Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mvutano Lebanon utaathiri vipi mwelekeo wa mazungumzo ya Iran na Marekani?
Baada ya siku yenye umwagikaji damu, ambayo imekuwa miongoni mwa siku zenye vurugu zaidi nchini Lebanon tangu kuanza kwa duru ya sasa ya vita kati ya Israel na Hezbollah, maswali yanaongezeka kuhusu uwezekano wa makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Marekani na Iran kuendelea kudumu. Hali hii inachangiwa na kutokubaliana wazi kuhusu iwapo Lebanon imejumuishwa katika makubaliano hayo.
Jumatano usiku, makubaliano yaliyosimamiwa na Pakistan yalionekana kuanza kukumbwa na mtihani mapema, kufuatia vitisho vya Iran vya kurejea vitani baada ya mashambulizi ya Israel nchini Lebanon.
Wawakilishi kutoka pande zote mbili wanatarajiwa kukutana Islamabad siku ya Ijumaa ili kujadiliana suluhisho pana zaidi la vita litakalovuka makubaliano ya kusitisha mapigano ya wiki mbili yaliyofikiwa dakika za mwisho kabla ya muda wa mwisho uliowekwa na Rais wa Marekani Donald Trump kwa Iran.
Hata hivyo, mapigano yanayoendelea na tofauti kuhusu masharti ya makubaliano yanatia shaka uwezekano wa kupatikana kwa usitishaji mapigano wa kudumu.
Makamu wa Rais wa Marekani Jay D. Vance aliihimiza Tehran kutoruhusu makubaliano hayo kuvunjika, akisema kuwa Marekani "haikuwahi kusema kuwa Lebanon ni sehemu ya usitishaji mapigano."
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Saeed Khatibzadeh, alisema katika mahojiano maalum na kipindi cha "Today" cha BBC kwamba mashambulizi ya Israel nchini Lebanon Jumatano yalikuwa "ukiukaji mkubwa" wa makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Marekani na Iran.
Waziri Mkuu wa Pakistan Shehbaz Sharif, ambaye alikuwa mpatanishi, alikuwa ametangaza kwamba usitishwaji wa mapigano ulikuwa unatekelezwa "kila mahali," ikiwa ni pamoja na Lebanon, lakini hilo lilikanushwa na Trump, kabla ya msemaji wa White House Caroline Leavitt kuthibitisha kwamba Lebanon itasalia kuwa mada ya majadiliano kati ya Trump na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, lakini "haikujumuishwa" katika hatua hii ya makubaliano ya kusitisha mapigano.
Afisa mmoja wa Marekani alisema kuwa mpango wa kusitisha mapigano wenye pointi kumi uliochapishwa na Iran sio masharti sawa na ambayo Ikulu ya Marekani ilikubali ili kumaliza vita.
Vyombo vya habari vya serikali ya Iran vilichapisha masharti ya mpango wenye vipengele kumi ambao ulijumuisha Lebanon katika mapatano hayo, huku Rais wa Irani Masoud Pezeshkian akisema kwamba usitishaji vita nchini Lebanon ni "mojawapo ya masharti muhimu" katika mpango wa Iran ambao ndio msingi wa mapatano na Marekani, kulingana na kile kilichoripotiwa na shirika la habari la ISNA.
Maombolezo ya kitaifa
Kwa upande wake, Hezbollah iliongeza mvutano kwa kutangaza Jumatano usiku kuwa ilirusha makombora kuelekea Israel kujibu kile ilichokiita "ukiukaji" wa makubaliano ya kusitisha mapigano. Ilisema wapiganaji wake walilenga makazi ya Manara kwa mashambulizi ya roketi aina ya Salvo, baada ya "upinzani" kuheshimu makubaliano huku "adui" akiyakiuka.
Katika hali hii ya mvutano, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araqchi alisema Marekani lazima ichague kati ya "kusitisha mapigano au kuendeleza vita kupitia Israel," akisisitiza kuwa haiwezi kufanya yote mawili. Aliongeza kuwa dunia inashuhudia "mauaji ya halaiki nchini Lebanon," na sasa jukumu liko mikononi mwa Washington.
Serikali ya Lebanon ilitangaza Alhamisi kuwa siku ya maombolezo ya kitaifa kwa waathirika wa mashambulizi ya anga ya Israel.
Rais Joseph Aoun na Waziri Mkuu Nawaf Salam walikaribisha makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Tehran na Washington, lakini pia wakalaani mashambulizi ya Israel.
Aoun alisema kuendelea kwa "mabomu ya kikatili ya Israel" na "mauaji ya halaiki" yaliyosababisha vifo na majeruhi wengi kunaonyesha Israel inaendelea na uchokozi wake licha ya juhudi za kimataifa za kupunguza mvutano. Salam naye aliwataka marafiki wa Lebanon kusaidia kusitisha mashambulizi hayo kwa njia zote zinazowezekana.
Jumatano, Israel ilifanya mashambulizi makubwa ya anga katika maeneo kadhaa ya Lebanon, ikiwemo Beirut, kwa muda wa takriban dakika kumi.
Wizara ya Afya ya Lebanon ilisema watu wasiopungua 203 waliuawa na zaidi ya elfu moja kujeruhiwa, ingawa takwimu hizo si za mwisho.
Jeshi la Israel lilisema lilitekeleza "shambulio kubwa zaidi lililoratibiwa" dhidi ya Hezbollah tangu vita vianze, likidai kulenga mamia ya wanachama wa kundi hilo, akiwemo kamanda wa uwanjani.
Katika mji wa Beirut, athari za mashambulizi zilionekana wazi katika maeneo yaliyolengwa bila onyo.
Waokoaji walitumia saa nyingi kuchunguza majengo yaliyoharibiwa na kutafuta manusura kwenye vifusi.
Chini ya vifusi, kulionekana picha za familia, vipande vya nguo na madaftari ya shule yaliyoharibika, taswira iliyoonyesha ukubwa wa uharibifu katika maeneo yenye wakazi wengi.
Mpiga picha wa AFP alisema shambulio moja katika eneo la Tallet al-Khayat lilisababisha sehemu ya jengo kuporomoka.
Watu wawili walionekana wamenaswa katika ghorofa ya juu huku waokoaji wakijaribu kuwafikia.
Shambulio jingine lililenga vitongoji vya kusini mwa Beirut karibu na usiku wa manane.
Shahidi mmoja, Yasser Abdullah, ambaye anauza mashine karibu na eneo lililolengwa, alisema alishuhudia shambulio moja lililokuwa "kali sana," na kuongeza kuwa watoto waliuawa na wengine walikatwa viungo.
Mwandishi wa BBC alizungumza na Abdul Qader Mahfouz, aliyekwenda kumtembelea ndugu yake aliyejeruhiwa, akisema kuwa "raia ndio wanaolipa gharama."
Maonyo ya kimataifa
Wizara ya Afya ya Lebanon inasema vita hivyo vimeua zaidi ya watu 1,700 hadi sasa, wakiwemo angalau watoto 130, bila kutofautisha kati ya raia na wapiganaji. Israel inasema imewaua takriban wapiganaji 1,100 wa Hezbollah.
Mapigano pia yamesababisha watu zaidi ya milioni 1.2 kuyahama makazi yao, takriban sehemu ya tano ya idadi ya watu wa Lebanon, wengi wao kutoka dhehebu la Shia, huku vijiji vya mpakani vikiharibiwa kabisa.
Mvutano huu unatokea ndani ya muktadha wa vita pana vilivyoanza baada ya Hezbollah kurusha makombora kuelekea Israel tarehe 2 Machi, ikisema ilikuwa kulipiza kisasi kwa kuuawa kwa Kiongozi Mkuu wa Iran Ali Khamenei mwanzoni mwa mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran tarehe 28 Februari, pamoja na mashambulizi ya karibu kila siku ya Israel dhidi ya Lebanon.
Israel inasema inalenga kuunda ukanda wa usalama mpakani ili kuharibu miundombinu ya Hezbollah na kuzuia wapiganaji wake kusogea karibu na mpaka, jambo linalozua hofu kuwa baadhi ya maeneo yanaweza kubaki chini ya udhibiti hata baada ya vita kumalizika.
Onyo la kimataifa limeongezeka kuhusu hatari ya hali kuwa mbaya zaidi.
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alisisitiza umuhimu wa kujumuisha Lebanon katika makubaliano yoyote ya kusitisha mapigano, akisema hilo ni sharti muhimu ili makubaliano yadumu.
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uingereza Yvette Cooper alitoa wito wa haraka wa Lebanon kujumuishwa katika makubaliano hayo, akielezea mashambulizi ya Israel kuwa "makosa kabisa."
Cooper alikiambia kipindi cha "TODAY" cha BBC Radio 4 kwamba Lebanon imeshuhudia kuhama kwa raia wengi na kuandamana na athari kubwa za kibinadamu, akiongeza kuwa kuongezeka kwa sasa ni "madhara" na lazima kuzuiliwe kwa kupanua usitishaji vita ili kujumuisha Lebanon.
Naye Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Türk alisema kiwango cha mashambulizi ya Israel ni "cha kutisha," akitaka jamii ya kimataifa kusaidia kumaliza hali hiyo.
Vile vile, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres alionya kuwa mashambulizi ya Israel yanaweka hatari kubwa kwa makubaliano ya kusitisha mapigano, huku Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu ikilaani vifo na uharibifu katika maeneo yenye wakazi wengi.
Imetafsiriwa na Mariam Mjahid