Timu 5 za kutazama katika Ligi Kuu ya England msimu huu

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 5

Msimu wa 2026/27 wa Ligi Kuu ya England, umeanza rasmi wikendi hii baada ya timu kukamilisha maandalizi yao kwa ajili ya mashindano hayo.

Hii inajumuisha kila kitu kuanzia kusajili wachezaji wapya hadi kuandaa mechi za maandalizi ya msimu na kufuatilia hali ya afya ya wachezaji wao walioumia au kuugua.

Arsenal ilitwaa ubingwa wa ligi hiyo mwaka jana kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 22, na timu hiyo itakuwa ikilenga kutwaa taji hilo kwa mara ya pili mfululizo na kufuata nyayo za Manchester City, ambayo ilitawala mashindano hayo kwa karibu miaka 10 chini ya Pep Guardiola.

Kwa upande mwingine, timu nyingine kama vile Liverpool na Manchester City, ambazo zimewahi kutwaa ubingwa huo hapo awali, nazo zitafanya kila liwezekanalo kurejea kwenye kundi la timu zinazowania taji hilo.

BBC imechambua timu tano ambazo zinatarajiwa kutawala Ligi Kuu msimu huu au hata kutwaa ubingwa mwishoni mwa msimu.

Arsenal mabingwa wa ligi kuu

Arsenal inatarajia kuendeleza juhudi zake za msimu uliopita ili kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 22.

Inatarajiwa kuwa timu yenye ushindani mkubwa katika ligi hiyo, ikizingatiwa mabadiliko yaliyotokea miongoni mwa timu kubwa, hasa katika nyanja ya ukocha.

Timu tisa kati ya 20 zinazoshiriki Ligi Kuu zitaanza msimu huu zikiwa na makocha wapya, huku nyingine, kama vile Manchester United na Tottenham, zikianza msimu zikiwa na makocha ambao wamehudumu kwa muda usiozidi mwaka mmoja.

Hata hivyo, kocha wa Arsenal, Mikel Arteta, amekuwa na timu yake tangu mwaka 2019 na amemaliza katika nafasi ya pili kwenye ligi karibu mara tatu mfululizo, jambo lililomwezesha kuielewa vyema sana ligi hiyo na ushindani wake.

Arsenal haikukaa bila kufanya lolote; iliendelea kusajili wachezaji ili kuimarisha zaidi kikosi chake, ikiwemo kumsajili kiungo Mbrazili Bruno Guimaraes kutoka Newcastle na winga Christos Tzolis kutoka Club Brugge.

Ripoti zinaonyesha kuwa klabu hiyo iko katika hatua za mwisho za kumsajili mshambuliaji wa Ufaransa na klabu ya PSG, Bradley Barcola, hivi karibuni.

Chelsea haitacheza Ulaya

Chelsea, ambao wamemsajili Xabi Alonso, wana nafasi sawa na klabu nyingine ndogo ambazo hazitashiriki mashindano yoyote ya Ulaya mbali na ligi ya ndani.

Ingawa timu tisa zitashiriki mashindano ya Ulaya, Chelsea hawakufuzu kutokana na kiwango chao duni msimu uliopita.

Kwa sababu hiyo, viongozi wa klabu hiyo walichukua hatua ya kufanya marekebisho ya kimuundo, wakianza kwa kumleta kocha mpya, Alonso, ambaye hapo awali aliinoa Bayer Leverkusen na Real Madrid; hata hivyo, hakupata fursa mwafaka akiwa Real, jambo lililosababisha aondoke mapema.

Katika jitihada za kujenga upya timu, Chelsea wamesajili wachezaji kadhaa, akiwemo Marco Palestra kutoka Atalanta na Morgan Rogers ,ambaye aliweka rekodi ya kuwa mchezaji ghali zaidi wa England pamoja na beki Maxence Lacroix kutoka Crystal Palace.

Kwa upande mwingine, wamewasajili wachezaji wenye uzoefu kama vile Danny Welbeck kutoka Brighton na Jordan Henderson kutoka Brentford, baada ya mkataba wake kumalizika.

Chelsea wana idadi kubwa ya wachezaji vijana kuliko timu nyingine yoyote katika Ligi Kuu, ambao watakuwa na uwezo wa kushindana kwa muda mrefu.

Kutokana na hali hii, inatabiriwa kuwa watacheza Ligi Kuu bila kuchoka, na bila kuwa na hofu kwamba wachezaji wao watapoteza nguvu.

Aston Villa ni mabingwa wa UEFA Europa League

Aston Villa ndio mabingwa wa Ligi ya Europa ya UEFA ya mwaka 2026, baada ya kuifunga SC Freiburg mabao 3-0.

Pia walimaliza msimu wa Ligi Kuu ya Uingereza wa 2025/26 wakiwa katika nafasi ya nne, pointi tano mbele ya Liverpool.

Aston Villa inaongozwa na kocha Unai Emery, ambaye alijiunga na klabu hiyo mwezi Novemba 2022. Tangu wakati huo, kocha huyo raia wa Uhispania amekuwa akijitahidi kuijenga timu, lakini msimu uliopita ndipo alipokuwa na mchango mkubwa zaidi.

Timu hiyo ina kikosi cha wachezaji vijana, ambao wengi wao wana umri wa kati ya miaka 21 na 31.

Licha ya kumuuza mmoja wa wachezaji wao mahiri mwaka jana, Morgan Rogers, wamewasajili mchezaji wa kimataifa wa Uswisi Johan Manzambi kutoka Freiburg na Mbrazili Jao Gomez kutoka Wolves, huku pia wakimchukua kwa mkopo kiungo wa Argentina anayechezea Chelsea, Alejandro Garnacho.

Mambo haya yote ni miongoni mwa sababu zinazotarajiwa kuipa timu ya Unai Emery fursa ya kufanya vizuri na kuendeleza mafanikio waliyopata msimu uliopita.

Manchester City imetawala Ligi Kuu ya England kwa muda mrefu

Ingawa inatabiriwa kuwa huenda ikakumbwa na changamoto, watu wa kabila la Hausa wana msemo kwamba "mzoga una nguvu kuliko Mungu Mfalme."

Walimpoteza kocha wao Pep Guardiola lakini wakampata Enzo Maresca kama mrithi wake, ingawa kocha huyo alishindwa kufanya vizuri katika klabu yake ya awali, Chelsea.

Kiungo wao mwenye ushawishi mkubwa, Bernardo Silva, naye aliondoka msimu huu na bado hawajatangaza mrithi wake.

Hata hivyo, mchezaji mwenye ushawishi mkubwa zaidi ni Rodri, ambaye anawaniwa vikali na klabu za Real Madrid na Barcelona.

Erling Haaland yuko nao, pamoja na Umar Marmoush na winga wa timu hiyo, Antoine Semenyo, ambaye alisajiliwa katika nusu ya pili ya msimu.

Manchester United itarejea kwenye Ligi ya Mabingwa

Manchester United inatarajiwa kuwa na mchango mkubwa katika msimu ujao.

Hii inafuatia juhudi za timu hiyo chini ya kocha Michael Carrick, ambaye alichukua mikoba hiyo mwezi Januari mwaka huu baada ya kufukuzwa kwa kocha wa zamani, Ruben Amorim.

Carrick aliiongoza timu ya United iliyokuwa katika nafasi ya saba, lakini walimaliza msimu wakiwa katika nafasi ya tatu.

Licha ya kumpoteza kiungo wao muhimu Mbrazil Casemiro, walifanikiwa kumsajili kiungo Youri Tielemans kutoka Aston Villa, na pia kumsajili Andrey Santos, ambaye naye ni Mbrazil, kutoka Chelsea.

Aidha, safu yao ya ushambuliaji, inayodhaniwa kuwa na uwezo wa kuwa na mchango mkubwa hapo baadaye, imeimarishwa kufuatia kurejea kwa Marcus Rashford kutoka Barcelona, ​​ambako alikuwa kwa mkopo.

Imetafsiriwa na Abdala Dzungu