Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Jinsi mwili wa mke wa rais ulivyoibiwa na kupatikana miaka 16 baadaye
Tahadhari: Ripoti hii ina maelezo ambayo yanaweza kuwasumbua baadhi ya wasomaji.
Eva Perón, Mke wa kwanza wa Rais mashuhuri wa Argentina, alifariki mwezi Julai mwaka wa 1952. Alifahamika pia na wengi kwa jina la Evita.
Saa chache baada ya Eva Perón kufariki tarehe 26 mwezi Julai mwaka wa 1952, Dkt. Pedro Ara alianza kazi.
Mtaalamu huyo mashuhuri wa anatomia kutoka Hispania alipewa jukumu la kuhifadhi mwili wa mke huyo wa rais wa Argentina, kwa njia iliyofanana na jinsi Warusi walivyohifadhi miili ya viongozi wao, Lenin na Stalin.
Baada ya kifo chake, mwili wake ulihifadhiwa katika majengo ya wizara ya leba nchini humo. Wafanyikazi walitakiwa kujenga sanamu na eneo la kumbukumbu.
Miaka mitatu baadaye, mwezi Septemba mwaka wa 1955, mume wake, Rais Juan Peron aliondolewa madarakani kupitia mapinduzi ya kijeshi na kumlazimu kuenda mafichoni.
Serikali mpya ilipochukua madaraka, iliamua kuondoa mwili wa Eva Perón kutoka kwenye mnara uliokuwa katikati ya jiji.
Na hivyo kuanza safari ya kusikitisha ya miaka 16 ambayo ilichangia Evita kuzikwa baada ya miaka 16.
Katika safari yake ya miaka 16 ya kurejea Buenos Aires baada ya mwili wake kuibiwa, mwili wa Eva Perón ulihifadhiwa katika maeneo mbalimbali.
Wakati mwingine uliwekwa katika Kituo cha Ujasusi wa Kijeshi, na wakati mwingine ulisafirishwa katika jiji hilo kwa kutumia gari .Wakati mmoja, mwili huo hata ulizikwa mjini Milan, Italia.
Mwili wa Evita pia ulipelekwa kwa mume wake aliyekuwa uhamishoni mjini Madrid, Hispania, kabla hatimaye kurejeshwa Buenos Aires na kuwekwa katika kaburi maalum lenye ulinzi mkali.
Evita hakufa hata baada ya kifo chake
Eva Perón alifariki kutokana na saratani ya njia ya uazazi, akiwa na umri wa miaka 33. Mume wake alikuwa na sababu za kisiasa za kutaka mwili wake uhifadhiwe.
Akiwa amekulia katika mazingira ya umaskini vijijini, pamoja na shughuli zake za kuwasaidia watu wakati akiwa Mke wa Rais, Eva alikuwa amejijengea umaarufu mkubwa miongoni mwa wafanyakazi na watu wa tabaka la chini, hadi kuwa nyenzo muhimu nchini Argentina.
"Kwa hiyo, mume wake alitaka kuhifadhi mwili wa mke wake ili kuendeleza au kutumia umaarufu huo," mwanahistoria wa Peronism, Flavia Fiorucci, aliiambia BBC mwaka wa 2011.
Peronism ni itikadi ya kisiasa nchini Argentina iliyojengwa kutokana na misingi ya mawazo ya Juan Perón na Eva Perón. Misingi yake mikuu ni haki ya kijamii, utaifa, uchumi na siasa za kipopulisti.
"Pia ilihusiana na umuhimu wa ishara katika mtazamo wa Perón na Peronism, kwa sababu Evita pia alikuwa amegeuka kuwa ishara ya nchi yake."
Hili lilionekana wazi zaidi katika wiki zilizofuata baada ya kifo chake.
Mtaalamu wa anatomia kutoka Hispania, Dkt. Ara, aliweza kuhifadhi mwili wa Evita ukiwa katika hali ya asili, kwa kutumia mbinu ya kuingiza mafuta ya taa na glycerine mwilini mwake.
Katika mazishi ya Eva Perón, zaidi ya watu milioni mbili walifika kuuona mwili wake, ambao uliwekwa hadharani kwa siku 14 katika jengo la Bunge la Argentina.
Mapenzi ambayo Evita alikuwa amejijengea miongoni mwa wananchi wa Argentina alipokuwa hai yaliendelea hata baada ya kifo chake.
Perón alipoondolewa madarakani mwaka wa 1955, utawala wa kijeshi ulioongozwa na Jenerali Pedro Aramburu, ulilenga kuondoa kila kitu kilichohusiana na Peronism, au itikadi ya Perón. Utawala huo ulihofia kwamba mwili wa Evita ungeweza kuwa alama ya upinzani.
Baada ya kuutoa mwili wa Evita kutoka katikati mwa mji wa Buenos Aires, Luteni Kanali Carlos Murri Koenig, mkuu wa ujasusi nchini Argentina, hakuuweka katika eneo moja. Badala yake, aliuhamisha kutoka sehemu moja hadi nyingine ndani ya jiji hilo.
Alifanya hivyo kwa kuhofia kwamba wafuasi wa Perón wangejaribu kuupata na kuutumia kama ishara ya upinzani.
Inasemekana wakati huo, mwili wa Evita wakati mwingine ulifichwa ndani ya gari lililokuwa limeegeshwa katika mitaa ya mji mkuu, wakati mwingine nyuma ya pazia la ukumbi wa sinema, na wakati mwingine nyuma ya pampu ya maji ya jiji.
Hata hivyo, kila jeneza hilo lilipohamishwa kwenda eneo jipya, maua na mishumaa vilionekana, ingawa haikujulikana ni nani aliyekuwa akiviweka.
Baadaye, Luteni Kanali Koenig aliupeleka mwili huo katika ofisi yake, ambako inasemekana angesimamisha jeneza wima na kuwaonyesha wageni waliomtembelea.
Wakati fulani, inasemekana Koenig alianza kuwa na uhusiano wa kupindukia na mwili aliokuwa akiulinda.
"Nilimfahamu kutoka shule ya kijeshi. Alikuwa mtu wa kawaida kabisa, lakini alipatwa na wazimu baada ya kuupata mwili wa Evita," alisema Kanali mstaafu wa jeshi, Hector Cabanías, katika makala ya mwaka wa 1997 iliyokuwa na jina "Evita, La Tumba Sin Paz," linalomaanisha "Evita, Kaburi Lisilo na Amani."
Msomi wa Argentina Cecilia Macon aliiambia BBC mwaka wa 2012 kwamba ni vigumu kubaini ukweli kamili kwa yaliyotokea, kwa sababu "hadithi za kubuni na historia zimechanganyika katika simulizi zinazomhusu Evita."
Moja ya simulizi maarufu ni kwamba Koenig alianza kuwa na msukumo wa kupindukia kuhusu mwili wa Evita, ambao ulikuwa chini ya uangalizi wake kabla ya kuondolewa katika wadhfa wake mwaka wa 1957.
Baadaye, Kanali Cabanías alipewa jukumu la kuhakikisha mwili wa Eva Perón unatoweka, na mwaka 1957 mipango iliwekwa ya kuupeleka Italia.
Wakati huo, Evita alizikwa katika makaburi ya Milan, Italia, kwa kutumia jina bandia Maria Maggi de Magistris.
Wakati huo huo, wafuasi wake nchini Argentina hawakumsahau Eva. Mara kwa mara, maandishi yaliweza kuonekana kwenye kuta za mji wa Buenos Aires yakisema: "Mwili wa Eva Perón uko wapi?"
Kurejeshwa kwa mwili wake kulikuwa moja ya madai makuu ya wafuasi wa Perón (Peronists) nchini Argentina wakati huo.
Kurejeshwa kwa mwili
Mwanahistoria Fiorucci anaamini kwamba hatua ya kijeshi ya kuuficha mwili wa Evita ulifanya suala hilo kuwa kubwa zaidi.
"Shambulio dhidi ya mwili wa Evita ilikuwa ishara ya shambulio dhidi ya wafanyakazi wa nchi hii."
Mwaka wa 1971, serikali nyingine mpya ililenga kurejesha utawala wa kidemokrasia nchini Argentina na ikakubali kumrudishia Juan Perón mwili wa Evita, huku ikilegeza baadhi ya vikwazo dhidi ya wafuasi wa Perón.
Wakati huo, aliyekuwa dikteta Juan Perón alikuwa uhamishoni katika nyumba moja ya kifahari iliyokuwa pembezoni mwa Madrid, Hispania, akiishi na mke wake wa tatu, Isabel. Siku moja, mwili wa Evita uliwasili hapo ukiwa ndani ya jeneza la fedha.
Carlos Spadoni, aliyekuwa msaidizi wa karibu wa Juan Perón wakati huo, aliiambia BBC mwaka wa 2012 kwamba alikuwa mtu wa kwanza kuuona mwili huo.
"Jenerali Perón, mtunza bustani na mimi tulitoa mwili kutoka kwenye jeneza," alisema.
"Tuliuweka juu ya meza na mikono yetu ikawa chafu kutokana na udongo. Kwa hiyo tulilazimika kuusafisha mwili. Isabel aliuhudumia kwa uangalifu mkubwa kwa kutumia pamba na maji"
Isabel alichana nywele zake za dhahabu. Zilikuwa ndefu kiasi, na alizisafisha kwa upole kwa kutumia kichanuo, kisha akazikausha kwa mashine ya kukausha nywele.
Simulizi mbalimbali zilisambaa kuhusu yaliyotokea baadaye, nyingi zikihusisha imani za nguvu za kimiujiza za José López Rega, aliyewahi kuwa waziri katika serikali ya Perón.
Moja ya simulizi hizo inasema kwamba Rega alimwomba Isabel alale kando ya mwili wa Eva Perón, ili nguvu za kisiasa au mvuto wa Evita uweze kumgusa.
Imani kama hiyo inaonyesha heshima kubwa, ambayo wafuasi wake walikuwa nayo kwa Evita.
Evita, ambaye hapo awali alikuwa mcheza dansi maarufu na baadaye akaingia madarakani pamoja na mume wake, hatimaye aligeuka kuwa kiongozi wa kiroho kwa baadhi ya wafuasi wake.
Ndiyo maana mwili wa Eva Perón ulianza kuchukuliwa kuwa mtakatifu na wenye umuhimu mkubwa wa kiishara na wafuasi wake, licha ya kuchukiwa na wapinzani wa Perón.
Mwaka wa 1973, Juan Perón alirejea madarakani nchini Argentina, huku Isabel akiwa makamu wake wa rais.
Wakati huo, mwili wa Evita bado ulikuwa nchini Hispania.
Hata hivyo, baada ya Juan Perón kufariki ghafla mwaka 1974, mwili wa Evita ulirejeshwa Buenos Aires.
Wakati Domingo Teixeira alipowasiliana kwa mara ya kwanza ili kurekebisha uharibifu uliokuwa umetokea kwenye mwili wa Evita, alikuwa ameketi katika baa moja katika mji mkuu.
"Wanaume wawili waliovalia mavazi meusi waliingia," aliiambia BBC mwaka wa 2012.
"Walifungua mlango na kututazama. Ilikuwa hatari, kwa sababu siku hizo watu walikuwa wakichukuliwa na 'kutoweshwa', na hawakuonekana tena."
Teixeira alikuwa mtaalamu wa kurejesha hali ya awali ya kazi za sanaa, vitu vya kale na mabaki ya binadamu, kurekebisha uharibifu au mabadiliko yaliyotokea na kuvirejesha katika hali yake ya awali.
Ingawa aliingiwa na hofu akidhani kwamba wanaume hao walikuwa sehemu ya kikosi cha serikali kilichohusika na mauaji, Teixeira alifarijika alipogundua kwamba wanaume hao walikuwa madereva tu.
Waliohusika walimpeleka kwa daktari binafsi wa zamani wa Eva Perón, Oscar Ivanisevic.
"Aliniambia, 'Tuna kazi kwa ajili yako. Unapaswa kuurejesha mwili wa Eva Perón katika hali yake ya awali.'"
Licha ya kufahamu hatari zilizokuwapo, Teixeira alikubali kufanya kazi hiyo.
"Kufanya kazi hiyo kulimaanisha kwenda kinyume na watu wote waliohusika kuuficha mwili huo, na wengi wao walitaka sana Evita asirudi kamwe. Nilijua kwamba jambo hilo lingeweza kuniletea matatizo," alisema.
"Kulikuwa na vitisho, vitisho kupitia simu. Wakati mmoja, gari langu lilichomwa moto."
Baadaye, wakati ukatili wa serikali na mateso yalipoongezeka chini ya tawala zilizofuatana nchini Argentina, mtaalamu huyo wa kurejesha vitu katika hali yake ya awali alilazimika kukimbilia uhamishoni.
Hatimaye, Evita alizikwa rasmi mnamo mwezi Oktoba mwaka wa 1976, katika mazishi yaliyohudhuriwa na idadi ndogo sana ya watu.
Ili kuhakikisha kwamba mwili wake hauibiwi tena au kukumbwa na madhara kama yale yaliyotokea hapo awali, ulihifadhiwa katika kaburi lenye ulinzi mkali, lililojengwa kwa mawe.
Kulikuwa na mlango wa siri kwenye sakafu ya kaburi , uliokuwa ukielekea kwenye chumba kilichofichwa chini ya ardhi.
Ndani ya chumba hicho kulikuwa na mlango mwingine wa siri, uliokuwa ukielekea kwenye chumba kikuu kilichokuwa na jeneza la Evita.
Miaka 24 baada ya kifo chake, nguvu ya kiishara ya Evita ilikuwa bado kubwa kiasi kwamba mwili wake ulilazimika kuzikwa mita tano chini ya ardhi.