Uvumbuzi 9 wa kijeshi wa ajabu zaidi kuwahi kubuniwa duniani

Chanzo cha picha, Getty
Kuanzia bunduki za kutapika risasi hadi 'kuku wa nyuklia', hizi ni baadhi ya mawazo ya kijeshi ya kushangaza ambayo hayakuwahi kufanikiwa.
Tangu mara ya kwanza ambapo binadamu alimpiga adui yake kichwani kwa rungu la mbao, binadamu wamekuwa wakitafuta mbinu mpya na bunifu za kuwaangamiza maadui zao.
Kando na mifumo ya kisasa ya vita kama droni, historia nayo imejaa mifano ya kushangaza zilizokuwa bunifu, na wakati mwingine zisizo na mantiki kabisa. Hapa ni uvumbuzi tisa wa kijeshi wa ajabu zaidi kuwahi kubuniwa.
Mbwa wa vifaru

Chanzo cha picha, Getty
Mwaka wa1941, Umoja wa Kisovyeti ulikuwa unapitia hali ngumu. Wanajeshi wa Hitler wa Wehrmacht walikuwa wameivamia nchi hiyo, wakaharibu jeshi lake la anga lilikuwa ardhini na kuangamiza majeshi yote katika mashambulizi makubwa, yaliyongozwa na vikosi vya vifaru vya Ujerumani vilivyozoea vita, vilivyojulikana kama Panzer.
Wasovieti walihitaji njia ya kuzuia vifaru vya Wanazi haraka. Afisa mmoja akatoa pendekezo la kikatili na la kushangaza, kwa nini wasitumie mbwa?
Mbwa hukimbia kwa kasi na ni vigumu kulenga wakiwa wanakimbia kuelekea kwenye uwanja wa vita.
Wasovieti waliwafunga wanyama hao vilipuzi vyenye nguvu, kisha wakawafundisha kukimbia kuelekea kwenye vifaru vya Ujerumani aina ya Mark IV, wakitumai kwamba wangeweza kuangamiza makumi ya magari hayo mazito kwa wakati mmoja.
Lakini Jeshi la Kisovyeti lilipowaachilia mbwa hao waliokuwa wamehukumiwa kifo, mbwa hao wa kijeshi walikimbia moja kwa moja kuelekea kwenye vifaru vyao wenyewe na kuvilipua.
Tatizo lilikuwa nini? Umoja wa Kisovyeti ulikuwa umewafundisha mbwa hao kutambua vifaru vinavyotumia dizeli, ilhali vifaru vya Ujerumani vilitumia petroli. Isitoshe, kelele kubwa za milio ya risasi wakati wa mapigano ziliwatisha wanyama hao, na hivyo wakakimbia kwa hofu na kurudi kwa walezi wao.
Bila shaka, mpango huo ulisitishwa kimya kimya, na hivyo kuwaokoa mbwa wengine wengi kutokana na hatima hiyo ya kikatili.
Moto wa Kigiriki

Chanzo cha picha, getty
Leo, Wabyzantine wanachukuliwa na baadhi ya watu kuwa ustaarabu uliopuuzwa zaidi katika enzi za kati, au sura ya mwisho isiyoridhisha ya falme ya Roma.
Hata hivyo, bila kujali mtazamo wako, tunaweza kukubaliana kwamba ilikuwa jambo la kushangaza kuona milki hii iliyokuwa na msimamo mkali wa kidini ikiwamiminia maadui wake aina ya 'napalm' ya enzi za kati.
Ulikuwa ukijulikana kama 'Moto wa Kigiriki' (Greek Fire) au naphtha. Kichocheo hiki cha moto, ambacho vyanzo vinaeleza kuwa mara nyingi kilirushwa kutoka kwenye meli, kilifanikiwa kugeuza meli nyingi za maadui kuwa misitu inayowaka.
Kwa bahati mbaya kwa maadui wa Wabyzantine, siri ya silaha hii iliyokuwa kama napalm ya awali yalilindwa kwa usiri mkubwa. Kiasi kwamba, hadi leo, wanahistoria bado hawajui kwa hakika walivyofanikiwa kubuni silaha hiyo ya kipekee ya kivita katika kipindi hicho.
Kuku wa Nyuklia

Chanzo cha picha, Getty
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Miaka ya 1950 ilikuwa kipindi cha wasiwasi mkubwa kwa wapanga mikakati ya kijeshi wa NATO.
Wakiwa na jukumu la kuiandaa Ulaya Magharibi kukabiliana na uvamizi mkubwa wa Wakomunisti, maafisa hao walisisitiza matumizi ya silaha za nyuklia za nguvu kubwa ambazo zingetumika kuangamiza mamia ya maelfu ya wanajeshi wa miguu na vifaru.
Wakati huo, vichwa vya nyuklia vingeweza kurushwa kwa makombora au kudondoshwa na ndege za mabomu, lakini pia vingeweza kuzikwa ardhini kama mabomu ya ardhini.
Mwaka 1957, Wizara ya Ulinzi ya Uingereza iliagiza mabomu 10 ya aina hiyo, kwa ajili ya kutumiwa Ujerumani Magharibi.
Mabomu hayo yaliyopewa jina 'Blue Peacock', wapanga mikakati waligundua haraka tatizo, mifumo ya kielektroniki ya mabomu hayo ingepoa kwa haraka na kushindwa kufanya kazi baada ya mabomu hayo kuzikwa ardhini kwa siku kadhaa.
Afisa mmoja mbunifu wa Wizara ya Ulinzi ambaye, kwa bahati nzuri, jina lake limepotea katika historia alibuni suluhisho la kushangaza, kumweka kuku ndani ya bomu hilo. Kuku huyo angekuwa kama kikanza cha kutoa joto, na kusaidia kuweka nyaya na mifumo ya ndani katika hali ya joto kwa muda wa wiki moja, hadi Warusi wangetokea upande wa pili wa upeo na bomu hilo kulipuliwa.
Kwa bahati nzuri, wazo hilo lilibaki kuwa wazo tu. Ingawa silaha hizo ziliagizwa, mradi huo ulionekana kuwa wa kikatili na wa ajabu kiasi kwamba ulifutwa, na hivyo kuwaokoa kuku hao maskini.
'Bunduki ya kutapika' (Vomit Guns)

Chanzo cha picha, US Navy
Kuna njia mbalimbali za kumdhoofisha au kumzuia mtu bila kumuua. Mwaka wa 2007, kampuni ndogo ya kijeshi isiyojulikana sana iitwayo Invocon iliamua kwamba kuwafanya watu watapike pia inaweza kuwa njia inayofaa.
Silaha hiyo, iliyojulikana kwa jina lisilo rasmi la 'bunduki ya kutapika', ilipendekezwa kwa Jeshi la Wanamaji la Marekani. Ilitumia mawimbi ya redio yaliyoelekezwa kwa mtu mmoja au kundi la watu, ambayo yangeweza kuathiri sikio la ndani na kuvuruga mfumo wa mwili wa kudumisha usawa, hivyo kusababisha kichefuchefu.
Kampuni hiyo ilisema madhara yaliyofuata yangekuwa "ugonjwa mkali", yaani hali ya kizunguzungu na kichefuchefu inayoweza kusababisha mtu kutapika.
Inaonekana Jeshi la Marekani halikukubali pendekezo hilo la Invocon, lakini shauku ya kutumia silaha za nishati kuelekezwa iliendelea.
Silaha za sauti zinazotumia mawimbi ya sauti au ultrasound hutumiwa mara kwa mara kuwazuia watu, ingawa mara nyingi huwa kwa sababu nguvu ya mawimbi hayo huwa kubwa kiasi cha kuumiza masikio na hata kusababisha kiwambo cha masikio kupasuka.
Bomu la mashoga (Gay Bombs)
Katika mjadala huu kuhusu silaha hatari na za kushangaza, ni vyema kukumbushwa kwamba wengi wetu tunapendelea mapenzi badala ya vita. Kwa kipindi kifupi mwaka 1994, hilo lilionekana kana kwamba lilikuwa sera rasmi ya Jeshi la Anga la Marekani pia.
Mwaka huo, watafiti katika moja ya maabara zake huko Ohio walipewa jukumu la kutengeneza silaha ambayo ingetawanya angani kiwango kikubwa cha vichocheo vya kingono (pheromones) miongoni mwa wapiganaji wa upande wa adui, kwa lengo la kuwafanya waache kutumia bunduki zao na badala yake kuvutiwa kingono wao kwa wao.
Silaha hiyo, iliyojulikana kwa njia isiyo rasmi na kwa jina lisilo na ladha nzuri la 'bomu la mashoga', huenda isingewahi kufanya kazi. Ingawa aina mbalimbali za wanyama huvutiwa kingono na pheromones za wenzao, ushahidi kwamba jambo hilo hufanya kazi kwa binadamu bado haujawa wa kutosha.
Bomu la Popo

Chanzo cha picha, Getty
Lytle Adams alikuwa daktari wa meno katika mji mdogo wa Irwin, Pennsylvania. Usiku, alikuwa mvumbuzi mwenye shauku ya kubuni vifaa na teknolojia mbalimbali, ingawa si kila mara alifanikiwa.
Mwaka 1942, Adams alipata wazo jingine, badala ya ndege za mabomu kudondosha vilipuzi vya kuwasha moto katika miji ya maadui usiku, vipi kama wangetumia popo?
Mabomu madogo yenye uzito wa takriban gramu 28 yangefungwa kwa kamba ambayo popo wangeweza kuikata kwa meno yao. Kisha bomu hilo la kuchoma moto lingedondoka chini na kusababisha uharibifu, huku popo wakiruka na kujiepusha na hatari.
Daktari huyo wa meno aliwasilisha wazo hilo kwa Rais wa Marekani Franklin D. Roosevelt ambaye, kwa kushangaza, aliamuru Idara ya Huduma ya Vita vya Kemikali ya Jeshi la Marekani kutengeneza mfano wa silaha hiyo.
Mradi huo ulifika mbali zaidi kuliko mtu angeweza kutarajia. Mwaka 1943, majaribio ya mfano wa silaha hiyo yalianza. Idadi ndogo ya popo wa kawaida wenye mikia huru walikamatwa kutoka kwenye mapango huko Texas. Kisha wanyama hao wadogo walilazwa kwa kuwawekwa kwenye jokofu, kabla ya kufungwa ndani ya silinda ya fedha ambayo baadaye ingedondoshwa kutoka kwenye ndege aina ya B-25.
Kwa bahati mbaya kwa popo hao wasiokuwa na uwezo wa kujitetea, hawakuamka ndani ya silinda hiyo na badala yake wakaanguka hadi kufa.
Jaribio jingine safari hii likitumia popo walio hai na macho lilishindikana baada ya wanyama hao kuwasha moto kwa bahati mbaya katika jengo la Jeshi la Anga. Tukio hilo lilisababisha mradi huo kusitishwa kimya kimya.
Kulikuwa na takriban popo milioni 20 katika mapango ambako wanyama hao walikamatwa.
Great Panjandrum

Chanzo cha picha, IWM
Unawezaje kusafisha ufukwe uliojaa wanajeshi wa adui wanaokufyatulia risasi wakiwa kwenye ngome imara za kujihami?
Swali hilo lilijibiwa kwa kutumia mizinga ya manowari, mashambulizi ya mabomu katika maeneo mbalimbali na mawimbi ya wanajeshi wa Muungano waliovamia ufukwe wa Normandy.
Katika baadhi ya fukwe, wanajeshi wa Uingereza walisaidiwa na kile kilichoitwa 'Funnies' vifaru vya Sherman vilivyofanyiwa marekebisho ili viweze kutoka majini hadi kwenye mchanga, kuondoa mabomu ya ardhini na kuweka waya wenye miiba.
Hata hivyo, uvumbuzi mmoja haukuwahi kushiriki katika uvamizi huo: Great Panjandrum.
Kifaa hicho kilifanana na gurudumu kubwa la mkokoteni lililowekwa roketi ndogo na vilipuzi vyenye nguvu. Kililenga kuelekezwa kwenye ngome za adui na kusonga bila kusita kuelekea huko kabla ya kulipuka.
Hata hivyo, majaribio ya silaha hiyo kwenye fukwe za Uingereza yalikuwa maarufu kwa kushindwa.
Great Panjandrum haikuweza kusonga katika mstari ulionyooka mara nyingi jambo ambalo halikufaa kabisa katikati ya mapigano. Zaidi ya hayo, roketi zake mara kwa mara zilionekana kwenda upande wake, zikianguka au kuruka kutoka kwenye muundo huo kwa kasi ya kutisha.
Bila shaka, kifaa hicho hakikuwahi kutumika katika mapigano halisi.
Awali, wahandisi walijaribu kukiongoza Panjandrum kwa kutumia nyaya za chuma, lakini gurudumu hilo lilikuwa na nguvu sana na likazikata nyaya hizo.
Bunduki zenye shoka

Chanzo cha picha, The Met Museum
Fikiria hili: unaamka baada ya usingizi mzuri ndani ya meli ya kivita ya Uswidi ya karne ya 18, kisha unaulizwa kama unapendelea kuwa na shoka au bunduki wakati wa kuivamia meli ya maharamia wa Denmark inayokuja upande wako.
Jibu la swali hilo? Kwa nini usiwe na vyote viwili?
Bunduki zenye shoka zilikuwa silaha zinazofaa kwa mabaharia waliokuwa wakihitaji silaha inayoweza kutumika kwa njia mbalimbali wakati wa kuvamia meli za adui.
Kama ilivyokuwa kwa bunduki nyingi za karne ya 18, sehemu ya bunduki iliyotumia mfumo wa flintlock ingeweza kufyatua risasi moja tu kabla ya kuhitaji kujazwa tena.
Baada ya risasi hiyo kufyatuliwa, baharia angeweza kutumia shoka lake kwa uhuru aidha dhidi ya mabaharia wengine au kukata kamba na vifaa vilivyoshikilia milingoti ya meli ya adui.
Tangu bunduki zilipovumbuliwa, watu wamekuwa wakijaribu kuzifungamanisha na mashoka. Mfano huu maridadi ulikuwa mali ya Grand Duke Ferdinand I de' Medici karibu mwaka 1580.
Kanuni ya Upepo
Kuiangusha ndege ya adui ni shughuli inayogharimu fedha nyingi. kutengeneza makombora na mabomu kunahitaji rasilimali.
Kuelekea mwisho wa Vita vya Pili vya Dunia, wanasayansi wa Ujerumani ya Nazi walikuwa wakitafuta kwa haraka mawazo mapya. Walifikiri kwamba huenda ndege zingeweza kulazimishwa kuanguka kwa kutumia hewa iliyobanwa.
Kwa kurusha mlipuko mkubwa wa hewa iliyolenga ndege za mabomu zilizokuwa zikiruka chini, walidhani mashine hizo dhaifu za angani zingeweza kupoteza mwelekeo kwa matumaini kwamba nguvu hiyo ingezifanya zianguke katika uwanja wa karibu.
Timu ya wahandisi iliyokuwa ikisimamia mradi huo ilikabiliwa na changamoto nyingi za kiteknolojia, mojawapo ikiwa swali la jinsi ya kulenga silaha inayorusha 'risasi' zisizoonekana za hewa.
Hata hivyo, mwaka 1945 waliweza kutengeneza mfano wa silaha hiyo. Ilifanana na pipa kubwa lenye ncha iliyopinda, ambalo walidai lingeweza kuvunja mbao zenye unene wa sentimita 10 kutoka umbali wa takriban mita 180.
Silaha hiyo iliwekwa karibu na daraja kwenye Mto Elbe. Lakini Windkanone ilionekana kutokuwa na ufanisi kabisa, kwani ilishindwa kuvuruga hata ndege moja.
Imetafsiriwa na Beldeen Waliaula na kuhaririwa na Ambia Hirsi
































