Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Iran haina namna zaidi ya kurejea katika meza ya mazungumzo
Mvutano kati ya Iran na Marekani unaendelea huku Trump akionya kuwa wanaweza kurejelea kuishambulia taifa hilo.
Trump katika semi zake alisema kuwa "Iran haina budi ila kutuma wajumbe wake nchini Pakistan kwa mazungumzo"
Akizungumza na televisheni ya CNBC, Trump alisema ana Imani kuwa wataafikia makubaliano.
Trump pia alisema wamefanikiwa kuweka kizuizi cha kijeshi cha baharini karibu na Iran.
Trump alipozulizwa iwapo ataongeza muda wa kusitisha mapigano alisema "sitaki kufanya hilo, mashambulizi yataendelea, kwasababu hiyo ndiyo itakuwa hatua sahihi."
Trump alikuwa ametangaza usitishwaji mapigano wa wiki mbili ili kutoa muda kwa mazungumzo kufanyika, duru ya kwanza ya mazungumzo hayo yaliyofanyika hayakuafikia maelewano, pande zote mbili zikilaumiana.
Iran ilikuwa imetangaza kuwa hawajaamua iwapo watatuma wajumbe wao nchini Pakistan kushiriki mazungumzo na Marekani.
Akizungumza na BBC, msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni wa Iran Ismail Bakei alisema kuwa "Tulikubali kushiriki katika mazungumzo haya na nia nzuri ila upande wa pili haukuwa na umakini wowote wakutaka kuafikia makubaliano na hawakuwa na nia njema. Walibadilisha misimamo yao mara kadhaa, na kutoa vitisho vya vita"
Je kutakuwepo na mazungumzo nchini Pakistan?
Bado haijabainika wazi iwapo mazungumzo hayo yatafanyika kusitisha vita vilivyoanza tarehe 28 mwezi Februari, baada ya marekani na Israel kuishambulia Iran.
Makubaliano ya kusitisha mapigano kwa muda yanatarajiwa kukamilika tarehe 22 mwezi Aprili.
Ila Trump amesema usitishwaji mapigano utadumu kwa muda hadi Iran ikubali kuafikia makubaliano
Bado haijulikani iwapo duru ya pili ya mazungumzo ya kupatikana kwa amani yatafanikiwa baada ya duru ya kwanza kutibuka.
Naibu rais wa Marekani JD Vance anayetarajiwa kuongoza mazungumzo hayo nchini Pakistan, bado hajaondoka nchini Marekani na safari yake imehairishwa.
Spika wa bunge la Iran ambaye pia anaongoza ujumbe wa Iran katika mazungumzo hayo, amesema kuwa "hatutakubali kufanya mazungumzo na vitisho vya kutushambulia"
Marekani na Iran wanalaumiana kwa kukiukwa makubaliano ya kustisha vita.
Kizuizi cha Kijeshi cha Marekani
Kituo kinachoendesha oparesheni za kijeshi cha Marekani (CENTCOM), kilitangaza kuwa majeshi ya Marekani yameamuru meli 27 za Iran kusitisha safari zake, tangu kuanza kwa kizuizi cha kijeshi cha Marekani.
Tarehe 19 mwezi Aprili jeshi la wanamaji la Marekani, waliizuia meli moja ya Iran ambayo ilikuwa inajaribu kuvuka kizuizi cha Marekani. Iran iliitaja hatua hiyo kuwa "uharamia".
Iran awali ilikuwa imezuia meli za "adui" kupita eneo la mlango bahari wa Hormuz. Trump aidha alitangaza kuwa hataondoa kizuizi cha kijeshi cha Marekani katika mlango huo wa bahari, hadi pale Iran itakubali kuafikia makubaliano.
Aidha balozi wa Iran katika Umoja wa Mataifa, Amir Saeid Said, amesema kuna dalili ya Marekani kuondoa kizuizi cha kijeshi katika bandari za Iran, na kusisitiza kuwa watashiriki duru ya pili ya mazungumzo baada ya kizuizi hicho kuondolewa.
Matakwa ya Iran ya kusitisha vita ni yepi?
Rais Donald Trump alisema kuwa makubaliano ya kusitisha vita kwa muda yaliafikiwa kwa masharti kwamba Tehran ifungue tena Mlango Bahari wa Hormuz, njia muhimu ya usafirishaji wa mafuta na bidhaa kutoka Ghuba ya Uajemi.
Iran ilikubali kuruhusu meli kupita katika Mlango Bahari wa Hormuz kwa muda wa wiki mbili, ila hili halikudumu kwa muda mrefu.
Iran pia ilitaka kuondolewa vikwazo vya kiuchumi vilivyowekewa na Marekani, kulipwa fidia kwa uharibifu uliotokea wakati wa vita, na kuachiliwa kwa mali ya Iran iliyozuiliwa na Marekani.
Naibu wa Rais wa Marekani JD Vance alisafiri kwenda Pakistan kwa duru ya kwanza ya mazungumzo ya amani, lakini alirejea Washington bila mafanikio baada ya saa kadhaa za majadiliano.
Kutokana na kutoafikiwa kwa makubaliano mapya, Marekani ilianza kuweka kizuizi cha kijeshi baharini dhidi ya Iran, na kuonya kuwawekea vikwazo zaidi vya kiuchumi.