Mama Fatma Karume: Mwanamke aliyeipika Zanzibar jikoni na kibarazani

Chanzo cha picha, DailyNews
Mama Fatma Karume, mjane wa Rais wa kwanza wa Zanzibar, Sheikh Abeid Amani Karume, amefariki dunia Jumatatu, Septemba 21, 2026, akiwa na umri wa miaka 97.
Taarifa ya kifo chake imetolewa na Makamu wa Rais wa Tanzania, Deogratius Ndejembi.
Katika salamu zake za rambirambi, Rais Samia Suluhu Hassan amesema Mama Fatma alikuwa sehemu muhimu ya historia ya Zanzibar, hususan katika harakati za kupigania uhuru, Mapinduzi ya Zanzibar na kuasisiwa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Amesema Taifa litaendelea kukumbuka na kuenzi mchango wake katika kuhifadhi kumbukumbu na urithi wa Taifa, pamoja na kuchochea maendeleo ya kisiasa, kiuchumi na kijamii.
Lakini Mama Fatma alikuwa mtu wa aina gani hasa? Zaidi ya kuwa mke wa Karume na 'First Lady' wa kwanza wa Zanzibar, na mama wa Rais wa 6 wa Zanzibar, Amani Abeid Karume
Harakati za Mapinduzi
Mama Fatma, ambaye jina lake kamili ni Fatma Gullam Hussein Jamal, alizaliwa Bumbwini, Kaskazini Unguja. Aliolewa na Abeid Amani Karume akiwa na umri wa miaka 15.
Lakini kabla ya kuwa mke wa rais 'First Lady', tayari alikuwa ameingia katika harakati za wanawake.
Katika mahojiano na Daily News yaliyochapishwa Oktoba 30, 2023, Mama Fatma alisema alijiunga na kundi la wanawake lililoshiriki katika harakati za kudai uhuru, akiwa karani wa kundi hilo na binti mdogo.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Miongoni mwa kampeni alizozikumbuka ni ile ya wanawake kudai haki ya kupiga kura. Kabla ya uchaguzi wa mwaka 1957, wanawake Zanzibar walikuwa wakizuiwa kupiga kura. Baada ya uchaguzi huo, ujumbe kutoka Lancaster House, London, (wakoloni waingereza waliokuwa wakitawala) ulifika Zanzibar. Mama Fatma alisema wanawake walitumia fursa hiyo kuwasilisha madai yao ya kutaka kupewa haki ya kupiga kura.
Kwa mujibu wa simulizi yake, Abdallah Mzee, ambaye alikuwa akizungumza Kiingereza vizuri, alitafsiri mazungumzo kati ya wanawake hao na mjumbe kutoka Lancaster House. Wanawake waliwasilisha hoja yao na baadaye wakaruhusiwa kupiga kura.
Lakini kulikuwa na vikwazo. Serikali ya kikoloni iliweka masharti kwamba mpiga kura awe anajua kusoma na kuandika na awe na angalau shilingi tatu.
Mama Fatma alieleza kwamba shilingi hizo tatu zilikuwa kiasi kikubwa sana kwa wakati huo. Alisema hata mshahara wa mwezi wa mumewe, Karume, ulikuwa shilingi tatu.
Wanawake wakaweka mpango wa kukabiliana na kikwazo hicho. Kwa msaada wa mashine za kushonea na maroli ya vitambaa kutoka nchi rafiki, ikiwemo China, waliunda vikundi vya ujasiriamali ili kuonyesha kuwa walikuwa na shughuli zilizowawezesha kupata fedha. Pia walifanya miradi ya upishi.
Mama Fatma alisema hatua hizo ziliwezesha wanawake wengi kusajiliwa kama wapiga kura, hata kama hawakuwa na zile shilingi tatu zilizokuwa zikitakiwa rasmi.
Alisisitiza kwamba wanawake hawakuwa wakishiriki katika harakati hizo kwa kuwahudumia waume zao tu, bali walikuwa sehemu ya siasa hai.
Na alipoulizwa kuhusu nafasi yake katika Mapinduzi ya Januari 12, 1964, Mama Fatma alisema wazi kwamba alishiriki mwenyewe katika Mapinduzi ya Zanzibar.
Baada ya Mapinduzi, Karume akawa Rais wa kwanza wa Zanzibar na Mama Fatma akawa 'First Lady' wa kwanza wa Zanzibar.
Kazi aliyoifanya jikoni mpaka kibarazani
Maisha ya Mama Fatma hayawezi kutenganishwa na ya Karume, lakini simulizi zake zinaonyesha kwamba nafasi yake haikuwa tu ya kuwa mke wa mwanasiasa.
Baada ya Mapinduzi, alihusishwa na Umoja wa Wanawake wa Afro-Shirazi Party na shughuli za kuwahamasisha wanawake kushiriki katika maisha ya kijamii na kisiasa.
Katika simulizi yake, alionyesha pia namna alivyoliona suala la uwezeshaji wa wanawake. Alisema wanawake wana nguvu ya kujenga au kubomoa na aliwataka kutumia fursa zilizopo kujiletea maendeleo ya kiuchumi.
Ndoa yake na Karume yenyewe ilikuwa sehemu ya safari hiyo. Ndoa yao ilikumbana na vikwazo vilivyotokana na ubaguzi wa rangi. Mama Fatma alikuwa na asili ya familia ya Kihindi upande wa baba, huku Karume akiwa Mwafrika, na alisema mazingira ya wakati huo yalifanya ndoa ya aina hiyo ionekane kama jambo lisilo la kawaida.
Hata hivyo, baba yake aliunga mkono ndoa hiyo. Familia yao ilipata mtoto wa kwanza, Asha, aliyefariki siku ya pili baada ya kuzaliwa. Baadaye walimpata Amani Abeid Karume, aliyezaliwa mwaka 1948, na Ali Abeid Karume, aliyezaliwa mwaka 1950. Amani akaja kuwa Rais wa Zanzibar kati ya mwaka 2000 na 2010.
Hivyo, hata maisha yake ya nyumbani yalikuwa yamezungukwa na matukio ambayo baadaye yakawa sehemu ya historia ya Zanzibar.
Anaondoka na historia ya miaka 92 isiyofutika

Chanzo cha picha, Dailynews
Aprili 7, 1972, maisha ya Mama Fatma yalibadilika tena baada ya Karume kuuawa kwa kupigwa risasi katika makao makuu ya Afro-Shirazi Party, Kisiwandui, Zanzibar.
Alikuwa amekuwa First Lady wa Zanzibar tangu Mapinduzi ya 1964.
Baada ya kifo cha Karume, Mama Fatma aliendelea kuishi na kumbukumbu za kipindi hicho na baadaye akawa mmoja wa watu ambao simulizi zao zilitumika kuelewa historia ya Zanzibar kutoka kwa waliokuwa wameishi ndani ya matukio hayo.
Katika mahojiano yake na Daily News mwaka 2023, alisema licha ya kusafiri sehemu mbalimbali, alihakikisha kila mwaka anakuwa Zanzibar wakati wa maadhimisho ya Mapinduzi. Alisema siku hiyo ilikuwa miongoni mwa kumbukumbu zake za kihisia.
Hivyo Mama Fatma aliishi kuona mumewe akiwa Rais wa kwanza wa Zanzibar na mwanawe baadaye akiwa Rais wa Zanzibar.
Lakini sehemu kubwa ya urithi wake iko katika simulizi alizoacha. Alizungumza kuhusu wanawake waliopigania haki ya kupiga kura, kuhusu Mapinduzi, kuhusu maisha yake na Karume, kuhusu michezo na kuhusu Zanzibar aliyoiishi kabla na baada ya 1964.
Na katika mahojiano yake ya miaka ya hivi karibuni,, hakujieleza kama mwanamke aliyebaki nyuma ya historia. Alijieleza kama mmoja wa wanawake walioshiriki katika kuijenga.
Kwa hiyo, kifo cha Mama Fatma Karume kinaondoa zaidi ya mjane wa Rais wa kwanza wa Zanzibar.
Kinaondoa mmoja wa mashahidi wa moja kwa moja wa vipindi muhimu vya historia ya Zanzibar, mwanamke aliyeshiriki harakati za wanawake, akawa First Lady wa kwanza baada ya Mapinduzi, akaishi tukio la kuuawa kwa Karume, na baadaye akaendelea kusimulia historia hiyo kwa sauti yake mwenyewe.
Anaondoka akiwa ameishi miaka zaidi ya 90. Lakini historia aliyoishi, na sehemu aliyokuwa nayo ndani yake, haifutiki.












