DR Congo yasitisha shughuli za uchimbaji madini Jimbo la Kivu Kusini
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imeweka marufuku ya muda wa miezi mitatu kusitisha shughuli za uchimbaji madini katika baadhi ya maeneo ya Jimbo la Kivu Kusini, kwa mujibu wa waraka wa Wizara ya Madini.
Hatua hiyo imechukuliwa kutokana na ongezeko la uchimbaji haramu wa madini na itahusisha wilaya za Mwenga na Shabunda, kulingana na waraka uliotolewa Mei 22 na kutiwa saini na Waziri wa Madini, Louis Watum Kabamba.
Katika kipindi hicho cha marufuku, timu maalum ya ukaguzi inayoongozwa na Ukaguzi Mkuu wa Madini itafanya tathmini ili kubaini uhalali wa shughuli za uchimbaji katika maeneo husika.
Serikali ya Kongo inalenga kupunguza udanganyifu katika sekta ya madini pamoja na uendelezaji haramu wa rasilimali za madini katika jimbo hilo.
Madini ya dhahabu, kasiteriti (bati) pamoja na koltani, ambayo hutumika katika teknolojia ya kisasa na hupatikana zaidi katika Jimbo la Kivu Kusini mashariki mwa nchi hiyo, huchimbwa zaidi na wachimbaji wadogo wadogo wa jadi.
Mwaka jana, Kongo ilipiga marufuku biashara ya madini kutoka maeneo kadhaa ya uchimbaji wa jadi katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Kivu Kusini yaliyoathiriwa na migogoro, kutokana na tuhuma kuwa madini hayo yalikuwa yakitumika kufadhili makundi yenye silaha mashariki mwa nchi.
Kongo pia ni miongoni mwa nchi zenye hifadhi kubwa zaidi duniani za kobalt, shaba na lithiamu.
Soma zaidi: