Tanzania: Waziri Katambi awasihi madereva kuepuka vurugu wakati wa mgomo

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, amefika katika Stendi ya Mabasi ya Magufuli jijini Dar es Salaam na kuzungumza na madereva wanaopinga baadhi ya changamoto zinazowakabili katika utekelezaji wa majukumu yao.
Katambi amewataka madereva kutokubali kushinikizwa kufanya vitendo vinavyoweza kuvuruga amani na utulivu nchini, akisema mgogoro huo unaweza kuathiri uchumi wa taifa.
“Msikubali kushinikizwa kuvuruga amani, kwani shughuli hii inaathiri uchumi wa nchi. Yeyote anayefanya vurugu, jitenge naye; mjue tunawaona,” alisema Katambi.
Aidha, Katambi amewataka madereva kutoruhusu suala hilo kutumiwa kwa maslahi ya kisiasa, akisisitiza umuhimu wa kutafuta suluhu bila kuingiza siasa katika changamoto zinazowakabili.
“Lakini isije mtu akatumia hadhara hii kwa maslahi yake. Hatupaswi kuiingiza kisiasa,” alisema.
Waziri huyo pia amewataka madereva na wananchi kwa ujumla kuepuka uharibifu wa mali wakati wa kushughulikia madai yao.
“Tujiepushe kuharibu mali kwa sababu ya hili,” alisisitiza Katambi.
Kuhusu changamoto zilizowasilishwa na madereva, Katambi amesema Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imepokea hoja zao na iko tayari kuzifanyia kazi.
“Kutokana na changamoto mlizowasilisha, Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani inawahakikishia dhamira ya kutatua changamoto,” alisema Katambi.
Kauli ya Katambi imekuja wakati kukiwa na mvutano kuhusu mfumo wa pointi za leseni, ambao madereva wanaupinga wakidai unaathiri ajira zao.
Chama cha ACT Wazalendo kimemtaka Waziri Katambi kujiuzulu, kikimtuhumu kushindwa kuchukua hatua kwa wakati na kusikiliza malalamiko ya madereva kuhusu mfumo huo.
ACT Wazalendo pia imesema inaunga mkono madereva katika kupinga kile inachokiita ukandamizaji na kusimamia usalama wa ajira zao.







































