Je, kaswende inaweza kuambukizwa kwa kubusiana?

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, සම්පත් දිසානායක
- Nafasi, බීබීසී සිංහල
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 7
Kabla ya mwaka 2021, Sri Lanka ilikuwa ikiripoti visa vya kaswende visivyozidi 100 kwa mwaka. Hata hivyo, kama anavyoeleza daktari bingwa Nimali Jayasuriya, idadi hiyo imeongezeka kwa kasi na kufikia visa 1,500 kwa mwaka.
Kufanya ngono bila kinga na kusita kupima ugonjwa huo ni miongoni mwa sababu kuu za kuongezeka kwa maambukizi. Kutokana na aibu na unyanyapaa uliopo katika jamii, watu wengi hujaribu kuficha hali zao za kiafya. Kaswende pia huitwa 'ugonjwa wa kimya' kwa sababu unaweza kubaki mwilini kwa muda mrefu bila kuonyesha dalili zozote zinazoonekana kwa watu wengi walioambukizwa.
Makala hii inaangazia mitazamo ya kijamii inayochangia kuenea kwa ugonjwa huo, huku ikieleza kwa kina umuhimu wa huduma za upimaji wa bure na zenye usiri kamili zinazotolewa katika kliniki za serikali, pamoja na mchango wake katika kuokoa maisha.
Sababu kuu ya ongezeko la kasi la maambukizi ya kaswende nchini Sri Lanka katika kipindi cha hivi karibuni ni kuongezeka kwa tabia za kufanya ngono katika mazingira hatarishi na bila kinga. Kama anavyoeleza daktari bingwa Nimali Jayasuriya, bakteria wanaosababisha ugonjwa huo wanaweza kuenea kwa haraka kupitia aina yoyote ya tendo la ngono lisilo na kinga, iwe kati ya wanaume wawili au mwanamume na mwanamke. Daktari huyo anasisitiza kuwa kaswende inaweza kuambukizwa kwa urahisi hata kupitia ngono ya mdomo.
Tabia ya kufanya ngono na watu wengine nje ya uhusiano wa kawaida imeongezeka. Mengi ya mahusiano hayo ya kingono hufanyika bila kutumia kinga, hali inayochangia kuenea kwa kasi kwa ugonjwa huo.
Aidha, kuongezeka kwa vituo vya masaji au 'spa' katika maeneo mbalimbali ya kisiwa hicho, pamoja na ongezeko la shughuli za kingono zinazohusishwa na baadhi ya vituo hivyo, kumechangia zaidi kuenea kwa maambukizi. Katika mazingira hayo, baadhi ya watu hubadilisha wenza wa ngono mara kwa mara, huku matumizi yasiyofaa ya kondomu yakiongeza hatari ya maambukizi.
Jinsi ya kutambua dalili za kaswende
Kaswende kwa kawaida hukua katika hatua nne, ambazo huwa na dalili tofauti kama ifuatavyo:
Hatua ya awali: Kidonda kimoja kisicho na maumivu hujitokeza katika sehemu ambayo bakteria wameingia mwilini, kama vile kwenye uume, uke, njia ya haja kubwa, mdomoni au kwenye midomo. Kwa lugha ya kitabibu, kidonda hicho huitwa chancre. Kwa kawaida huwa kidonda kisafi kinachoweza kuhisi kama kifundo kidogo unapokigusa. Wanawake, hasa, wanaweza wasitambue maambukizi hayo kwa sababu kidonda hakiumi.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Hatua ya pili: Katika hatua hii, bakteria huenea mwilini kupitia damu na mfumo wa limfu. Dalili zake zinaweza kujumuisha kuvimba kwa tezi za limfu, vidonda mdomoni na vipele katika sehemu mbalimbali za mwili. Madoa meusi au malengelenge yanaweza kujitokeza hasa kwenye viganja vya mikono na nyayo za miguu. Vilevile, uvimbe unaofanana na vipele unaweza kutokea katika maeneo ya siri. Macho, ubongo na masikio pia vinaweza kuathirika.
Hatua fiche: Hii ni hatua ambayo bakteria hubaki mwilini bila dalili zinazoonekana kwa nje. Hata hivyo, kulingana na hatua ya ugonjwa na uwepo wa vidonda vinavyoambukiza, maambukizi bado yanaweza kuenezwa kwa mtu mwingine.
Hatua ya mwisho: Ugonjwa unapokaa mwilini kwa muda mrefu bila kutibiwa, unaweza kusababisha uharibifu mkubwa wa viungo vya ndani. Madhara yanaweza kujumuisha matatizo makubwa ya moyo, uharibifu wa mfumo wa fahamu unaoweza kusababisha kupooza, kupoteza uwezo wa kuona au kusikia, pamoja na kutokea kwa uvimbe unaoharibu tishu na viungo vya mwili.
Je, kaswende inaweza kuambukizwa kwa kubusiana?
"Kwa kawaida, ugonjwa huu hauambukizwi kwa kubusiana tu au kugusana kwa kawaida. Hata hivyo, wakati mwingine dalili za kaswende zinaweza kujitokeza katika sehemu tofauti za mwili.
"Tuseme kidonda cha awali kimetokea kwenye midomo ya mtu. Ugonjwa huu hauambukizwi kupitia majimaji ya kingono pekee, bali unaweza pia kuambukizwa kupitia mgusano wa moja kwa moja kati ya eneo lililoambukizwa na sehemu nyingine ya mwili wa mtu mwingine.
"Hata hivyo, maambukizi haya hayatokei kwa kugusana tu na ngozi yenye afya. Lakini ikiwa midomo au mdomo wa mtu mwenye kidonda cha kaswende vitagusana na sehemu yenye jeraha dogo kwa mtu mwingine, maambukizi yanaweza kutokea. Hasa ikiwa mtu mwenye kaswende ana kidonda kinachoonekana, ugonjwa huo unaweza kuambukizwa kupitia mgusano huo.
"Kwa hiyo, ugonjwa huu hauambukizwi kwa kawaida kwa kumbusu mtu ambaye hana dalili zozote zinazoashiria maambukizi," alisema daktari bingwa Nimali Jayasuriya.
Je, kaswende inaweza kutibika kabisa?
Daktari bingwa Nimali Jayasuriya anasema kuwa kaswende inaweza kutibika kabisa kwa kutumia dawa zinazofaa.
"Ndiyo, kaswende inaweza kutibika kabisa. Tiba kuu ni sindano ya dawa iitwayo benzathine penicillin. Kulingana na hatua na aina ya ugonjwa, baadhi ya wagonjwa huhitaji sindano moja, wengine mbili, na wengine tatu.
"Hata hivyo, ikiwa bakteria wameenea mwilini na huenda wameathiri mfumo wa fahamu, mgonjwa anaweza kuhitaji matibabu ya takribani siku 10. Ukikamilisha matibabu uliyoelekezwa na mtaalamu wa afya, ugonjwa huu unaweza kupona kabisa," alisema.
Nini hutokea ikiwa kaswende haitatibiwa?
"Ikiwa mtu hatapata matibabu, kama nilivyoeleza awali, ugonjwa unaweza kubaki mwilini kwa muda mrefu katika hatua fiche na hatimaye kuathiri mfumo wa fahamu, moyo na viungo vingine kama ini na wengu. Viungo hivyo vinaweza kushindwa kufanya kazi ipasavyo au kuharibika kabisa.
"Kwa kweli, wakati mwingine tunakutana na watu wengi ambao hawajui kuwa wana ugonjwa huu. Tunapokea wagonjwa kutoka katika wodi za magonjwa ya mfumo wa fahamu katika hospitali za serikali, wakiwemo wazee.
"Tunapowachunguza, tunagundua kuwa wana matatizo ya mfumo wa fahamu. Baadhi wamepooza, hawawezi kuona au kusikia. Ni wakati wanapofanyiwa vipimo ndipo inathibitishwa kuwa wana kaswende.
"Hii ina maana kwamba ugonjwa ulikuwa umejificha na kuendelea kukaa mwilini kwa muda mrefu bila wao kujua, hadi uliposababisha madhara hayo makubwa," alisema daktari huyo.
Je, kaswende inaweza kusababisha kifo?
Kaswende inaweza kusababisha kifo ikiwa haitagunduliwa na kutibiwa kwa wakati. Mara nyingi, kifo hutokana na madhara makubwa yanayosababishwa na ugonjwa huo unapokaa mwilini bila matibabu.
Bakteria wanaosababisha kaswende wanaweza kuathiri moyo na kusababisha matatizo makubwa ya moyo, yakiwemo kushindwa kufanya kazi kwa moyo, ambayo yanaweza kusababisha kifo.
Hata pale kifo kisipotokea, madhara ya muda mrefu ya ugonjwa huo yanaweza kuathiri sana maisha ya mgonjwa. Madhara hayo yanaweza kujumuisha kushindwa kutembea, kupooza kwa sehemu au mwili mzima kutokana na uharibifu wa mfumo wa fahamu, kupoteza uwezo wa kuona na kupoteza uwezo wa kusikia.
Kwa nini watu wengi huiita kaswende ugonjwa wa ajabu?
"Katika hatua fiche, kama nilivyoeleza, mara nyingi hakuna dalili zinazoonekana. Ugonjwa unaweza kuwa mwilini na mtu akajua kuwa ana kaswende baada tu ya kupimwa damu.
"Kwa sasa, tunawapima takribani wajawazito milioni 2.4 kila mwaka ili kubaini maambukizi ya kaswende. Kupitia uchunguzi huo, tunabaini takribani wajawazito 100 wenye maambukizi.
"Hii inaonyesha jinsi ugonjwa huu unavyoweza kubaki fiche. Hatuwezi kuugundua kwa kutazama dalili pekee, lakini unaweza kuwa mwilini. Watu wengi walioambukizwa hawaonyeshi dalili zinazoonekana," alisema daktari bingwa huyo.
Kaswende huathirije mtoto aliye tumboni?
Mama anapoambukizwa kaswende wakati wa ujauzito na asipopata matibabu yanayofaa, ugonjwa huo unaweza kusababisha madhara makubwa kwa mtoto aliye tumboni.
Kwa mujibu wa daktari bingwa Nimali Jayasuriya, bakteria waliomo mwilini mwa mama wanaweza kuvuka kondo la nyuma na kumwambukiza mtoto.
Madhara makubwa yanaweza kujumuisha kuharibika kwa mimba au mtoto kufariki akiwa tumboni. Katika baadhi ya visa, mtoto anaweza kuzaliwa hai lakini akawa katika hatari kubwa ya kufariki katika siku za mwanzo baada ya kuzaliwa.
Ikiwa mtoto ataishi, anaweza kuzaliwa akiwa na hali inayojulikana kama kaswende ya kuzaliwa (congenital syphilis). Katika hali hii, bakteria huenea mwilini mwa mtoto na kusababisha matatizo mbalimbali, yakiwemo kuvimba kwa ini na wengu, maambukizi makubwa ya ngozi, matatizo ya kuona na ukuaji usio wa kawaida wa mifupa.
Kadiri mtoto anavyokua, anaweza pia kupata matatizo ya kimuundo na uharibifu wa viungo vya ndani, pamoja na kupoteza uwezo wa kusikia. Madhara hayo yanaweza kuendelea katika maisha yake yote.
Hata hivyo, ikiwa mama atapimwa mapema wakati wa ujauzito na kupata matibabu yanayofaa, hatari ya kumwambukiza mtoto inaweza kuzuiwa kwa kiwango kikubwa sana.
Je, mtu mwenye kaswende anaweza kuwaambukiza wanafamilia anaishi nao?
Kwa mujibu wa daktari bingwa Nimali Jayasuriya, hakuna hatari ya kawaida ya kuambukizwa kaswende kwa kuishi nyumba moja na mtu mwenye ugonjwa huo.
Kaswende huambukizwa hasa kupitia mgusano wa moja kwa moja na vidonda vinavyoambukiza wakati wa ngono. Haienei kwa sababu tu watu wanaishi nyumba moja, wanakaa pamoja au kushiriki shughuli za kawaida za kila siku.
Kwa hiyo, wanafamilia hawapaswi kuwa na hofu isiyo ya lazima ikiwa mmoja wao ana kaswende. Hata hivyo, ni muhimu kufuata ushauri wa wataalamu wa afya kuhusu kuepuka mgusano na vidonda vinavyoambukiza na kuhakikisha mgonjwa anapata matibabu sahihi.
Daktari huyo pia anasisitiza umuhimu wa kukamilisha matibabu kwa mujibu wa maelekezo ya mtaalamu wa afya. Matibabu yanayofaa huponya kaswende, lakini mgonjwa anaweza kuambukizwa tena iwapo atakutana na bakteria hao baada ya kupona.
Njia rahisi zaidi ya kupata kipimo cha kaswende bila malipo nchini Sri Lanka
Njia rahisi na ya kuaminika ya kupima kaswende bila malipo nchini Sri Lanka ni kutembelea kliniki za serikali za magonjwa ya zinaa zinazoendeshwa chini ya Mpango wa Kitaifa wa Kudhibiti Magonjwa ya Zinaa na UKIMWI (NSACP).
Kwa mujibu wa daktari bingwa Nimali Jayasuriya, kuna kliniki 40 za aina hiyo zinazohudumia wilaya mbalimbali nchini humo. Mtu hahitaji rufaa kutoka kwa daktari mwingine ili kupata huduma; anaweza kwenda moja kwa moja katika kliniki na kupimwa ikiwa ana wasiwasi au dalili za maambukizi.
Kliniki hizo zimeweka mifumo ya kulinda usiri wa taarifa za wagonjwa. Taarifa za kitabibu, zikiwemo majina na maeneo wanayoishi, huhifadhiwa katika mifumo ya kompyuta inayolindwa kwa nywila, kwa lengo la kuzuia watu wasiohusika kuzifikia.
Kwa kawaida, kliniki hizo hufunguliwa kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 10:00 jioni siku za kazi, na kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 6:00 mchana Jumamosi. Baadhi ya kliniki kubwa pia hutoa huduma Jumapili.
Kondomu zinapatikana bila malipo katika kliniki hizo ili kusaidia kupunguza hatari ya maambukizi mapya. Hivyo, kutembelea kliniki ya serikali ya magonjwa ya zinaa ni njia muhimu ya kupata vipimo na matibabu kwa usiri.
Ni ugonjwa gani wa zinaa unaoongoza kwa maambukizi nchini Sri Lanka kwa sasa?
Kwa mujibu wa daktari bingwa Nimali Jayasuriya, herpes ni miongoni mwa magonjwa ya zinaa yanayoonekana kwa wingi nchini Sri Lanka kwa sasa.
Tofauti na kaswende, ambayo husababishwa na bakteria na inaweza kuponywa kwa matibabu sahihi, herpes husababishwa na virusi. Hakuna tiba inayoweza kuondoa kabisa virusi vya herpes mwilini, ingawa dawa zinaweza kusaidia kudhibiti dalili na kupunguza milipuko ya ugonjwa huo. Virusi hivyo hubaki mwilini kwa maisha yote.
Kama ilivyo kwa kaswende, watu wengi wenye herpes wanaweza wasionyeshe dalili zinazoonekana. Hali hii inaweza kuchangia kuenea kwa ugonjwa huo, hasa pale watu wanapofanya ngono bila kujua kuwa wameambukizwa.
Daktari huyo pia anasisitiza kuwa mtu mwenye ugonjwa wa zinaa kama herpes au kaswende anaweza kuwa katika hatari kubwa zaidi ya kupata maambukizi ya VVU (HIV), hasa ikiwa ana vidonda au malengelenge katika maeneo ya siri. Vidonda hivyo vinaweza kurahisisha virusi vya HIV kuingia mwilini wakati wa ngono.
Katika uchunguzi wa wagonjwa wanaofika kliniki, daktari huyo anasema baadhi yao hukutwa na maambukizi zaidi ya moja kwa wakati mmoja, kama vile VVU pamoja na kaswende au herpes.
Ujumbe muhimu ni kwamba kupima mapema, kupata matibabu yanayofaa na kutumia kinga wakati wa ngono ni hatua muhimu za kuzuia maambukizi na madhara yake.



































