Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mkapa alivyofika Mahakamani kutoa ushahidi kesi ya Mahalu
Mjadala kuhusu mashahidi katika hatua ya utetezi ya kesi ya uhaini inayomkabili Tundu Lissu unakumbusha tukio la miaka 14 iliyopita, wakati Rais Mstaafu wa Tanzania Benjamin Mkapa alipofika mahakamani kutoa ushahidi katika kesi ya aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Mahalu.
Ilikuwa mwaka 2012, wakati Mahalu alipokuwa akikabiliwa na mashitaka ya uhujumu uchumi yaliyohusiana na ununuzi wa jengo la Ubalozi wa Tanzania nchini Italia.
Mahalu alidaiwa kutoa taarifa za uongo kuhusu bei ya jengo hilo, huku upande wa mashtaka ukidai kuwa thamani halisi ya jengo ilikuwa tofauti na kiasi kilicholipwa na serikali.
Katika hatua ya utetezi, Mahalu alimtaja Mkapa kuwa mmoja wa mashahidi wake.
Na Mkapa, ambaye alikuwa amestaafu urais mwaka 2005, alifika katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, kutoa ushahidi.
Unatajwa huo ulikuwa ushahidi wa kwanza kwa rais wa zamani wa Tanzania katika kesi iliyokuwa ikimkabili aliyekuwa balozi wakati wa utawala wake.
Mkapa alikuwa kiapo na kutoa ushahidi mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Ilvin Mugeta.
Mkapa alisema nini mahakamani?
Akiwa mbele ya Mahakama, Mkapa alisema serikali yake ilikuwa inafahamu kuhusu ununuzi wa jengo hilo na ilikuwa imeuridhia.
Alieleza kuwa kabla ya ununuzi huo, jengo lilikuwa limefanyiwa tathmini na mamlaka husika za serikali, na thamani yake ilikuwa imekubalika.
Mkapa pia alieleza kuwa yeye mwenyewe alikwenda Italia na kulizindua rasmi jengo hilo lililokuwa limekuwa ofisi ya Ubalozi wa Tanzania nchini humo, Februari 2003.
Katika ushahidi wake, Mkapa aliulizwa pia kuhusu malipo ya takriban shilingi bilioni 2.9 yaliyofanyika kupitia akaunti mbili tofauti.
Alisema alikuwa ameelezwa kuwa kulikuwa na sharti hilo kutoka kwa muuzaji wa jengo na kwamba serikali haikuona tatizo, kwa kuwa jengo lilikuwa tayari limefanyiwa tathmini na serikali ilikuwa na uhitaji wa kuwa na jengo lake nchini Italia.
Wakati huo, wakili Alex Mgongolwa, aliyemuongoza Mkapa kutoa ushahidi kwa upande wa utetezi, aliiambia BBC kuwa kufika kwa rais huyo mstaafu mahakamani kulionyesha umuhimu wa kuheshimu misingi ya sheria, akiwemo kiongozi aliyewahi kushika nafasi ya juu nchini.
Kesi hiyo ilihusisha madai kwamba ununuzi wa jengo hilo uliisababishia serikali hasara ya takriban dola milioni 3.098, sawa na shilingi bilioni 2.9 wakati huo.
Kwa nini tukio hili linakumbukwa sasa?
Miaka 14 baadaye, mjadala kuhusu nani anaweza kutoa ushahidi katika kesi ya jinai umeifanya historia hiyo ya Mkapa kurudi kwenye mjadala.
Tukio la mwaka 2012 linaonyesha kwamba rais mstaafu wa Tanzania amewahi kufika mahakamani kama shahidi wa upande wa utetezi.
Lakini mazingira ya kesi ya Mahalu na yale ya kesi ya sasa ya Tundu Lissu ni tofauti, na suala la nani anaweza kuitwa kutoa ushahidi katika kesi ya Lissu linategemea hoja za kisheria na uamuzi wa Mahakama.
Kwa sasa, kinachokumbukwa ni tukio lenyewe tu kwamba mwaka 2012, rais wa zamani wa Tanzania alifika Mahakama ya Kisutu, akaapa na kutoa ushahidi katika kesi ya aliyekuwa balozi wa Tanzania.
Katika kuitabu chake cha 'My Life, My Purpose', Mkapa alisema sababu iliyosababisha kwenda Mahakamani kama shahidi ni kwa sababu alikuwa anafahamu ukweli wa jambo hilo lililotokea wakati na chini ya utawala wake.
Mahalu alishinda kesi hiyo.