Mwanamke ahukumiwa kifo kwa madai ya "kitendo cha aibu" Makka

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 7

Familia ya mwanamke wa Bangladesh aliyekuwa amehukumiwa kifo nchini Saudi Arabia kwa madai ya kufanya "vitendo vya aibu" wamesema hawakujua iwapo binti yao alikuwa ametenda kosa ambalo lingeweza kuadhibiwa kwa hukumu ya kifo. Pia wamedai kuwa walipata taarifa za utekelezaji wa hukumu hiyo kupitia simu kutoka kwa rafiki wa binti yao aliyekuwa nchini Saudi Arabia.

Ikumbukwe kwamba Jumatano iliyopita (Oktoba 14), vyombo vya habari vya serikali ya Saudi Arabia viliripoti utekelezaji wa hukumu ya kifo dhidi ya mwanamke na mwanaume mmoja raia wa Bangladesh.

Shirika la habari la Saudi Arabia, Saudi Press Agency (SPA), lilinukuu taarifa ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi hiyo ikisema kwamba mwanaume na mwanamke wa Bangladesh walishtakiwa kwa "kufanya vitendo vya aibu" ndani ya msikiti mmoja uliopo katika mji mtakatifu wa Makka.

Kwa mujibu wa maafisa wa Saudi Arabia, vyombo vya usalama viliwakamata watuhumiwa hao, na baadaye mahakama ikatoa uamuzi uliothibitisha mashtaka yaliyokuwa yakikabili wawili hao.

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Saudi Arabia ilieleza kwamba hukumu hizo zilitolewa kutokana na uzito wa kosa hilo, kukiukwa kwa utakatifu wa msikiti, pamoja na mazingira ambayo vitendo hivyo vilifanyika. Katika muktadha huo, mamlaka za Saudi Arabia ziliwahukumu wawili hao adhabu ya kifo chini ya mfumo wa ta'zir (adhabu inayotolewa kwa hiari ya mahakama kwa makosa ambayo adhabu yake haijaainishwa moja kwa moja katika sheria za Kiislamu).

Hukumu hiyo ilitekelezwa tarehe 14 Oktoba 2026, baada ya rufaa yao kukataliwa na mahakama za juu.

Ingawa mamlaka za Saudi Arabia hazikueleza wazi ni lini watu hao wawili walikamatwa, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Bangladesh, Shama Obaid, amesema walikamatwa mwaka 2023.

Familia za watu hao wawili sasa zimethibitisha taarifa hiyo, zikisema kwamba ndugu zao walikuwa wamezuiliwa nchini Saudi Arabia kwa takribani miaka mitatu kabla ya hukumu ya kifo kutekelezwa.

Idhaa ya BBC Bangla ilizungumza na familia za raia hao wa Bangladesh waliokuwa wamehukumiwa kifo. Familia hizo zimedai kuwa hazikupokea taarifa rasmi kutoka kwa mamlaka za Saudi Arabia wala kutoka kwa maafisa wa Bangladesh kuhusu utekelezaji wa hukumu hiyo.

"Mwanamke huyo alikwenda Saudi Arabia kwa visa ya kazi akiwa na matumaini ya kuboresha hali ya uchumi ya familia."

Dada wa mwanamke wa Bangladesh aliyekuwa amehukumiwa kifo amesema aliarifiwa kuhusu kunyongwa kwa dada yake kupitia simu kutoka kwa rafiki wa marehemu aliyekuwa nchini Saudi Arabia.

Aliiambia BBC kwamba familia hiyo haikupata taarifa rasmi kutoka kwa mamlaka za Saudi Arabia kabla ya utekelezaji wa hukumu hiyo.

Kwa mujibu wa dada yake, alisema:

"Rafiki yake alinipigia simu na kuniuliza, 'Dada, mmefanikiwa kupata taarifa zozote?' Nikamjibu kwamba hatuna habari yoyote. Kisha akaniambia kuwa dada yangu hayuko tena duniani. Baadaye alinipatia pia video, ambayo nilikuja kuiona kwenye mitandao ya kijamii."

Hata hivyo, baada ya kupokea taarifa hizo za awali, familia iliendelea kuwa na mashaka na haikuzungumza hadharani kuhusu tukio hilo. Wanasema picha waliyopelekewa mwanzoni haikufanana na binti yao, na pia hawakuwa wamepokea taarifa yoyote rasmi kutoka serikalini au mamlaka husika.

Baba wa mwanamke huyo aliyenyongwa alisema alisita kuamini habari hizo kwa sababu mwanamke aliyeonekana kwenye picha aliyotumiwa na rafiki wa binti yake kutoka Saudi Arabia hakuwa akifanana na binti yake.

Kwa mujibu wa familia, marehemu alikuwa mdogo wa mwisho kati ya dada wanne. Alienda Saudi Arabia mwaka 2023 kwa visa ya kazi akiwa na matumaini ya kusaidia kuboresha hali ya maisha ya familia yake.

Baba yake ni mfanyakazi wa vibarua, na familia inasema kuwa binti yao alikamatwa takribani miezi sita tu baada ya kuwasili Saudi Arabia.

Dada yake alisema:

"Mambo haya yalianza miezi sita baada ya kuondoka kwenda Saudi Arabia. Alituambia kwamba alikuwa gerezani, lakini hakueleza sababu. Alitukataza kumuuliza maswali na akaahidi kwamba angerudi nyumbani na kutueleza kila kitu."

Familia inaeleza kuwa wakati wote alipokuwa gerezani, alikuwa akiwasiliana nao takribani mara moja kwa mwezi. Mara ya mwisho kuzungumza naye ilikuwa Jumanne iliyopita, siku moja kabla ya mamlaka za Saudi Arabia kutangaza kwamba hukumu ya kifo ilitekelezwa Jumatano.

Dada yake aliongeza:

"Alizungumza nasi Jumanne. Alipiga simu tena Jumatano, lakini hatukuweza kupokea simu yake."

"Sikujua kwamba mwanangu angenyongwa."

Mama wa mwanaume wa Bangladesh aliyekuwa amehukumiwa kifo amesema kupitia BBC Bangla kwamba mwanawe alikuwa amezungumza na familia yake akiwa gerezani nchini Saudi Arabia Jumapili iliyopita.

Huku akilia, mama huyo alisema:

"Tulijua kwamba alikuwa gerezani, lakini hatukuwahi kufikiria jambo hili lingetokea. Hata mwanangu mwenyewe hakutuambia kwamba angehukumiwa kifo."

Baba yake pia alisema alipata taarifa kuhusu utekelezaji wa hukumu ya mwanawe Jumatano iliyopita.

"Nilizungumza na mwanangu Jumapili. Aliniuliza kuhusu afya yangu. Kisha Jumatano nikapata habari kwamba hukumu ya kifo ilikuwa imetekelezwa dhidi yake."

Baba huyo anadai kuwa mwanawe alikaa karibu miaka mitatu gerezani nchini Saudi Arabia, lakini katika kipindi hicho hakupokea mawasiliano yoyote kutoka kwa serikali wala msaada wowote kuhusu hali ya mwanawe.

"Kwa miaka yote hiyo nilikuwa nikiulizia kama ubalozi wa Bangladesh ulikuwa umefuatilia suala hilo, lakini hakuna aliyekuwa na taarifa. Hakuna afisa kutoka Bangladesh aliyewahi kumtembelea gerezani wala kufahamu hali yake."

Ametaka mwili wa mwanawe urejeshwe Bangladesh haraka iwezekanavyo na uchunguzi ufanyike ili haki itendeke katika suala hilo.

"Sijauona uso wa mwanangu kwa miaka mitatu na miezi mitatu. Angalau ninatamani kumuona kwa mara ya mwisho."

Kwa mujibu wa mama yake, kijana huyo alihitimu masomo ya madrasa kabla ya kusafiri kwenda Saudi Arabia kupitia wakala mnamo Novemba 10, 2022.

Alikuwa mtoto wa kwanza katika familia yenye watoto wawili wa kiume na wawili wa kike. Alifanya kazi ya usafi mjini Riyadh na inadaiwa alikuwa akisafisha katika msikiti ambamo baadaye alituhumiwa kufanya "vitendo vya aibu".

Mama yake alisema:

"Aliwekwa gerezani miezi michache tu baada ya kufika Saudi Arabia. Mwezi mmoja baada ya kufungwa alinipigia simu na kusema, 'Mama, labda watanifunga kwa muda kisha wataniruhusu niondoke.'"

Alipoulizwa kama mwanawe aliwahi kueleza sababu ya kukamatwa kwake, mama huyo alisema:

"Hapana, hakuwahi kutuambia sababu kamili."

Hata hivyo, mwanafamilia mwingine alidai kwamba baadaye kijana huyo aliieleza familia kuhusu uhusiano wa kimapenzi kati yake na mwanamke mmoja.

Kwa mujibu wa mama yake, mwanawe alisema kwamba siku moja akiwa kazini, polisi walifika na kumkamata.

Familia inaeleza kuwa baada ya kufungwa gerezani, alikuwa akiwasiliana nao kwa simu fupi karibu kila wiki, na katika mazungumzo hayo aliwahi kutaja uwepo wa uhusiano wake wa kimapenzi na mwanamke huyo.

Mazungumzo yao ya mwisho yalifanyika Jumapili, siku tatu kabla ya hukumu ya kifo kutekelezwa.

Mama yake aliongeza:

"Mwanzoni mwanangu hakuweza kujitetea vizuri kwa sababu ya changamoto ya lugha. Tulipomfuata wakala aliyempeleka Saudi Arabia, alituambia kwamba baada ya kumfikisha huko hakuwa na wajibu mwingine wowote."

Wakazi wa eneo hilo waliiambia BBC kuwa kijana huyo alikuwa na umri wa takriban miaka 22. Baba yake alikuwa akifanya kazi za kilimo kwenye mashamba ya watu wengine, lakini kutokana na umri mkubwa sasa hana uwezo wa kufanya kazi hizo.

Kutokana na hali ngumu ya maisha ya familia, kijana huyo alipelekwa kufanya kazi nje ya nchi kupitia wakala. Hata hivyo, alikamatwa mwaka 2023, takribani miezi sita baada ya kuwasili Saudi Arabia.

Mamlaka za Bangladesh zimesema nini?

Kwa upande mwingine, Shamma Obaid Islam, Waziri wa Nchi anayeshughulikia Mambo ya Nje wa Bangladesh, amesema kuwa baada ya taarifa za kunyongwa kwa raia hao wawili kujulikana, serikali ya Bangladesh ilituma barua rasmi kwa serikali ya Saudi Arabia siku mbili zilizopita ikiomba maelezo ya kina kuhusu kesi hiyo na wananchi wa Bangladesh waliohukumiwa kifo.

Akizungumza na waandishi wa habari, alisema serikali kwa sasa inasubiri kupokea nakala kamili ya uamuzi wa mahakama na taarifa zinazohusiana na mwenendo wa kesi hiyo.

Aidha, Abdullah Zafer bin Abiyah, balozi wa Saudi Arabia nchini Bangladesh, aliitwa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Bangladesh mjini Dhaka ili kutoa maelezo zaidi kuhusu tukio hilo na utekelezaji wa hukumu hizo.

Kwa mujibu wa Shamma Obaid Islam, Saudi Arabia ni mojawapo ya mataifa muhimu zaidi kwa wafanyakazi wa Bangladesh wanaotafuta ajira nje ya nchi, na fedha wanazotuma nyumbani kutoka huko ni chanzo kikubwa cha mapato ya kigeni kwa Bangladesh.

Alisema:

"Kuna zaidi ya raia 400,000 wa Bangladesh wanaoishi na kufanya kazi nchini Saudi Arabia, na ni wajibu wetu kuhakikisha usalama wao."

Aliongeza kuwa raia wengi wa Bangladesh wanatumikia vifungo katika magereza mbalimbali nchini Saudi Arabia, na mamlaka za Saudia mara kwa mara huwasilisha orodha kwa serikali ya Bangladesh zikionesha nani amekamatwa, lini alikamatwa na kwa sababu gani.

"Tunachunguza iwapo majina ya watu hawa wawili yalikuwa katika orodha hizo au la. Hatujapokea pia taarifa kama hizo kutoka kwa familia zao. Kile tunachokijua ni kwamba tukio hilo lilitokea mwaka 2023 na walikamatwa mwaka huo huo."