa kutowarejesha Marekani raia wanaoambukizwa Ebola kwa matibabu.
Kituo hicho kinachojengwa katika Kambi ya Jeshi la Anga ya Laikipia na kusimamiwa na jeshi la Marekani kitahudumiwa na maafisa wa Huduma ya Afya ya Umma ya Marekani. Lengo lake ni kuwaweka karantini raia wa Marekani wanaoshukiwa kukumbana na virusi hivyo wakati wa mlipuko mkubwa wa Ebola unaoendelea katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Mamlaka zinasema visa vinavyoshukiwa vya Ebola sasa vimevuka 1,000 huku takriban watu 250 wakihofiwa kufariki.
Hadi sasa hakuna Mmarekani aliyethibitishwa kupelekwa katika kituo hicho nchini Kenya, lakini ndege zimewekwa tayari kuwahamisha raia waliokumbana na virusi hivyo “wakati wowote,” kwa mujibu wa afisa mmoja mwandamizi wa serikali aliyekuwa akizungumza na wanahabari kwa masharti ya kutotajwa jina.
Maafisa hao walisema awamu ya kwanza ya kituo hicho ambayo ni sehemu ya karantini yenye vitanda 50 itakuwa tayari kuanza kazi Ijumaa, ingawa hawakufafanua iwapo kitakuwa tayari kupokea wagonjwa mara moja. Kituo hicho pia kinatarajiwa kupanuliwa baadaye na kuwa na uwezo wa vitanda 250.
Awamu ya pili inayotarajiwa kuanza wiki ijayo itaongeza vyumba maalumu vya kutenga wagonjwa na mifumo ya kudhibiti maambukizi, vitakavyosafirishwa kutoka Marekani kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa watakaoonyesha dalili au kuthibitishwa kuwa na Ebola.
Operesheni hiyo nchini Kenya inahusisha zaidi ya maafisa 30 wa huduma ya afya ya umma waliopatiwa mafunzo ya siku tatu katika Kituo cha Kijeshi cha Joint Base Andrews, Maryland, kuhusu huduma za Ebola, taratibu za karantini na matumizi ya vifaa vya kujikinga kabla ya kuondoka kuelekea Kenya Jumatano usiku.
Baadhi yao waliwahi kuhudumia wagonjwa wa Ebola wakati wa mlipuko wa mwaka 2014 hadi 2015 nchini Liberia.
Kundi jingine la maafisa linatarajiwa kupata mafunzo mwishoni mwa wiki hii kabla ya kupelekwa Kenya wiki ijayo.
Afisa huyo alisema kituo hicho kitakuwa na vyumba vitatu vya kutenga wagonjwa vyenye uwezo wa kuhifadhi wagonjwa wanne kila kimoja pamoja na vyumba viwili vya juu vya kudhibiti maambukizi vyenye uwezo wa kuhifadhi wagonjwa wawili kila kimoja.
Hospitali hiyo ya muda ipo Laikipia, takriban kilomita 190 kaskazini mwa Nairobi. Eneo hilo lina kambi ya jeshi la anga na makazi ya wanajeshi yanayoweza kutumika kuwahifadhi wahudumu. Pia eneo hilo lina kituo cha mafunzo cha Jeshi la Uingereza nchini Kenya, ambacho ni miongoni mwa vituo vikubwa zaidi vya kijeshi vya Uingereza barani Afrika.
Shirika la Madaktari wa Magonjwa ya Kuambukiza la Marekani limesema kituo hicho kipya nchini Kenya kinaibua maswali makubwa kuhusu rasilimali, muda wa maandalizi na ubora wa huduma watakazopata Wamarekani watakaopelekwa huko.
“Katika kipindi ambacho mlipuko huu bado ni changamoto kuudhibiti, maamuzi yanapaswa kuongozwa na sayansi, uwazi na kile kilicho bora kwa wagonjwa pamoja na afya ya umma,” shirika hilo lilisema katika taarifa.
Shirika hilo liliongeza kuwa Wamarekani wanaokumbana na ugonjwa hatari wanastahili kuwa na uhakika kwamba maamuzi kuhusu matibabu yao yanafanywa kwa kuzingatia ushahidi wa kisayansi, maandalizi ya kutosha na usalama wa wagonjwa wakati wa mlipuko unaoendelea.
Kwa sasa hakuna chanjo wala tiba iliyoidhinishwa rasmi kwa aina hii ya virusi vya Ebola inayojulikana kama Bundibugyo.
Madaktari bingwa wa magonjwa ya kuambukiza waliowahi kuhudumia wagonjwa wa Ebola wanasema tiba kuu ni kubaini maambukizi mapema, kutenga wagonjwa kwa ufanisi na kutoa huduma za hali ya juu za kusaidia mwili. Wanasema maambukizi yanaweza kusababisha viungo vya mwili kushindwa kufanya kazi ndani ya siku chache.
Iwapo wagonjwa wataugua kabla ya kuhamishwa, maafisa walisema kituo cha Kenya kitakuwa na uwezo wa kutoa dawa za kingamwili pamoja na dawa ya kuzuia virusi aina ya remdesivir, ambayo haijaidhinishwa rasmi kutibu Ebola lakini hutumiwa mara nyingi kwa matumizi maalumu. Wagonjwa pia watapatiwa maji mwilini na msaada wa kupumua ndani ya kituo hicho.