Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Tangazo la Marekani la mashambulizi ya kiuchumi ni kukiri kushindwa kijeshi - Iran

Brigedia Jenerali Hossein Mohebibi, msemaji wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, amesema kauli za Marekani kuhusu mashambulizi ya kiuchumi ni sawa na kukiri kwa njia isiyo ya moja kwa moja kuwa imepata pigo kubwa katika mapigano ya kijeshi.

Moja kwa moja

Na Mariam Mjahid

  1. Mwendesha mashtaka wa mahakama ya ICC akosoa madai ya kuilenga Afrika

    Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ICC, inakabiliwa na changamoto zinazoongezeka kutoka kwa baadhi ya nchi, hususan barani Afrika.

    Katika mazingira hayo, Naibu Mwendesha Mashtaka wa ICC, Msenegali Mame Mandiaye Niang, amekuwa Dakar kama sehemu ya ziara yake katika nchi wanachama wa Mkataba wa Roma. Lengo lake ni kueleza jukumu la mahakama hiyo na kujibu shutuma zinazoikabili.

    Akizungumza na BBC News Africa, Niang amekanusha madai kwamba ICC inalenga Afrika, akisema mahakama hiyo imeanzisha uchunguzi kadhaa barani humo kwa ombi la nchi zinazohusika.

    Amesema ICC inazingatia kanuni ya ukamilishano, ambapo mahakama ya kimataifa huingilia pale mifumo ya kitaifa inaposhindwa au kutokuwa tayari kushughulikia uhalifu mkubwa.

    Niang pia amekataa tuhuma kwamba ICC inaingilia mamlaka ya nchi, akisisitiza kuwa waathiriwa wa ukatili barani Afrika bado wanahitaji haki.

    “Bado kuna watu wanaoteseka, kuna waathiriwa wengi. Na kama hatuwezi kuwarudishia kila kitu walichopoteza, basi angalau tunapaswa kuwapatia haki kwa kiasi fulani'', anasema Mame Mandiaye.

    Kuhusu baadhi ya nchi za Afrika, zikiwemo wanachama wa Muungano wa Nchi za Sahel, AES, kutangaza kujiondoa ICC, Niang amesema ni jambo la kusikitisha kuona kutokuelewana kuhusu jukumu la mahakama hiyo.

    Amesema licha ya vikwazo vilivyowekwa na Marekani dhidi ya baadhi ya maafisa wa ICC, mahakama hiyo haitarudi nyuma katika kutekeleza majukumu yake.

    “Ni vikwazo tunavyovijutia, lakini havitatufanya turudi nyuma,” amesema Niang.

    Soma Zaidi:

  2. Watu 30 wamefariki dunia baada ya dampo la taka kuporomoka Guinea

    Takribani watu 30 wamefariki dunia baada ya mlima wa taka kuporomoka na kuangukia nyumba zilizokuwa karibu katika mji mkuu wa Guinea, Conakry, kufuatia mvua kubwa.

    Watu wengine 22 wamejeruhiwa, huku sita kati yao wakiwa katika hali mbaya.

    Tukio hilo lilitokea majira ya saa nane usiku katika eneo la Dar es Salaam jijini Conakry. Serikali ya Guinea imesema dampo hilo liliporomoka ghafla baada ya mvua kubwa, huku ikihofiwa kuwa watu kadhaa wamekwama chini ya vifusi.

    Serikali imetuma idadi kubwa ya vikosi vya usalama, ikiwemo jeshi, kushiriki katika shughuli za uokoaji.

    Akizungumza na vyombo vya habari vya ndani, mwanamke mmoja amesema watoto wake watano wamefariki katika tukio hilo.

    Mamlaka zinaendelea na shughuli za uokoaji, huku zikihofia kuwa watu zaidi huenda wamefunikwa na vifusi na hivyo idadi ya vifo ikaongezeka.

    Waziri Mkuu wa Guinea, Amadou Ouari Ba, ametembelea eneo la tukio na kutathmini hali ilivyo.

    Awali, kiongozi wa eneo hilo, Lansine Sila, aliliambia shirika la habari la AFP kuwa kulikuwa na hofu ya idadi kubwa ya waathiriwa. Amesema hadi wakati huo miili 18 ilikuwa imepatikana na kupelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti.

    Soma Zaidi Hapa:

  3. Waziri Mkuu wa Uingereza aanza ziara yake ya kwanza nje ya nchi

    Waziri Mkuu wa Uingereza, Andy Burnham, anatarajiwa kuzuru Kyiv Jumatatu ya tarehe 24 Agosti 2026, katika ziara yake ya kwanza nje ya nchi tangu alipokuwa Waziri Mkuu.

    Burnham anatarajiwa kuonyesha mshikamano wa Uingereza na Ukraine, huku akishiriki pia katika maadhimisho ya miaka 35 tangu Ukraine ilipopata uhuru.

    Pia ataongoza kwa mara ya kwanza mkutano wa Coalition of the Willing, muungano ulioanzishwa na Uingereza na Ufaransa chini ya Waziri Mkuu wa zamani, Keir Starmer.

    Burnham pia atapokea tuzo kwa niaba ya wananchi wa Uingereza, ikiwa ni kutambua mchango wa Uingereza katika kuiunga mkono Ukraine, kabla ya kushiriki katika sherehe za Siku ya Uhuru.

    Ziara hiyo inafanyika wakati mashambulizi ya Urusi nchini Ukraine yakiongezeka. Ijumaa, shambulio katika kituo cha ununuzi liliripotiwa kuua watu wasiopungua 16.

    Burnham amesema Ukraine ina uhakika na uungwaji mkono wa Uingereza.

    Wakati huo huo, Moscow imeionya Uingereza kuhusu "madhara" yanayoweza kujitokeza kutokana na matumizi ya ndege zisizo na rubani zinazotolewa na Uingereza kwa Ukraine, ambazo Kyiv imekuwa ikitumia kushambulia miundombinu ya Urusi.

  4. Tangazo la Marekani la mashambulizi ya kiuchumi ni kukiri kushindwa kijeshi - Iran

    Brigedia Jenerali Hossein Mohebibi, msemaji wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, amesema kauli za Marekani kuhusu mashambulizi ya kiuchumi ni sawa na kukiri kwa njia isiyo ya moja kwa moja kuwa imepata pigo kubwa katika vita vya kijeshi.

    Akizungumza na waandishi wa habari katika mkoa wa Alborz kaskazini mwa Iran, Mohebibi amesema kama Marekani na washirika wake wangekuwa wamefanikiwa kijeshi, kusingekuwa na haja ya kuzungumzia hatua hizo za kiuchumi.

    Amesema majeshi yanayoichukia Iran yamelazimika kwa kiasi kikubwa kuondoa meli zao katika eneo hilo, huku juhudi za kufungua Mlango wa Hormuz na kudhoofisha uwezo wa Iran wa kujilinda zikishindwa.

    Kwa mujibu wa shirika la habari la Iran, IRNA, msemaji huyo amezitaka vyombo vya habari nchini humo kuwaelimisha wananchi kuhusu uhalisia wa vita na pande zinazohusika, kwa kutoa taarifa sahihi.

    Amesema vyombo vya habari havipaswi kuruhusu upande ulioshindwa kwenye vita vya kijeshi kujijenga mbele ya umma kama mshindi.

    Soma pia:

  5. Hujambo na karibu kwa matangazo ya moja kwa moja ya tarehe 24 Agosti 2026.