Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Trump: Nimewaagiza wapatanishi kutoharakisha kufanya makubaliano na Iran

Makubaliano yanayojadiliwa yanaripotiwa kuhusisha kuongeza muda wa kusitisha mapigano hadi siku 60, kufungua tena Mlango-Bahari wa Hormuz na mpango wa mazungumzo zaidi kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran.

Moja kwa moja

NaMariam Mjahid

  1. Shambulio kubwa la Urusi dhidi ya Ukraine laua watu wanne na kujeruhi makumi

    Urusi imefanya mashambulizi makubwa na ya maangamizi dhidi ya Ukraine usiku wa kuamkia Jumamosi, ikirusha mamia ya droni na makombora kadhaa.

    Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskyy, amesema mji mkuu Kyiv ndio ulikuwa shabaha kuu, ingawa maeneo mengine pia yalilengwa, huku takribani watu 100 wakijeruhiwa.

    Watu wanne waliuawa katika mji mkuu na maeneo ya karibu, huku milipuko ikisikika usiku kucha.

    Mamia ya majengo ya makazi, shule, nyumba ya opera na jumba la makumbusho yaliharibiwa.

    Wizara ya Ulinzi ya Urusi imesema kuwa ilitumia kombora la hypersonic aina ya Oreshnik katika mashambulizi hayo, ambayo ilieleza kuwa ni kujibu “mashambulizi ya Ukraine dhidi ya miundombinu ya kiraia”. Hata hivyo, jeshi la Ukraine limekanusha kulenga raia.

    Mapema Jumatatu, miundombinu ya nishati iliharibiwa katika shambulio la makombora katika eneo la Belgorod nchini Urusi linalopakana na Ukraine, ikiwa ni pamoja na mji wa Belgorod, kwa mujibu wa shirika la habari la Interfax likinukuu mamlaka za eneo hilo.

    Hakukuwa na vifo vilivyoripotiwa, lakini huduma za umeme na maji zilikatika, taarifa hiyo ilisema.

    Eneo la Yaroslavl nchini Urusi, kaskazini mashariki mwa Moscow, pia lililengwa na mashambulizi ya droni, gavana wake Mikhail Yevrayev alisema kupitia Telegram.

    Rais wa Urusi Vladimir Putin alianzisha uvamizi mkubwa dhidi ya Ukraine Februari 2022.

    Jeshi la Ukraine limesema pia lilifanya shambulio katika eneo la Starobilsk lililoko mashariki mwa Ukraine linalodhibitiwa na Urusi usiku wa Ijumaa, likieleza kuwa lililenga kitengo maalum cha kijeshi cha droni cha Urusi.

    Viongozi wa Ulaya wamelaani mashambulizi hayo ya Urusi yaliyofanyika mapema Jumapili, yakija baada ya onyo la Zelensky kwamba Urusi ilikuwa inapanga mashambulizi mapya na huenda ilijiandaa kutumia kombora la Oreshnik.

    Inaripotiwa kuwa kombora hilo husafiri kwa kasi zaidi ya mara 10 ya sauti, ni vigumu kulizuia, na lina uwezo wa kubeba vichwa vya kawaida na vya nyuklia.

    Soma zaidi:

  2. Zaidi ya visa 900 vinavyoshukiwa ni Ebola vimegundulika DR Congo - WHO

    Zaidi ya visa 900 vinavyoshukiwa kuwa Ebola, ikiwemo visa 101 vilivyothibitishwa, vimegunduliwa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, amesema Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Tedros Adhanom Ghebreyesus, siku ya Jumapili.

    Haya yanajiri baada ya wakazi wenye hasira katika mji ulio katika kitovu cha mlipuko wa Ebola mashariki mwa Kongo kushambulia na kuchoma hema lililokuwa sehemu ya kituo cha afya kinachotibu wagonjwa wa virusi hivyo, wahudumu wa afya wamesema Jumamosi. Tukio hilo lilikuwa la pili la aina hiyo katika eneo hilo ndani ya wiki moja.

    Kwa mujibu wa taarifa za awali, hakuna mtu aliyejeruhiwa katika shambulio hilo, lakini wagonjwa walipokimbia ili kuepuka moto huo, watu 18 wanaoshukiwa kuambukizwa Ebola walitoroka katika kituo hicho na hadi sasa hawajulikani walipo, alisema mkurugenzi wa hospitali ya eneo hilo.

    Wakazi hao wenye hasira walifika katika kliniki iliyopo katika mji wa Mongbwalu usiku wa Ijumaa na kuchoma moto hema lililokuwa limewekwa kwa ajili ya wagonjwa wanaoshukiwa na waliothibitishwa kuwa na Ebola, lililokuwa likiendeshwa na shirika la misaada la Madaktari Wasio na Mipaka (MSF), alisema Dk. Richard Lokudi, mkurugenzi wa hospitali ya Mongbwalu, akizungumza na shirika la habari la Associated Press.

    “Tunalilaani vikali tukio hili, kwani limesababisha hofu miongoni mwa wahudumu na pia kusababisha kutoroka kwa watu 18 wanaoshukiwa kuambukizwa katika jamii,” alisema.

    Siku ya Alhamisi, kituo kingine cha matibabu katika mji wa Rwampara kilichomwa moto baada ya ndugu wa marehemu kuzuiwa kuchukua mwili wa mwanafamilia wao aliyeshukiwa kufariki kutokana na Ebola.

    Soma zaidi:

  3. Mshukiwa wa shambulio karibu na Ikulu ya Marekani atambuliwa

    Siku moja baada ya milio ya risasi kusikika karibu na Ikulu ya Marekani na maafisa wa usalama kutangaza kuwa mshukiwa alipigwa risasi na kuuawa na maafisa wa siri waliokuwa kazini, vyombo vya habari vya Marekani vimeripoti utambulisho na historia ya mtu huyo.

    Kwa mujibu wa CBS, mshirika wa habari wa BBC nchini Marekani, mshukiwa aliyetekeleza shambulio hilo ametambuliwa kuwa Nasser Best, mwenye umri wa miaka 21, ambaye alikuwa akifahamika kwa vyombo vya sheria na alikuwa na historia ya matatizo ya afya ya akili.

    Milio ya risasi ilisikika muda mfupi baada ya saa kumi na mbili jioni kwa saa za Washington siku ya Jumamosi, hali iliyowalazimu waandishi wa habari waliokuwa wakirusha matangazo nje ya Ikulu ya Marekani kujilaza chini na kukimbilia ndani ya jengo hilo kwa usalama.

    Maafisa wa Ujasusi wa Marekani waliokuwa wakilinda eneo hilo walijibu mashambulizi hayo kwa kufyatua risasi na kumlenga mshukiwa.

    Baada ya tukio hilo, mshukiwa alikimbizwa hospitalini lakini baadaye alitangazwa kufariki dunia kutokana na majeraha aliyoyapata.

    Mtu mmoja aliyekuwa karibu na eneo la tukio pia alijeruhiwa, ingawa maafisa wa idara ya upelelezi hawakutoa taarifa zaidi kuhusu hali yake. Hakuna afisa wa usalama aliyeripotiwa kujeruhiwa katika shambulio hilo.

    Vyanzo vinavyofahamu uchunguzi huo vimesema mshukiwa alitumia bastola aina ya revolver kutekeleza shambulio hilo.

    Chanzo kimoja kilichozungumza na CBS kuhusu uchunguzi huo kilisema kuwa Nasser Best aliwahi kujaribu kuingia katika Ikulu ya Marekani mwezi Julai 2025, na baadaye alipelekwa katika kituo cha afya ya akili baada ya kukamatwa na maafisa wa usalama karibu na jengo hilo.

    Kwa mujibu wa taarifa hizo, alikuwa akiishi mjini Washington, D.C., kwa miezi 18 iliyopita.

    Soma zaidi:

  4. Asilimia 95 ya makubaliano kati ya Iran na Marekani imekamilika - Fox News

    Shirika la habari la Marekani, Fox News, limeripoti kuwa maafisa waserikali wametangaza kwamba asilimia 95 ya masharti ya makubaliano yanayojadiliwa kati ya Tehran na Washington tayari yamekamilishwa.

    Katika vipindi vyake vya habari na uchambuzi vilivyorushwa Jumapili, Fox News ilijadili maendeleo ya mazungumzo yanayoendelea kati ya Marekani na Iran, huku wachambuzi na wageni mbalimbali wakieleza kuwa pande hizo mbili zimepiga hatua katika masuala muhimu, yakiwemo kuongeza muda wa usitishaji mapigano, kufunguliwa tena kwa Mlango Bahari wa Hormuz na kuondolewa kwa vikwazo vya kijeshi vya majini dhidi ya Iran.

    Hata hivyo, FOX News pia iliangazia wasiwasi uliopo miongoni mwa baadhi ya wanasiasa na wadau wa kisiasa nchini Marekani kuhusu misimamo ya serikali ya Iran, kwa kuonyesha matamshi ya hivi karibuni ya Mohsen Rezaei, aliyewahi kuwa kamanda wa Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran.

    Katika kauli yake ya karibuni, Rezaei alionya kuwa Iran inaweza kujiondoa katika Mkataba wa Kimataifa wa Kuzuia Uenezaji wa Silaha za Nyuklia (NPT) ikiwa hali ya sasa itaendelea bila mabadiliko.

    Kauli hiyo imeongeza uzito wa mjadala kuhusu mustakabali wa mazungumzo hayo, wakati juhudi za kidiplomasia zikiendelea kutafuta suluhisho la kudumu kwa mzozo uliopo kati ya Iran na Marekani.

    Soma zaidi:

  5. Mwanaanga wa China kuishi mwaka mzima anga za juu huku Beijing ikijipanga kuelekea Mwezini

    China imezindua safari mpya ya anga za juu inayojumuisha watu watatu kuelekea kituo chake cha anga cha Tiangong Space Station, ambapo mmoja wa wanaanga hao atatumia mwaka mzima akiwa katika mzunguko wa Dunia.

    Hatua hiyo inachukuliwa kuwa sehemu muhimu ya maandalizi ya mpango wa Beijing wa kupeleka binadamu Mwezini ifikapo mwaka 2030.

    Misheni hiyo, inayojulikana kama Shenzhou-23, imezinduliwa siku ya Jumapili kwa kutumia roketi ya Long March 2F kutoka kituo cha kurushia vyombo vya anga cha Jiuquan kilichopo katika Jangwa la Gobi, kaskazini magharibi mwa China.

    Katika kipindi cha miongo mitatu iliyopita, China imewekeza mabilioni ya dola katika sekta ya anga huku ikilenga kujiimarisha kama moja ya mataifa yanayoongoza katika uchunguzi wa anga za juu.

    Tangu mwaka 2021, misheni za Shenzhou zimekuwa zikituma wanaanga watatu kwa wakati mmoja katika kituo cha Tiangong kwa safari za takribani miezi sita. Hata hivyo, safari hii itakuwa ya kipekee kwa kuwa itashuhudia mwanaanga mmoja akibaki angani kwa muda wa mwaka mzima kwa mara ya kwanza katika historia ya mpango wa anga wa China.

    Miongoni mwa wanaanga walioko katika misheni hiyo ni Li Jiaying mwenye umri wa miaka 43, ambaye amekuwa mwanaanga wa kwanza kutoka Hong Kong kushiriki katika safari ya anga. Kabla ya kujiunga na mpango wa anga wa China, Li aliwahi kufanya kazi katika jeshi la polisi la Hong Kong.

    Wanachama wengine wa misheni hio ni Zhu Yangzhu, mhandisi wa anga mwenye umri wa miaka 39, na Zhang Zhiyuan, mwenye umri wa miaka 39 na aliyekuwa rubani wa Jeshi la Anga la China. Kwa wote wawili, hii ni safari yao ya kwanza kwenda angani.

    Wakiwa katika kituo cha Tiangong, wanaanga hao wanatarajiwa kutekeleza miradi mbalimbali ya kisayansi inayohusu sayansi ya maisha, sayansi ya vifaa, fizikia ya vimiminika na tiba.

    Jaribio muhimu zaidi katika misheni ya Shenzhou 23 ni kufuatilia athari za kukaa kwa muda mrefu katika mazingira yenye mvutano mdogo wa nguvu za uvutano yaani gravity. Utafiti huo unalenga kusaidia maandalizi ya safari za baadaye za kuelekea Mwezini na hata sayari ya Mirihi.

    Shirika la Anga la China limesema kuwa mwanaanga atakayechaguliwa kubaki angani kwa mwaka mmoja atatangazwa baadaye kulingana na maendeleo ya misheni hiyo.

    Mtaalamu wa unajimu na profesa katika Chuo Kikuu cha Macquarie nchini Australia, Richard de Grijs, amesema changamoto kuu za safari za muda mrefu angani ni pamoja na kupungua kwa msongamano wa mifupa, kudhoofika kwa misuli, kuathiriwa na mionzi ya anga, matatizo ya usingizi pamoja na uchovu wa kisaikolojia na kitabia.

    Ameongeza kuwa mifumo ya uhakika ya kuchakata maji na hewa, pamoja na uwezo wa kukabiliana na dharura za kiafya mbali na Dunia, ni mambo muhimu yatakayochangia mafanikio ya safari za muda mrefu za anga katika siku zijazo.

    Soma zaidi:

  6. Katika Picha: Jinsi Arsenali ilivyosherehea kukabidhiwa rasmi kombe la EPL 2026

    Ilikuwa siku ya kipekee kwa kocha Mikel Arteta kuifurahia. Akiwa mbele ya mmiliki wa klabu, Stan Kroenke, ambaye alishuhudia mchezo huo akiwa uwanjani katika moja ya ziara zake nadra za kuifuatilia timu ana kwa ana, Arsenal walisherehekea ubingwa wao wa kwanza wa ligi tangu mwaka 2004 baada ya kuichapa kwa urahisi Crystal Palace.

    Arsenal walithibitisha ubora wao kwa ushindi huo muhimu, huku Crystal Palace wakionekana kuwa na mawazo zaidi kuelekea fainali yao ya michuano ya Ulaya inayowasubiri. Ushindi huo ulihitimisha safari ndefu ya kusaka taji la ligi na kuwapa Mashabiki wa Arsenal sababu ya kushangilia baada ya kusubiri kwa zaidi ya miongo miwili.

  7. Trump: Nimewaagiza wapatanishi kutoharakisha kufikia makubaliano na Iran

    Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema amewaagiza wapatanishi wa Marekani “kutoharakisha kufikia makubaliano” na Iran, baada ya hapo awali kuashiria kuwa pande hizo zilikuwa karibu kufikia mwafaka.

    Makubaliano yanayojadiliwa yanaripotiwa kujumuisha kuongezwa kwa usitishaji mapigano kwa siku 60, kufunguliwa tena kwa Mlango Bahari wa Hormuz, pamoja na mpango wa kuendelea na mazungumzo kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran.

    Katika ujumbe aliouchapisha kwenye mitandao ya kijamii, Trump alisema mazungumzo yanaendelea kwa “mtazamo chanya”, lakini akasisitiza kuwa:

    “Pande zote mbili zinapaswa kuchukua muda wao na kuhakikisha kila jambo linafanyika kwa usahihi.”

    Siku ya Jumamosi, Trump alisema kuwa makubaliano hayo yalikuwa “kwa kiasi kikubwa yamejadiliwa”, hali iliyozua matarajio kwamba tangazo rasmi lingeweza kutolewa wakati wowote.

    Kwa upande wake, maafisa wa Iran pia wameashiria kuwepo kwa maendeleo katika mazungumzo hayo. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmail Baghaei, alisema kuwa pande hizo mbili ziko:

    “Karibu sana sio mbali sana” kufikia makubaliano.

    Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Marekani, makubaliano yanayojadiliwa kwa sasa si suluhisho la mwisho, bali yanaacha baadhi ya masuala magumu zaidi yaamuliwe katika mazungumzo ya baadaye.

    Masuala hayo ni pamoja na matakwa ya Iran ya kuondolewa vikwazo vya kiuchumi, kurejeshewa fedha zake zilizozuiwa nje ya nchi, pamoja na shinikizo la Washington kwa Iran kupunguza shughuli zake za nyuklia.

    Ripoti hizo pia zinasema kuwa mapendekezo ya makubaliano hayo yamezua mgawanyiko ndani ya Chama cha Republican, huku baadhi ya wanachama wakidai kuwa masharti yake yanaipa Iran nafuu kubwa kupita kiasi.

    Pia unaweza kusoma:

  8. Hujambo na karibu kwa matangazo ya Jumatatu ya tarehe 25 mwezi Mei 2026.