Marekani yaishambulia Iran mara ya pili ndani ya siku tatu

Chanzo cha picha, US Navy via Getty Images
Jeshi la Marekani limetekeleza mashambulizi mapya dhidi ya Iran, likilenga eneo la kijeshi katika mji wa kimkakati wa bandarini wa Bandar Abbas.
Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani katika Mashariki ya Kati (Centcom) imesema vikosi vyake pia vilidungua droni nne za mashambulizi za Iran ambazo “zilikuwa tishio katika eneo la Mlango wa Hormuz”.
Kwa mujibu wa Centcom, eneo lililoko Bandar Abbas lilishambuliwa wakati likiwa linajiandaa kurusha droni ya tano. Vyombo vya habari vya Iran viliripoti kuwa milipuko ilisikiwa mashariki mwa mji huo.
Mashambulizi hayo yanakuja wakati wa usitishaji mapigano wenye hali tete kati ya Marekani na Iran, pamoja na mazungumzo yanayoendelea ya kumaliza vita vya miezi mitatu vilivyosababisha usafiri wa meli katika Mlango wa Hormuz kuvurugika na bei za nishati duniani kupanda kwa kasi.
Hii ni mara ya pili ndani ya siku tatu kwa Marekani kushambulia maeneo nchini Iran, huku ikisema mashambulizi hayo yalifanywa kwa kujilinda.
Mashambulizi hayo mapya yanaongeza hofu ya kuvunjika kwa usitishaji mapigano uliopo.
Centcom ilieleza hatua zake kuwa “za tahadhari, za kujihami pekee, na zinazolenga kudumisha usitishaji mapigano.”
Mapema wiki hii, jeshi hilo lilithibitisha kutekeleza mashambulizi mengine ya “kujilinda” kusini mwa Iran Jumatatu, ambapo lilisema lililenga maeneo ya makombora ya Iran pamoja na boti zilizokuwa zikijaribu kutega mabomu katika Mlango wa Hormuz.
Kutokana na mzozo huo, maelfu ya meli za biashara na mafuta zimekwama katika eneo hilo.
Centcom imesema mashambulizi hayo yalilenga “kulinda wanajeshi wa Marekani dhidi ya vitisho vya vikosi vya Iran.”
Iran imeyalaani mashambulizi hayo na kuyataja kuwa “ukiukaji mkubwa wa usitishaji mapigano”, huku ikionya kuwa haitaliacha “tendo lolote la uhasama bila majibu.”
Rais wa Marekani, Donald Trump, pia ametishia kurejesha mashambulizi makubwa ya mabomu iwapo Iran haitakubali masharti ya Washington.
Pia unaweza kusoma:



