Jinsi Mahmoud Ahmadinejad alivyogeuka fumbo la vita Iran

Ahmadnejad

Chanzo cha picha, Isna

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 7

"Unapaswa kujua kwamba utawala huu unaochukiwa uko karibu kuanguka. Kwa uwezo wa Mungu utaanguka na hakuna mtu atakayeweza kuuokoa. Utawala huu umefikia mwisho wake na hivi karibuni utatoweka kwenye ramani ya dunia."

Kauli hii ilimfanya Mahmoud Ahmadinejad kuwa mmoja wa watu wanaojulikana zaidi duniani kwa msimamo wake mkali dhidi ya Israel kwa miaka mingi. Alihoji ukweli wa Holocaust, aliita Israel "utawala wa bandia," na alitetea kuendelezwa kwa mpango wa nyuklia licha ya vikwazo vya kimataifa.

Misimamo hiyo ilimfanya mwanasiasa huyo mwenye kauli kali kuwa mmoja wa watu ambao maafisa wa Israel walikuwa wakiwataja mara kwa mara kuelezea kile walichokiita "tishio la Iran" kwa dunia.

Sasa, jina hilohilo limeibuka tena katika moja ya simulizi za kushangaza zaidi kuhusu vita vya hivi karibuni vya Iran. Ripoti ya The New York Times inasema kuwa kabla ya vita kuanza, Marekani na Israel walikuwa wamezingatia uwezekano ambao Mahmoud Ahmadinejad angeweza kujinasua kutoka katika udhibiti wa vyombo vya usalama vya Jamhuri ya Kiislamu na kuwasilishwa kama chaguo la baadaye la uongozi wa Iran.

Ripoti hiyo inasema kuwa wazo hilo awali lilikuwa sehemu ya mpango wa Israel kwa kipindi cha baada ya kuondolewa kwa kiongozi wa Jamhuri ya Kiislamu na kuyumba kwa muundo wa mamlaka.

Mahmoud Ahmadinejad na washirika wake wa karibu bado hawajajibu ripoti hiyo. Pia hakuna taarifa kuhusu alipo au hali yake.

Simulizi ya The New York Times ilionekana ya ajabu kiasi kwamba hata wachambuzi wengi wa Marekani na Israel waliipokea kwa mashaka. Swali kuu ni rahisi: Kwa nini Israel na Marekani wamtegemee mtu ambaye kwa miaka mingi alikuwa ishara ya kauli kali zaidi za chuki dhidi ya Israel ndani ya Jamhuri ya Kiislamu?

Mkanganyiko huo uliwafanya baadhi ya wachunguzi kujiuliza ikiwa taswira ya Mahmoud Ahmadinejad imekuwa ngumu na yenye sura nyingi zaidi kuliko ilivyoonekana kwa miaka yote hii.

Ahmadinejad: Adui ambaye alikuwa na manufaa kwa Israel?

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Ili kuelewa uzito na unyeti wa simulizi hili, ni lazima kurudi kwenye miaka ya kupanda kwa Mahmoud Ahmadinejad katika siasa za Iran. Alichaguliwa kuwa meya wa Tehran mwaka 2003, wakati ambapo hakuwa mtu anayejulikana sana katika uwanja wa siasa za nchi hiyo.

Ahmadinejad aliingia madarakani mwaka 2005 kwa kaulimbiu ya haki, maisha ya kawaida, na mapambano dhidi ya ufisadi, lakini muda mfupi baadaye akawa mtu maarufu duniani, si kwa sababu ya sera zake za ndani, bali kutokana na matamshi yake kuhusu Israel, Marekani na Holocaust.

Mnamo Oktoba 2005, katika mkutano wa "Dunia Isiyo na Uzayuni" mjini Tehran, Mahmoud Ahmadinejad alisema kwamba "dunia bila Marekani na Uzayuni inawezekana." Katika hotuba hiyo hiyo, alirudia kauli inayohusishwa na Ruhollah Khomeini, akitoa matamshi yaliyotafsiriwa na vyombo vya habari vya Magharibi kama wito wa "kuifuta Israel kutoka kwenye ramani."

Takribani mwaka mmoja baadaye, mkutano wenye utata wa "Holocaust " ulifanyika mjini Tehran; mkutano ambao, kutokana na uwepo wa watu maarufu wanaokanusha Holocaust, ulisababisha wimbi kubwa la maoni kimataifa.

Baadhi ya maafisa na wachambuzi wa Israel walikuja kusema waziwazi miaka baadaye kwamba Mahmoud Ahmadinejad, kupitia matamshi yake makali na kukanusha Holocaust, kwa kweli alikuwa ameifanyia Israel kazi ya manufaa. Mwaka 2008, mkuu wa zamani wa Mossad, Ephraim Halevi, alimwelezea kama "zawadi kubwa zaidi ya Iran kwa Israel" kwa sababu, alisema, kauli za Ahmadinejad zilifanya iwe rahisi kwa dunia kuchukulia kwa uzito kile kilichoitwa tishio la Iran.

Jambo hili limewafanya baadhi ya wakosoaji wa Ahmadinejad kujiuliza ikiwa sera na matamshi yake kwa vitendo yaliinufaisha Israel zaidi kuliko Iran au hata serikali yake mwenyewe.

Aliita vikwazo vya kimataifa "karatasi zilizochanika," akaifikisha suala la nyuklia katika hatua nyeti zaidi, akasababisha maazimio kadhaa kutolewa dhidi ya Iran katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, na kuiweka nchi chini ya "Sura ya Saba ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa," hali inayomaanisha kutambuliwa kama "tishio kwa amani na usalama wa kimataifa."

Baadhi ya wachunguzi wa kimataifa waliamini kwamba kwa njia isiyo ya moja kwa moja, alisaidia Israel kuwasilisha simulizi ya "tishio la Iran" kwa dunia kupitia ushahidi wa moja kwa moja na mwenye sauti kubwa.

Bila shaka, wafuasi wa Ahmadinejad wanasisitiza kwamba katika kipindi hicho alikuwa akifuata sera kali na za kiitikadi ndani ya mfumo rasmi wa Jamhuri ya Kiislamu, na kwamba lengo lake lilikuwa kweli kuikabili Israel na Magharibi, si kuwasaidia.

Kubadilika kwa sura baada ya kupata madaraka

Lakini Mahmoud Ahmadinejad hakuwa yule yule baada ya kumaliza urais wake. Kulikuwa na mvutano kati yake na Ali Khamenei pamoja na taasisi za usalama, alizuiwa kushiriki uchaguzi mara kadhaa na polepole alijaribu kubadilisha taswira yake kutoka kuwa mwanasiasa wa serikali kikamilifu hadi kuwa kiongozi anayekosoa, mwenye umaarufu wa watu, na hata kupinga baadhi ya miundo ya mamlaka.

Hata hivyo, uungwaji mkono wa Kiongozi wa Jamhuri ya Kiislamu wakati wa utawala wake katika Ikulu ya Pasteur ulihakikisha kwamba, angalau kwa mtazamo wa nje, Ahmadinejad hakutengwa kama baadhi ya marais wa zamani, na aliendelea kufanya kazi kama mwanachama wa Baraza la Uangalizi wa Maslahi ya Mfumo.

Katika miaka hiyo kwenye mitandao ya kijamii, Ahmadinejad alijijengea taswira mpya; akitweet kwa Kiingereza, akiwapongeza timu ya mpira wa miguu ya Chuo Kikuu cha Michigan au kunukuu mashairi ya Tupac Shakur, mmoja wa wasanii mashuhuri wa hip-hop wa Marekani.

Hata alimpongeza Donald Trump kwa kile alichokiita "kupambana na rushwa ya kisiasa nchini Marekani."

Mahmoud Ahmadinejad

Chanzo cha picha, Getty Images

Raz Zimet, mkurugenzi wa programu ya Iran na mhimili wa Shia katika Taasisi ya Utafiti wa Usalama wa Taifa ya Israel Institute for National Security Studies, aliandika akijibu ripoti ya The New York Times kwenye mtandao wa X kwamba:

Mahmoud Ahmadinejad wakati wa urais wake alikuwa mtu ambaye kwa upande mmoja alitoa wito wa kuangamizwa kwa Israel na kukanusha Holocaust, lakini kwa upande mwingine alichukua misimamo inayokinzana na isiyotarajiwa wakati fulani.

Zimet pia aliandika kwamba katika miaka ya hivi karibuni, Ahmadinejad amejaribu kujionesha kama mtu "mwenye msimamo wa wastani" na anayekubalika zaidi kwa jamii ya Iran na hata kwa watazamaji wa Magharibi, lakini ingawa baadhi ya kura za maoni zinaonesha bado ana uungwaji mkono katika sehemu ya jamii ya Iran, uungwaji huo hautoshi kumwezesha kushika madaraka katika nchi yenye zaidi ya watu milioni 90.

Kwa mujibu wake, tatizo kuu la hali kama hiyo ni kwamba Ahmadinejad hana msingi imara wa kisiasa wala uungwaji mkono wa moja kwa moja wa Jeshi la Iran.

The Atlantic na simulizi ya kumuachilia Ahmadinejad

Kabla ya ripoti ya The New York Times, jarida la Marekani The Atlantic pia lilikuwa limeripoti kuhusu shambulio dhidi ya makazi ya Mahmoud Ahmadinejad eneo la Narmak.

Chapisho hilo liliandika kwamba baadhi ya ndugu wa Ahmadinejad walisema shambulio hilo siku ya kwanza ya vita halikuwa kwa lengo la kumuua yeye, bali kulenga vikosi vya usalama vilivyokuwa vimewekwa mlangoni mwa mtaa wake; vikosi hivyo, walidai, vilikuwa vikimwekea Ahmadinejad ulinzi na udhibiti wa karibu.

Ripoti ya The New York Times iliendeleza simulizi hiyo zaidi, ikisema kwamba mpango wa Marekani na Israel kuhusu Ahmadinejad ulikuwa sehemu ya mpango mpana wa kubadilisha uongozi wa Iran. Kwa mujibu wa New York Times, Ahmadinejad alikuwa na ufahamu wa sehemu ya mpango huo lakini baadaye alikatishwa tamaa nao. New York Post pia, katika taarifa yake ya ukosoaji kuhusu suala hilohilo, liliandika kwamba simulizi hil imepokelewa kwa mashaka makubwa na wataalamu.

Sehemu hii ya hadithi inaifanya hoja kuwa nyeti zaidi: Ikiwa Ahmadinejad alikuwa na ufahamu wa sehemu ya mpango huo kabla ya shambulio, taarifa hizo zilimfikiaje na kupitia nani? Na kama hakuwa na ufahamu, kwa nini waliopanga mpango kama huo walidhani kwamba angeweza kutumika katika hali ya mzozo kama huo?

Siku ya kwanza ya vita, makazi ya Mahmoud Ahmadinejad huko Narmak, Tehran, yalilengwa na shambulio. Katika picha hii, iliyopigwa mwaka wa 2014, wageni wanaonekana wakizungumza na Ahmadinejad katika uchochoro anaoishi.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Siku ya kwanza ya vita, makazi ya Mahmoud Ahmadinejad huko Narmak, Tehran, yalilengwa na shambulio. Katika picha hii, iliyopigwa mwaka wa 2014, wageni wanaonekana wakizungumza na Ahmadinejad katika uchochoro anaoishi.

Danny Citrinovich, mtafiti mwandamizi katika Taasisi ya Usalama wa Taifa ya Israel na aliyekuwa mkuu wa kitengo cha Iran katika Kurugenzi ya Ujasusi wa Kijeshi ya Israel, aliandika kwenye mtandao wa X kwamba jaribio la "kumtawaza" Mahmoud Ahmadinejad linaonesha ukosefu mkubwa wa uelewa kuhusu mfumo wa kisiasa wa Iran.

Aliandika kwamba Ahmadinejad alikuwa "mtu mwenye matarajio" mwenye historia ya kauli za chuki dhidi ya Wayahudi, ambaye ingawa alikuwa na migogoro na Ali Khamenei na jeshi la Iran, hakuwa na msingi halisi ndani ya muundo wa mamlaka, na IRGC haikuwahi kumuunga mkono.

Citrinovich alibainisha kwamba kumuweka Ahmadinejad madarakani kungehitaji mfumo mzima wa Jamhuri ya Kiislamu kuporomoka, akisema: "Tukio kama hilo haliwezi kutokea kutoka angani au kwa mashambulizi ya kijeshi."

Yossi Melman, mwanahabari mkongwe wa Israel anayefuatilia kwa muda mrefu masuala ya Mossad na taasisi za ujasusi, pia aliandika kwenye X: "Hadithi hii ina ushamba wa ajabu kwa viwango vingi."

Alisema kwamba kama ripoti ya The New York Times ni ya kweli, inaonesha jinsi Mossad na ujasusi wa kijeshi wa Israel "walivyokosa kuelewa Iran." Pia alisema kwamba kama dhana hiyo itawekwa kando, wazo la kwamba mipango ya vita ilitegemea kuangusha Iran kupitia mashambulizi ya anga au kutumia makundi ya kikabila ni "ndoto isiyo na uhalisia."

Raz Zimet pia aliunga mkono mtazamo, akisema tatizo kuu la mifano kama hiyo ni kurahisisha mno jamii ya Iran na kupuuza ugumu wa muundo wa mamlaka ndani ya Jamhuri ya Kiislamu.

Alionya kwamba kama Marekani na Israel kweli wanatafuta mabadiliko ya kisiasa Iran, hawapaswi kudanganywa na "suluhisho za kichawi," iwe ni viongozi walio uhamishoni, makundi ya kikabila, au wanasiasa wasio na msingi halisi wa kisiasa au uungwaji mkono wa kitaasisi.