Nini kipo nyuma ya kuimarika kwa uhusiano kati ya DR Congo na Israel?

Chanzo cha picha, PRIME MINISTER OF ISRAEL / X
- Author, Didier Bikorimana
- Nafasi, BBC Gahuza
- Akiripoti kutoka, Nairobi
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 8
Wachambuzi wawili wanaofuatilia masuala ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na eneo la Maziwa Makuu waliambia BBC News kuwa mvutano wa sasa katika uhusiano wa nchi hiyo na Israel unahusishwa na vita vinavyoendelea mashariki mwa nchi hiyo pamoja na uhusiano wa Israel na Rwanda pamoja na Marekani.
Mapema mwezi huu, Rais wa DRC Félix Tshisekedi alifanya ziara ya kikazi mjini Jerusalem akiambatana na maafisa wengine akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje Thérèse Kayikwamba kufuatia ziara ya Rais wa Israel Isaac Herzog jijini Kinshasa mwezi Novemba mwaka jana.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi, pande zote mbili zilitangaza kuwa ziara ya Tshisekedi ililenga kuimarisha uhusiano wa kiusalama na kiuchumi kati ya nchi hizo mbili.
Profesa Jason Stearns, anayefundisha sayansi ya siasa katika Chuo Kikuu cha Simon Fraser nchini Canada, anasema kuwa uhusiano wa Tshisekedi na Israel "umekuwa mzuri siku zote" lakini "kwa sasa Tshisekedi anaihitaji Israel zaidi kuliko wakati wowote uliopita, na nadhani hii inatokana hasa na sababu za kijeshi, ingawa kuna pia kipengele cha kisiasa."
Dkt. Richard Moncrieff, mkurugenzi wa eneo la Maziwa Makuu katika kituo huru cha kimataifa cha utafiti kuhusu utatuzi wa migogoro (International Crisis Group), anasema kuwa uhusiano unaozidi kukua kati ya nchi hizo mbili ni "matokeo ya mazungumzo ya ngazi ya juu sana" ambayo yamekuwa yakiendelea tangu Tshisekedi alipofanya ziara yake ya kwanza nchini Israel mwezi Oktoba 2021.
"Mazungumzo hayo yanajikita katika masuala ya kibiashara na diplomasia, lakini muhimu zaidi, yanazingatia masuala ya kijeshi na usalama," anasema Moncrieff.
Tangu mwezi Novemba 2021, jeshi la serikali ya DRC (FARDC) limekuwa likipambana na kundi la waasi la M23, ambalo liliteka maeneo makubwa ya majimbo ya Kivu Kaskazini na Kivu Kusini mashariki mwa nchi hiyo, ikiwemo miji ya Goma na Bukavu, mapema mwaka wa 2025.
Rwanda imetuhumiwa katika ripoti za wataalamu wa Umoja wa Mataifa kwa kulisaidia kundi hilo, tuhuma ambazo imekuwa ikizikanusha mara kwa mara.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Makubaliano ya amani ya mwaka 2025 kati ya Rais wa Rwanda Paul Kagame na Rais wa DRC, yaliyoandaliwa kwa usuluhishi wa Rais wa Marekani Donald Trump, bado hayajamaliza vita hivyo vya miaka mitano, licha ya mapigano katika eneo la mashariki mwa DRC kuendelea na kusimama mara kwa mara kwa karibu miaka 30.
Stearns anasema kuwa kushindwa kwa jeshi la DRC (FARDC) kuyarejesha maeneo hayo mikononi mwao kumemfanya Tshisekedi "kutafuta msaada popote anapoweza, ikiwemo kutoka Israel, nchi ambayo ina uwezo mkubwa sana katika nyanja hii."
"Sababu nyingine, ambayo nadhani ni muhimu sana, ni kwamba Tshisekedi ana hamu kubwa ya kuonyesha Marekani ambayo ndiyo mshirika wake mkuu kwamba yuko pamoja nao."
Moncrieff anakubaliana na hilo, akisema kuwa "kudumisha uhusiano mzuri na Marekani" ndilo jambo muhimu zaidi ambalo DRC inataka kuona katika uhusiano wake na Israel, kwa kuwa Marekani ni msuluhishi katika mzozo kati ya Rwanda na DRC kuhusiana na vita vinavyoendelea mashariki mwa nchi hiyo.

Chanzo cha picha, Richard Moncrief
Moncrieff anasema: "Kwa sasa, DRC inahisi kuwa inasikilizwa vyema mjini Washington na [viongozi wake] wanataka hali hiyo iendelee. Na kwa kuwa na uhusiano wa karibu na Israel, wanaona kuwa hilo linawapa sifa nzuri mbele ya watoa maamuzi muhimu mjini Washington."
Anasema kuwa Rwanda ina historia ya kuwa na "uhusiano mzuri sana" na Marekani kwa miaka mingi, huku vyama vyake vya siasa na serikali zikibadilika, "lakini sasa inakabiliwa na changamoto mjini Washington na tumeona mara nyingi katika miezi minane iliyopita, maafisa wa Marekani wakiikosoa Rwanda kwa shambulio lake la uchokozi dhidi ya DRC."
Uhusiano huu mzuri, kama Moncrieff anavyosema, unaweka shinikizo kwa Rwanda na unaweza hata kusababisha Marekani kuacha kuishinikiza serikali ya DRC kuhusu masuala mbalimbali, ikiwemo haki za binadamu na muhula wa tatu ambao inaonekana Tshisekedi anautaka.
"Lakini Rwanda ina uwezo wa kutumia mkakati wa muda mrefu; ina marafiki imara mjini Washington na nadhani ina uwezo wa kuhimili matatizo haya na kusubiri kuona nini kitatokea, hasa ikiona mabadiliko ya kisiasa baada ya uchaguzi wa katikati ya muhula nchini Marekani," alisema mnamo Novemba mwaka huu.
Mchambuzi huyo anasema sababu nyingine inayofanya DRC kuikaribia Israel ni kwamba DRC ina mfumo dhaifu sana na usio na ufanisi mkubwa wa kijeshi na ujasusi, lakini serikali ya sasa "ina fedha nyingi", na inajaribu kuziba pengo hili katika sekta ya kijeshi na ujasusi kwa kutumia fedha hizo kwa Israel, nchi inayojulikana kwa kuuza vifaa vingi vya kijeshi na ujasusi pamoja na utaalamu nje ya nchi.
Moncrieff anasema kuwa katika miaka ya hivi karibuni, DRC imeendelea kununua vifaa vya kawaida vya kijeshi kama vile virusha roketi, teknolojia ya ndege zisizo na rubani (drones), na teknolojia ya ufuatiliaji.
Mahusiano kati ya Israel na Rwanda

Chanzo cha picha, SIMON FRASER UNIVERSITY
Tshisekedi pia aliahidi kuhamisha ubalozi wa DRC kutoka Tel Aviv kwenda Jerusalem.
Marekani, Guatemala, Honduras, Kosovo, Papua New Guinea, Paraguay na Fiji ni miongoni mwa nchi nyingine ambazo tayari zimehamisha balozi zao, hatua iliyoibua utata kwa sababu Israel inadai Jerusalem nzima kuwa yake, huku Wapalestina wakidai Jerusalem Mashariki kuwa yao na kuamini kuwa itakuwa mji mkuu wao wakati taifa lao litakapoundwa hapo baadaye.
Hata hivyo, Israel tayari ina uhusiano wa muda mrefu wa kijeshi na kiintelijensia na Rwanda, uhusiano unaojumuisha pia historia ya pamoja ya mauaji ya kimbari.
Stearns anaona ni jambo la kutatanisha kwa Israel kuwa na marafiki wawili ambao ni maadui kutokana na vita vinavyoendelea mashariki mwa DRC.
"Kwa upande wa Israel, nadhani hakuna mgongano halisi hapa. Israel inajaribu kupanua ushawishi wake duniani kote, ikitafuta marafiki popote inapoweza kuwapata.
"Bila shaka, inakabiliwa na shinikizo kubwa la kidiplomasia kutokana na vita vyake huko Gaza na hatua zake maeneo mengine ya Mashariki ya Kati. Hivyo, inajihisi kutengwa. Kwa hiyo, jambo lolote linaloweza kuiondoa katika hali hiyo ya kutengwa ni muhimu kwa Israel."
Israel ilianzisha mashambulizi dhidi ya Gaza ikiwa ni jibu kwa mashambulizi yaliyofanywa na vuguvugu la Hamas la Palestina kusini mwa Israel mnamo tarehe 7 Oktoba 2023.
Israel na Marekani pia zilifanya mashambulizi ya anga dhidi ya Iran mnamo Februari 2026; Iran ilijibu kwa kufanya mashambulizi ya anga dhidi ya Israel, vituo vya kijeshi vya Marekani, na washirika wa Marekani katika eneo hilo, na pia ilifunga Mlango-bahari wa Hormuz ambao kwa kawaida hupitisha kiasi kikubwa cha mafuta yanayotumiwa kote duniani jambo lililosababisha kupanda kwa bei ya mafuta.
Stearns anasema Israel inafurahia kuendeleza uhusiano mzuri na pande zote mbili, akiongeza: "Bila shaka, hali ni tofauti kuhusiana na DRC. Ninaamini kuwa katika mkutano waliokuwa nao na wenzao nchini Israel, waliwaambia kuwa wanataka Israel ipunguze ushirikiano wake na Rwanda. Nadhani Israel iliwaambia kuwa italifanyia kazi suala hilo, lakini nadhani haitachukua hatua yoyote kulihusu."
"Sidhani kama upande wa Kongo utasisitiza sana juu ya hoja hiyo." "Ninaamini kuwa upande wa Kongo [DRC] utakuwa na hamu kubwa ya kupokea msaada wa kijeshi kutoka Israel, na upande wa Rwanda utakuwa na hamu kubwa ya kuendelea kununua vifaa vya kijeshi kutoka Israel..."
Moncrieff pia anasema kuwa DRC inataka Israel ipunguze uhusiano wake na Rwanda kwa sababu, ingawa Rwanda imejitahidi katika sera yake ya mambo ya nje kuwa na uhusiano wa kiwango sawa na ule wa nchi za Ghuba na ina uhusiano mzuri na nchi nyingi za Kiarabu, "bila shaka kuna watu nchini DRC wanaoamini kuwa Israel imeendelea kuunga mkono upande wa Rwanda, na ikumbukwe kuwa kwa sasa DRC na Rwanda zipo vitani."
Kuhusu uhusiano wake na DRC, Moncrieff anaongeza kuwa Israel pia inatafuta soko kwa ajili ya sekta yake ya vifaa vya kijeshi.
Je, vita mashariki mwa DRC vinakaribia kuisha?
Haijulikani wazi ni kwa kiwango gani ushirikiano wa kijeshi na wa kiintelijensia unaendelea sasa kati ya DRC na Israel.
Stearns anasema kuwa mikataba mingi inaainishwa kama siri za ulinzi, ingawa anabainisha kuwa tangu enzi za Rais wa zamani Joseph Kabila, Israel imekuwa na mikataba ya kijeshi na DRC, ambayo baadhi yake inahusu ununuzi wa vifaa na utoaji wa mafunzo.
Kufuatia ziara ya hivi karibuni ya Tshisekedi nchini Israel, Stearns anasema ilibainika kuwa DRC ilipokea msaada wa kutoa mafunzo kwa 'brigedi' moja ya jeshi la FARDC, ingawa haijulikani wazi ni 'brigedi' ipi iliyohusika.
Moncrieff anaona kuwa katika uhusiano wake na pande hizi mbili ambazo ni washirika lakini pia wapinzani, Israel itajaribu "kuuzia pande zote mbili na kujaribu kudumisha uwiano huo".
Aliongeza: "Haina nia ya kuchukua upande wowote [katika mzozo huo]. Haina kauli kali za kidiplomasia kuhusu vita hivyo. Nadhani inataka kuwa na uhusiano mzuri na pande zote mbili."
Lakini kufikia sasa, Stearns anasema hakuna dalili kwamba vita mashariki mwa DRC vinakaribia kwisha na mapigano yanaendelea.
"Nadhani tumefikia hatua ambapo wale wote wanaohusika na vita hivyo wanaona kuwa kuna maslahi makubwa katika kuendeleza vita na pia katika kuvimaliza.
"Ninachomaanisha hapo ni – hebu tuchukue wahusika wakuu watatu. Unapozungumza na viongozi wa M23, ni wazi kuwa hawaoni makubaliano yoyote ya amani ambayo serikali ya Kongo inaweza kuwapa kuwa yenye manufaa kwao... Kwa hivyo kwao, hali ya sasa [mapigano] ndiyo chaguo bora zaidi."
"Kwa upande wa serikali ya Kongo, inaendelea kusisitiza juu ya suluhisho la kijeshi mashariki mwa Kongo ingawa hawajafanikiwa kupata suluhisho hilo."
Na kwa sasa, huku Tshisekedi akikabiliwa na shinikizo kubwa kuhusiana na hali ya kisiasa ya ndani anajaribu kufanya marekebisho ya katiba, na kuna uvumi pamoja na ripoti kwamba huenda akataka kusalia madarakani kwa muhula wa tatu.
Baada ya mwaka wa 2028, wakati ambapo muhula wake wa mwisho chini ya katiba ya sasa utakapomalizika. Huu ni wakati mgumu sana kwake kuwa na sauti kuu katika suala muhimu zaidi nchini Kongo, nalo ni lile la uvamizi na ukaliaji wa [maeneo ya] mashariki mwa Kongo...
"Kwa hivyo, hatakuwa na makubaliano muhimu [ambayo kwa kawaida huhitajika] kwa ajili ya makubaliano yoyote ya amani anayoyataka."
Stearns anasema kuwa kwa sasa Kinshasa ina nia kubwa ya kuendeleza uimarishaji huu wa kijeshi.
"Na nadhani hali hiyo hiyo inatumika kwa Rwanda. Hivi sasa, licha ya kuwekewa vikwazo na serikali ya Marekani, na kukosolewa na pande nyingi, mashirika yasiyo ya kiserikali pamoja na serikali mbalimbali kwa kutuma askari mashariki mwa DRC, [upande wa Rwanda] umeonyesha utayari mdogo sana wa kuondoka."
"... ingawa Marekani imekuwa ikiahirisha muda wa mwisho wa kuondolewa kwa askari, inaonekana hakuna hatua zozote zilizochukuliwa huko ardhini. Hivyo, mistari ya mapigano [kwenye uwanja wa vita] vya mwaka jana inaanza kufanana kabisa na ile ya mwaka huu."
Stearns anasema kuwa kutokana na sababu hizi zote, vita vitaendelea, isipokuwa kama upande mmoja kati ya pande zinazopigana utakubali kuchukua msimamo, upande mmoja utaongeza nguvu zake za kijeshi, au mmoja wa wapatanishi wa amani atafanya makubaliano mengi mno na pande zinazopigana au kuweka shinikizo kubwa mno.
"Sioni lolote kati ya hayo likitokea kwa sasa," alisema. "Kwa hivyo, ukweli wa kusikitisha ni kwamba ikiwa vita vitaendelea, hadi wakazi milioni sita wa Kongo katika eneo la mashariki mwa nchi hiyo wataendelea kuyahama makazi yao na kuteseka."
Imetafsiriwa na Seif Abdallah na kuhaririwa na Mariam Mjahid































